Sijawahi kuandika tanzia kwa kiongozi mkubwa wa taifa, hasa taifa hilo likiwa ni la mbali sana, ambalo kikwetu ningeliweza kusema halinihusu ndewe wala sikio. Lakini nikiwa Mzanzibari, naiona nchi yangu ya Zanzibar ina jambo linalohusiana na taifa la Singapore ambalo Lee Kuan Yew aliyefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 23 Machi 2015 akiwa na umri wa miaka 91 alisaidia pakubwa kuliasisi miaka 50 iliyopita na kulifanya liwe kama lilivyo leo – kituo kikuu cha kibiashara na fedha kusini mashariki mwa bara la Asia.

Singapore ilipata uhuru wake tarehe 31 Agosti 1963 kutoka kwa Muingereza, miezi takribani minne tu kabla ya Zanzibar, ambayo nayo pia ilikuwa chini ya Muingereza. Wakati Singapore ilijiunga na jirani yake Malaysia katika kile kilichoitwa Shirikisho la Malaya tarehe 16 Septemba 1963, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu iwe huru, Zanzibar ilijiunga na jirani yake Tanganyika siku 100 baada ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964.

Sababu za Singapore kujiunga kwenye Shirikisho la Malaya na za Zanzibar kujiunga kwenye Muungano na Tanganyika zinafanana – kuzilinda serikali zao changa, udogo wa ardhi wa nchi hizi za visiwa, fursa za kutumia masoko na rasilimali za mataifa makubwa waliyoungana nayo na pia kile kilichoitwa kuwa kitisho cha kusambaa siasa za ukomunisti, ambao katika miaka hiyo ya ’60 ulifanywa uonekane kama hivi leo unavyoonekana ugaidi duniani.

Hata hivyo, kinyume na Zanzibar, Singapore ilidumu kwenye muungano na Malaysia kwa miaka miwili tu. Hali ya kutokuridhika ndani ya Singapore ilikuwa ni kubwa sana, na mara kadhaa kuliripotiwa visa vya wale waliojiona wazalendo zaidi kwa Singapore ambao hawakuafikiana na nguvu kubwa ilizokuwa nazo serikali ya Malaysia kwao. Tarehe 9 Agosti 1965, bunge la Malaysia likapiga kura kwa kauli moja kuifukuza Singapore kutoka kwenye muungano huo.

Na hapo ndipo tafauti kati ya Zanzibar na Singapore ilipoanza na tangu hapo mataifa haya mawili yamekuwa hayawezi tena kusomwa kwenye muktadha mmoja. Kutoka mwaka 1965 chini ya uongozi wa Rais Yusof bin Ishak na Waziri Mkuu Lee Kuan Yew, hadithi ya Singapore kiuchumi na kisiasa imekuwa hadithi ya nchi ya miujiza.

Nchi ya visiwa vipatavyo 60, ambayo hadi inapata uhuru kutoka kwa Muingereza miaka 50 iliyopita ilikuwa haimiliki hata kiberiti chake chenyewe, hivi leo ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea duniani. Ni ya tatu kwa kuwa na pato kubwa kwa mtu, ni moja kati ya nchi nne zilizo vituo vikuu vya fedha na ni moja ya bandari tano zenye shughuli nyingi kabisa ulimwenguni.

Mafanikio yote haya yanaunganishwa moja kwa moja na mtu ambaye hivi leo Singapore inaomboleza kifo chake, Lee, ambaye anatajwa kuwa kiongozi pekee duniani aliyeweza kuindoa nchi kutoka dunia ya tatu na kuwa dunia ya kwanza.

Lakini kuifikisha pahala ilipofika kunamaanisha kitu kimoja cha uhakika: kwamba Lee alikuwa na mtazamo madhubuti kuhusu nchi yake – nao akiuelezea kwa kusema kuwa rasilimali pekee ya nchi hiyo ni watu wake na utamaduni wao madhubuti wa kufanya kazi.

Miongoni mwa hoja za wale ninaowaita ‘apologists’ wa Muungano, ni kuwa hali mbaya iliyonayo Zanzibar miaka 50 baada ya uhuru na Muungano huo inatokana na Wazanzibari kuwa wavivu na wasio na maadili ya kuchapa kazi. Wanakupa mifano mingi ya makundi ya wazee na vijana wanaoshinda mitengoni tangu asubuhi hadi usiku wakipiga soga.

Hata hivyo, Singapore ya mwaka 1965 ilikuwa na hali mbaya na mbovu zaidi ya kimaadili miongoni mwa vijana na watu wake waliokuwa hawaoni njia ya ‘kutoka’ hadi pale akina Lee na wenzake walipowasha mwenge wa nuru na kuongoza njia. Serikali ya Lee ilikuwa na sheria kali kabisa kupambana na uvivu, ufisadi na uhalifu. Pia ilichukuwa hatua kali kupambana na ubaguzi, kwani mwenyewe Lee alisisitiza kuwa Singapore ni nchi ya watu mchanganyiko na kwamba hilo litabakia hivyo milele.

Matokeo yake, hivi leo taifa hilo dogo la watu milioni tano tu linazungumza lugha nne: Kimalay, Kimandarin, Kitamil na Kiingereza. Mjengeko wa utawala wake wa juu unaakisi mchanganyiko na heshima ya kila kundi linalounda taifa hilo. Rais wake wa sasa, Tony Tan Keng Yam, ni Mchina kwa asili kama alivyo Waziri Mkuu Lee Hsien Loong, ambaye ni mtoto wa Lee Kuan Yew. Lakini Spika ni Halimah binte Yacob mwenye asili ya Malaysia, wakati Jaji Mkuu ni Sundaresh Menon mwenye asili ya Kitamil.

Kwa wanaohoji kuwa kamwe Zanzibar haiwezi kuwa kama Singapore hata kama isingelikuwa kwenye Muungano, wanasutwa na uongozi na maisha ya Lee yanayotuonesha kuwa Singapore isingelikuwa kama ilivyo leo laiti ingelibakia kwenye Shirikisho la Malaya na ikawa katika mgawanyiko, kwa sababu uhuru wa kujiamulia, uwezo wa kujiendesha na moyo wa kujipenda kama taifa ndio misingi ya kwanza kwa taifa lolote kuendelea duniani.

Lee alifundisha somo hilo kwetu sote na kwalo nitamuita mwalimu kwetu. ‘Maalim’ Lee aliutumia muda wake madarakani kuijenga Singapore yake, ndivyo pia alivyoishi na kwavyo akafia.

Tafauti na viongozi kadhaa wanaotawala kikandamizi bila ya kuimarisha mataifa yao na ambao wanapofika kuumwa hulazimika kwenda kutibiwa na pengine kufa kwenye nchi za kigeni, Maalim Lee aliuvuta hadi upumzi wake wa mwisho akiwa kwenye kitanda cha Hospitali Kuu ya Singapore – akiwa Mnazi Mmoja yake.

Kwaheri Maalim Lee.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.