WIKI iliyopita, Joseph Mihangwa,mwandishi mwenzangu wa Raia Mwema,aliandika makala gazetini humu chini ya kichwa cha maneno “Dini za kigeni ni tishio kwa Umoja Afrika.” Ni makala yasiyo na nia njema.Sifichi, binafsi yalinichafua.

Nilianza kuingia hasira lakini nikajirudi nikikumbuka kipande cha wimbo wa kale wa Pate kisemacho: “hasira hasara mno, mno hasarani.”

Makala hayo yalinichafua kwa sababu mbili. Moja ni kwamba kuna baadhi ya mambo yaliyoandikwa humo ambayo si sahihi. Si sahihi kihistoria wala si sahihi kimantiki.Kwa hakika, mna mahali ambamo Mihangwa ameinyonganyonga mantiki utadhania anainyonga shingo ya kuku.

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Sababu ya pili ni usafihi ambao Mihangwa ameunyunyiza hapa na pale katika makala mazima. Kwa mfano, kuna pahala ameandika: “Siku zote popo si wa kutegemewa; kwani utii na uaminifu wake hautabiriki.”Kwa ufupi, popo haaminiki.
Ni maneno mazito hayo. Mazito kwa sababu “popo”anayemzungumza ni mwenyeji wa Afrika ya Kaskazini. Unaweza kuirefusha maana yake ya “popo” kuwa ni Mwafrika aliyechanganya damu au aliye na utamaduni wa Kiarabu na unaweza kuirefusha zaidi maana yake ya “popo” kuwa ni Mwafrika aliye Mwislamu.
Hoja kama hizi za “kipopo” lazima tuzipopoe kwani ni za hatari. Ni hoja za kibaguzi, za chuki, zinazoweza mara moja, kama kufumba na kufumbua, ikazusha balaa kama tunalolishuhudia siku mbili hizi Afrika ya Kusini.

Rais wa zamani wa Congo, Joseph Kasavubu.
Rais wa zamani wa Congo, Joseph Kasavubu.

Hoja kama hizo ni hoja zinazowagawa Waafrika na zinazotumiwa na maadui wa Afrika kuligawa bara la Afrika, kulidhoofisha na kulifanya lisiweze kuungana. Ile lugha waitumiyao maadui wa Afrika ya “Afrika, Kaskazini mwa Sahara” na “Afrika, Kusini mwa Sahara” ni sehemu ya mkakati wao wa kuigawa Afrika.
Msamiati wa “Afrika nyeusi”, anaoutumia Mihangwa, ni msamiati wa ukoloni mamboleo unaopendwa kutumiwa na wale wanaochochea mgawanyiko wa Afrika.
Ni sawa na lugha waliyokuwa wakiitumia ilipokuwako Sudan moja. Wakisema “Waislamu wa Kaskazini na Wakristo wa Kusini” au “Waarabu wa Kaskazini na Waafrika wa Kusini.”
Msamiati huo ulitumiwa kupalilia moto uliowashwa kwa kuni nyingine lakini ulisaidia kutimiza lengo la kuigawa Sudan na kuikata pande mbili. Matokeo yaliyokusudiwa tunayashuhudia.
Nililikuna bongo langu kwa muda mrefu nikijiuliza iwapo niyagusie machache kati ya aliyoyaandika Mihangwa au niyapuuze yote. Waarabu wana usemi wao: “Jawab safih, skut.” Yaani jawabu ya safihi ni kumkalia kimya. Kumwacha na yake na kuuacha usafihi wake umzongereshe mwenyewe.

Makamu wa Rais wa zamani wa Kenya, Joseph Murumbi.
Makamu wa Rais wa zamani wa Kenya, Joseph Murumbi.

