IKIWA kila Mtanzania atachukuwa kalamu na karatasi na kuyaeleza maisha yake tangu Tanganyika iwe huru mwaka 1961 na Zanzibar iwe Jamhuri mwaka 1964, tutapata hadithi ndefu sana. Nusu karne ushei si muda wa dhihaka.
Ikiwa kila mmoja wetu ataandika kitabu kuhusu maisha yake yalivyokuwa katika kipindi hicho pengine vitabu hivyo vitaweza kugusa mbingu kwa urefu wake, tukivipanga kimoja juu ya kimoja.
Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Mambo mengi yametokea katika kipindi hicho; mengi zaidi yangeweza pia kutokea lakini hayajatokea. Kuna mafanikio yaliyopatikana bila ya shaka; miongoni mwao yako ya kupigiwa mfano.Hayo lakini ni machache yakilinganishwa na yale ambayo yangaliweza kupatikana na hayakupatikana.

Hayo yasiyopatikana yangaliweza kulinyanyua taifa letu na kulifanya lihishimike kwa maendeleo yake.Hili ni taifa lenye ardhi kubwa sana na utajiri usio kifani.
Leo, zaidi ya nusu karne baada ya uhuru, bado taifa hili linakabiliwa na maadui walewale watatu: umaskini, njaa na magonjwa. Tena maadui hao wamezidi nguvu — umaskini umezidi, njaa imezidi na magonjwa yamezidi.
Tanzania imejaa umaskini juu ya kuwa ina utajiri mkubwa wa maliasili na malighafi. Idadi kubwa mno ya wakaazi wake ni watu wanaohangaika kila uchao kujipatia riziki zao za siku hadi siku. Yote hayo ni matokeo ya sera mbovu na tabia mbi za uongozi.
Yasitoshe hayo, kuna na ubinafsi uliowavaa watawala. Saa zote watawala hao wamo mbioni kujenga miundombinu ya matumbo yao badala ya kushughulikia kujenga miundombinu ya kulipatia taifa maendeleo na kuwafariji wananchi.Ndio maana nchi hayendi, haiendelei.Imekwama, imesakama.
Kwa utajiri ilionao na msasa wa kisiasa iliopigwa katika zama za Ujamaa Tanzania haikutakiwa kuwa hivi. Leo hii ingepaswa iwe mstari wa mbele miongoni mwa nchi zilizo na uadilifu mkubwa wa kisiasa na ustawi wa kiuchumi barani Afrika. Lakini sivyo ilivyo.
Kwa nini tunakubali?
Moja ya sababu zilizotufanya tusiyapate maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni naksi ya watawala walio imara na wenye nia ya dhati ya kupigania maslahi ya umma.
Sababu nyingine ni hulka yetu ya kuyaachia mambo yawe, bila ya sisi, umma, kuchukuwa hatua zinazostahiki za kupambana na watawala wetu. Na ni wao, hao watawala wetu, wanaoipalilia hulka hiyo kwa lengo la kuzidumaza nguvu zetu tusiweze kupambana nao.
Hulka hiyo labda ndiyo sababu inayowafanya wenyejiwa Zanzibar, kwa mfano, washike tama na wamshukuru Mungu wanapokatiwa umeme kwa muda wa miezi mitatu mtawalia bila ya kulalamika. Labda hiyo ndiyo sababu pia inayowafanya wateja wa huduma nyingine zinazotolewa na serikali wasiweze kulalamika wanaponyimwa huduma hizo au wanapotolewa njiani kwa kupewa huduma duni.
Wateja hao na raia, kwa jumla, hawana pa kwenda kuishtaki serikali inapowakosea. Taasisi ambazo kwa kawaida ndo ziwe zinawasaidia wananchi (kwa mfano, polisi au mahakama) huku kwetu zimetiwa mikononi mwa serikali na haziwezi kuiendea kinyume, hata ikiwa serikali ndiyo mkosa na haina haki.
Vyama vya wafanyakazi vinavyopaswa kuwapigania wafanyakazi vimepwaya na havifanyi kazi zao. Ni wazi kwamba panahitajika mageuzi makubwa nchini Tanzania ili nchi inyanyuke na iweze kujikokota kuelekea kwenye maendeleo. Yanayohitajika si mageuzi ya uongozi tu bali pia mageuzi ya utamaduni wetu wa kisiasa.
Duniani misimu hugeuka. Historia hubadilika. Na kuna nyakati ambapo nyakati zenyewe huisuta historia pale historia inapojisuta yenyewe. Yote hayo tumeyaona kwa wenzetu barani Afrika wasiokubali kuonewa. Tumewaona jinsi walivyoinuka na kusimama kidete kupigania haki zao na hatimaye kuleta mageuzi nchini Burkina Faso, Tunisia na Misri. Sisemi kwamba wenzetu hao wamekwishafanikiwa moja kwa moja.
Kazi ya kuleta mageuzi si kazi ndogo, ni kazi pevu. Hukabiliwa na mizengwe kama ilivyokabiliwa Misri lakini walichokithibitisha Wamisri ni kwamba umma ukisimama imara kudai haki zao unaweza kuleta mageuzi. Hayo bado hatujayashuhudia kwetu.Tungali tukionewa na kubughudhiwa na watawala. Tulivokaa ni kama tu radhi kunyanyaswa.

