boraboraOKTOBA ya mwaka huu haitokuwa chapwa asilani kwa Watanzania, hasa wiki zake mbili za mwisho. Kipupwe kitakuwa kinamalizika. Polepole kiangazi kitaanza kuwaka, kikijiingiza kwa ghadhabu na nchi nzima itahanikiza harufu.

Haitokuwa harufu ya kiangazi wala ya kipupwe. Wala haitokuwa harufu ya asumini au ya waridi.
Mbali na harufu hiyo ambayo, kwa hakika, tunaweza kuinusanusa kwa mbali tangu sasa, kutakuwa na mengine yatayowashughulisha Watanzania. Kila mojawapo, kati ya hayo,kwa kiasi chake. Na kila mmojawao, miongoni mwa Watanzania, atalikimbilia litalomkuna.
Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Kuna watakaoiadhimisha Siku ya Nyerere Oktoba 14.Kuna wataofunga funga ya Ashura Oktoba 23. Kuna watakaoisherehekea Siku ya Umoja wa Mataifa Oktoba 24.

Hata hivyo,takriban taifa zima litagubikwa na wingu la matarajio Oktoba 25. Hakuna atayeweza kulikwepa.Kwa vile Oktoba 25 itaangukia Jumapili, makanisa yatajaa kwa wingi siku hiyo. Maombi ya waombaji yatakuwa ya dini naya dunia. Ya kiroho na ya kujaza tumbo.
Polepole, na mpaka sasa bila ya kishindo kikubwa, tarehe hiyo inanyemelea na uchaguzi mkuu nao unanyemelea ukishikwa mkono na tarehe hiyo. Na ni huo uchaguzi mkuu utaokuwa na harufu itayohanikiza nchi nzima, harufu ambayo tangu sasa twainusanusa.
Uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa na maajabu yake lakini uchaguzi wenyewe hautokuwa tukio la ajabu.
Sasa Watanzania wamekwishazoea. Kila baada ya miaka mitano, mnamo tarehe na mwezi mahsusi unaotangazwa kabla, wananchi wanakubali kujipanga foleni toka jua linapochomoza hadi linapotua.
Wamewekewa utaratibu maalumu na saa maalumu kwa zoezi hilo. Kwa jumla, wanaufuata utaratibu huo, hata ikiwa kwa muda huo watabanwa na njaa au watapigwa na jua. Yote watayavumilia. Ndivyo demokrasia inavyotaka.
Kila mmojawao huwa na siri yake na siri hiyo huizika kifuani mwake. Ni siri ya nani na nani wa kumpa kura zake.
Imesalia miezi saba tu sasa kabla ya wananchi kupiga kura zao kuwachagua viongozi wao, toka madiwani, wabunge na Rais. Kipindi hiki ni kipindi muhimu sana kwa amani na utulivu nchini kote. Ni kipindi cha vyama na wanasiasa wao kufanyia kampeni za kuwavutia wapiga kura. Si kipindi cha kutishana.
Lazima tuwakumbushe wanasiasa wetu na washabiki wao kwamba zoezi la uchaguzi ni zoezi la ushindani wa kisiasa, ushindani wa vyama vya siasa au vya itikadi za kisiasa. Si zoezi la uhasama, la kupalilia chuki, kuchochea mapigano, kuingiliana mwilini na kutwangana. Siasa nazo zina ustaarabu wake na mipaka yake.
Neno ‘siasa’ limetokana na neno la Kiarabu ‘siyasa,’ ambalo asili yake lilikuwa na maana ya kuwatunza farasi(kwa kuwalisha, kuwanadhifisha na kuwachana). Si neno lenye asili ya ‘ugomvi’.
Hata katika Kiswahili tunalitumia neno ‘siasa’ kuwa na maana nyingine, sawa na ‘busara’ au ‘maarifa’. Kwa mfano, tunasema: “Alitumia siasa kuwasuluhisha katika ugomvi wao,” au “Fanya mambo kwa siasa,” unapokuwa unamwambia mtu afanye mambo kwa busara.
