LICHA ya sifa lukuki tulizonazo, na ambazo mimi kama Mzanzibari najifaharisha nazo, Wazanzibari tuna udhaifu wetu wa kibinaadamu. Hatupendi kuambiwa ukweli. Kama walivyo wengine, tukiambiwa ukweli mchungu, huja juu kama moto wa kifuu.

Na hili hasa huja katika masuala ya siasa za Uzanzibari. Nakusudia inapoguswa hadhi, heshima na kile tunachoamini kuwa ni utaifa wa Zanzibar. Baya zaidi ni kwamba, tofauti na wenzetu wengine, sisi hasira zetu ni za mkizi – hujirusha na kujiingiza wenyewe kwenye dau la mvuvi na, hivyo, tukampunguzia tabu mvuvi huyu kutunasa. Ya nini wakati tumekwisha kuingia wenyewe!?

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.

Sakata inayoendelea sasa baina ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idi Pandu Hassan, ni mfano mmoja tu kati ya mingi inayoelezea ukweli huu. Unaweza kuona namna ambavyo Wazanzibari tumechokozeka na namna ambavyo tunajibu uchokozi huo: kwa ghamidha na hasira. Lakini subiri kidogo uone mwisho wake: Zanzibar itaingia tena mtegoni kuliko ilivyokuwa hapo kabla!

Mtazamo wangu ni kwamba pale Waziri Mkuu Pinda alipojibu bungeni, wiki iliyopita, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo, kwamba Zanzibar si nchi alikuwa amepatia lakini alikuwa ’amepinda’ kidogo panapohusisha siasa za Muungano kuelekea Zanzibar; na kwamba Mwanasheria Pandu alipopinga kwa kusema kwamba Zanzibar ni nchi alikuwa ameupindua ukweli juu chini chini juu, yumkini kutokana na kwamba taasisi anayoiwakilisha (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar – SMZ) inaamini juu ya mapinduzi daima, ikiwemo kuupindua ukweli. Nitafafanua.

Majibu ya Waziri Mkuu Pinda yalikuwa wazi: kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano (kwa hakika na hata ya Zanzibar), Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hivyo haisimami kama nchi kamili. Katika Katiba zote mbili, kwenye sura zake za kwanza ambako kunaelezewa eneo la nchi, mipaka na mamlaka yake, ukweli huo ndio ulivyoandikwa. Kwa hivyo, Pinda alisema kile kilichomo kwenye Katiba ambayo aliapa kuilinda. Kisheria hivyo ndivyo ilivyo.

Lakini kila siku pana tofauti baina ya sheria na siasa. Ingawa wanasiasa ndio hutunga na kupitisha sheria, wao hufanya hivyo kwa kusukumwa na mambo mengi, yakiwamo matashi binafsi na maslahi ya kitambo wanayofaidika nayo. Mara nyingi, kwa hivyo, hisia za kibinaadamu ndizo huwasukuma wanasiasa wakashinikiza kutungwa na kupitishwa kwa sheria fulani ambayo huwa na maslahi kwao kwa kipindi hicho kifupi.

Bila ya shaka, ndivyo hata huu Muungano wenyewe ulivyokuja kupata uhai wake. Zilikuwa hisia za Mwalimu Julius Nyerere za kutaka kuidhibiti na kuimiliki Zanzibar na upande mwengine zilikuwa hisia za Sheikh Abeid Karume kuingia madarakani na kujilindia madaraka hayo. Wote wawili wakatumiana kupata muradi wao. Wakashinikiza hisia zao za kisiasa ziundiwe sheria na sasa sheria ndiyo iliyopo mbele yetu.

Sasa sheria ikisha kutungwa na kupitishwa na vyombo husika (hata kama yenyewe haikupitishwa kisheria kama anavyohoji Alhaji Aboud Jumbe kwenye The Partnership), bado huwa ni sheria tu. Na sheria ni msumeno, hukereza pande zote bila kujali tena ikiwa zile hisia za wanasiasa walioitaka itungwe zimeendelea kubakia au la.

