Ingawa waliletwa wapishi wengine kuchoma ndafu na kutengeneza pilao ya kuwalisha watu mithili ya Biblia, bado Hidaya wako amekimbia kupika hiki na kile kiasi kwamba bora usije maana unaweza kunikana nisivyotamanika na michirizi na mikunjo ya uchovu. Lakini matokeo yake … sifuri. Umeona akitangazwa kwenye gazeti lolote? Thubutu. Na watu wengine alioweza kuwashawishi kuandamana kwake walikuwa wachache tu na haiwezekani kuwashawishi wengine wakati ambapo wala mkakati haujulikani. Kwa hiyo …

Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.

Mpenzi Frank,
Vipi hali yako mpenzi wangu? U mzima mwenzangu maana mara nyingine kimya chako kinatia kiherehere aisee. Nakaa nakuwazia wewe tu.

Tena nilianza kupatwa na wasiwasi. Umebadilika shujaa wangu? Umejiunga na wanaoenda kupata kikombe cha babu huko Dodoma au kwingineko? Maana kweli nakumbuka jinsi nchi nzima ilivyokurupuka kwenda kwa babu yule wakati ule ili wapone kimwili. Na matokeo yake sote tunajua. Sasa naona kwamba tumepata mkombozi wa kutuponyesha kisiasa pia. Kikombe kimoja tu kwake, mambo yote poa tehe tehe tehe. Tuone kama anaponya au anapenya tu.

Lakini kama kwa babu yule, lazima na wengine wa kuiga wajitokeze. Basi si nilikuambia kwamba bosi aliona mikiki yake inatosha kumfikisha nyumba nyeupe na yeye na baada ya kuona mafanikio ya mheshimiwa mwenzie, yeye naye kaamua kuingia ulingoni.

Nakuambia mpenzi, imekuwa shughuli pevu kwelikweli.

Ingawa waliletwa wapishi wengine kuchoma ndafu na kutengeneza pilao ya kuwalisha watu mithili ya Biblia, bado Hidaya wako amekimbia kupika hiki na kile kiasi kwamba bora usije maana unaweza kunikana nisivyotamanika na michirizi na mikunjo ya uchovu. Lakini matokeo yake … sifuri. Umeona akitangazwa kwenye gazeti lolote? Thubutu. Na watu wengine alioweza kuwashawishi kuandamana kwake walikuwa wachache tu na haiwezekani kuwashawishi wengine wakati ambapo wala mkakati haujulikani. Kwa hiyo …

Mmmh! Naona sasa nataka kuandika tamati bila hata kuonyesha chanzo.
Baada ya mafuriko ya Dodoma, bosi akarudi nyumbani na meneja wake wa kampeni.
‘Mnaona? Mnaona watu wanavyofurika kwa yule? Nitawaonyesha jinsi ambavyo mimi ni maarufu zaidi?’
Mama Bosi na Binti Bosi walitazamana na kunyanyua makope. Hatimaye MB alisema:

‘Sawa mume wangu. Lakini naomba tukubaliane kitu kimoja.’
‘Sema mke wangu.’
‘Fanya upendalo baba lakini ukiona kwamba kuna ukame badala ya mafuriko, uache kabla ya kujiabisha.’
Kama MB alifikiri kwamba kubali yaishe yatamsaidia alikosea sana. Wacha bosi afokefoke hovyo.
‘Upumbavu mtupu. Nimesema sina mke miye, sina mtoto miye. Familia zingine zinawapa nguvu mtu wao akigombea. Lakini nyie kazi yenu ni kukatisha tamaa tu.’

MB akanyamaza lakini BB kama kawaida yake akathubutu kuweka kichwa chake kitanzini.
‘Siyo hivyo baba. Si tumesema ufanye upendalo. Ila utumie hii kama kipima joto. Kama joto linaonekana kwelikweli, ni safi. Lakini joto likigeuka barafu …’
‘Funga mdomo na kejeli zako. Nitawaonyesha.’

Na bosi akatoka na meneja wake kwenda kupanga mambo yao. Kisha usiku kucha nikamsikia akipiga simu maana bosi kwenye simu Bwana … hana dogo. Utadhani anaongea na mtu wa nyumba kwa tatu bila simu’
‘Ndiyo Bwana. Huwezi kuwaleta walimu mia moja hivi? Sawa kabisa. Na waambie kwamba anayetoa atapokea mara dufu ha ha ha. Ndiyo. Wasije mikono mitupu lakini wakijaza viganja wataona. Kabisa. Jaza viganja nijaze mifuko ha ha ha.’
Haya na baada ya dakika tano.

‘Kwani viongozi wa dini si binadamu Bwana? Nani hataki kula? Badala ya chakula cha Bwana watakula chakula cha Bwana Mkubwa ha ha ha! Eti nini? Si wachote sadaka kidogo kisha watarudisha. We vipi Bwana. Kama hutaki basi nimtafute mwingine ambaye atatumia vizuri posho zangu.’
Na tena.

