KUNA dhambi kubwa inatendeka Zanzibar. Ni siasa chafu ambayo fumbo zuri la maneno linalostahili kuiita, ni “siasa za kijambazi.” Na kwa kadiri nionavyo, ni muhimu na lazima Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kama anadhibiti dola hii, akatoa uongozi wa hekima kuzuia mchuruziko mkubwa wa damu.

Rais Ali Mohammed Shein akihutubia kwenye maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Ali Mohammed Shein akihutubia kwenye maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.

Hakuna binadamu mwingine; na sababu ni dhahiri: Wasaidizi wake wanatupiana maneno yasiyojenga ingawa mmoja nimemsikia akisema “nampenda sana yeye.”

Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais, kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kiongozi wa serikali katika Baraza la Wawakilishi, ametajwa kumwambia mfanyabiashara mmoja kuwa yeye hampendi Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais.

Lakini akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara kijijini Makunduchi, Jumapili iliyopita, Maalim Seif, ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema, “mwambieni mimi nampenda sana tena sana.”

Bila ya shaka, Maalim Seif amezipata salamu za Balozi. Na hayo ndo majibu kwake. Kwa namna anavyoendesha siasa za kistaarabu – na hili linathibitishwa kwa matukio mengi – unaweza kuamini Maalim anampenda Balozi kwani hata mara moja hajathibitika kuzipalilia siasa chafu.

Amekuwa mbele katika kuleta maridhiano na kushuhudiwa katika vikao mbalimbali akizungumzia uongozi mwema kiasi cha kuwa kaulimbiu kuu kwenye ilani yake ya uchaguzi ya 2010 alipogombea tena urais.

Mwenendo wa Balozi Seif unajulikana na makada wenzake kiasi cha kupata kujadili safu hii mara kadhaa. Ni habari za kawaida Zanzibar kusikia anaupalilia urais alionao Dk. Shein.

Unapokuta wanasiasa wasiojiheshimu wanapanga mipango ya kuvuruga amani na utulivu katika nchi, ambayo wao ni viongozi, maneno mazuri ya kutumia kuwatathmini ni hayo ya kuakisi siasa za kijambazi.

Maneno haya aliyatumia Dk. Omar Ali Juma (Mwenyezi Mungu amrehemu), akiwa Waziri Kiongozi Zanzibar, kabla ya uchaguzi wa 1995.

Aliyatumia katika kuzieleza siasa za kishenzi zilizokuwa zikifanywa kabla ya uchaguzi wa kwanza nchini uliohusisha vyama vingi, baada ya mfumo wa siasa za ushindani kivyama kurudishwa 1992.

Mwanasiasa yule ambaye ninamkumbuka kusema kweli – kwa namna nilivyoona alikuwa kiongozi mwema kiasi chake kwa jamii – aliendelea kuyatumia maneno haya alipokuwa ameteuliwa mgombea mwenza wa CCM.

Sina shaka alikuwa akikemea wanasiasa aliojua ni wa CCM. Alijua vizuri akikemea kiaina dhulma walizokuwa wakitendewa Chama cha Wananchi (CUF).

Baada ya mfumo wa ushindani kivyama kurudishwa, na hasa kukaribia uchaguzi mkuu wa 1995, Zanzibar ilishuhudia matukio ya kikatili ambayo kwa sura yake, yalistahili kuitwa ya kijahili.

Kinyesi kumwaga visimani na kupakwa kwenye kuta za madarasa; majengo ya serikali kuripuliwa kwa mabomu ya petroli; matawi/maskani za CCM kuchomwa moto na makanisa nayo kuchomwa.

Kadhia ya moto ilizikumba pia mali kama viwanda vidogo vilivyokuwa vikimilikiwa na wafanyabiashara wanaodhaniwa wakifadhili CUF.

Makusudio ya kuchoma moto maskani/matawi ya CCM yalifanana na kumwaga vinyesi visimani na kupaka kwenye madarasa – kutaka wafuasi wa CUF wakamatwe na kuswekwa vituo vya polisi na hata kushitakiwa mahakamani.

Lakini makusudio ya kuteketezwa mali za waliodhaniwa wafadhili wa CUF, yalikuwa kuwadhoofisha kiuchumi ili waache kuunga mkono chama hicho tishio la kweli kwa CCM Zanzibar.

Dk. Omar, mzaliwa wa Wawi, Wilaya ya Chake Chake, Pemba, aliyesomea tiba ya wanyama (Vetenari), alijua wapangaji wa ushenzi ule ni CCM, watekelezaji walikuwa walinzi chini ya serikali za CCM.

