Uchafu ni kitu ksichopendeza katika jamii yeyote ile iliyostaarabika, na uchafu ukigundulika kuchafua sehemu ni lazima ushughulikiwe kwa kuondoa.

Mzee Nassor Hassan Moyo
Mzee Nassor Hassan Moyo

Kwa vyama vya siasa usaliti au kwenda kivyume na maadili ya chama ni uchafu hivyo yule mwanachama anayegundulika kwenda kinyume na maadili ya chama au kufanya kitendo chochote kinachoaminika kuwa kinakhalifu misingi ya chama hicho, mara nyingi huitiwa mkutano wa dharura, aidha yeye kwa kuwapo muhusika ama kutokuweko kwenye mkutano huo hujadiliwa na ikiridhiwa kwamba amefanya makosa hayo basi huondoshwa katika chama hicho ili kuondoa uchafu katika chama.

Na Ali Mohamed Ali
Na Ali Mohamed Ali

Muasisi wa chama kilichofanya mapinduzi ya Zanzibar (ASP), muasisi wa chama kinachotawala (CCM), muasisi wa Muungano wa Tanzania, muasisi wa serikali ya mwanzo ya Mapinduzi ya Zanzibar na muasisi wa Kamati ya Maridhiano iliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar, Mzee Hassan Nassor Moyo, amefukuzwa kutoka CCM – chama ambacho anashikilia kadi Nambari 7 ikimaanisha yeye ni mtu wa saba kukabidhiwa chama ambacho leo kinakisiwa kuwa na wanachama wapatao milioni 5 kote Tanzania.

Si jambo geni kwa mwanachama kufukuzwa uanachama hapa Zanzibar au Tanzania kwa ujumla. Hata vyama vya upinzani vimeshawafukuza uanachama mara kadhaa wanachama wao, kwa mfano, Chama cha Wananchi (CUF) kimewahi kumfukuza mwenyekiti wake wa kwanza, James Mapalala,  mwanzoni kabisa mwa chama hicho kuanzishwa, kisha kikaja kumfukuza aliyekuwa mbunge wake wa kuteuliwa, Mama Naila Jidawi, kabla ya hivi karibuni kuwafukuza akina Hamad Rashid na kundi lake. CHADEMA pia ilimfukuza David Kafullila na hivi karibuni Zitto Kabwe, Kitilla Mkumbo na Samson Mwangamba ambao sasa wanaunda chama cha ACT-Wazalendo.

Lakini kimsingi wote waliofukuzwa uwanachama kutoka upinzani waliendelea kubakia salama, wengine wakiendelea kushikilia nafasi zao walizopata kupitia vyama hivyo kama vile ubunge kwa Naila Jidawi na Hamad Rashid kwa amri ya mahakama.  Lakini kwa upande mwengine, mara kadhaa waliofukuzwa kutoka CCM sio tu kuwa walipoteza hapo hapo madaraka yao yote ya kichama na kiserikali baada ya fukuzo lao, lakini pia hawabaki salama.

Historia inamkumbuka aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, ambaye alifukuzwa kwenye nafasi zote za uongozi kwenye chama na kuvuliwa pia urais, lakini hakubaki salama, aliwekwa chini ya ulinzi mkali nyumbani kwake na baadaye kuhamishiwa kizuizini Tanganyika kwa miezi sita. Ulifika pia wakati wa Maalim Seif Sharif Hamad, Marehemu  Soud Yussuf Mgeni, Hamad Rashid Mohamed, Juma Duni na wengineo, wote hao walifukuzwa chama; waliokuwa na nyadhifa walinyang’anywa zikiwemo za kichama na kiserikali, lakini bado haikutosha na hawakuwa salama waliishia kubambikwa kesi za ziada na hatimaye ‘kuwekwa lupango’ kwa miaka kadhaa.

Mfano mwengine hai tulinao ni Mansour Yussuf Himidi, ambaye naye alifukuzwa uanachama kwa kile kinachoaminika kukisaliti chama chake ambacho alikiasisi baba yake na yeye kuzaliwa na kukulia katika chama hicho. Haitoshi pia aliishi katika siasa za juu akiwa kiongozi kupitia chama hicho na pia kushika nyadhifa za juu za serikali kupitia chama hicho, lakini alifukuzwa na kuvuliwa nyadhifa zote za chama na serikali. Pia hakubaki salama. Ilimbidi aishie ‘lupango’ japo kwa wiki chache kwa kile kinachoaminishwa alimiliki silaha kinyume na sheria ya Zanzibar.

Sasa naye Mzee Moyo ameshafukuzwa CCM. Ingawa yeye ni tofauti na hao niliowatolea mifano, kwa kuwa hayuko katika madaraka ya serikali wala kichama kwa muda mrefu sasa, hivyo sidhani kama anaweza kurushiwa paka wa kuiba nyaraka za serikali, lakini kama ilivyo kwa Rais Mstaafu Abeid Amani Karume alivyosema Dodoma mwaka juzi, “Mimi mwaka 1970 nilijiunga na chama cha Afro Shirazi Party na kadi yangu hii hapa” na akaitoa kuionyesha hadharani.

Ninamaanisha kwamba iwapo Rais Karume anayo kadi ya ASP hadi sasa, naamini Mzee Moyo na yeye bado anayo kadi hiyo, na pia bado naamini Mzee Moyo bado anayo kadi yake ya CCM yenye Namba 7 ya uanachama. Na kwa kuwa mkutano wa kumfukuza uanachama ulipoitishwa, yeye hakuitwa ili kurejesha kadi hiyo, hivyo nina imani yaweza kuwa kosa kwa yeye kubakia na kadi hiyo.

Sina lengo la kumuombea mzee wa mwenzangu yamkute kama yaliyowakuta waliomtangulia kufukuzwa, bali ni kuelezea hofu yangu kutokana na mifano niliyoitanguliza. Bado swali langu ni lile lile: “Je, kufukuzwa uanachama kwa Mzee Moyo kwatosha kumbakisha salama?”

Imehaririwa na Mohammed Ghassani

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.