Jumanne ya tarehe 10 Machi 2015, mke wa aliyekuwa rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, alitiwa hatiani na mahakama ya nchi hiyo kwa makosa matatu – kuhujumu usalama wa nchi, kuchafua amani na utulivu na kuandaa magenge yenye silaha baada ya uchaguzi mkuu wa Disemba 2010.

Katika uchaguzi huo, mumewe alikuwa ameshindwa na waziri mkuu wa zamani na rais wa sasa, Alassane Ouattara, lakini akakataa kuyatambua matokeo na akaamua kung’ang’ania madarakani. Ghasia zilizozuka baada ya hapo, ziliangamiza roho za watu wasiopungua 3,000 katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Simone Gbagbo, ambaye mashabiki wake walimpagaza majina ya “Iron Lady” (jina alilopewa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Bi Margareth Thatcher) au “Hillary Clinton of the Tropics”, hakuwa mtu mdogo kwenye historia ya siasa za mageuzi nchini mwake. Katika miaka ya ’70 alikosana na rais wa wakati huo, Félix Houphouët-Boigny, kwa kumkosoa hadharani, ambaye naye alikijibu kitendo hicho kwa kumtupa jela.

Simone pia hakuwa mbumbumbu kiasi hicho. Ni msomi wa historia, isimu na fasihi simulizi aliyehudumu kwenye nafasi kubwa kubwa katika vyama vya wafanyakazi, makanisa na asasi za kijamii kabla yeye na mumewe hawajaanzisha chama chao cha kisoshalisti,  Ivorian Popular Front (FPI), miaka ya ’90, ambapo yeye Simone alichaguliwa kuwa mbunge.

Lakini wakosoaji wake wanasema kadiri mwanamke huyu alivyopanda juu kwenye uluwa, ndivyo alivyozidi “kuharibika”, akiamini ana nguvu kubwa zaidi. Wengine wanasema ni Simone hasa ndiye aliyekuwa injini ya maamuzi ya mumewe, Laurent.

Na mwenyewe Simone alikuwa hafichi ukweli huo. Mwaka 2001, mwaka mmoja baada ya mumewe kuingia madarakani kwa uchaguzi uliomuengua Ouattara asiwe mgombea kwa sababu za uzawa wa mmoja wa wazazi wake mwenye asili ya Burkina Faso, Simone aliliambia jarida la kila wiki la Kifaransa, l’Express, kwamba mawaziri wote walikuwa wakimuheshimu na wakimchukulia kuwa yuko juu yao.

“Nina kile kinanichostahikia kuwa waziri. Niliingia kwenye mapambano ya kisiasa dhidi ya utawala uliopita bega kwa bega na wanaume. Nilikaa jela miezi sita, nilipigwa, nilidhalilishwa, nusura nife. Sasa baada ya majaribu yote kama hayo, ni jambo la kawaida kwamba watu hawanichezei.”

Na ni kweli kuwa hakuwa mwanamke wa kuchezea. Hata kwenye uchaguzi huo wa mwaka 2010 uliomfungisha jela, inasemekana Lauret alishakubali kushindwa na Ouattara, lakini ni Simone aliyemshikisha adabu akimuambia “hakuna ruhusa ya kuachia madaraka”. Matokeo yake, wote wawili wakalazimika kwenda kujificha katika handaki la nyumba yao, ambako baadaye walikuja kutolewa kwa aibu na hizaya na wanajeshi waliokuwa wakimuunga mkono Ouattara – Simone akiwa na gwaguro, mumewe akiwa na fulana ya ndani.

Sasa Simone anatumikia miaka yake 20 jela akiwa tayari na umri wa miaka 65, huku akitakiwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague, akaungane na mumewe, Laurent, kukabili mashitaka mengine ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Mtoto wake Simone aliyempata kwa ndoa yake ya kwanza na ambaye alimzaa nchini Ufaransa, Michel, naye pia alihukumiwa pamoja na mama yake kutumikia kifungo cha miaka mitano kwa ushiriki wake kwenye ghasia hizo hizo za baada ya uchaguzi wa 2010.

Akina Gbagbo hawakushitakiwa peke yao. Kuna wenzao 82 pamoja nao, huku waendesha mashitaka wakitaka mwenyekiti wa chama chao cha FPI, Affi N’Guessan, afungwe kwa uchache miaka miwili jela kwa sababu hiyo hiyo ya kushiriki kwenye upangaji wa machafuko.

