Lengo la makala hii ni kukusadia wewe kijana wa Zanzibar kuwa mwanamapinduzi wa kweli katika mwaka huu wa 2015, ambao sote tunakubaliana kuwa ni mwaka wa maamuzi na hasa kwa kuwa huwa tunasema kuwa nchi yetu ni nchi ya kimapinduzi.

Lakini kabla ya kufika huko, turudi nyuma kidogo kwenye historia ya hivi karibuni, ambayo vijana wenzangu wengi tunaikumbuka. Tangu nchi yetu irudi tena katika mfumo wa nyama vingi mwaka 1992, ambapo ulimwengu na mataifa yaliyoendelea yanaamini kwamba huo ndio mfumo bora zaidi katika kuingoza nchi ama dunia kwa ujumla, nchi zetu za Zanzibar na Tanzania zimeshaingia katika uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi mara nne –  mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 – na sasa tumo katika mwaka 2015 ambapo tumebakiwa na miezi mitano kuingia kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwishoni mwa mwaka 2015.

Kitu kimoja kipo wazi kwa upande wa Zanzibar: katika chaguzi zote hizo hakuna hata mwaka mmoja wagombea wa nafasi ya urais mshindi kufikia asilimia angalau 60%. Kwa mujibu wa tovuti ya http://www.zanzibarassembly.go.tz,  katika mwaka 1995  aliyetangazwa kushinda alipata asilimia 50.2% na aliyemfuatia alitangazwa kupata asilimia 49. 1%, kwa mwaka 2000  mgombea aliyetangazwa kushinda alipata asilimia 56% na aliyefuatia alipata asilimia  44%, katika mwaka 2005 mgombea aliyetangazwa kushinda alipata asilimia 53% na aliyemfuatia alipata asilimia 47%  na tukimalizia mwaka 2010,  mgombea wa chama kilichotangazwa ushindi  alipata asilimia 50.1% na mgombea aliyefuatia alipata asilimia 49.1%. Katika mara zote nne, chama kilichoshinda kilipata  wastani wa asilimia 52%  na kilichofuatia kilishinda kwa wastani wa asilimia 47%.

Na Ali Mohamed Ali
Na Ali Mohamed Ali

Katika chaguzi tatu za awali – yaani mwaka 1995, 2000 na 2005, kulikuwa na utaratibu wa kikatiba ambao unamruhusu mshindi kuchukuwa kila kitu, kwa maana ya kwamba hata kama alimshinda mpinzani wake kwa asilimia ndogo, yeye ndiye ambaye aliunda serikali peke yake. Hilo, likijumlishwa na namna chaguzi hizo zilivyofanyika mukiwemo matukio ya uvunjwaji wa haki za binaadamu katika jitihada za chama tawala kusalia madarakani, lilizua mzozo usiomalizika visiwani Zanzibar.

Lakini kabla kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Zanzibar iliingiya katika uchaguzi mwengine wa kihistoria, pale Kamati ya Maridhiano ilipowasilisha pendekezo lao kwa serikali katika kutafuta suluhu za magomvi hayo yasiyokwisha kila baada ya uchaguzi. Kamati hiyo iliyoundwa na washiriki sawa kutoka katika pande zote za vyama vyenye wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi, yaani CCM na CUF, ilipendekeza kuanzishwe serikali shirikishi.

Ndipo hoja ile ikapokewa na upande wa serikali ikapelekwa Baraza la Wawakilishi, nalo Baraza kwa kupitia taratibu zake likakubali kwamba ipo haja ya kufanywa kura ya maoni itayowashirikisha wananchi moja kwa moja kupata ridhaa yao  juu ya uanzishwaji wa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Tarehe 01 Agosti 2010, matokeo hayo yalitoa ushindi wa kura za NDIO kwa asilimia 66.40% dhidi ya kura za HAPANA asilimia 33.90%.

Hapa, katika huu uamuzi wa muundo gani wa serikali unafaa uwepo Zanzibar palitendeka kitendo cha kimapinduzi na kila aliyeshiriki kukifanikisha alikuwa ni mwanamapinduzi na ndipo ambapo napenda nipazungumzie kidogo,  kwa kuwa sababu mbili: moja, ndipo panapoonesha dhahiri kwamba watu walielewa nini hasa maana na umuhimu wa uchaguzi na, pili, matokeo yake yalionesha dhahiri nani mshindi na nani aliyeshindwa.

