Jioni ya tarehe 29 Machi 2015, msafara wa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliokuwa wakitoka Makunduchi, kusini Unguja, kuelekea Mjini Magharibi, ulishambuliwa njiani na ‘watu wasiojulikana.’ Hilo neno ‘watu wasiojuilikana’ tuliwache hivyo hivyo kwenye alama za mashaka, maana ni mtazamo wangu kwamba ni kinyume chake, yaani ni ‘watu wanaojuilikana’ na wale wanaopaswa na wenye wajibu wa ‘kujuwa’ mambo kama haya.

Kwa mujibu wa mmoja wa watu waliokuwamo kwenye msafara huo “gari ya ‘majanjawidi’ ikiwa katika mwendo wa kasi iliupita msafara wao na kisha kuwarushia watu waliokuwemo katika gari hiyo visu na nondo.” Muda mchache uliopita, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa amewaomba watu wote walioshiriki mkutano huo huko Makunduchi, waondoke kwenye msafara mmoja kurudi mjini. Inaonekana alishakuwa na wasiwasi juu ya kile ambacho kingelitokea na ushauri wake ulilenga, yumkini, kukizuwia kisitokee.

Siku tano kabla ya hapo, ofisi za CUF jimbo la Dimani, mkoa wa Mjini Magharibi, zikateketezwa kwa moto na ‘watu wasiojuilikana’ na kusababisha hasara kubwa. Mashuhuda wa tukio hilo, ambalo lilitokea mtaa wa Kisauni saa 8: 00 usiku, wanasema watu hao walifika na gari aina ya Pick-up na kuvunja mlango wa ofisi hizo na kuliripua jengo hilo kwa petroli. Kwa mujibu wa Diwani wa wadi ya Tomondo, Hassan Hussen Yussuf, jengo hilo lilikuwa na vifaa mbalimbali vya thamani na fedha taslimu za malipo ya uchukuaji wa fomu za wagombea walizolipia.

Kuchomwa kwa ofisi za CUF Dimani kulikuja siku tatu tu baada ya chama hicho kufanya mkutano kwenye eneo la jirani na hapo kwa kile kilichosema ni “kumgotoa” Mansoor Yussuf Himid, ambaye anarudi kugombea uwakilishi kwa tiketi ya CUF katika jimbo la Kiembesamaki. Mansoor alikuwa mwakilishi wa jimbo hilo hapo kabla kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kabla ya kufukuzwa kutokana na msimamo wake kuelekea Muungano wa Tanzania na nafasi ya Zanzibar kwenye Muungano huo. Kwenye mkutano huo kulizungumziwa kuwepo kwa njama za kuiingiza Zanzibar katika machafuko kabla ya kura ya maoni ya Aprili 30 mwaka huu na kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25. Wito wa wazungumzaji wa CUF kwenye mkutano huo ilikuwa “kutochokozeka” na “kutoondoshwa kwenye mstari.”

Mkutano huo nao ulitanguliwa na mkutano wa wazee wa CUF kwenye ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani Zanzibar, ambako pamoja na mengine mengi, Maalim Seif naye alizungumzia mipango hiyo ya fujo zinazopangwa na zilizokwishafanywa huko nyuma. Na yeye akasogea mbele zaidi kwa kurejelea tamko la “kutofukua makaburi” lau chama chake kitachukuwa madaraka kamili baada ya uchaguzi wa Oktoba. Kwa hakika, aliwakemea wote waliomo kwenye chama chake, ambao wanadhani kwamba ikiwa CUF itaingia madarakani, itakuwa zamu yao ya “kutesa.”

Mstari wa makala hii unapigwa hapa ambapo nadhani pana haja ya kushereheshwa na sio kutafsiriwa tu. Kusherehesha – kwa wasioufahamu vyema msamiati huu na asili yake – kuna maana ya kuchambua tafsiri, wakati kutafsiri ni kuhamisha maana kutoka chanzo kimoja kupeleka chengine. Asili ya neno kusherehesha ni kwenye madarasa ya dini, ambako masheikh wanaotafsiri Qur’an huchambuwa maana ya kile walichokitafsiri kwa upana na marefu.