Kwa nini tunakubali?

Kwa wenzetu kuna vimbunga vya mageuzi. Watawala wao hutikiswa wakatikisika. Wetu tunawadekeza kwa kuwapandisha pembeani. Wakishakaa juu ya pembea wakauonja uroda huwa hawataki kuteremka.

Ndio maana tunapokwenda kuwashika miguu na kuwataka watusikilize, hutupiga mateke. Mfano ni ile Rasimu ya Katiba ya wananchi iliyopendekezwa na Tume ya Katiba na iliyotupiliwa mbali na watawala. Tunasema wee mpaka tunachoka, watawala wetu hawatujali. Inakuwa kama wanaona raha kuyahini matumaini yetu.

Kwa nini tunakubali?

Hapawezi kupatikana maendeleo bila ya kufanyika mageuzi. Nionavyo ni kwamba umma unayataka mageuzi. Lakini watawala wetu hawayataki.Wanayaogopa na wao wanatufanya tuwaogope wao.
Kwa nini tunakubali?

Tukiwaangalia watawala wetu, tunawaona kuwa ni watu wenye kupenda kusengenyanya. Mifano imejaa tele hasa siku hizi uchaguzi mkuu unapokaribia.Wamekwishaanza kuparurana wenyewe kwa wenyewe. Wanaonekana kuwa ni watu ambao wakipata nafasi wanaweza hata wakachinjana kwa uchu wao wa madaraka.

Si kwamba wanayataka madaraka ili waliendeleze taifa na wazinyanyue hali za maisha za wananchi wenzao. Kila nikiwatazama naona kuwa hawana dhamira hizo. Wanayataka madaraka ili wajiendeleze wenyewe.

Hawa ni watu ambao wapatapo nyadhifa serikalini na pakizuka matatizo badala ya kukaa na kuyajadili na kuyapatia ufumbuzi, huhiari kulala nayo na kuendelea kuwa nayo kwa muda mrefu, pengine kwa miaka. Hayo ndiyo tunayoyashuhudia, kwa mfano, kuhusu ufisadi uliokithiri na wenye kushamiri nchini.

Jinamizi hilo la ufisadi lilipoanza kuchomoza watawala wetu wangelishika panga na kulikata kichwa. Hawakufanya hivyo.Labda wasingaliweza kufanya hivyo kwa sababu wangefanya hivyo wangebidi wavikate vichwa vyao wenyewe kwanza au vya wake zao au vya wengine walio karibu nao walioukumbatia ufisadi.