Na, kwa hakika, hisia hasa ni jambo la kitambo tu na maslahi ya wanasiasa si kitu cha kudumu: hubadilikabadilika kutokana na wakati, mazingira na muelekeo wa kilimwengu. Ikifika hapo, utawakuta wakikipinga kitu kile kile walichokipigania kiwe sheria ambacho sasa huwa kiko dhidi yao. Lakini sheria huwa ipo na haijali hayo.

Kuna mifano mingi inayoonyesha kwamba hata Sheikh Karume alifika mahala pa kujiona yuko pale wanapaita Waingereza kwenye loosing end. Kwa kujiona kuwa kumbe alipoteza kuingia kwenye Muungano na Mwalimu Nyerere, alikuwa mara kwa mara akifanya vitimbi dhidi ya Muungano wao lakini tayari alikwisha kufeli na hivyo akashindwa kufanya chochote zaidi ya kuyaacha mambo yaporomoke mbele ya macho yake. Sheria haikuwa tena na wakati na hisia zake kama Karume maana ilikwisha mnyima nguvu ya kuwa yeye mwenyewe. Na namna hiyo – ya kupoteza chembechembe za nguvu – ndiyo ambayo imekuwa ikiikumba Zanzibar kwa miaka yote sasa!

Mwangwi huu wa kushindwa kwa Karume kukidhi hisia zake za kisiasa ndani ya Muungano wake na Nyerere ndio hasa unaosikika sasa kutoka kwa Mwasheria Mkuu wa Zanzibar  Pandu. Licha ya kuwa kwake mwanasheria, lakini katika hili anapiga bobo la kisiasa tu. Ukweli anaujua uko wapi (au angalau angelitakiwa aujuwe ulipo). Na kama haujui, basi yupo kwenye nafasi aliyonayo kwa bahati mbaya kama ilivyo kwa mamia ya wengine kwenye SMZ (kama ilivyothibitishwa mwaka juzi na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Ramadhan Muombwa).

Mwanasheria Pandu anapindua ukweli kwa kuchanganya makusudi baina ya vile ambavyo sisi Wazanzibari wengi tungetaka iwe na vile hasa ilivyo. Wengi wetu tungetaka iwe hivyo alivyosema Pandu: Zanzibar iwe ni nchi kamili, yenye kila chake na kila lake na kisha ndiyo iwe sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa hakika hasa, sisi tunahesabu kwamba hakuna nchi inayoitwa Tanzania, bali kuna Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – kama ilivyokuwa ikiitwa hapo mwanzoni kabla ya manyau ya kisiasa-kisheria hayajafanywa kuliondoa jina hilo.

Kwa wengi wetu, bado nafsini tunabeba utaifa wa Uzanzibari ingawa kwenye paspoti zetu na fomu nyingine tunazojaza kiofisi huandika Watanzania. Wengi wetu hatutofautishi baina ya Uzanzibari kama utaifa na Uzanzibari kama uzalendo. Hivyo ndiyo hasa tunavyotaka iwe; na Mwanasheria Pandu anazijua hisia za wengi wetu, ndiyo maana akasema alivyosema.

Bali je, hivyo ndivyo ilivyo? Hapana, sivyo. Sivyo kwa kuwa miaka 44 iliyopita, Zanzibar ilipatwa na kile ambacho leo hii Jakaya Kikwete angelikiita ‘ajali ya kisiasa.’ Ilikuwa ajali kwa kuwa ilikufa dungu msooni, kwa kutumia maneno ya Al-Arham Ali Nabwa, ikaambiwa ilokula iziteme na mchezoni haimo.

Kwa kusaini Mkataba wa Muungano, Sheikh Karume aliamua, labda bila kujua, kuipotezea Zanzibar kila kile ambacho ilikipigania: uhuru, utaifa, uzalendo, uchumi imara na uwezo wake wa kuchagua mustakabali gani ifuate kwa maslahi ya vizazi vyake. Na tangu hapo vitu hivyo havijarudi tena.

