Kuna mambo mawili matatu ya kuyaweka sawa kabla ya kuingia kwenye kiini cha mjadala wenyewe. Kwanza ni kujibu swali ambalo niliwahi kuulizwa kitambo, la ikiwa kweli kuna kitu kinachoitwa “ajenda ya Zanzibar” katika Muungano wa Tanzania. Msingi wa swali hilo ni ukosoaji wangu dhidi ya wale ninaowaona kuwa ni “maadui wa ajenda” hiyo ndani na nje ya Zanzibar. Niliulizwa pia ikiwa ajenda hiyo inabebwa na kundi lolote maalum la kisiasa au kijamii na ambalo linaweza kuambiwa linawawakilisha Wazanzibari wote.

Jibu ni kwamba ajenda ya Zanzibar ipo, imekuwepo na itaendelea kuwepo. Neno “ajenda” lenye asili ya Kilatini, agendum, lina maana ya orodha ya mambo yanayozingatiwa au kupangwa kufanywa na pia mpango au programu ya kiitikadi kufikia malengo ya jumla na malengo mahsusi. Kwa fasili yake hiyo, Zanzibar imekuwa na ajenda yake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayolenga madaraka na mamlaka zaidi ya kujitawala, kujiamulia na kujitendea.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, siku ya makabidhiano ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, siku ya makabidhiano ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.

Ukifuatilia mtiririko wa matukio na matokeo yake ndani ya kipindi cha miaka 50 ya Muungano, utaishuhudia ajenda ya Zanzibar kwa uwazi kwa kuiona orodha ya mambo yanayoyazingatiwa na Zanzibar na pia mpango wa kuyafikia malengo yake. Kwa mfano, licha ya vyote unayokosolewa, Mkataba wa Muungano una ajenda ya Zanzibar ndani yake. Unasema lipi na lipi ambalo Zanzibar italisalimisha kwenye mamlaka ya tatu (Serikali ya Muungano) na yapi na yapi yataendelea kusalia kwenye mamlaka yake (Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, SMZ). Na kwa yote – yale yaliyosalimishwa kwenye mamlaka ya tatu na yale yaliyosalia kwake – Zanzibar ina mpango wake wa kiitikadi kufikia malengo yake ya jumla. Itikadi hii imefumwa katika utambulisho wa Uzanzibari unaoakisi utaifa wa Zanzibar. Kwa hivyo, utaifa wa Zanzibar ndiyo kiini cha ajenda ya Zanzibar; na ndilo lengo kubwa na mahsusi, maana lengo linaweza kuwa kubwa na bado likawa pia mahsusi.

Hapana shaka, lengo kubwa na mahsusi linahitaji pia taasisi kubwa na mahsusi ya kulifikia; na hapa ndipo linapozuka lile swali lililoambatanishwa na la hapo juu: je, lipo kundi ndani ya Zanzibar ambalo linawakusanya Wazanzibari wote kwenye ajenda hii ya Zanzibar?

Jibu lake ni ndiyo na hapana. Ndiyo kwa kuwa kihistoria, taasisi hiyo imekuwa ni Serikali ya Zanzibar yenyewe kupitia viongozi wake wa juu kama ambavyo makala hii itaonesha hapo baadaye. Hapana kwa sababu si kila Mzanzibari anaiamini ajenda ya Zanzibar, na hivyo hata wakati ambapo SMZ inasimama kama taasisi kwa ajili ya ajenda hiyo, hutokezea Wazanzibari wakatenda kinyume. Wako, ambao hata kama ni wachache, hawaiamini ajenda hii na ambao wangependelea zaidi “Ajenda ya Muungano” kuelekea Zanzibar. Wako pia ambao wanaiamini, lakini hawataki kuonekana kuwa wanaiamini kwa kuhofia jambo moja ama jengine.

Hata hivyo, hili halina uhusiano wowote na mgawanyiko wa vyama vya siasa, kwa mfano kama CCM na CUF, au mgawanyiko wa kihistoria na uzawa. Kwenye matukio na matokeo yake mbalimbali, Zanzibar imethibitisha kitu kimoja: kwamba vyovyote ambavyo Wazanzibari wanagawanyika, kuna kitu ambacho daima huwa kinawaunganisha; na kitu hicho ni ajenda ya Zanzibar.

