Wakati Rais Nicolae Ceauşescu wa Romania alipokuwa anakaribia kilele cha anguko lake, alimuita waziri wake wa ulinzi, Vasile Milea, kumtaka ampe tathmini ya kweli, bila kumficha chochote, juu ya nguvu halisi za jeshi mbele ya upinzani ambao ulikwishavuuka mipaka ya kudhibitika. Swali hasa alilomuuliza ni ikiwa kwa hali ilivyo, inaweza kulichukua jeshi siku ngapi za ziada kumlinda?

Lakini Milea, ambaye siku chache baada ya mkutano huo na Ceauşescu alikutikana ofisini mwake “amejiua” kwa kujipiga risasi karibu na moyo, hakuwa mkweli kwa Ceauşescu, kama ambavyo hutokea mara kadhaa kwa wasaidizi wa watawala makatili. Akampa takwimu za uongo juu ya nguvu, silaha na idadi ya wanajeshi waliokuwa wamebakia upande wa mtawala anayeanguka.

Ceauşescu alimteua Victor Stănculescu kuchukuwa nafasi ya Mile.  Stănculescu akaikubali nafasi hiyo kwa shingo upande na matokeo yake akafanya kila kile kilicho kinyume na bosi wake na hivyo akachochea anguko la Ceauşescu badala ya kumsaidia kuendelea kusalia madarakani.

Kwa mfano, aliwaamuru wanajeshi kurejea makambini na sio kuwashambulia waandamanaji ambao walikuwa wakiyavamia makao makuu ya Chama cha Kimomunisti, badala yake akamshauri Ceauşescu na mkewe Elena kukimbia kwa helikopta na hivyo kumgeuza “kiongozi anayewakimbia watu wake” na sio anayesimama akawaongoza.

Baadaye, mwenyewe Stănculescu alikuja kukiri kwamba wakati huo ni kama kwamba alikuwa anapokea amri mbili kwa wakati mmoja – moja kutoka kwa Ceauşescu aliyekuwa akipigania utawala wake usiporomoke na nyengine kutoka kwa umma uliokuwa umechokana naye. Akachagua kufuata amri ya umma.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 visiwani Zanzibar ni kama kwamba tayari mstari umeshachorwa na pande zote mbili zenye nguvu za kisiasa. Kwa upande wao,  watawala wameshaamua wapi lilipo chaguo lao na, kwa upande mwengine, wananchi nao wameshaamua la kwao.

Mstari huo unaochorwa kati ya pande mbili zinazoongoza Serikali moja ya Umoja wa Kitaifa una maana kubwa sana kwa mwenendo wa mambo ndani ya Tanzania nzima kwa ujumla na sio kwa Zanzibar peke yake.

Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndicho mshirika mkuu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa – na hivyo ndicho chenye nguvu ya kikatiba kuongoza kwa sera na programu yake – kimeamua kung’ang’ania bunduki, vifaru na mizinga. Kila siku iendayo kwa Mungu kinasema wazi kuwa kinategemea njia hiyo moja tu kusalia kuongoza nchi – yaani nguvu za vyombo vya dola na mawakala wao.

Sifa moja ya CCM ni kuwa haisemi hayo kwa uficho wala kwa mafumbo. Kinasema hivyo kwa uwazi na ufasaha wa hali ya juu kupitia ngazi zake zote za uongozi – wa chini, kati na hata wa juu.

Msikilize Asha Bakari Mtama, kwa mfano, ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM ngazi ya taifa, akirejelea kauli ile ile ya kila siku kuwa serikali ya Zanzibar ilitokana na Mapinduzi  na hivyo haitapatikana kwa kupiga kura.

“…. nasema na nitarudia tena na siogopi kusema serikali hii ni ya kimapinduzi sio ya mchezo. Hawawezi, hawawezi, hawawezi kutupindua.”

Kauli hiyo aliitoa kwenye mkutano wa hadhara wa mikoa miwili ya kisiwani Pemba mapema mwaka 2014, lakini hapo hapakuwa pa mwanzo wala pa mwisho; wala haisemi peke yake kiasi cha kusema inatolewa na kiongozi mmoja asiye na maana.

Kauli kama hii ameshaitoa mwahala mwingi, mukiwemo kwenye Bunge Maalum la Katiba mbele ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta.

Kauli kama hii pia hurejelewa kwenye mikutano mengine kadhaa ya CCM, hasa visiwani Zanzibar. Marehemu Salmin Awadh, aliyekuwa mwakilishi wa jimbo la Magomeni  na mnadhimu mkuu wa CCM, aliwahi kufika umbali wa kusema kwamba vifaru vya jeshi vitatumika kuilinda CCM madarakani.

“Sasa wao (wapinzani) kama wana ubavu, basi wachukuwe (serikali). Lakini hatutotoa (madaraka ya kuongoza serikali) kwa kura. Mutapiga kura katika chaguzi zote, na Chama cha Mapinduzi kitashinda.”

Hakuna kiongozi yeyote wa juu wa CCM, si wa Zanzibar wala wa Tanzania Bara, aliyewahi kujitokeza kuwakemea wana-CCM hawa wanaoyasema haya majukwaani, na kwa hakika mara kadhaa huwa yanasemwa mbele yao, akiwamo Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana. Hilo linasema ukweli mmoja tu – CCM kwa ujumla wake imeshaamua kuhisabu mizinga yake kujilindia madaraka yake visiwani Zanzibar.

Kinyume chake ni pale unapofuatilia mikutano ya hadhara ya mshirika mdogo kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo, Chama cha Wananchi (CUF), ambayo imejikita kwenye kuutayarisha umma kwa kile inachokiita chama hicho “Mwaka wa Maamuzi” 2015.

Humo huambiwa watu wajitokeze kwa wingi kwenye kujiandikisha kupiga kura. Kwamba wasichoke kukabiliana na vikwazo vya kupata haki yao hiyo kutoka kwa masheha, ambao sasa chama hicho kinasema kitawapeleka mahakamani kwa kuwazuia Wazanzibari wenye haki kupata vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Humo unasikia umma ukiambiwa kuwa muda wa CCM kusema hawatowi serikali na wasitowe kweli umepita, kwani zama za mageuzi hazizuiliki. Wanatayarishwa kuitetea na kuilinda Zanzibar kwa kura zao na kuiamini kura kuwa ndio njia pekee ya kupata madaraka ya nchi.

Ni bahati mbaya sana kwamba bado CCM makao makuu Chimwaga inadhani kuwa njia pekee ya kuidhibiti Zanzibar ni kupitia khofu na wasiwasi miongoni mwa raia, na kwamba hilo litakuwa na athari kwa Zanzibar pekee katika wakati ambapo upinzani dhidi ya CCM hiyo hiyo ni mkubwa zaidi pia huko Bara, huku ukisaidiwa sana na kashfa za kifisadi na ukosefu wa usalama.

Lakini bahati mbaya zaidi ni kwa kwa wana-CCM ndani ya Zanzibar yenyewe ambao hawajang’amua kuwa anguko la Ceauşescu wa Romania linawanyemelea na wao.

Hikima ya kujifunza inawataka wauangalie uhalisia. Vifaru vinaendeshwa na watu. Mizinga inafyatuliwa na watu. Na ni watu pia wanaodai mabadiliko.

One thought on “Mtawala anayeanguka huhisabu vifaru na mizinga”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.