Wakati uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar ukikaribia, nimeonelea nizitazame kampeni zilizipo Ireland ya Kaskazini na namna ya siasa zao zinazofanana na za hapa petu.

Rais wa chama cha Sinn Fein, Gerry Adams.
Rais wa chama cha Sinn Fein, Gerry Adams.

Kwa ufupi tu, Ireland ya Kaskazini imegawika katika makundi mawili: la kwanza ni la wafia-muungano wa Uingereza (Unionists). Hawa ni wapenzi wa muungano uliopo baina yao na Himaya ya Muingereza. Na kundi la lipi ni la wale ambao wameiweka dira ya nchi kuwa katika jamhuri moja ya Ireland nje ya muungano wa Uingereza. Vyama vikubwa katika sehemu yao ni UDP chenye mapenzi na Muungano na chama cha Sinn Fein chenye kujikurubisha zaidi na siasa za kujitenga na muungano.

Sin Fein hushiriki katika uchaguzi mkuu wa Uingereza na kushinda karibu viti vitano katika House of Commons huku vikisusia kushiriki katika bunge hilo la Himaya. Katika mahojiano ya hivi karibuni, mmoja wa viongozi wa juu wa Sinn Fein ambae pia ni Naibu Waziri Kiongozi wa Ireland ya Kaskazini, aliulizwa jambo linalohalalisha chama chake kuendelea kususia bunge huku kikishiriki katika uchaguzi. Majibu yake anasema kwamba kushiriki katika House of Commons ni kuukubali ukoloni wa Muingereza katika ardhi ya Ireland ambayo ni moja. Halafu anaendelea kwa kusema kwamba ingelikuwa msimamo wao huu haukubaliwi na wapiga kura, kwa nini hushinda viti zaidi ya vitano katika bunge kwa muda wote ambao wamekuwa wakisusia? Anachokiona ni kwamba msimamo huo ni msimamo wa wapiga kura wao.

Na Foum Kimara
Na Foum Kimara

Kwa upande wa UDP, ambao ni wapenzi wa Muungano, wanasema hushiriki katika bunge hilo na huwa na nguvu za kuwekeza maslahi zaidi katika Ireland ya Kaskazini. Mfano, katika suala la mageuzi kwenye mfumo wa ustawi wa jamii ambapo sera za Muungano ziliwaathiri pia wananchi wa Ireland ya Kaskazini, DUP inasema kwamba ushiriki wa Sinn Fein katika House of Commons ungeliweza kuzuia sera hizo kutotumika katika Ireland ya Kaskazini. Sinn Fein inapinga hilo ikisema kuwa sio tu kwamba wabunge 18 wa  Ireland ya Kaskazini hawawezi kamwe kuwa na wingi wa kutosha kupinga sera hizo, bali baya zaidi ni kuwa ushiriki wao unahalalisha sera hizo kutumika katika ardhi yao.

Lakini kuna tafauti gani ya SNP ya Scotland na Sinn Fein ya Northern Ireland wakati vyama vyote viwili vinabeba ajenda ya wazi kabisa ya kujitenga na Muungano wao na Uingereza? Tafauti ni kuwa SNP imefanikiwa kujijenga zaidi katika Scotland kutokana na kuwamo kwao katika House of Commons. Viti walivyonavyo katika House of Commons vimesaidia kuwapa sauti na hata kuziangusha serikali pale zisipokubaliana nazo.

Mfano katika miaka ya ’70, ni wabunge wa SNP walioweka nguvu ya mwisho ya kutokuwa na imani na serikali ya chama cha Labour baada ya chama hicho kwenda kinyume na makubaliano yao ya awali na SNP. Baya zaidi, serikali iliofuata ya Conservatives iliwanyonya zaidi SNP kiasi kwamba uchaguzi uliofuata wabunge wa SNP walipoteza viti vyao kwa Labour kama ni adhabu ya kushirikiana na Conservatives na kudharau maslahi mapana zaidi ya wananchi wa Scotland.