Tuanze na la kwanza, yaani la watu kuelewa maana na umuhimu halisi wa uchaguzi. Watu wote ambao waliweka nia ya kuingia katika kupiga kura ya maoni, walijuwa umuhimu wa serikali ya umoja wa kitaifa kwa kufuatilia midahalo na mikutano mbalimbali ambayo ilikuwa ikielezea dhamira ya mfumo huo mpya kwao. Waliopata nafasi ya kutowa taaluma hiyo kwa umma waliweka utaifa na maslahi ya nchi mbele kuliko maslahi ya chama. Watu waliungana kwa pamoja bila kujali maslahi ya vyama wakionelea bora maslahi ya nchi kwanza. Hivyo walipofanya maamuzi, walikuwa  wamezingatia nini maana na umuhimu wa uchaguzi ule.

Hili linatusogeza kwenye la pili, ambalo ni tafauti kubwa ya kura baina ya washindi na walioshindwa. Asilimia 66 za NDIO kwa asilimia 33 za HAPANA inasema kwamba ule msingi wa kuelekea kwenye upigaji kura hiyo ya maoni ulikuwa na mchango mkubwa kwenye kupatikana kwa matokeo yenyewe. Maana yake ni kuwa ingasa si kila mtu alipendelea iwepo serikali ya aina hiyo, cha msingi ni kuwa utaifa uliyazidi maslahi binafsi ya wachache na utaifa ukashinda kwa asilimia hizo ambazo hazikuwa na utata wala mzozo. Taaluma iliyotolewa kabla ya uchaguzi wenyewe, mazingira ya kuaminiana yaliyojengwa na uwelewa wa wapiga kura juu ya nini hasa wanataka kwa taifa lao ni vitu ambavyo haviwezi kupuuziwa kwenye matokeo ya Kura ya Maoni ya tarehe 1 Agosti 2010, ambayo ilikuwa ni hatua ya kimapinduzi.

Sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa ngazi mbalimbali, kuanzia udiwani, uwakilishi, ubunge na hata wa urais, ndani ya miezi mitano kutoka sasa. Nasaha zangu kwako mwanachama wa chama chochote cha siasa na usiyekuwa na chama ni kuwa tuingieni katika uchaguzi kwa kuzingatia kuelewa maana halisi ya uchaguzi na kuweka utaifa wa nchi kwanza.

Kama tulivyofanya mwaka 2010 kwenye Kura ya Maoni, sasa pia tunapaswa kuachana na maslahi ya vyama na kuangalia upepo wa matumaini ya nchi yetu unakovumia. Ni hisia hizo  ndizo zilizokufanya ufikie maamuzi ya kuleta serikali ambayo nayo ikaleta matumaini ya kuondoa fujo za katika na za kila baada ya chaguzi Zanzibar.

Lakini si la amani pekee la kukufanya uchukuwe maamuzi gani ifikapo Oktoba mwaka huu. Fuatilia pia viashiria vinavyoonesha kupotea kwa Zanzibar na vipi itapotea na weka hofu yako ukitafakari itakuwaje iwapo sisi na vizazi vyetu tutakuwa hatuitwi Wazanzibari ambapo nipo kwetu?

Tumia muda wako kuwahoji wale wanaotabiria  kupotea kwa Zanzibar iwapo tutakipa ushindi chama fulani kwa upande wa Zanzibar ili ikuingie dhana na maana halisi na umuhimu wa uchaguzi katika kulitetea jina hilo na Uzanzibari wako kwa ujumla.

Kwa mfano, wapo wanaosema Zanzibar itapotea iwapo itaongozwa na CUF. Wahoji na wakupe hoja za msingi ni kwa nini ipotee na kwa misingi ipi. Usikubali kuvyeshwa hoja zilizopowa. Fanya tathimini  juu ya hao unaombiwa kwamba wana lengo la kuirudisha Zanzibar katika ukoloni wa Kiarabu. Tafuta mafungamano yaliyopo. Ukifanya hivyo, nina hakika unaweza kufanya maamuzi sahihi juu ya khatma na maslahi ya nchi yako uipendayo ya Zanzibar.

Kuna upande mwengine ambao unasema kwamba wamewahi kuwasikia viongozi kutokea Serikali ya Muungano (CCM) kwamba hawawezi kuiachia Zanzibar wala kuipatia mamlaka yake ya kutambuliwa kama nchi kwa sababu wao wananufaika zaidi na Zanzibar pamoja na udogo wake.

Kwa mfano, wanasema walimshuhudia Waziri Samuel Sitta akizungumza na Sauti ya Amerika (VoA) akipandikiza chuki zisizokuwa na msingi, kwamba kukiwa na uraia pacha, Waarabu wa Oman wataipinduwa tena Serikali ya Zanzibar na watatawala kimabavu.