Leo inasikitisha kuwasikia wanasiasa — hasa wale wanaojitia kuwa ni wanasiasa — wakizitumia sivyo siasa. Kwao wao tofauti za kisiasa ni chuki na ugomvi. Na wanaziongezea matusi kama kachumbari ya kuzitia ladha. Lakini kinyume chake siasa zao huwa zinachusha,zinakirihisha na zinawafedhehesha wao na chama chao.
Kwetu Zanzibar chuki za kisiasa zimekuwa jambo la kawaida. Inasikitisha, kwa mfano, kusikia kwamba usiku wa Ijumaa iliyopita maskani tatu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilichomwa moto katika kisiwa cha Tumbatu, mkoa wa kaskazini Unguja. Inadhaniwa kwamba kilichosababisha tukio hilo ni siasa.
Chama cha Wananchi (CUF) nacho kimedai kwamba bendera zake zilichomwa moto. Matokeo ya yote hayo ni kwamba mkutano uliokuwa umepangwa na CUF huko Tumbatu ulibidi uzuiwe na polisi usifanyike.
Hilo pengine ndilo lililokuwa lengo la CCM. Inawezekana hata hizo maskani tatu zilizotiwa moto zikawa zimetiwa moto na waliotaka kuchochea CUF isiruhusiwe kuwa na mkutano wake wa hadhara Tumbatu. Njama za kisiasa ni za aina kwa aina.
Maskani ya Kisonge ya CCM iliyo mjini Unguja inajulikana kwa bao lake jeusi ambapo uchafu wa kila aina huandikwa dhidi ya wanasiasa wa upinzani. La hatari zaidi ni yale maneno yanayoandikwa kwenye bao hilo yasemayo kwamba CCM hakitatoa serikali hata kama chama hicho kitashindwa kwenye uchaguzi;kwamba anayetaka kuihodhi serikali itambidi atumie nguvu.
La kushangaza ni kwamba vyombo vya dola havioni umuhimu wowote wa kuchukuwa hatua dhidi ya uchochezi dhahiri wa aina hiyo. Wala viongozi wa ngazi za juu wa CCM hawaoni kwamba kuna haja ya dharura ya angalau kuwakemea wenye kuhusika na uovu huo.
Halafu kuna viongozi wa chama hicho waliofurutu ada kwa matusi ya nguoni dhidi ya viongozi wa upinzani. Mmoja wao ambaye ni aibu kubwa kwa chama chake ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini, Borafya Silima Juma. Adabu zangu haziniruhusu kuyakariri hapa matusi yake.
Yanayoshangaza kumhusu bwana huyu ni mawili: kwanza, kwamba mtu mwenye tabia kama yake ameweza kuchomoza kuwa kiongozi katika chama kikubwa chenye historia ndefu kama kilivyo CCM; pili, kwamba chama chake hakijamchukulia hatua yoyote ile.
Matamshi ya Borafya ni matamshi ya kihuni. Zake si siasa.Ni aibu si kwa CCM tu bali kwa taifa zima. Siku hizi amewaandama viongozi watatu wa CUF: katibu mkuu wa chama hicho Seif Sharif Hamadi, ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, mwakilishi wa Mji Mkongwe na Mansour Yusuf Himidi, aliyehamia CUF baada ya kufukuzwa kutoka CCM kwa msimamo wake wa kutaka Zanzibar irejeshewe mamlaka yake kamili.
Matusi ya Borafya yanasema mengi kuhusu jamii yetu na yanatufanya tujiulize maswali kadhaa. Hivi ndivyo tulivyo?Tunajipima vipi mbele ya wenzetu? Tutathubutu vipi kujinata kwamba tuna utu, kwamba tumestaarabika na tumeendelea kimaadili?Nani atatuheshimu ikiwa wenyewe hatujiheshimu?
Na inavyoonyesha ni kwamba CCM siyo tu kwamba kinavumilia uhuni lakini ni chama kinachowaogopa wahuni wake. Bara kinawaogopa mafisadi wake na Zanzibar kinawaogopa wahuni wake.
Majaaliwa ya Tanzania ya leo ni kwamba vyama vyote vikuu vya siasa vina itikadi inayofanana. Vinatofautiana katika kutia shadda na mada juu ya sera zao lakini si katika falsafa ya kimsingi ya sera zenyewe.