Ukiitazama SNP na Sinn Fein utakuta moja imeweza kusogea mbele zaidi na kuyaweka maslahi ya wananchi wao mbele kwa kushiriki katika siasa za ushindani katika bunge la muungano wao. Leo hii SNP imeunda serikali yake yenyewe ndani ya Scotland, ikaweza kuitikisa himaya nzima ya Muungano wao kwa ile kura ya maoni ambayo imewapa mengi zaidi yenye maslahi nayo kwa khofu ya anguko la himaya nzima waliyokuwanayo Waingereza. Ukiitazama Sinn Fein, bado ipo katika msuguano na UDP wakiwa na serikali ya umoja ya Ireland ya Kaskazini, huku bunge la muungano likiendelea kuweka vipingamizi kwenye maslahi makubwa kwa nchi yao.

Kwa sasa, ipo haja ya Sinn Fein kutazama upya ajenda yake ya kutoshiriki katika bunge la Muungano, ikiwa lengo ni kufufua mabadiliko ya kweli katika ardhi yao. UDP imekuwa kama CCM Zanzibar, udogo wao na woga wa mabadiliko umewafanya wawe na sauti ndogo katika House of Commons kiasi kwamba ni vigumu kufanikiwa katika kusimamia yale yenye maslahi na Ireland ya Kaskazini mithali CCM inavyoshindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanzania.

Siasa za Ireland ya Kaskazini na za hapa visiwani Zanzibar zinafanana kwa namna ya makundi yalivyogawika katika sehemu mbili hasa katika masuala ya utaifa wa Zanzibar na Muungano. Tafauti ni kwamba siasa za Ireland ya Kaskazini zina mahusiano zaidi na udini baina ya UDP na Sinn Fein, kwa vile Sinn Fein ni yenye wingi wa wafuasi wa madhehebu ya Katoliki, huku UDP ukiwa na wafuasi wengi wa madhehebu ya Kiprotestanti. Mgogoro wao unabeba utaifa na makundi ya kiimani baina yao kiasi kwamba ni rahisi kuzijuwa sehemu za vyama vyao kwa kutazama tu mgawanyiko wa wakaazi kwa misingi ya imani zao.

Ireland ya Kaskazini imeweza kujinasua katika mgogoro wa miaka kwa kuundwa kwa serikali ya umoja baina ya UDP na Sinn Fein. Nasi Zanzibar tumeweza kupiga hatua kwa miaka mitano sasa kwa serikali ya wote, lakini pole pole tumekuwa tukijivuta katika siasa za nyuma za mifarakano bila ya kutathmini athari zake. Kwa upande wetu, wachache waliokataa maridhiano ndio waliopenya katika serikali ya umoja na kutumia njia za kuimaliza isiweze kuendelea. Watu hao ambao wanaitwa “wahafidhina” kwenye siasa za Zanzibar kwa kutaka kwao kung’ang’ania mfumo wa kale wa utawala na siasa, wanatumia kisingizio cha kuupendelea mfumo uliopo wa Muungano kuihujumu serikali ya umoja wa kitaifa.

Naangalia mdahalo wa Ireland ya Kaskazini na kucheka kwa jinsi walivyo na ubishani wa jadi hasa baina ya UDP na Sinn Fein, lakini wameweza kuunda serikali ya umoja na kuheshimiana katika uongozi wao wa pamoja bila ya matusi na uchochezi wa kibaguzi. Hiyo ndiyo raha ya kuwa na serikali ya aina hii, ikiwa imejengwa juu ya misingi na dira.

Naamini kwamba siasa za mashindano ni muhimu sana katika jamii yoyote yenye muamko wa mabadiliko, na naamini pia unaweza kuunda serikali ya umoja na vyama vilivyounga serikali hiyo vikabaki na tafauti zao, ikiwa tu uongozi wa juu utaweka msisitizo wa faida ya kuwapo kwa mfumo wa aina hio.

Lakini unapokuwa na kiongozi asiyekubali mfumo huo lakini akawa mtendaji mkuu wa serikali husika, basi ni sawa na kupiga ngumi ukuta. Tutarudi tu nyuma tulipotokea na athari zake ni mbaya zaidi. Hiyo ndiyo hatari inayoikabili Zanzibar yetu.

Imehaririwa na Mohammed Ghassani

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.