Huu, hata hivyo, ni ukweli ambao Wazanzibari hawataki kuambiwa, yumkini nikiwamo mimi mwenyewe ninayeandika haya. Sitaki mgeni wa Zanzibar, tena hasa mgeni huyo akiwa ni kiongozi wa Serikali ya Tanzania, aniambie kuwa sina nchi, sina dola, sina utaifa, sina utambulisho. Nitakuwa mkali kwelikweli. Nitaripuka kwamba amenidhalilisha. Naweza hata kufikia umbali wa kumtaka aniombe radhi, ingawa hata kama hakuniomba, kwa hakika, nitakuwa sina la kumfanya, maana yeye ndiye mwenye nguvu zote.

Tena ukweli kama huu ukiwaambia watu kama Mwanasheria Pandu, katika vinara wa kundi la wahafidhina wa Zanzibar, ndiyo huwa mbaya zaidi, maana kundi hili, licha ya kuujua ukweli halitaki wananchi waujue, sababu hawataki kukiri Sheikh Karume alifanya kosa la kihistoria. Basi wakiambiwa hivyo, si mno kutishia kuirudisha Afro-Shiraz yao.

Kuirudisha Afro-Shirazi ndiye paka-nyau wanayemtumia kila mara kuwatishia wenzao wa Bara ili wakubaliane na mtazamo wao. Inaaminika ndiye waliyemtoa mwezi Machi uliopita  kule Butiama katika kuzuia kufikiwa kwa makubaliano ya kisiasa ambayo yangewaleta pamoja Wazanzibari kupitia serikali inayowajumuisha wote.

Lakini huku ni kupindua tu ukweli mkavu ulioko mbele yetu kwa lengo la kujibereuza ama kuwatupia wengine lawama kwa makosa yetu wenyewe (kama hivyo kusema kuwa Waziri Mkuu Pinda ameteleza ulimi). Kwa hakika ni aina fulani ya ugonjwa ambao wanasaikojia huuita perplexity complex.

Si hatari sana kwa mtu mmoja katika 100 akiugua ugonjwa huu, maana wenzake 99 wanaweza kumsaidia, lakini ni hatari ikiwa wote wanaugua kwa wakati mmoja, maana hawatatambua kuwa ni tatizo. Watadhani ndiyo kawaida na wataishi nao kama mwenza na si adui yao. Ndivyo ilivyo kwa sisi Wazanzibari na viongozi wetu. Tunaugua ugonjwa wa kujibereuza.

Ni kweli, hata hivyo, kwamba naye Waziri Mkuu Pinda ‘alipinda’ katika jibu lake. Kupinda kwenyewe ni vile kwenda kwake nje kidogo ya mstari wa siasa za Muungano, ambazo kila siku zimezingatia kanuni ya unafiki wa Kiingereza – mbele ya macho yako Mwingereza hawezi kukushambulia wala kukufanya ujihisi ovyo, lakini ukimpa mgongo ‘anakuchomeka kisu.’ Ndivyo ambavyo imekuwa siku zote kwa upande wa viongozi wakuu wa Serikali ya Muungano wa Bara – huwa hawawaonyeshi wenzao wa Zanzibar kwamba wanakwenda siko, bali huwasubiri wageuke tu ‘wawachomeke visu’ migongoni.