Baada ya kutafakari nikaona si uungwana kufanya hivyo kwani Mihangwa ni mmoja wa waandishi wa Tanzania ninaowastahi. Kwa hivyo, badala ya kumpuuza ni kheri kumkosoa. Aidha, si busara kuuacha upotoshaji wake utubabaishe Waafrika, hususan vijana wetu.
Ndipo nilipoamua kwamba ku-“skut” sito-“skut”. Nitaandika. Sitostaajabu ikiwa, kwa kuunukuu huo usemi wa Kiarabu, nimewaudhi wenye chuki na “Uarabu” au chochote chenye kuhusika na utamaduni wa Kiarabu au Uislamu, barani Afrika.
Ijapokuwa mengi ya maneno ya Kiswahili yana asili ya Kiarabu watu kama hao huona karaha mtu akinukuu maneno ya Kiarabu lakini huona raha mtu akinukuu maneno ya Kizungu, hata kilatini ambacho siku hizi kimekufa.
Hoja alizozitoa Mihangwa wiki iliyopita alikwishazitoa mwaka 2010 katika Raia Mwema (toleo la 122). Hakufanya vibaya kuzikariri. Alipoteleza ni kuushadidia upotoshaji wa historia.
Nionavyo, kwa muhtasari, asemacho Mihangwa ni kwamba mtu hawezi kuwa Mwafrika, mwenye hisia za Kiafrika, ila awe mweusi. Kwetu Zanzibar, fikra kama hizo tunaziita fikra za “ugozi,” na za ubaguzi usio na haya. Zimechangia sana kutufanya tusiendelee.

Mpigania uhuru wa Kenya, Pio Gama Pinto.
Mpigania uhuru wa Kenya, Pio Gama Pinto.

Miongoni mwa maswali yanayomwenda akilini mwake Mihangwa ni: “ni nani anayeweza kuitwa Mwafrika wa kweli? Ni ipi Afrika ya kweli na Waafrika wa kweli?”
Jibu la kizalendo ni kwamba hakuna “Afrika ya kweli” na “Afrika danganyifu.” Iliyopo ni Afrika moja na tunataka tuzidi kuijenga iwe na umoja wa kweli, umoja wa kisiasa.
Umoja tunaoutaka ni umoja ambao kila nchi itakuwa na usawa; umoja wa haki; si umoja utaoruhusu au kuhalalisha nchi yoyote barani humo imezwe na dubwesho moja la kisiasa au la kiserikali lisilozitendea nchi zote haki sawa.
Afrika ya “ugozi”, Afrika aitakayo Mihangwa haipo. Haijawahi kuwako na wala haitakuwapo. Bara la Afrika daima limekuwa bara la mchanganyiko. Huo ndio utamu wake, ndio haiba yake na hatimaye mchanganyiko huo ndio utaokuwa nguvu yake.
Uafrika si rangi. Uafrika, hasa katika enzi hizi za utandawazi au utandaridhi, ni imani.

Ndiyo maana Afrika daima itawalaani mahaini wake akina Moise Tshombe aliyekuwa mweusi kama makaa na itaendelea kuwaenzi wazalendo wa Kiafrika kama akina Pio Gama Pinto wa Kenya aliyekuwa na asili ya kutoka Goa au mpigania uhuru wa Zanzibar, Ruti Bulsara, aliyekuwa na jadi ya Kiparisi kutokea India au Joe Slovo wa Afrika ya Kusini aliyekuwa Kamanda wa Umkhonto we Sizwe, lililokuwa Jeshi la Ukombozi la chama cha ANC.
Slovo aliyekuwa na asili ya Kiyahudi alizaliwa Lithuania na alihamia Afrika ya Kusini pamoja na wazazi wake alipokuwa na umri wa miaka minane.
Sijui Mihangwa atawaweka wapi wananchi wa Cape Verde ambao wengi wao ni machotara au makrioli, yaani watu waliochanganya damu.

Joe Slovo, mpigania uhuru wa Afrika ya Kusini.
Joe Slovo, mpigania uhuru wa Afrika ya Kusini.