Mamia ya wafuasi wa CUF walikamatwa na kushitakiwa mahakamani. Ila watenda dhambi, wahalifu wakubwa, walilindwa wasidhurike.

Baada ya uchaguzi, na pale Dk. Salmin Amour Juma alipofanikiwa kutwaa madaraka kwa dhulma, na kutambia ushindi aliouita wa “goli moja,” matukio hayo yakashamiri.

Dk. Salmin aliunda serikali kwa chuki akiwatenga CUF ambao walipata karibu kura sawa na CCM – yeye akitangazwa kupata asilimia 50.2 huku Maalim Seif akigaiwa asilimia 49.8.

Wakubwa wanasema Dk. Salmin alikataa ushauri wa Mwalimu Nyerere kuunda serikali ya pamoja, mfano wa iliyopo sasa tangu baada ya uchaguzi wa 2010.

Basi wafuasi wa CUF wakawa ndio wa kukamatwa. Wakawa wa kupigwa mijeledi iliyopewa jina maarufu la “Melody.” Utasikia tu jana melody walikuwa wapi, hapo mtu anauliza bakora zilitupwa sehemu ipi. Ni enzi za nguvu ya kundi la taarab la East African Melody.

Ushetani ule ulikoma pale wananchi wa Shumba mjini walipowakamata maofisa usalama wa taifa walioingia kijijini kwao na madumu ya mafuta ya petroli na chupa za kuripulia.

Wanausalama wale walizungukwa kijeshi wakiwa katika gari Landrover ya serikali, na kujikuta katikati ya umma wakilazimishwa kusema aliowatuma. Fedheha ilioje kwa askari wa serikali kutesa wananchi.

CCM wakabadilisha mbinu uchaguzi wa 2000 uliomuingiza Ikulu Amani Abeid Karume. Kukaibuka makundi ya vijana waliofugwa na viongozi na kufundishwa uharamia kwa kutumia marungu, mapande ya nondo na misumari iliyochomekwa kwenye vipande vya mbao.

Ikawa simulizi za kila siku. Wahuni wale wakipita mitaa iliyokuwa ngome za CUF na kushambulia wananchi. Mashambulizi yalifanywa majumbani usiku na mitaani mchana kweupe. Ilikuwa kazi ya kishetani iliyosaidiwa na serikali.

Muafaka wa 2002 haukusimama. Aliyoyasema Profesa Ibrahim Lipumba mbele ya Rais Benjamin Mkapa, kuasa viongozi wajifunze ili kuepuka kurudi kusaini muafaka mwingine, yakasadifu.

Sikio la kufa. Kwa kukosa uongozi mwema, Mpaka alipuuza kwa kushindwa kudhibiti CCM wenzake wa Zanzibar. Siasa za kijambazi zikaendelea huku wafuasi wa CUF, wakiwemo viongozi, wakisakamwa na kushitakiwa.

Uchaguzi wa 2005 ukafanyika ndani ya hofu kubwa ya machafuko. Kwa siku tatu wafuasi wa CUF walizingira ofisi zao Mtendeni, kushinikiza viongozi wao waache kuwazuia kupigania ushindi wao.

Hali ilitulia aliposhika Jakaya Kikwete ambaye katika hotuba yake ya kuzindua bunge la tisa, chini ya spika Samuel Sitta, aliahidi kutafuta ufumbuzi wa alichoita “mpasuko wa Zanzibar.”

Hakutimiza vizuri dhamira yake. Bali hali haikuwa mbaya kama zamani. Maridhiano yaliyokuja 2009, na hatimaye sheria 2010, yalitokana na Wazanzibari wenyewe, ambao hata yeye aliwaasa, ndio wenye jukumu na wakiitaka amani itakuwa.

Kwa kuwa ni jambo la kikatiba sasa, iliundwa serikali ya umoja wa kitaifa ikishirikisha viongozi wa CCM na CUF. Kwa bahati mbaya sana, serikali hii imejishika tu ngazi ya mawaziri. Haikwenda zaidi. Ni hapo tu.

Tangu chini waliko Masheha, viongozi wa mitaa, mpaka makatibu wakuu na wakurugenzi, wapokea amri za CCM. Wasiotii hawakai ofisini kwa amani, kila siku wanalazimika kupambana na fitina.

Fitina ya mwisho imemkumba Othman Masoud Othman, mtaalamu mbobezi wa sheria aliyefukuzwa kazi kwa shinikizo za CCM wakichukizwa na msimamo wake wa kusema ukweli kuhusu kumezwa kwa mamlaka ya Zanzibar kupitia katiba mpya ya jamhuri.