Wapo wanaosema walimsikia na kumshuhudia Waziri Wiliam Lukuvi wa CCM kutokea Bara akiwaambia wafuasi kanisani kwamba ili Tanzania Bara iendelee kuitawala Zanzibar, basi waunge mkono serikali mbili (nayo inamaanisha kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa na kuiunga mkono CCM). Waziri huyo alitamka pia kwamba Zanzibar ni nchi ya Kiislamu na maadui zao Wakristo wa Bara watapata njia rahisi ya kuivamia Tanganyika na kuishambulia kwa vile Tanganyika kuna Wakisto wengi.

Bado nasisitiza usiwakubalie hadi wakupatie ushahidi wa picha ya “vidio” uhakikishe ndiye muheshimiwa anaezungumzwa kutamka maneno hayo yanayoashiria kuigeuza Zanzibar ni koloni la Bara?Je, ni kweli anasema maneno hayo yanayopandikiza chuki baina ya Waislamu na Wakiristo wa Bara? Ukifanya hivyo, utajuwa nini umuhimu wa uchaguzi na maana yake.

Wapo pia wanaosema kwamba hata dhamira ya mmoja wa waasisi wa Muungano, Marehemu Julius Nyerere, ilikuwa ni kwamba ifike siku ionekane Zanzibar imepotea kabisa wakimaanisha kwamba kuwe na Serikali Moja tu na kusiwe tena na Serikali ya Zanzibar. Wanasema Nyerere alitaka waitafute Serikali hiyo moja na kuimaliza Zanzibar kwa taratibu sana, kwani wakifanya papara na  haraka zaidi  Wazanzibari watagutuka na watadai kuvunja Muungano, na hapo lengo la kuimaliza Zanzibar itakuwa halikutimia. Na kwa kuwa mwasisi mwenzake wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Karume, alishawaambia Wazanzibari kuwa Muungano ni koti wakiona linawabana basi walivue, ndio maana Nyerere akawapa dhana ya kufanya taratibu wa kuimaliza Zanzibar.

Lakini pia usikubali kirahisi hivi unavyosikia kuhusu siri hiyo ya Nyerere na wafuasi wake kuimaliza Zanzibar jumla jamala. Waombe hao wanaokuambia hivyo wakupatie vielelezo vya ushahidi wa kauli hizo ili uthibitishe mwenyewe; na hapo utajua nini maana ya uchaguzi na umuhimu wake.

Yapo mambo mengi yanayoelezwa na pande zote mbili za vyama vikuu vya siasa vya Zanzibar, yaani CCM na CUF, ambayo ndiyo kampeni ya kuingilia katika madaraka ya juu ya kuingoza nchi yetu tunayoipenda ya Zanzibar. Na kama unataka chama kimoja kati ya hivyo ndicho kichukuwe uongozi, jiulize kitailindaje Zanzibar na Uzanzibari wako.

Lakini huwezi kuamua juu ya chama gani kiiongoze Zanzibar , mpaka kwanza uwe mpigakura, maana huu sio tena wakati wa kufanya Mapinduzi ya silaha. Hivyo usiamini kuwa chama unachokitaka kitaongoza kwa kutumia silaha na vikosi vya kijeshi, bali kwa kura. Na hivyo, nakunasihi kwanza hakikisha unakuwa mpiga kura kwa kujiandikisha kuwa mpiga kura,  halafu nakunasihi achana na urithi katika kufanya maamuzi, achana na  kauli za kunyweshwa, achana na  mawazo ya kuchangiwa yasiyokuwa na nyongeza yako mwenyewe,  acha ushabiki wa kufuata upepo, fanya utafiti juu ya kila neno linalozungumzwa na kulitafakari, angalia upande mzuri wenye kuleta matumaini upande ambao utakaoibakisha nchi yako katika mikono yako na maslahi yake kwa ujumla kwa vizazi sasa, kesho na keshokutwa, kwa kuchagua upande ambao unapigania kudumisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kulinda Utaifa na amani ya nchi yetu tuipendayo ya Zanzibar.

Ukifanya hayo niliyoyashauri, naamini hutatetereka katika kufanya maamuzi kwa kuwa utakuwa umeelewa “maana na umuhimu wa uchaguzi wa  Zanzibar wa Oktoba 2015.”

Kama utaweza kumchagua mgombea ambaye ana mwelekeo wa kuibakisha Zanzibar katika mamlaka yake, utakuwa umechaguwa uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imetunza amani ya nchi yetu, na hivyo utaingia katika historia ya kuwa mwanamapinduzi, kwani lengo la mapinduzi lilikuwa ni kuwa na  “Serikali ya Zanzibar yenye mamlaka yake kamili” na si kuwa na aina mpya kutawaliwa.

Imehaririwa na Mohammed Ghassani

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.