Afrika ina mifano mizuri ya wapi ufisadi unakopigwa vita kwa dhati lakini sio kwetu. Nitaitaja miwili tu ya hivi karibuni: Machi 23, mahakama maalum ya Senegal yenye kupinga ufisadi ilimhukumu Karim Wade, mtoto wa Rais wa zamani Abdoulaye Wade, kifungo cha miaka sita na ikamtoza faini ya dola za Marekani milioni 228. Alishtakiwa kwa kosa la kujilimbikizia dola za Marekani milioni 240 kwa njia za kifisadi. Wizi wake haukuwa wizi wa kipuuzi na adabu aliyopewa pia haikuwa ya kipuuzi.

Mfano wa pili ni wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, nchi ambayo ukiitaja tu hukujia harufu ya ufisadi. Tuliona Jumamosi iliyopita jinsi Uhuru alivyochukuwa hatua ya haraka na kuwasimamisha kazi mawaziri wake wanne na maofisa wengine 12 wa ngazi za juu serikalini kufuatia madai ya ufisadi.

Waziri mwengine wa tano alijichukulia hatua mwenyewe kwa kuuacha uwaziri akisubiri achunguzwe kwa madai hayo. Mawaziri na maofisa hao walioathirika walitajwa katika ripoti maalum kuhusu ufisadi serikalini Kenya iliyotolewa mwanzoni mwa wiki iliyopita na Tume Dhidi ya Ufisadi ya nchi hiyo. Uhuru ameipa Tume hiyo muda wa siku 60 kuyachunguza madai hayo. Uongozi imara aina hiyo ndio unaotakiwa, sio ule wa kusitasita, wa kuwaonea haya mafisadi.

Wiki moja kabla ya hapo, Uhuru alichukuwa hatua nyingine imara alipoikatalia Uingereza ombi la kuitaka Kenya iongeze muda wa kandarasi ya kuliruhusu Jeshi la Uingereza liwe linafanya mazoezi na kupata mafunzo Nanyuki, Kenya.
Uingereza imezoea kwamba wanajeshi wake walioko Kenya huwa hawashtakiwi chini ya sheria za Kenya pale wanapofanya kosa la jinai. Safari hii Uhuru amekataa. Amesisitiza kwamba si yeye wala mwengine yeyote anayeweza kuikiuka Katiba ya Kenya. Kwa hivyo, wanajeshi wa Uingereza wataoshtakiwa kwa makosa ya jinai watabidi washitakiwe kwa mujibu wa sheria za Kenya.

Kwa ufupi, Uhuru Kenyatta anataka mkataba wowote baina ya Kenya na Uingereza uwe unafuata kanuni na sheria za Kenya. Huo ni msimamo ulio madhubuti na wa kizalendo. Ni msimamo unaostahiki kupongezwa na kupigiwa mfano kwa viongozi wetu waliokaa kama waliozubaa.

Mifano hiyo ya Senegal na Kenya ni mifano ya uongozi ulioazimia kutokuwa na mchezo kuhusu vita dhidi ya ufisadi. Ule mfano wa ziada wa Kenya unaonyesha pia uongozi wenye kujiheshimu na ulioazimia kuilinda heshima na uungwana wa taifa lisikaliwe kichwani na dola kubwa. Kwetu, mara kwa mara watawala wetu hutulaghai kwamba wanaupiga vita ufisadi. Na sisi tunakubali tukijuwa kwamba wanatugeuza mafala.
Kwa nini tunakubali?

Tunaduwaa na tunajikuta tunawapa watawala wetu shubiri;nao huwa hawatosheki huchukuwa pima. Tunawaruhusu wajitoe kimasomaso kwa makosa na dhambi wazitendazo. Jaza yetu ni kwamba huzidi kutunyanyasa, kutusaliti, kutudhalilisha, kutudanganya, kutukandamiza. Wanaipiga pute hata heshima na utu wetu. Na sisi tumo tu tunajiendea kama hatujafanyiwa ubaya, kama hatujadhulumiwa.
Kwa nini tunakubali?

Ukweli ni kwamba watawala wetu wamebobea katika kila aina ya maasi ya kisiasa na ya kijamii. Wanatuibia mali, wanatuibia kura; wanatufanyia yote hayo, na zaidi ya hayo, na sisi tunakubali. Kwa nini tunakubali?

CHANZO: RAIA MWEMA

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.