‘Watoto wa shule hapana mama. Hujui wanatusanifu eti mikutano yetu inajaa watoto wa shule tu. Lazima tuonyeshe kwamba wazee wazima na heshima zao wananiomba … Eti nini? Hawataki? Eti mkono mtupu haulambwi. Nani kawaambia watatoka mikono mitupu? Wanataka kiasi gani? Ha ha ha … ama kweli wazee wa siku hizi duh! We toa ahadi tu ili mradi waje.’

Hivyohivyo usiku kucha mpenzi. Na mambo yalipangwa kwa ajili ya wikiendi iliyopita. Bosi akatuma mabasi ya kuwaleta watu kutoka sehemu mbalimbali. Akaweka hema kwenye bustani yake ya nyumba ya waziri. Akawaita wapishi na wahudumu na mambo yote aliyoyasahau aliachiwa Hidaya wako.

Basi ikaja siku ya siku. Asubuhi na mapema, nilishangaa kusikia nazi zinavunjwa kila kona ya nyumba pamoja na getini. Ilibidi nicheke. Bosi anataka watu wamwamini yeye wakati yeye hawaamini, eti wataleta ndumba kwake. BB alishindwa kujizuia. Wakati wa chai alimwuliza baba:

‘Hivi baba wageni wanakula wali wa nazi?’
Bosi alishtuka maana hakuona anakoelekea.
‘Kwa nini? Wali ni wali tu. Mpaka nazi!’
‘Niliposikia nazi zote zinavunjwa leo asubuhi nilijua tutajinoma leo.’
Bosi akakunja uso lakini alijilazimisha kucheka.
‘Usinichezee leo na kuharibu mudi yangu. Leo ni leo. Watu watatambua kwamba kuna mchezaji mpya. Messi akae pembeni, Ronaldo akae pembeni nakuambia.’

Bosi alijaribu kupiga chenga kama Messi akaishia kuangukia kochi puuu! Sote ilibidi tujizuie tusicheke. Mgombea kwelikweli.

Basi baada ya hapa nikasaidia kutoa vyakula vyote viwe tayari kwa mafuriko kwa wageni. Muda ukapita, saa nne, saa tano, saa sita, hakuna dalili, isipokuwa kundi kubwa la waandishi wa habari ambao walikuja kushuhudia. Walivyojinoma nadhani walitaka kushuhudia msosi tu wakati wanasubiri maelfu ya watu. Nikamwona bosi anazidi kushikwa na wasiwasi. Kila dakika anapiga simu.

‘Wako wapi? Wako wapi? Unasema wanakuja. Saa ngapi jamani?’
Mwisho saa tisa hivi wakaanza kuingia mojamoja. Mabasi mengine yalifika yamebeba watu watatu tu.
‘Tumesubiri bosi, tumesubiri, tumebembeleza lakini kila mtu alisema hana muda huo.’

Lakini wakati bosi alianza kukata tamaa ghafla wakaingia kundi kubwa la watu kwa fujo. Bosi alifurahi.
‘Si niliwaambi …’

Kabla hajamaliza alitambua kwamba si wale aliowaalika bali ombaomba wote, na watoto waishio mitaani, na wengine wenye matatizo wote wakavamia. Sijui waliambizana saa ngapi na walijikusanya saa ngapi maana kabla bosi hajaweza kufanya lolote walikuwa wameshafika kwenye masufuria na kuanza kula. Bosi alipoona kwamba waandishi wanataka kuwapiga picha, alitoa amri picha zisipigwe. Sijui aliwahonga pia maana hakuna picha iliyotoka.

Baada ya hapo bosi alitaka kuwaita wale akina Fanya Fujo wanaojua demokrasia ni rungu tu. Lakini bahati nzuri MB alimshawishi bosi afanye hivyo.

‘Utaeleweka vibaya mume wangu. Waache wale.’
‘Lakini si hao niliowakaribisha.’
‘Si hoja. Maadam wameshakuja, utafanya nini?’
Kwa hiyo bosi aliwaacha na baada ya kushiba sana wakaanza kuimba sifa za bosi eti anafaa sana kuwa kiongozi ajaye na yeye. Lakini bado bosi hakutaka picha zipigwe.
Sasa mpenzi unaonaje? Ataendelea kugombea? Na nafurahi mimi si katika wale wa kufanya mpango wa mamajusi kwa bosi duh!

Akupendaye mwenzangu. Niko tayari kuandamana kuja kwako wakati wowote uwe kiongozi wa maisha yangu.
Hidaya

Chanzo: Raia Mwema, Toleo Na. 399 la 3 Aprili 2015

2 thoughts on “Kikombe kimoja tu kwake, mambo yote poa tehe tehe tehe”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.