Makundi ya vijana maharamia yameanza kushambulia wafuasi wa CUF.

MAALIM Seif Shariff Hamad, mwanasiasa shupavu, mkweli, kinara wa kupigania Zanzibar yenye mamlaka kamili, amesema anampenda sana makamo mwenzake wa rais, Balozi Seif Ali Iddi.

Yeye Maalim ni makamo wa kwanza, Balozi wa pili. Wasaidizi wakuu na wa karibu wa Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Mimi binafsi, pangu pakavu tia mchuzi, ninasema pasina kigugumizi, ninampenda sana Dk. Shein kama binaadam, na sasa Rais. Anajua kuwa hii yangu, kama ilivyo ile ya Maalim Seif kwa Balozi Seif, nayo ni kauli thabiti.

Ninazidi kumsihi Dk. Shein asiziachie siasa za kijambazi zinazochimbwa na wasaidizi wake watokao Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni siasa zisizofaa kwa maana nyingi – hazijengi chama hicho wala nchi. Zinabomoa vyote viwili, CCM na nchi.

Chama kinachoishi kwa mipango ya hila, huku viongozi wake, wakubwa na wanaowafuatia, wakipinga rushwa kwa maneno zaidi ya vitendo, hakiwezi kuungwa mkono na umma, si katika nchi yenye amani wala yenye machafuko.

Matarajio ni chama hicho kuogopwa na kupoteza imani ya umma. Hatimaye na chenyewe hupotea na kubakia jina.

Kama hiki cha CCM kinachoitawala jamhuri, kimefika hapo, sijui na hayanihusu; watajua wanaokimiliki, kukiamini na kukishabikia. Ni jukumu lao halali.

Najua wapo Wazanzibari wengi, tena wengine wana elimu zao, wana fedha zao, wanaishi kutokana nacho – chama na wao damdam. Wanadhani, na labda wanaamini, kikifa nao wamekufa. Hii imani inayothibitisha ujinga wao.

Chama, tena cha siasa, sio kile cha kuweka na kukopa, ni kitu kingine, bali akili zao ni zao. Wanatakiwa waishi kwa akili zao, si chama. Akili zao ndio mtaji wao kimaisha.

Nilishasema baada ya ushetani kukoma na Wazanzibari kushiriki uchaguzi mkuu wa 2010, kwa amani na utulivu wa kihistoria, kiasi cha wafuasi wa CUF kukubalia viongozi wao kuridhia kushindwa uchaguzi kwa kutarajia kuwa sehemu ya kugawana keki itakapokuja kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa shirikishi kweli, ilidhaniwa mambo kangaja, siasa za fitina zitakwisha.

Viongozi wahafidhina katika CCM wamerudisha akili kwao. Wameamua hasa kujiandaa kudhibiti madaraka na wanatamka hadharani kuwa serikali haitachukuliwa kwa vikaratasi – yaleyale waliyoyatamka miaka ile.

Ndani ya Baraza la Wawakilishi, taasisi mhimili iliyo chombo cha kutunga sheria, wanapinga hoja inayolenga kunyoosha haki za wananchi kwa maslahi mapana ya nchi, majimboni wanategeshea matukio ya uhalifu yasiyohojiwa na dola.

Hawataki kila mwananchi apatiwe kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ambacho wanajua kinahitajika pia kwa mahitaji mengine yasiyokuwa uchaguzi. Visingizio viso maana. Wanajua wakiachia haki, watajidhulumu.

Huo upande mmoja. Wa pili, Jeshi la Polisi, taasisi ambayo kikatiba ina jukumu la kutunza amani, hivyo kutarajiwa kuwa na kasi na kutumia mbinu za kisayansi katika kudhibiti wanaochochea vurugu, linacheza mduara – ngoma ambayo wachezaji huzunguka duara.

Mwezi sasa kijijini Chwaka, ndani ya kisiwa cha Tumbatu, wahuni walianzisha uchochezi lakini hakukamatwa yeyote, hata yule kijana anayelikana, maana alionekana akichoma maskani za chama alicho cha CCM.

Vijana wa mwakilishi, wakati mwingine mwenyewe akiwa kwenye starehe zake mjini, wanatumwa kuhujumu mali za chama chao wenyewe, ili ipatikane sababu ya Polisi kutumwa kukamata vijana wa CUF.

Aibu ilioje, polisi hawa wameamua kubadilisha kanuni za utumishi wao kwa jina la PGO (Police General Orders) na siku hizi kujigeuza wa kutumwa na hata wanasiasa wachovu.

