Kongamano la Wannsee nchini Ujerumani lililofanyika mwezi Januari 1942 lilipitisha azimio lililokuja kupewa jina la “die Endlösung der Judenfrage”, yaani “suluhisho la mwisho kwa tatizo la Mayahudi”, ambalo baadaye lilikuja kujulikana kwa kifupisho chake cha Endlösung, yaani “suluhisho la mwisho”.

Suluhisho hili la mwisho ulikuwa mpango wa utawala wa Kinazi wakati wa Vita ya Pili vya Dunia kukiangamiza kabisa kizazi cha Mayahudi kupitia njia mbalimbali za mauaji, ikiwemo kuwavutisha gesi ya sumu, kuwauwa na kuwatesa. Kwa mujibu wa historia ya kimapokeo ya Ulaya, thuluthi mbili ya Mayahudi barani humo iliangamia.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, siku ya makabidhiano ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, siku ya makabidhiano ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.

Mauaji hayo yamekuwa alama kubwa sana kwenye historia ya kisiasa, kiuchumi na kijamii barani Ulaya na ulimwengu mzima wa Magharibi. Yalikuja baadaye kuamua mahusiano na mustakabali wa kimahusiano kati ya mataifa sio ya Ulaya tu, bali pia ulimwengu mzima, likiwemo la kuanzishwa kwa Dola la Kiyahudi la Israel.

Akiandika juu ya namna suluhisho hilo la mwisho lilivyoimaliza thuluthi mbili ya Mayahudi, Raul Hilberg anasema kwamba “katika awamu ya kwanza ya suluhisho la mwisho kwenye Shirikisho la Jamhuri za Kisovieti, wauaji waliwaendea watu wanaotaka kuwauwa, lakini kwenye awamu yake ya pili kote barani Ulaya, ni wale waliouawa ndio waliokuwa wakiwaendea waliotaka kuwauwa.”

Japokuwa si kila mtu anakubaliana na visa na mikasa vilivyomo kwenye masimulizi ya kimapokeo ya kile kilichokuja kuitwa “Holocaust”, lakini kwa muktadha wa makala hii ya leo, nataka uzingatie mambo matatu: kwanza, hiyo “thuluthi mbili ya Mayahudi” iliyoangamizwa; pili, ufahamu wa “tatizo” lenyewe la Mayahudi na, tatu, hilo “suluhisho la mwisho.”

Nataka uzingatie hayo kwa minajili ya kulinganisha na dhana kama hizo kwenye muktadha wa siasa za Tanzania panapohusika Zanzibar. Ninataka tuihusishe dhana ya thuluthi mbili ya Mayahudi walioangamizwa barani Ulaya kupitia mkakati huo ulioitwa suluhisho la mwisho kwa tatizo la Mayahudi na dhana ya thuluthi mbili ya kura za Bunge Maalum la Katiba itakavyotumiwa kuiangamiza Zanzibar kupitia mkakati uliopewa jina la “Katiba Iliyopendekezwa”, ambayo itapigiwa kura miezi michache ijayo na ambayo, kwa hakika, inasimama kama “suluhisho la mwisho kwa tatizo la Zanzibar” ndani ya Muungano.

Hoja yangu ni kuwa pana mfanano wa kinyume-mbele kwenye kadhia hizi mbili: Kwa Ulaya, mpango wa suluhisho la mwisho uliiangamiza thuluthi mbili ya Mayahudi ambao kwa ujumla wao walionekana kuwa tatizo; kwa Tanzania, thuluthi mbili ndiyo inayotumika kutoa suluhisho la mwisho kuimaliza Zanzibar, ambayo inaonekana kuwa tatizo kwa mustakabali wa Tanzania.

Nitafafanua kwa kuanza na vipi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – na hapa nakusudia sehemu ya tabaka linaloitawala hasa nchi kwa maana halisi ya kuitawala – linavyoichukulia Zanzibar kuwa ni tatizo, kama vile ambavyo kuna sehemu ya wanasiasa, watunga sera na wanamikakati wenye nguvu barani Ulaya, ambao walikuwa wakiamini kabisa kwamba jamii ya Mayahudi ilikuwa ni tatizo kubwa kwa mustakabali wa bara hilo.