Kwa mfano, hata katika kilele cha ugomvi wao juu ya Katiba Inayopendekezwa, pande mbili zinazounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, CCM na CUF, zinakubaliana kuwa SMZ inastahiki kuwa na nguvu zaidi ya ilizonazo sasa katika kuamua, kusimamia na kutekeleza sera zake za uchumi, ukiwemo udhibiti wa masuala ya kifedha, kodi, mikopo na vyanzo vyengine vya mapato.

Kwa hivyo, mtu anaweza kuhitimisha kuwa ingawa kumekosekana taasisi moja kubwa na imara kwa ajili ya lengo moja kubwa na mahsusi la ajenda ya Zanzibar, daima kumekuwa na vuguvugu ambalo limo ndani ya makundi na taasisi zote zinazowawakilisha Wazanzibari kupitia nyanja zote za maisha – siasa, jamii na hata dini.

Ndiyo maana Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar yalipita ndani ya Baraza la Wawakilishi mwaka 2010, wakati ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria mukiwa na wawakilishi wengi zaidi wa CCM na pakiwa hapana Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa kuwa yalikuwa yamebeba ajenda ya Zanzibar. Ndiyo maana pia kura ya maoni ya mwaka huo huo ikapita kwa wingi mkubwa kwa kuwa msingi wake ulikuwa ni Maridhiano ya Wazanzibari na hivyo pia ajenda ya Zanzibar.

Swali linalobakia sasa ni lile linaloihusisha ajenda ya Zanzibar na ya Tanzania nzima kwa ujumla ndani ya mwaka 2015; na swali kubwa zaidi ndani yake ni je, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza kuikwepa ajenda hii ya Zanzibar ndani ya mwaka huu, kisha nayo ikabakia kuwa imekwepeka?

Jibu ni hapana. Tangu ulipoanza mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano, Wazanzibari walishaamua wazi kwamba bila ya ajenda yao pasingelikuwa na Katiba Mpya. Katika hatua za awali walionesha kwa ujumla na umoja wao, bila ya kujali ufuasi wa vyama au dini zao. Serikali kwa umoja wake ikawa kweli ya Umoja wa Kitaifa kuisimamia ajenda ya Zanzibar. Wengi wetu tunawakumbuka wajumbe wa Baraza la Mawaziri na hata wa Baraza la Wawakilishi kutoka pande zote mbili zinazounda serikali wakisimama imara kuitetea ajenda hiyo. Asasi za kiraia na kijamii nazo zikafanya hayo hayo.

Lakini kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda kuelekea ukusanyaji wa maoni ya wananchi kupitia Tume ya Jaji Warioba na kisha kuundwa kwa Bunge Maalum la Katiba na yaliyofuatia baada ya hapo, ile kamba iliyowaunganisha Wazanzibari kwenye vyombo hivyo, ikaanza kuonekana kidogo kidogo ikikatika. Ajenda ya Zanzibar sasa ikawa inasemewa kwa sauti kali na upande mmoja. Upande mwengine “ukaufyata”! Na hadi sasa umeendelea kuufyata na pale unapoufyatua huwa ni kwa kuugeukia upande mwengine na sio kuiendeleza ajenda ya Zanzibar.

Je, hili linamaanisha kuwa ajenda ya Zanzibar imeshakufa na, kwa hivyo, sasa kunaweza kupatikana katiba isiyozingatia na inayoikwepa kabisa ajenda ya Zanzibar?

Bahati mbaya kwa wale niwaotao “Tanganyika-neo-supremacists” (wakoloni mambo leo wa Kitanganyika) ni kwamba jibu la hapa pia ni hapana. Ajenda ya Zanzibar ni kubwa na mahsusi mno kuweza kufa kifo cha kawaida kama hiki inachopangiwa kwenye Katiba Inayopendekezwa.

Kwa nini? Wanaofuatilia historia ya Muungano wanafahamu kwamba ajenda ya Zanzibar ilibebwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Kwanza Zanzibar na kiongozi wa serikali hiyo, Sheikh Abeid Amani Karume. Kupitia kwake, tunajifunza orodha ya mambo ya kutimizwa na Zanzibar yenye madaraka na mamlaka makubwa zaidi na itikadi iliyojikita kwenye utaifa wa Zanzibar. Utambulisho wetu.

Alipozimwa wiki tatu kabla ya Muungano kutimiza miaka minane, kuna waliodhani kwamba ajenda ya Zanzibar ingezimwa naye, lakini kama walivyokuja kuandika wafuasi wa chama chake cha Afro-Shirazi (ASP), kumbe kilikuwa kimezikwa kiwiliwili chake tu, bali fikra zake sahihi zingeendelea mbele daima.

