Ilikwishajulikana tangu mapema kuwa theluthi mbili 2/3 ya Kura za Zanzibar isingepatikana!

Lakini zilifinyangwafinyangwa mpaka tukatangaziwa kuwa zimepatikana! Hili lilikuwa ndani ya uwezo na ghilba za kibinadamu!

Lililotarajiwa baada ya hapo ni Kura ya Maoni kuhusu hiyo Katiba waliyoipendekeza kwa kulazimisha theluthi mbili!

Kwa mujibu wa Sheria ya kutunga Katiba Mpya, Mchakato mzima ulikuwa umepangwa kwenye mhimili wa Kalenda zaidi, ambayo hiyo si mali ya Binadamu!

Kama ilivyokuwa mwenye 2/3, ushauri ulitolewa na watu mbalimbali kuwa haingepatikana na kwamba bora Bunge hilo la Katiba lingesitishwa kwanza ili walau kunusuru pesa kwenye mfuko wa hazina ili kuwezesha mambo mengine kufanyika, kama vile ajira mpya za walimu, ambao kwa ukosefu wa fungu serikalini, mpaka sasa wamekaribia kugongana misinu miwili, huku waliotangulia bado wako majumbani kwa wazazi wao!

Lilipofuatia hili la Uboreshwaji wa Daftari la Mpiga Kura kwa mfumo wa BVR nchi nzima ili wapiga Kura waweze kuipigia kura ya Maoni katiba Pendekezwa ndani ya siku zisizozidi 90, humo humo zikiwemo siku za Uelimishwaji na kampeni humo humo!

Hili nalo washkadau walilipigia kelele sana, lakini upande mmoja Serikali ikishikilia msimamo wake kuwa ni lazima kura itapigwa April 30!

Walisahau kuwa Kalenda ni ya Mungu, na hakuna binadamu awaye yote awezaye kulisimamisha jua hata kwa nukta 1!

Sasa hatimaye wamekiri na kukubali kuwa Kura ya maoni haiwezekaniki tena kupigwa hapo April 30, maana zoezi la uandikishaji wapigakura bado liko mbali sana! Zoezi limesimamishwa hadi wananchi watakavyotangaziwa baadaye!

Na kwa nionavyo mimi, kwa mujibu wa kalenda ya matukio muhimu ya Taifa letu, Kura ya Maoni kuhusu Katiba hiyo, haina nafasi tena kwa mwaka huu!

Serikali ingesikiliza ushauri wa upande wa pili, bila shaka wangenusuru ufujaji wa pesa uliofanyika katika zoezi hili, na mipango mingi ya Serikali ingesonga pasipo mikwamo inayojidhihirisha hivi sasa!

Chanzo: Imeandikwa na Geoffrey Ng’humba https://www.facebook.com/geoffrey.nghumba?pnref=story

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.