Kuhusu uchumi, vyama vyote vinafuata itikadi ya ulibirali mamboleo. Katika siasa vinafuata itikadi ya demokrasia ya ulibirali. Hata hicho kinachojidai kwamba kinafuata ujamaa, yaani CCM, kinaupigia tarumbeta tu huo ujamaa.
CCM kinafuata kwa dhati sera za demokrasia ya ulibirali, ingawa kwa vitendo vyake kinaonyesha kwamba kimeukiuka mwiko si wa ujamaa tu bali hata na wa demokrasia ya ulibirali.Miongoni mwa kanuni za demokrasia hiyo ni kulinda haki za binadamu, kuwa na utawala wa kisheria na kupinga ufisadi. Ilivyo ni kwamba, kinyume na mambo, ndani ya CCM ya leo lila na fila hutangamana.
Viongozi wake, buheri wa hamsini, wanayavamia na kuyapapia yaliyo haramu katika ujamaa. Miongoni mwayo ni ubinafsi, uroho wa mali na ufisadi (wa kiuchumi na wa kimaadili). Hakuna kinachowasumbua.
Ndio maana tukaona kuwa viongozi wa aina hiyo wako tayari kulitosa taifa ilimradi yao yawe yanawaendea.
Ubaya, au hatari, iliyopo ni kwamba katika uchaguzi mkuu wananchi watatakiwa wawachague watu ambao wengi wao, kwa kawaida, ni watu wasioaminika.
Watu hawa, mabibi na mabwana (na wengi wao ni mabwana, tena mabwana wenye kuushadidia mfumo dume), ni watu usioweza kuwaamini. Huwezi kuyaamini wayasemayo.
Sisemi kama ni waongo. Nisemacho ni kwamba aghalabu huwa hawawezi kusema kweli. Mara nyingi, ndimi zao hukosa nidhamu. Hujisemea tu mambo ovyo ovyo bila ya kupima yatakuwa na athari gani katika jamii. Ni kama walivyo akina Borafya, kina shashimashishi. Hiyo ndiyo hulka yao.
Kuna na jengine wanalopenda kulifanya: wana tabia ya kutoa ahadi wasizozitimiza. Kwa hakika, huahidi mambo wakijuwa kwamba hawana nia wala uwezo wa kuyatekeleza.
Wanababaishababaisha na wanaitwa waheshimiwa, ingawa kuna miongoni mwao wanaostahiki kupelekwa wakapumzike korokoroni kwa makosa ya jinai wayafanyao. Makosa hayo ni pamoja na ya wizi wa mali ya umma, kukiuka haki za binadamu na kutawala vibaya.
Dhambi moja kubwa wanayoifanya wanasiasa wa sampuli hii ni kuugeuza utamaduni wa taifa na kuufanya uwe utamaduni wa “omba omba.” Serikali inazoea kuomba kwa wafadhili, wanasiasa walio madarakani wanaiomba serikali na wananchi wa kawaida wanawaomba wanasiasa. Hiyo ndiyo elimu ambayo wanasiasa wetu wanawapa wananchi.
Ndio maana tunakuwa na mafundo vichwani mwetu. Wanasiasa wetu wanatukanganya; wanatufunza tabia mbaya. Wanaona kuwa njia rahisi ya kuzipata kura za wananchi ni kwa kuwahonga wananchi. Nimeambiwa kwamba hongo kubwa zinatolewa na CCM/Zanzibar.
Wanasiasa wakishazoea kuwahonga wananchi inakuwa rahisi nao wenyewe pia kuhongwa ama na mitajiri mikubwa ya ndani ya nchi au ya nje ya nchi au na hata na madola makubwa. Ni hatari kubwa.
Jamaa mmoja mfuasi wa CCM/Zanzibar amenisikitikia kwamba mambo yanakwendashaghalabaghalandani ya chama chake lakini mimi naona yamepindukia hata hiyo shaghalabaghala. Labda ni‘baghalashaghala’. Mkorogeko moto mmoja.
Chanzo: Raia Mwema, Toleo Na. 397 la 18 Machi 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.