Sijui ikiwa Pinda ni mgeni wa siasa hizi, lakini wenzake wa Zanzibar hawajazoea kuambiwa hivyo. Ama hunyamaziwa tu wakisema, au huitwa chumbani wakafungiwa, bila ya watu wengine huku nje kujua kuwa kuna kitu kinatokezea. Wakitoka hapo utasikia tu, kwa mfano, Rais wa Zanzibar si tena Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Sasa ati baada ya kutokea mtafaruku huu wa maneno kidogo, Waziri Mkuu Pinda anasema amemuagiza Mwanasheria wa Tanzania akutane na mwenzake wa Zanzibar kukubaliana namna ya kutafsiri kifungu cha Katiba kinachozungumzia u-nchi wa Tanzania na Zanzibar! Ni hili ambalo lilikuwa aliseme mwanzo, kisha wakitoka kwenye kikao hicho, waje waandike kabisa kwamba ‘Zanzibar si nchi’ na isomeke hivyo kwa herufi kubwa zilizokozeshewa. Wala asitarajie kwamba atapata upinzani wowote kutoka Zanzibar kwa hili. Kwa Zanzibar ‘imejitolea’ mangapi ‘kuimarisha’ Muungano huu hata ishindwe dogo hilo!

Nimalizie kwa angalizo: sijasema kwamba, kama Mzanzibari, ninaridhika na hali halisi ilivyo. Mimi pia ninaishi kwenye ile njozi ya mamia ya maelfu ya Wazanzibari wengine. Siridhiki kwamba hatuna chetu, hatuna letu; na kwamba leo hii tunaweza kuambiwa ukweli huo na ukasadifu. Kama Mzanzibari mwingine yeyote, hili linaniumiza na natamani ningekuwa na njia ya kufanya hali ikawa vyenginevyo.

Ndiyo maana ni ushauri wangu kwamba Wazanzibari tujue kosa letu na tufanye kitu kuhusiana na kosa hilo. Kosa letu kubwa ni kujikubalisha kutumiwa kisiasa kwa maslahi binafsi na ya kitambo sana, na si ya taifa na ya kudumu.

Historia ina mengi ya kusema kuhusu ukweli kwamba siasa za Muungano kuelekea Zanzibar zimekuwapo tangu miaka ya ’50 na zimelenga kuitawala Zanzibar. Kulifanikisha hilo, kwa namna moja ama nyingine, ni sisi Wazanzibari wenyewe tuliotumiwa: ama kupitia vyama vyetu vya siasa au asili ya uzawa wetu. Siasa na uzawa zimetumika dhidi ya Zanzibar na si kwa maslahi yake na mwisho wa siku tumejikuta kwamba iliyopoteza ni Zanzibar kama nchi.

Hata hivyo, bado tunayo fursa ya kubadilisha mtazamo wetu, Wazanzibari, na wenzetu, wa Bara, katika kulielekea suala hili; na dalili ziko hivyo. Tunaona ambavyo kauli ya Waziri Mkuu Pinda ilivyotuunganisha sote kihisia. Sababu ni kuwa tumeguswa kama Wazanzibari. Tunaweza, kwa hivyo, kuanzia kwenye mambo kama haya na kwenda mbele pamoja.

Kwa dhamira nzuri, wenye dhamana ya utawala Zanzibar wanaweza kutangaza mgogoro wa kikatiba, ambao unakubalika kwa mujibu wa Katiba iliyopo na kuwaita Wazanzibari wote pamoja. Tusio na dhamana ya utawala tunaweza kuitikia mwito huo wa viongozi wetu. Kisha sote, kwa pamoja, tukadai kile kilicho bora zaidi kwa nchi yetu hata kama kitu hicho hakitakuwa kujitoa kwenye Muungano.

Naamini Zanzibar imo kwenye Muungano si kwa sababu potofu zinazotolewa kuwa eti Zanzibar ni nchi ndogo isiyoweza kuwa peke yake au kwa kuwa tunategemea zaidi Bara kwa uchumi wake. Ni kwa kuwa siasa za Muungano kuelekea Zanzibar zinafanana sana na zile za Syria kuelekea Lebanon. Tukizichukua kwa pupa, zinaweza kuhatarisha maisha yetu zaidi kuliko kuyatengeneza!

Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema, Toleo Na. 038, la tarehe 16 Julai 2008.

2 thoughts on “Pinda kapinda lakini Pandu kapindua”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.