Ndio, si bwanamkubwa Haji Omar Kheri, mfalme wa Tumbatu, aliwatishia vijana wa Chwaka, ambao wamechagua kuipenda CUF sio CCM, atawafanyizia kama serikali ilivyowafanyizia masheikh wa Uamsho?

Hatua za kufikia huko ndio zimeanza. Masheikh wanaoza akili na viwiliwili Segerea jijini Dar es Salaam, huku serikali ikiendeleza hadithi za “upelelezi haujakamilika.”

Ebo, inawahusu nini watuhumiwa, kama upelelezi wa hayo wanayotuhumiwa kuyatenda haujakamilika, si wangeachiwa mpaka serikali iukamilishe?

Hayaendi hivyo katika nchi hizi. Ukamatwe, uteswe, udhalilishwe, ndipo uje kuambiwa “Jabir Idrissa huna kesi ya kujibu, uko huru.” Naona mimi na watuhumiwa tunafikiri kivyetu, na watawala kivyao. Labda sisi tuko sahihi – watawala wanatekeleza udhalimu. Wanaona raha kabisa.

Masheikh Farid, Mselem na wenzao, wakiwemo vijana wabichi waliokuwa ndo kwanza wamo katika kuhangaikia maisha, wanazo haki. Najua kwa uhakika usio shaka, Mwenyezi Mungu anazilinda; ameahidi anayemtweza kiumbe wake, atamtia adabu iumizayo.

Anaowashughulikia kikatili Mtumbatu, wananchi wanyonge wafuasi wa CUF, wana haki zao na zinastahili kulindwa. Kama wenye dhamana wanapuuza, aliyewaumba yupo macho anazilinda.

Pamoja na mbinu nyingi, wanajimbo wa Makunduchi wanaiacha CCM. Watu 600 wamechukua kadi za CUF, wengi wakiwa vijana. Ushindi ulioje kwa CUF kumegua ngome ya CCM eneo hili.

Sasa kwa kukasirika umma unahama CCM na kujiunga CUF, waonako nia ya dhati ya mabadiliko yanayoigusa nchi, wababe wa siasa za Zanzibar, wanapanga uharamia barabarani.

Vijana wahuni wanavamia msafara wa wana-CUF wanaotoka Makunduchi, kushuhudia umma wa wana-CCM walioasi na kuhamia CUF tena kwa kukabidhiwa kadi na kipenzi cha Wazanzibari wapenda mabadiliko, Maalim Seif.

Maharamia waliofadhiliwa na makada wahafidhina wa CCM wanacharanga mapanga, nondo na marungu watu wema wanaotekeleza maamuru ya katiba ya kushiriki siasa kwa kuchagua chama watakacho.

Wafuasi 25 wa CUF wamejeruhiwa kwa uvamizi huo na wanne mpaka leo hawajatoka hospitalini. Wanne hawa wamelazimika kukimbizwa hospitali jijini Dar es Salaam kupata tiba yenye utulivu kutokana na majeraha makubwa waliyopata maeneo ya kichwa na usoni.

Mmoja ameshonwa nyuzi tele juu ya pua, kutokea shavu la upande mmoja mpaka la upande mwingine. Mwingine ametobolewa kwa nondo karibu jicho kung’olewa.

Uharamia mtupu, ujinga na siasa za kijambazi? Polisi wanajua vizuri mipango hii, hawajali kwa woga tu kuwa ah, haya mambo ya wakubwa.

Mtu unaamini hivyo kwa kuwa haiyumkiniki tangu 29 Machi tukio lilipofanywa, hakuna aliyekamatwa, ingawa inajulikana waliofanya walitumia gari ya kiongozi wa CCM.

Hata kama mwenyewe amekana hadharani, si polisi waseme wamekuta nini walipochunguza namba za usajili za gari ilotumiwa na maharamia ambazo zimetajwa. Mbona haitoki taarifa zaidi ya kukiri tukio limetokea na watu wamejeruhiwa?

Polisi wanajipa dhima kubwa kulea wahalifu wanaoumiza wananchi kwa kisingizio cha siasa. Haya yanatokea wiki mbili baada ya wahuni kuteketeza kwa moto ofisi za kisasa za CUF jimbo la Dimani.

Basi kama ni tukio la moto wa kawaida, si Polisi waseme wazi? Hivi wanaponyamaza, watajivuaje lawama kuwa wenyewe wanashiriki kuvuruga amani kwa kulinda wanamaskani wa CCM wanaotuhumiwa?

Chanzo: Makala ya Jabir Idrissa katika gazeti la Mawio la tarehe 30 Aprili 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.