Nafasi huenda isitoshe, lakini kuna mifano na kauli kadhaa zilizoanzia tangu kabla ya Uhuru wa 1963, Mapinduzi na Muungano wa 1964 zilizotolewa na watu wa aina hiyo kuonesha siasa yao kuelekea Zanzibar. Kwa mfano, mmoja wa waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema hata kabla ya Muungano kwamba kama angelikuwa na uwezo, basi angelivisukuma visiwa vya Zanzibar katikati ya Bahari ya Hindi. Aliwahi pia kumuambia mwakilishi wa Malkia Elizabeth wa Uingereza wakati wa kuelekea uhuru wa Zanzibar wa 1963 kwamba asingelivumilia kuwa na jirani Mwarabu na Muislamu kando ya mlango wake.

Kauli mbili za karibuni kabisa ni moja ile ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye kuelekea kukusanywa kwa maoni ya Katiba Mpya alisema yeye anaamini suluhisho ni kuwa na Serikali Moja tu, ambayo itazima “hivi vijinenoneno” vyote vya kero za Muungano, nyengine na ni ile Waziri William Lukuvi ambaye alisema Zanzibar ikiachiwa peke yake italeta Waarabu na utawala wa Kiislamu.

Hapo katikati, Rais Jakaya Kikwete na mtangulizi wake Benjamin Mkapa wamewahi kutoa kauli zinazofanana katika kuielezea hali ya Zanzibar, ambayo hapa nitaifupisha kwa sentensi yenye suali walilolitumia kwa pamoja ingawa kwenye maeneo na matukio tafauti: “Inakuwaje Wapemba hao hao ambao wanafaidika na fursa za Muungano wawe wa mwanzo wanaoonesha hisia za kujitenga na wenzao kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?”

Bila ya kusahau ya Phileomon Sarungi, ambaye wakati huo akiwa waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati wa utawala wa Mkapa, aliwahi kusema kwamba Muungano na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni kama watoto pacha na kwamba jeshi lisingelikuwa tayari kuwaachia wanaotaka kuuvunja Muungano.

Katika mazingira na matukio tafauti, kauli hizi na watunga mikakati na wasimamiaji wa sera za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanasema kitu kimoja: Zanzibar ni tatizo, Zanzibar kuna matatizo. Na hapana shaka, penye tatizo panatakiwa suluhisho.

Lakini swali kubwa ni kama lile ambalo jamii ya Kiyahudi barani Ulaya imekuwa ikijiuliza tangu hapo: “Tatizo ni nini? Tatizo letu ni lipi?” Mimi ni Mzanzibari na suali hili nimejiuliza kwa mwaka wa 20 huu tangu nilipopata akili ya kufuatilia mambo. Najua kuwa ndani ya jamii yangu ya Kizanzibari muna matatizo kama vile ambavyo yamo kwenye kila jamii ya binaadamu duniani – umasikini, ukosefu wa usawa, uhalifu na ukosefu wa uwajibikaji, miongoni mwa mengine mengi.

Tunalo pia tatizo ambalo linakuzwa zaidi kuliko uhalisia wake – la ubaguzi wa kikabila na asili za wakaazi wa visiwa vya Zanzibar. Lakini je, matatizo yetu ya ndani ndio sababu ya kuundiwa mkakati wa suluhisho la kudumu la kuimaliza Zanzibar kupitia thuluthi mbili ya kura za Wazanzibari wenzetu, kama kweli thuluthi hiyo mbili ilipatikana?

Nirejee tena. Historia ‘rasmi’ ya Magharibi inatuambia kuwa thuluthi mbili ya Mayahudi iliangamizwa kupitia kile kilichoitwa “suluhisho la mwisho kwa tatizo la Mayahudi”. Zanzibar nzima sasa inataka kuangamizwa kwa kutumia thuluthi mbili iliyoambiwa imepatikana kwenye Bunge Maalum kupitisha Katiba Iliyopendekezwa, ambayo hapa ndio huo mpango wa “suluhisho la mwisho la tatizo la Zanzibar.”

Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ndiyo ambayo imebeba hilo “suluhisho la kudumu la tatizo la Zanzibar.” Ni juu ya Wazanzibari sasa kuamua ikiwa kweli watakubali “suluhisho” lililotayarishwa kuwamaliza na kuimaliza nchi yao watakubaliana nalo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.