Naifikiri 2015 ya baada ya uchaguzi na ushindi mnono wa wanamageuzi wa kila asili na matumaini mapya ya wananchi katika ujenzi wa Zanzibar mpya. Nazungumzia ushindi wa Wazanzibari ambao si wa CUF wala CCM bali wa wananchi wote katika nguvu ya uongozi wa wanamageuzi. Safu ya uongozi uliojaa hamu, ari na kiu ya kushindana katika kuibadili nchi kuelekea katika maendeleo bora barani Afrika. Ushindi utakaoleta heshima kwa wananchi wote, Pemba na Unguja na ushindi utaosimama kuhakikisha Muungano wa kweli wenye heshima, usawa na haki kwa kila upande.

Na Foum Kimara
Na Foum Kimara

Nafikiri namna ardhi ya Zanzibar itakavyong’ara kwa neema za Mwenyezi mungu kutokana na maelewano baina yetu na misingi mizuri ya insafu, haki na uadilifu. Nafikiri namna ya wananchi watavyofaidika katika miezi mitatu ya mwanzo na chakula cha bei nafuu, huduma za afya, mabadiliko ya elimu na kubwa msingi wa uchumi wenye manufaa na Zanzibar.

Nafikiri namna ya majadiliano ya kuujenga Muungano wa haki na faida yake kwa miaka 100 mbele kwa umoja wetu ambao hakuna milele atakayelalamika kwani utakuwa na usawa, haki na heshima kwa kila mshirika.

Natazama mwaka wa kwanza tokea “Team Mabadiliko” kuingia katika safu ya utawala. Naitizama CCM ya wakati huo yenye vijana wasomi waliojaa hamasa ya kuikosoa serikali inapoteleza na kuwa ni sehemu ya serikali inayoongoza nchi kwa uadilifu, usawa na haki.

Natazama sherehe za kwanza za “Team Mabadiliko”madarakani na zile hotuba za kueleza mafanikio katika kupunguza kasi ya umaskini nchini, kuhuisha uchumi nchini na kusimama na wanyonge katika kufanikisha elimu bora, afya bora, chakula bora, makaazi bora na ajira kwa vijana wa Kizanzibari.

Nafikiri namna itavyokuwa kwa mahakama zetu zisizojali nasaba wala ukuu wa mtu bali sharia kwa kila mwananchi kwa usawa.

Navitizama vikosi vya ulinzi na usalama wa nchi jinsi vitavyojiendesha bila ya msukumo wa kisiasa vikiwa na mishahara mizuri, vitendea kazi na muamko wa kutokomeza rushwa katika taifa letu. Namtazama kamishna wa kwanza wa Zanzibar mpya na uhuru wake katika kuhakikisha jeshi la polisi linajiendesha kisayansi na kwa manufaa ya wananchi wetu.

Naangalia barabara visiwani zikiwa na ubora wa hali ya juu, umeme wa uhakika, bandari, viwanja vya ndege, kilimo, mifugo na uvuvi uliotoa ajira kwa vijana wengi visiwani na kuweza kutupatia chakula cha ndani bila ya kutegemea nchi jirani.

Natizama viwanda vipya na soko jipya la “Brand Zanzibar” kwa ghiba ya Uajemi na kwa Ulaya kama ilivyo kwa Afrika nzima na kwa visiwa vyengine vyenye mfanano nasi.

Natazama namna tulivyoweza kusambaza maji katika mtaa, kijiji na shehia visiwani kwetu.

Naufikiria utalii wa kisasa wenye manufaa ka nchi na wananchi. Namuona rais wetu akiheshimika kwa ubora wa uongozi wake, akipokea malalamiko kwa kila pale penye matatizo mikono miwili, akisaidiwa na makamo wake wawili wenye kuheshimiana na waliobobea katika siasa safi, zenye nguvu ya mabadiliko na mustakbali mpana wa maslahi ya Wazanzibari.

Nalitazama baraza dogo la mawaziri linalobeba jukumu la uongozi badala ya utukufu wa kuongoza. Lililo na utayari katika utumishi wa umma, likiwa na usafi na unyenyekevu kwa walipa kodi wake. Kwa mara ya kwanza kiongozi wa Zanzibar anashinda tunzo ya Mo Ibrahim kwa kigezo cha uongozi uliotukuka barani Afrika.

Nautazama ushrikiano wa kweli wa umajumui usio na hatamu za kutawaliana bali ukiongozana katika maendeleo yenye maslahi na washirika. Naitazama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mpya yenye uwakilishi mzuri wa Zanzibar na iliyo na utayari katika mafungamano mapana kwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wake badala ya ung’ang’anizi wa mkubwa kwa mdogo.

Nawaona vijana wetu mashuleni wakiwa na uamuzi katika mfumo wa elimu wautakao. Nayatazama matokeo ya Kidato cha Nne kwa furaha kwa jinsi vijana wetu walivyofanikiwa kufuzu mitihani yao. Navitazama vyuo vikuu vyetu vikipanda daraja katika Afrika na kushika nambari za juu kwa elimu bora na mfumo bora wa utoaji wa elimu. Natathmini namna ya tulivyojipanga kuhakikisha ajira kwa wahitimu wetu.

Miaka mitano imemaliza na uchaguzi umewadia. Zanzibar mpya katika kilele cha ustaarabu wake na siasa za kiungwana imejawa na hamasa ya mabadiliko makubwa zaidi ya maendeleo kutokana na wimbi la demokrasia na siasa safi. Vyama kwa mara ya kwanza vinalumbana kwa sera na hakuna tena wafiadola watakobeba kura bila ya maslahi ya wananchi. Kwa mara ya kwanza sera ndizo zinazotoa mshindi badala ya vitisho, matusi na ubaguzi.

Naiona Zanzibar njema isio na ishara zozote za ubaguzi wowote, yenye raia wanaojitambua kwa watwani yao badala ya magenge ya udini, ukabila, rangi na asili. Zanzibar iliyo mstari wa mbele katika wema, ihsani, uadilifu na heshima kwa kila mmoja.

Naiona Zanzibar ya Wazanzibari waliobeba heshima ya maridhiano na kuuweka Uzanzibari wao kama nyenzo nzito ya umoja wa maendeleo yao.

Inshallah tutafika. Pamoja Daima. Zanzibar Moja.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.