Kuzimwa kwa Karume kulifuatiwa na kuunganishwa kwa ASP ya Zanzibar na Tanganyika African Union (TANU) ya Tanganyika na kuzaliwa CCM; na kisha katiba ya Mwaka 1977, ambayo inatumika sasa kuongozea Muungano. Vyote viwili, Katiba ya 1977 na CCM vilibuniwa kwa namna ambavyo lengo kuu lilikuwa ni kuidhibiti ajenda ya Zanzibar kama ilivyoelezewa kwenye Mkataba wa Muungano kwa kutumia mamlaka ya chama kushika hatamu, upande mmoja, na ukuu wa katiba, kwa upande mwengine. Lakini kwa kuwa ajenda ya Zanzibar iliyomo kwenye Mkataba wa Muungano isingeweza kuzimwa na chochote chengine – hata kwa kifo cha Karume, kwa kifo cha ASP, kwa uzawa wa CCM wala kwa uanzishwaji wa Katiba ya 1977 – Karume hakuzikwa na ajenda hiyo. Ilibakia duniani.

Ni kweli kuwa vyote viwili, CCM na Katiba ya 1977, vimekuwa vikifanya kila kile ambacho kingeliuvunja msingi wa ajenda yenyewe, lakini hilo halikuwezekana kwenye uhalisia. Badala yake, ajenda ya Zanzibar ilisonga mbele na kuja kujitokeza miaka michache baadaye chini ya Rais Aboud Jumbe Mwinyi, licha ya yeye mwenyewe kuwa muwezeshaji mkubwa wa uzawa wa CCM na Katiba ya 1977 na ambavyo vilikuja baaye kumzima mwenyewe tarehe 30 Januari 1984. Tena ajenda ya Zanzibar haikuzima pamoja naye. Ikasonga mbele.

Wakajitokeza akina Seif Sharif na wenziwe mara tu baada ya kuzimwa Jumbe. Kisha akaja Rais Salmin Amour na Awamu yake ya Tano akiwa nayo mkononi. Mageuzi makubwa yakatangazwa (ingawa si yote yaliyotekelezwa) kwenye ajenda ya Zanzibar kiuchumi na hata kisiasa. Alipoondoka, akaja Amani Karume ambaye naye akaendeleza pale walipowacha watangulizi wake, lakini akiongezea jambo jengine kubwa na muhimu sana kwenye ajenda hiyo – Maridhiano ya Wazanzibari, ambayo yalizaa baadaye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Serikali hii, kama ilivyooneshwa hapo awali, iliwahi kusimama pamoja kusimamia ajenda ya Zanzibar tangu ulipoanza mchakato wa Katiba Mpya kwa maana ya njia na lengo. Bahati mbaya, baadaye msimamo huu wa pamoja ukakhalifiwa kuhusiana na njia gani itumike kuisimamisha ajenda ya Zanzibar, lakini fahamu kwamba hitilafu hiyo haimo kwenye ajenda yenyewe – pande zote mbili zinaendelea kuamini juu ya mamlaka zaidi, madaraka zaidi na utambulisho wa Zanzibar.

Matokeo yake ni kuwa hivi sasa ajenda ya Zanzibar ina mashiko mapana na mizizi mirefu zaidi kwenye jamii ya Zanzibar kuliko ilivyowahi kuwa hapo kabla. Uungwaji mkono kwa ajenda ya Zanzibar katika kiwango cha umma wa Wazanzibari haujawahi kushuhudiwa ndani ya miaka 50 hii ya Muungano. Maana yake ni kuwa hata kama Serikali ya Zanzibar itashindwa kama taasisi moja kubwa na madhubuti kuisimamia ajenda ya Zanzibar, umma umeshatangulia kwenye hilo. Umma, kama yalivyo matakwa ya kikatiba, ndio wadhamini sasa wa ajenda hii.

Ushahidi? Hali halisi iliyopo Zanzibar miezi michache kabla ya Kura ya Maoni ya Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa 2015 ni tafauti kabisa na ilivyowahi kutokea huko nyuma.

Kwa hivyo, kwa matokeo yoyote ya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu yatakavyokuwa, kwa mara nyengine tena Serikali ya Muungano itapaswa kukabiliana uso kwa uso na ajenda ya Zanzibar. Na huenda safari hii ikakabiliana nayo kwa gharama kubwa zaidi, maana Zanzibar itakuwa inaiangalia Serikali ya Muungano moja kwa moja machoni; na sio tena mbirikimo mbele ya komanzi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.