Ikiwa tutafuata usuli wa umamani kwake, basi Samuel “Ifuma” Sitta – aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba – si mgeni wa mila na vitiba vifuatwavyo na Waislamu wa nchi yake. Hilo jina la “Ifuma” ndilo alilopewa umamani kwake, Unyanyembe, ambako yeye ni mjukuu wa Chifu Fundikira, akiwa mtoto wa Hajjat Kagoli Said Fundikira, dada wa toka-nitoke wa Chifu Abdullah Said Fundikira. Ukoo mzima wa Unyanyembe ni Waislamu wa enzi na enzeli wala si wa kusilimu juzi na jana, ingawa hata kama wangekuwa hivyo, panapohusika Uislamu haijalishi nani kaja mwanzo na nani kaja mwisho.

Sitta amelala kwenye tumbo la Waislamu na miongoni mwa mila maarufu katika jamii za Waislamu wa eneo hilo ni dua iitwayo ‘halbadiri’ ambayo inaaminika kuwa aina fulani ya mashitaka ya mnyonge kwa Mungu dhidi ya dhalimu. Kwa mujibu wa mapokeo, baina ya dua ya mnyonge na Mungu pana pazia jepesi sana kiasi cha kwamba watu wanaonywa wachelee sana apizo la mtu aliyedhulumiwa, maana linaweza kujibiwa pale pale linapotolewa.

Kwenye halbadiri, mnyonge humuomba Mungu amrudi dhalimu huyo hapa hapa duniani kwa adhabu anayoinuilia yeye muombaji. Kwa mfano, ikiwa mtu ameibiwa mali yake, huweza kunuia kuwa mwizi airejeshe mali hiyo kama ilivyo na mahala alipoichukuwa. Mwenye mali anaweza kulala na kuamka akakuta fedha zake zilizochotwa kwenye bweta zimerudishwa kama zilivyo.

Lakini wengine huwa hawaombi kurejeshewa mali, bali huwaombea wizi wao maumivu, majanga au idhara ya waziwazi. Kwa mfano, hutaka mwizi wake apatwe na ukurutu mwili mzima, afanye tenzi kwenye makalio, au – kwa anwani ya makala hii – hutaka mwizi wa kuku atangetange na kuku huyo wiki nzima mitaani huku akikiri kuwa ni yeye ndiye aliyeiba. Hilo likitokea, husemwa kuwa “halbadiri ya mbayana” imemkumba mwizi huyo.

Na, naam, halbadiri ya mbayana imekuwa ikiwakumba viongozi mbalimbali wa CCM na serikali zake tangu Bunge Maalum la Katiba likiendelea, hadi likamalizika na sasa tunapozungumzia tena kadhia ya Sitta. Wanaofuatilia makala zangu, wanafahamu kuwa hii ni mara ya pili kuandika kuhusu mwanasiasa huyu tangu kutolewa kile kiitwacho “Katiba Iliyopendekezwa“, ambayo hadi sasa hatujajua rasmi ikiwa itapigiwa kura ya maoni au la.

Mara ya kwanza ni pale alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika mwezi Februari 2015, ambapo alielezea kuwa bunge hilo lilishindwa kupitisha kipengele kinachoruhusu Watanzania kuwa pia na uraia wa nchi nyengine kwa sababu serikali ilihofia Waomani wenye asili ya Zanzibar wanaweza kutumia nafasi hiyo kurudi na kuipindua serikali ya Zanzibar.

Mbali ya kuwa hoja yake hiyo ilikuwa na upotoshaji na pengine wa makusudi, maana Oman hairuhusu raia wake kuwa na uraia wa nchi nyengine, nilisema pia kuwa alichokifanya Sitta kilikuwa ni kupandikiza fitina dhidi ya Wazanzibari. Leo hii naongeza kuwa hata huko kusema kwenyewe alikosema, nako kulikuwa ni matokeo ya halbadiri ya mbayana.

Akiwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Sitta anajuwa fika kwamba alishindwa kuzipata thuluthi mbili za wajumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar. Lakini kwa kuwa fedha nyingi ilishaliwa na CCM yake iliona haya kuondoka Dodoma bila ya rasimu ya katiba, ndipo kwa kushirikiana na wapanga mikakati ndani na nje ya bunge hilo akalazimisha kutangaza kupitishwa kwa rasimu hiyo kimagube.

Wazanzibari hawakuridhika na dhuluma hiyo. Walikasirika na waliapiza, pengine hata kama si kwa kukaa kitako na kumsomea Sitta na wenzake halbadiri, lakini angalau kwa kuwalaani. Husemwa kuwa “salala” 40 za wadhulumiwa ni sawasawa na halbadiri nzima. Na hii imemkumba Sitta.