Na machotara wa Cape Verde wamechanganya damu chungu nzima. Wazungu wa mwanzo kuishi huko walikuwa mabaharia wa Kihispania na wa Kitaliana. Wakafuatiwa na walowezi wa Kireno. Baadhi ya Wareno hao walikuwa Waislamu na wengine walikuwa Mayahudi.
Wote walifululizia kwenda kuishi Cape Verde wakikimbia mateso ya Mahakama ya Kanisa Katoliki dhidi ya waumini wa dini za Kiislamu na Kiyahudi hasa katika karne za 15 na 16.
Damu nyingine za wananchi wa Cape Verde ni za Waholanzi, Wafaransa, Waingereza, Waarabu (kutoka Lebanon na Morocco), Wachina (hasa kutoka Macau), Wahindi, Waindonesia, za Wamarekani, damu za Wabrazil (wenye asili za Kireno na Kiafrika) na damu za watu kutoka nchi nyingine za Amerika ya Kusini.
Yapo baadhi ya mambo aliyoyaandika Mihangwa ambayo ni sahihi na hayapingiki. Mfano kwamba Waethiopia na Wamisri wa kale walikuwa watu weusi.
Juu ya hayo, kuna mengine aliyoyaandika yenye kushangaza. Mfano ni pale alipouliza ni nchi ngapi za “Afrika ya Kiarabu” zilizowahi kushiriki katika ukombozi wa nchi za Afrika bila uswahiba wa kidini? Kwa “Afrika ya Kiarabu” anakusudia mataifa ya Afrika ya Kaskazini.
Inaonyesha hajui mchango mkubwa wa Morocco, ilipokuwa chini ya utawala wa Mfalme Mohamed wa Tano na Mfalme Hassan wa Pili, babu na baba wa Mfalme Mohamed wa sasa, katika ukombozi wa Afrika. Chini ya tawala zao, Morocco ilivisaidia kwa hali na mali vyama vya ukombozi vya nchi kadhaa za Kiafrika, na si kwa sababu za kidini.

Mfalme Hassan wa II wa Morocco
Mfalme Hassan wa II wa Morocco

Hata vuguvugu la kupigania uhuru Kenya lilifadhiliwa kwa kiwango kikubwa na Morocco. Joseph Murumbi, Makamu wa Rais wa kwanza wa Kenya, kabla ya uhuru akisafiria pasi ya Morocco.
Babake Murumbi alikuwa Goa na mamake alikuwa Mmasai. Lakini wenzake kina Jomo Kenyatta hawakufikiri kuwa mchanganyiko wake wa damu ulimpunguzia Uafrika wake.
Nadhani hata Mihangwa asingemkatalia Uafrika wake; labda angeutilia shaka lau babake Murumbi angetokea Afrika ya Kaskazini au “Afrika ya Kiarabu,” kama aitavyo sehemu hiyo ya Afrika. Au pengine angekereka lau babake Murumbi angekuwa Mjapani kwa sababu Mihangwa ameandika:
“Tanzania imo mbioni kuimarisha mizizi ya ulaghai huu kwa kukubali kuanzisha Uraia wa nchi mbili kwa wageni na kwa Watanzania. Kwa mtindo huo, hatutashangaa siku moja, kwa mfano, Bunge letu kuongozwa na Spika Mjapani.”
Kutakuwa na ubaya gani, au patatendeka dhambi gani, ikiwa patazuka Mtanzania mwenye asili ya Kijapani akaliongoza Bunge? Akitokea, tumpime kwa macho yake ya kubana au kwa uzalendo wake?
Inavyoonyesha Mihangwa angekereka lau Rais wa zamani wa Congo Joseph Kasavubu angelikuwa rais wa Tanzania.
Mimi ningekereka lakini kwa sababu za imani, za itikadi za siasa na sio kwa sababu za jinsi yake. Babu yake Kasavubu, mzaa babake,alikuwa Mchina.Hilo lingemtaabisha Mihangwa.
Pengine angelikuwa raia wa Gabon, Mihangwa angeanzisha kampeni ya kumpinga Jean Ping, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, asiwe mgombea urais wa nchi hiyo.

Jean PING
Mkuu wa zamani wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping.

