Baada ya uchaguzi wa 2005, nilikuwa mmoja wa vijana wa Kizanzibari ambao tulikuja na wazo la “kijuha” kwenye mazungumzo ya kawaida na hivyo sikushangaa kwamba lilipingwa mara moja na wenye akili zao zilizotulia. Wazo lenyewe lilikuwa hivi: Chama cha Wananchi (CUF) kijimeguwe chenyewe kwa makusudi na kisha sehemu ya watu wake wenye uwezo na ushawishi wakajiunge na Chama cha Mapinduzi (CCM) na huko wakashawishi mageuzi ya kimsingi kwenye siasa za Zanzibar, maana hakukuwa na namna yoyote CUF peke yake ingeliweza kuigeuza siasa ya nchi.

Msingi wa shauri hili ulikuwa ni kile nilichokiona kuwa kosa lililofanyika kwenye siasa za mageuzi visiwani Zanzibar baada ya kurejea tena mfumo wa vyama vingi kwenye miaka ya ’90, ambalo ni upinzani kuwachukuwa watu wote wenye uwezo wa kufikiri na kuona mbali na kukiwachia chama tawala wale wote walio kinyume chake. Kichwani mwangu mulikuwa na picha ya jitihada za aliyekuja kuwa waziri mkuu wa kwanza kwenye serikali ya mseto ya Kenya, Raila Odinga.

Matokeo yake, kwa kiwango changu cha uchambuzi hadi wakati huo baada ya chaguzi tatu za vyama vingi, upinzani ukawa unajikuta kila mara ukipambana na majuha waliokuwa tayari kufanya lolote alimradi tu wabakie madarakani, lakini ukiwa hauna watu wa kuzungumza nao kutoka upande wa CCM kwa kuwa akili hizi mbili zilikuwa zinafikiri tafauti na zina maono tafauti kuelekea Zanzibar moja.

Kama nilivyotangulia kukiri, hili lilikuwa wazo la kipuuzi na hivyo haikuwa ajabu kwamba lilipuuzwa. Mtu mmoja aliniambia lilikuwa “wazo geni na baya”, lakini akasema ilikuwa bora nilivyolitoa kwa kuwa lingewafanya wana-CUF wajuwe kuwa kuna wanaofikiri tafauti. Mwengine akachukuwa juhudi za makusudi kunionesha kwamba hoja yangu haikuwa na msingi, kwani bado ndani ya CCM walikuwamo ambao CUF ingeweza kufanya nao kazi wakiwa huko huko na wakawa kwa maslahi ya Zanzibar. Akaniambia “Kijana tulia, siasa si usheza”.

Kisha mwaka 2009 yakaja Maridhiano ya Wazanzibari ambayo kwa upande wa CCM yaliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Amani Karume, na wenzake wa chama chake. Siasa za Maridhiano zilikuwa na mtazamo wa ujenzi wa daraja baina ya pande tafauti za kisiasa visiwani Zanzibar kwa maslahi ya wote. Katika dhati yake, daraja huwa na kazi ya kuunganisha pande ambazo vyenginevyo huwa hazikutani, lakini halina kazi ya kuzichanganyisha pande hizo kama lilivyokuwa shauri langu la kumeguka CUF na kujichanganyisha kwenye CCM. Kuunganisha na kuchanganyisha hakuna maana moja.

Daraja la Maridhiano likaziunganisha pande mbili na moja ya matokeo yake ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hata hivyo, ujenzi wa daraja lenyewe haukuwa kitendo kilichofanyika na kukamilika, bali ulikuwa – na bado unaendelea kuwa –  mchakato unaopaswa kuendelea na, hivyo, kazi ya ujenzi inapaswa kuendelea.

Jambo la bahati mbaya ni kwamba wakati huu ujenzi ukiendelea, kisa cha nyumba ya Juha kinalazimishwa kirudi vichwani mwetu. Kwenye kisa hicho, Juha na ndugu zake walirithi fedha za kutosha kutoka kwa baba yao ambaye alikufa akiwa amemuacha mama yao mzee na mgonjwa. Wakaamua kwamba wajenge nyumba ya ghorofa tatu – ghorofa ya kwanza akae Juha na familia yake, ya pili akae mama yao na ndugu zake na ya juu wakae wapangaji ili kupata fedha za kumlisha mama na ndugu zake.

Kwa kuwa yeye ndiye kaka mkubwa akawa anakusanya fedha za wapangaji, lakini kwa kuwa ni Juha, akili zake huingia na kutoka na hivyo badala ya kumnunulia chakula na kumuhudumia mama yao, akawa anazila peke yake. Ndugu zake walipomjia juu, akawaambia: “Sasa sikizeni nyiye na mama yenu na wapangaji wenu. Mimi nishapata kiwanja mahala pengine na naichukua nyumba yangu – hii ghorofa ya kwanza – nakwenda kuihamishia huko. Kama munaweza zuwiyeni ghorofa zenu!”

Fuatilia kinachoendelea sasa ndani ya visiwa vya Zanzibar miongoni mwa rubaa za kisiasa na hutachelewa kugundua namna Juha anavyowatishia wenziwe kwenye nyumba ya pamoja. Wakati viongozi wa CUF wakiranda huku na huko kupigania kuuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuyalinda Maridhiano, wenzao wa CCM wanachukuwa jitihada kama hizo pia kuivunja serikali hiyo na kuyauwa Maridhiano.

Hakuna umbali ambao hadi sasa CUF haijakwenda kuhakikisha kuwa Maridhiano na Umoja wa Wazanzibari vinadumu, likiwemo hata la kurejea tangazo lake la asili kwamba serikali itakayoongozwa nao haitoruhusu chochote kile kitakachofasiriwa kuwa ni “kufukuwa makaburi” mulimozikwa machafu waliyotendewa viongozi na wanachama wa CUF visiwani Zanzibar ndani ya kipindi hiki cha miaka 27 ya siasa za vyama vingi .

Kinyume chake pia, hakuna umbali ambao CCM haijakwenda kuhakikisha kuwa Maridhiano na Umoja wa Wazanzibari unakufa kifo cha moja kwa moja. Mara tu baada ya mwasisi wa Maridhiano hayo kutokea CCM alipoondoka madarakani, kila siku inayokwenda kwa Mungu, basi huwa ni siku ya Juha kuibomoa kidogo kidogo nyumba yao ati akijidanganya kuwa atakwenda kuihamishia kiwanja chengine.

Hapana shaka, Juha kwa kuwa kwake juha, hana akili za kuaminika. Zingelikuwa za kuaminika, angelijua kuwa hawezi kuibomoa na kuihamishia nyumba kwenye kiwanja chengine na bado akawa na nyumba. Labda anaweza kuondoka na miti, matufali na milango – kila kimoja kikiwa kwake – lakini hivyo havitakuwa tena na thamani ya kujenga nyumba kama hii ambayo walijenga na ndugu zake kwa fedha za urithi, ili kuwasitiri wao na mama yao.

Kwa hivyo, ni jukumu la Wazanzibari wenye mapenzi ya kweli kwa nchi yao kutokumruhusu Juha huyu akaibomoa nyumba yao. Ila kwa kuwa si lengo kabisa kumuangamiza Juha kwa kuwa ni kaka yao, basi lazima wamtowe kwenye ghorofa ya kwanza ambayo ndiyo iliyoshikilia ghorofa nyengine za jengo lao na wamuhamishie ghorofa ya juu.

Mwaka 2015 ndio mwaka wa kumuhamisha Juha ghorofa ya chini.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.