Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, aliwashutumu viongozi wa kisiasa wanaokosoa utendaji wa Tume yake katika kufanikisha zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kusema wametangaza kuakhirishwa kwa uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva.

Pamoja na kukanusha kutokuwepo kwa mpango huo, pia Jaji Lubuva aliwataka viongozi wa kisiasa watangaze sera zao kwa wananchi na kufanya maandalizi ya uchaguzi kwa sababu utakuwepo kama ulivyopangwa na akakosoa vikali hoja za kwamba tume haitaweza kukamilisha zoezi hilo kwa wakati.

Pamoja na kile kilichoonekana kama azma ya mwenyekiti huyo wa NEC kutaka tu kujitetea dhidi tuhuma zilizotolewa kwa tume anayoiongoza, bado NEC inapaswa kuwa wazi na kuueleza umma wa Watanzania kwamba hakuna kiongozi aliyetangaza kuakhirishwa kwa uchaguzi, bali viongozi wameonyesha tu wasiwasi wao juu ya kukamilika kwa zoezi hilo kikamilifu na kwa wakati. Kwa hivyo, hoja sio kuwa na daftari tu, bali ni kuwa na daftari sahihi na linalokubalika.

Na Said Miraj Abdullah
Na Said Miraj Abdullah

Ni muhimu sana kwa Tume hiyo kuonesha kwa vitendo hali ya kukamilika kwa zoezi hilo badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari na kubishana na wadau wake. NEC inapaswa kuelewa kwamba ni lazima kwa viongozi wa vyama vya siasa kuwa na khofu hiyo kwa sababu zifuatazo:

(1) Daima utendaji wa Tume umekuwa ukilalamikiwa na vyama kwamba sio wa haki.
(2) Daftari lililokuwepo lilikua na mapungufu makubwa na Tume hii hii iliyokuwa ikilitetea huko nyuma, sasa ilikubali kwamba kweli halifai na ndio maana ikaanzisha hili la BVR ambalo wanaliita ni bora zaidi. Kwa mfumo huu wa tume kukitetea kitu kwa nguvu zote na kisha kuja kukikataa kwa mapungufu yake, kwa nini vyama vinapoonyesha wasi wasi vilaumiwe?
(3) Uandikwaji wa daftari la sasa usipochukuliwa kwa umakini mkubwa ndio linaweza kuwa baya zaidi, sasa hapo vyama kuonyesha wasi wasi wake tatizo liko wapi?
(4) Mwenendo wa kazi hii ya uboreshaji imekua ya kusua sua na haiendani na muda kwa nini wadau wasilalamike?
(5) Mara kadhaa tume kabla ya kuanza kwa zoezi hili ilitangaza tarehe ya kuanza kazi ya uandikishaji na kuziakhirisha mfano tume ilifikia hadi kuwaeleza viongozi wa vyama vya siasa katika moja ya vikao vyake na viongozi hao kwamba zoezi lingelianza siku moja tuu baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa! Hivi uongozi wote wa tume ulipitikiwa na uzito wa jambo la uchaguzi na kupanga kuwa kazi ya uandikishaji wa daftari ianze siku moja tuu bada ya uchaguzi huo wakati mwahala mwengine hata huo uchaguzi ulikua haujafanyika, hivi hii ilikua ni kwa bahati mbaya au ni hila za makusudi?
Vyama vililiona hilo na kulikataa, tena eti tume ili wataka viongozi wa vyama washiriki katika kuwahamasisha wananchi ili wajitokeze kwa wingi kujiandikisha hivi ni kweli tume iliamini kwamba jambo hilo lingeliwezekana?
(6) Muda uliokadiriwa katika mkoa wa Njombe umeongezeka mara dufu, ukweli ni kua muda uliotumika kwa Mkoa wa Njombe ni mrefu sana na kwa kauli yake Mwenyekiti ni kua kesho ndio watakamilisha kila kitu, ukilinganisha muda uliotumika kwa mkoa mmoja wa Njombe ni kwa nini anaeonyesha wasi wasi kwa tume kukamilisha zoezi hilo kwa wakati kutokana na muda uliobakia na wingi wa maeneo aonekane amekosea?
(7) Tume imetangaza kukamilisha uandikishaji kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Iringa mwishoni mwa mwezi wa tano, jee mtu kuhoji uwezekano wa kumalizia mikoa iliyobaki kwa muda miezi michache iliyo baki baadae na kuwahi uchaguzi ni kosa?

Ushauri kwa tume.
Badala ya kubishania hoja ya kuwepo au kutokuwepo kwa uchaguzi ni vyema ijibu masuali yafuatayo, kwani hilo pekee linaweza kumfanya kila mtu kuona maandalizi kamili ya tume sio kwenye daftari tuu bali kwa uchaguzi mzima.

(1) Ni lini daftari la kudumu la wapiga kura linaloandaliwa litakamilika rasmi?
(2) Lini daftari la kudumu la wapiga kura litawekwa hadharani kwa kuanzia na Njombe ambapo inadaiwa limekamilika?
(3) Ni lini vyama vya siasa kama wadau wakuu wa uchaguzi vitakabidhiwa nakala ya daftari hilo kwa uhakiki?
(4) Ni upi uataratibu wa kalenda ya uchaguzi na elimu ya uraia?
(5) Lini kampeni za uchaguzi zitaanza rasmi?
(6) Ni ipi tarehe ya uchaguzi?
(7) Ni lini tume itakutana na vyama kupanga ratiba ya mikutano ya kampeni?
(8) Ni lini tume itakutana na wadau ili kupitia maadili ya uchaguzi na kuyaboresha?
(9) Ni lini tume itatoa ratiba ya mafunzo kwa viongozi na mawakal wa vyama?
(10) Ni lini Tume itatangaza zabuni ya vifaa vya uchaguzi ikiwemo karatasi za kura?
(11) Zitachapishwa nchi gani?

Kuna masuala mengi ambayo tume inapaswa kuyatolea ufafanuzi mapema, ili vyama viweze kujipanga na kushiriki kwa yale vitakayo weza, ni muhimu tume kujua kwamba uchaguzi huu wa mwaka huu ni mgumu kuliko uchaguzi wowote kutokea na wananchi wengi wana shauku ya kuona mambo yakiwekwa wazi na kua ya uhakika.

Sasa ikiwa hata ratiba ya kujiandikisha tuu inatolewea pale ambapo tume tayari inakwenda, hayo mambo mengine itakuwaje? Mbona tume imekua ikitoa ratiba pale tuu ambapo wako tayari kuingia mkoa huo na hawatoi ratiba kamili ya zoezi hilo kwa mikoa yote ili vyama vijiande mapema kwa ratiba ya kuwahamasisha watu kama walivyo fanya wenzao wa Zanzibar kutangaza ratiba yote kwa ujumla,

Viongozi wameonyesha wasi wasi wao, Tume watoeni wasi wasi huo na mashaka waliyonayo, hilo ndio lilikua jawabu sahihi?

Jaji na tume kwa ujumla mnapaswa kuelewa kwamba hakuna alie tangaza kwamba uchaguzi umeakhirishwa ila watu wameonyesha wasiwasi wao tuu na kumtaka yeye atoe tamko kwamba kweli watafanikisha kazi hio, kwa wakati, usahihi na uadilifu.

Ikiwa bahari haiweki amana ya kitu kinachoelea, basi ndio kila kitu kitakuja juu hadharani wakati ukifika, na hapo kweli ikidhihiri ndio uongo utajitenga.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.