Babake Ping alikuwa Mchina.Kwa hivyo, kwa mantiki ya Mihangwa, Jean Ping ni “Mwafrika bandia”.
Kadhalika Mihangwa ama hajui au amesahau mchango wa Algeria kwa ukombozi wa Afrika ya Kusini na nchi nyingine zilizokuwa bado zikitawaliwa na wakoloni baada ya Algeria kuwa huru.Na Algeria haikutoa msaada huo kwa sababu za kidini.
Wala Gamal Abdel Nasser aliyekuwa Rais wa Misri hakusaidia ukombozi wa nchi za Kiafrika kwa sababu za kidini.

Asingefanya hivyo kwa sababu nchini mwake kwenyewe akiwakandamiza wanaharakati wa Kiislamu wa kundi la “Ikhwan Muslimin”.
Mihangwa anaendelea kunishangaza anapozungumzia “utamaduni wa Kiafrika” kana kwamba Afrika ina utamaduni mmoja, hata katika hiyo anayoiita “Afrika Nyeusi”.
Afrika haina utamaduni mmoja; ni bara lenye tamaduni mbalimbali. Huenda baadhi yao zikawa zinafanana lakini huwezi kusema kwamba ni utamaduni mmoja.
Na sijui Mihangwa anamzungumzia Profesa Ali Mazrui yupi anapoandika kwamba Mazrui hakuwahi“kutoa mawazo ya kujenga kwa Bara la Afrika, mbali na kujishughulisha na siasa za migogoro ya kimataifa na mitafaruku ya kidini – kati ya Ukristo na Uislam.”

Marehemu Muammar Gaddafi wa Libya
Marehemu Muammar Gaddafi wa Libya

Ni wazi kwamba Mihangwa hakumsoma Mazrui sawasawa wala hakufuatilia harakati zake na mawazo yake kuhusu Afrika. Angelijiuliza tu kwa nini Chuo Kikuu cha Morgan State University kiliamua kumtunukia Mazrui Tuzo ya DuBois-Garvey kwa Umajumui wa Kiafrika.
Pengine Mihangwa ameyasahau tu mengi ya Mazrui kama alivyosahau jinsi nchi za Kiafrika zilivyosimama kidete kuiunga mkono Libya wakati nchi hiyo ilipowekewa vikwazo na madola makuu. Kama hakusahau basi asingeliuliza: “Afrika nyeusi inajitoa mhanga vipi kwa ndugu zao wa “Afrika ya Kiarabu” wanapopata majanga, kuonesha kwamba Waafrika ni wamoja?”
Amesahau jinsi Nelson Mandela alivyomkaripia Bill Clinton kuhusu Libya kama alivyosahau kuwa Mu’ammar Qadhafi ndiye aliyekuwa mkunga wa Muungano wa Afrika.
Jengine alilolisahau Mihangwa ni kutwambia walikotokea Waberber, wenyeji asilia wa Afrika ya Kaskazini.
Historia inatwambia kwamba Waberber wamekuwa wakiishi Afrika ya Kaskazini miaka 10,000 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (Yesu Kristo).
Hii leo wametapakaa Algeria, Morocco, Tunisia, Libya, Mauritania, Mali na Niger. Na wapo hata Misri. Wengi wao wana rangi ya dhahabu. Nao pia ni “Waafrika bandia”?
Hii tabia ya Waafrika kubaguana wenyewe kwa wenyewe baina ya “wenye nchi” na “wananchi”; na baina ya Waafrika “wananchi” na Waafrika “wageni” ndiyo sababu kubwa ya Waafrika kufika hadi ya kuchinjana wenyewe kwa wenyewe Afrika ya Kusini.
Mauaji hayo ni aibu yetu sote kama ulivyo ubaguzi baina ya “Waafrika wa kweli” na “Waafrika bandia.” Ubaguzi aina hiyo ndio pingamizi kubwa kwa Umoja wa Afrika.

Chanzo: Raia Mwema tarehe 22 Aprili 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.