Mkasa wa kuinuka na kuanguka kwa akina Gbagbo una mengi ya kuzingatia panapohusika hali ya Zanzibar kwenye mwaka huu wa uchaguzi. Zanzibar Daima inasema ikirejea juu ya matayarisho ya matumizi ya nguvu na hila yanayotangazwa waziwazi na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kisingizio cha kulinda Serikali ya Mapinduzi na uhalali wa Muungano. CCM haina kisisi katika kulitamka hilo hadharani.

Wengine wanaamini kuwa kauli za baadhi ya viongozi wakubwa wa chama hicho tawala kwamba watatumia vyombo vya dola kulinda nafasi yao madarakani ni kelele za debe tupu, ambazo lengo lake pekee ni kuwatia watu khofu wasijitokeze kwenye kupiga kura au wakijitokeza basi wajihisabu kisaikolojia kuwa hawataweza kukiondosha chama hicho madarakani, lakini si kweli kwamba CCM ina nia wala uwezo wa kuyatenda iyasemayo.

Wengine – mwandishi wa makala hii akiwa miongoni mwao – wanaamini kuwa hicho hasa ndicho ambacho CCM itakifanya, maana ina historia ya kukifanya. Kama Simone Gbagbo alivyoandaa makundi ya kihalifu yenye silaha kumlinda mumewe asiondoke madarakani hata baada ya kushindwa kwa kura, Zanzibar pia ina makundi ya aina hiyo, yaliyopewa mafunzo na ambayo mara kadhaa yametumika hapo kabla. Mwandishi wa makala hii alikuwa sehemu ya timu za utafiti kwa miaka 10 – kutoka mwaka 2000 hadi 2010 – na alishuhudia na kurikodi matukio mengi ya mashambulizi yaliyofanywa na vijana walioitwa Janjawidi, Unguja na Pemba.

Hivi sasa makundi hayo yamebadilishwa majina na kuitwa ‘mazombi’ au ‘masoksi’. Bahati mbaya ni kuwa matukio ya kihalifu yaliyopoteza roho za Wazanzibari kadhaa, kuwaweka vilema vya kimwili na kiakili na kuharibu mali zenye thamani kubwa ya fedha ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka 20 tangu kurudi tena kwa mfumo wa vyama vingi, hayajawahi kupatiwa nafasi ambayo matukio ya Ivory Coast yamepatiwa ndani na nje ya nchi hiyo. Yumkini kheri ya kupatikana kwa Maridhiano ya Wazanzibari na Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyafukia hayo kwenye shimo la sahau na msamaha.

Lakini kinachosahauliwa na wana-CCM, ambao wanaowekeza kwenye yale yale yaliyowahi kutokea huko nyuma, ni kwamba kila leo ina kesho – na kesho hiyo inaweza sana ikawa kesho ya akina Gbagbo. Wala hapa tusizungumzie kesho ya waandaaji wa uhalifu dhidi ya ubinaadamu visiwani Zanzibar kwenye kizimba cha ICC, mjini The Hague. Huko ni mbali na kuna nahau nyingi. Mojawapo ni kile kinachoonekana kuwa ni upinzani kwa dhati na uadilifu wa mahakama hiyo ya “Kizungu” dhidi ya viongozi wa mataifa ya Kiafrika, na pia mchakato wa kufikishana huko lazima ushirikishe serikali kuu ya Muungano, ambayo yenyewe ni mmoja wa wahusika wa uovu unaotajwa hapa.

Hapa tuzungumzie tu kile kile ambacho kimetokea ndani ya Ivory Coast – taifa la Kiafrika, mahakama za Kiafrika na utawala wa Kiafrika. Kesho hiyo haijaiahidi Zanzibar kwamba haitafika milele eti kwa sababu tu uhalisia wa kijinchi kiduchu cha Zanzibar iliyo kwenye Muungano na ‘Jitanganyika’ kubwa ni tafauti na Ivory Coast inayojitegemea kwa kila kitu.
Hapana. Madhali Zanzibar ina leo, basi lazima itakuwa na kesho yake, na chembilecho Dk. Salmin Amour, rais wa awamu ya tano ya Zanzibar: “Mambo yana zama na zamu!”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.