Kwa maoni yangu, kauli za “kutochokozeka”, “kutoondoka kwenye mstari”, “kutokufufua makaburi” na “kutolipiza kisasi” ni za muhimu sana katika kujenga siasa za Maridhiano visiwani Zanzibar na kulivuta kundi ambalo hadi sasa linayapinga Maridhiano hayo kwa kuwa tu lina wasiwasi juu ya hatima yake, endapo CUF itaingia madarakani. Lakini kwa umuhimu huo huo pia, panahitajika kuchorwa mstari na kuwekwa vituo ili kundi lililokwishaamua kuiangamiza Zanzibar, liujuwe pia ulipo mpaka kati ya kile wenzao wanachokichukulia kuwa ni uvumilivu lakini wao wakakiona ni ubwege.

Kwa namna yoyote ile, sidhani ikiwa CUF inakusudia kulipa kundi hilo la ‘watu wasiojuilikana’ hundi safi mkononi mwao ili liijaze litakavyo, kisha liondoke zake bila kuguswa. Sidhani hivyo, maana huko ni kwenda kinyume na hata misingi mikuu ya kuundwa kwa CUF yenyewe, ambayo ni haki za binaadamu na utawala wa sheria. CUF haivuni chochote kwa kuwapunguzia khofu watu hawa zaidi ya kuwahakikishia kile kinachoitwa ‘impunity’, yaani uwezo wa kukwepa sheria. Wanachofahamu wao pale wakiambiwa kwamba “makaburi hayatafukuliwa” ni kuwa wamepewa ruhusa ya kuendelea kupiga, kujeruhi na hata kuua, wakijuwa kuwa hatimaye hakuna mahakama wala jela inayowasubiri. Huo ndio uzoefu wao, maana hawajaanza leo wala jana kuyafanya haya.

Akili ile ile ya kutia moto mabanda ya skuli na vinyesi kwenye visima, ndiyo akili ile ile iliyounda Melody, kisha ikaja na Janjawidi na Mbwa Wakali na Ubaya Ubaya. Madhara yale yale ya miaka ya ’90, ndiyo yaliyokuwa ya 2000, 2005 na sasa 2015. Kundi hili, lenye akili hizi, halihitaji kuambiwa kuwa makaburi yake hayatafukuliwa, ikiwa bado linaendelea kuyatenda yale yale. Makaburi yao yanapaswa kufukuliwa na maovu yao kuanikwa hadharani na, zaidi kuliko yote, kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Zanzibar ijayo baada ya Oktoba 2015 inapaswa kuwa ya kuvumuliana na kushirikiana kuijenga kiuchumi, kijamii na kisiasa, lakini hilo halipaswi kuwapa watu nafasi mwanya wa kuichafua salama ya Wazanzibari hivi sasa, kisha wakategemea msamaha na kuvumiliwa baadaye.

Kwa hivyo, ingawa ni sahihi kabisa kujenga moyo wa Maridhiano na kuondosheana wasiwasi kwa wale waliotenda uovu katika zama za ujahili, si sahihi hata kidogo kuwajengea imani waovu wa zama za leo – ambazo ni zama za nuru. Hawa ni akina Abu Jahl. Hakuna chochote kitakachowabadilisha na kuwafanya waikumbatie salama ya Wazanzibari wote. Hawa lazima waelezwe kinagaubaga kuwa kuna mahakama, kuna jela, na kuna adhabu.

Wakati tunajitahidi kuwazuwia vijana wetu wasipande jazba na kuingia kwenye machafuko, kwani nako pia kutakuwa kwa faida ya kundi hilo la ‘watu wasiojuilikana’, tunapaswa kuchora mstari na kuweka alama zetu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.