Inaonekana kwenye salala hizi, ilinuiliwa kuwa Sitta na wenzake wote walioshiriki kwa njia moja ama nyengine kuidhulumu Zanzibar kwenye Bunge lile la Katiba, wabainishwe hapa hapa duniani na kila mtu akiona – waaibike, wafedheheke. Sasa Mungu ameitikia kilio hiki cha wadhulumiwa na madhalimu wanafedheheka pakubwa. Wanatembea na yule kuku wa kuiba kwenye mifuko ya makoti yao, popote wendapo, ndani na nje ya nchi.

Ndio maana mwezi huu wa Aprili 2015, akizungumza na Watanzania wanaoishi Uingereza, Sitta akalazimika kumtoa kuku huyo kotini mwake na kumuonesha hadharani, pale alipotomeshwa na suala la hatima ya Muungano na nafasi ya Zanzibar. Angalia vidio hiyo hapo chini kwa utulivu ujionee mwenyewe mtu mzima wa miaka 72 kutoka Unyanyembe anavyoaobika.

Sitta anasikikana kwenye vidio hii akijikanganya mwenyewe tangu mwanzo hadi mwisho wa kujibu suali hili. Mwanzoni anasema Muungano hautaamuliwa kwa kura ya maoni, lakini kisha anasema ikipigwa kura ya maoni kuamua hatima ya Muungano, basi “Zanzibar kutokana na kuchochewa kuwa utaifa ni kitu kizuri, kikubwa, tutakuwa na bendera yetu, tutakuwa na kiti Umoja wa Mataifa, wanaweza kupiga kura ya kuukataa Muungano.”

Katikati yake anaonesha Tanganyika inamaanisha nini hasa kwenye Muungano huu – ndio Tanzania yenyewe. “Juzi juzi (Zanzibar) walichelewa kulipia umeme, deni kama la bilioni 50. Tanzania haikutetereka. Tulisikilizana tu, mambo yaende polepole.” Ndivyo anavyosema kwa kujiamini, na bila kujua kuwa anaunga mkono kile kile ambacho wanaotaka mageuzi ya kimsingi kwenye Muungano wanachokihoji, yaani hali ya Tanganyika kujifanya kuwa ndiyo Tanzania pekee, na Zanzibar ni mgeni mwalikwa tu kwenye Muungano ulioizaa hiyo Tanzania yenyewe.

Lakini ya mbayana zaidi ni sababu zake tatu anazozitaja kuwa kwa nini hakuwezi kuwa na mabadiliko ya kimsingi (ambayo kimakosa watu wote wa aina yake huwaaminisha wengine mageuzi hayo yanamaanisha kuuvunja Muungano).

Ya kwanza? Anasema kama hilo likitokea, patazuka vita vya kidini “kwa sababu Zanzibar watajitahidi wapate taifa ambalo litakuwa rafiki kwao lakini liwe na uhasama na Bara na liweke vifaa vyake pale Zanzibar“ kama vile kituo kikubwa cha televisheni ambacho kitawachochea “Waislamu wa Bara wajisikie wanaonewa. Tangu alfajiri munapigwa tu maneno: ‘Waislamu wa Bara amkeni! Jiondoeni kwenye makucha na minyororo ya Wakristu,‘“.

Ya pili? Kama ya kwanza, hofu dhidi ya Uislamu na Waislamu wa Zanzibar. “Huu mnaosikia al-Shabaab, al-nini, inaweza kuzuka pale napo kwa sababu Zanzibar ni asilimia 99 Waislamu.“

Na hii ya pili inapingana na ya tatu: “(Wazanzibari) ni ndugu zetu wa damu. Watu walioko Zanzibar wametoka Bara. Ndio maana mtu si jambo la ajabu ukienda kule unayakuta makabila yale yale – Wayao, Wamwera…yaani wako hivyo hivyo.“ Kama si halbadiri ya mbayana, unakuta nukta hizi tatu zinavyogongana zenyewe kwa zenyewe. Kwanza, Zanzibar ni Waislamu lakini kisha Wazanzibari hawa ni Wayao na Wamwera kutoka Bara lakini ambao sasa wakipatiwa kura ya turufu wataamua kuuvunja Muungano kwa fikira za utamu wa uhuru, bendera, na kiti Umoja wa Mataifa. Kisha yakitokea hayo, watakuwa na athari ya moja kwa moja kwa usalama wa Bara, sehemu walikotokea kwa asili zao.

Swali kuu baada ya yote? Hivi mbele ya wajiitao Watanzania, Wazanzibari ni nani? Je, ni maadui watarajiwa ambao lazima wapigwe vita tangu sasa, na au ni ndugu wa damu ambao lazima wasaidiwe na wapewe ushirikiano?

Kwa waliokumbwa na halbadiri ya mbayana, kama alivyo Samuel Ifuma Sitta, majibu yake kwayo ni ya kubabaisha na kuaibisha, maana wamenuiliwa waaibike – watembee na kuku wa kuiba.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.