Tarehe 7 Machi 1965, mamia ya Wamarekani weusi na weupe wenye msimamo wa haki sawa kwa raia wote wa taifa hilo walikusanyika kwenye kitongoji kiitwacho Selma katika jimbo la Alabama nchini Marekani kwa nia ya kuandamana hadi makao makuu ya jimbo hilo Montgomery kwa lengo la kupigania haki ya Mmarekani Mweusi kutumia haki yake ya kikatiba ya kupiga kura.

Mfumo uliokuwapo Marekani wakati huo ulikuwa unawazuwia Wamarekani weusi kutumia haki hiyo, ingawa ilishawekwa kwenye katiba ya nchi takribani miaka 100 nyuma kupitia kile kiitwacho Marekebisho ya 15 ya Katiba ya Marekani. Lakini wakati wanafika kwenye Daraja la Edmud Pettus, vyombo vya usalama vikawashambulia na kuwajeruhi vibaya wengi wao.

Siku mbili baadaye, mpigania haki Dk. Martin Luther King, akawakusanya watu wengine wapatao 2,500 kurudi tena kwenye Daraja la Edmund Pettus kabla ya kugeuza na kurejea nyuma kwa kuheshimu amri ya mahakama iliyowazuia kufanya maandamano kamili.

Tarehe 21 Machi, waandamanaji wanaokisiwa kufikia 25,000 wakaungana kuelekea Montgomery na wakafanikiwa kuingia kwenye mji huo mkuu wa Alabama. Siku nne baadaye, waandamanaji hao wakaingia kwenye lango la makao makuu ya serikali ya Alabama wakiwa wamesaini barua dhidi ya Gavana George Wallace.

Miezi michache baadaye, bunge la Marekani (Congress) likapitisha mswaada wa Sheria ya Haki ya Kupiga Kura ambayo rais wa wakati huo, Lyndon B. Johnson, aliisaini kuwa sheria kamili tarehe 6 Agosti 1965. Sheria hiyo ilikusudiwa kuondosha vikwazo ambavyo aliwekewa Mmarekani mweusi katika ngazi zote – tangu serikali za mitaa hadi majimbo – kumzuia kutumia haki yake ya kupiga kura akiwa kama raia na kama anavyopewa haki hiyo na katiba karne nzima nyuma.

Mkasa huu maarufu kama Maandamano ya Selma kwenda Montgomery umesimuliwa leo tarehe 7 Machi 2015 kwa muhtasari kwenye mtandao wa Ikulu ya Marekani, White House.

Hapa nimeukariri na kuutafsiri kwa lengo maalum la kueleza mshabihiano baina ya Marekani ya miaka 50 nyuma na Zanzibar ya leo kwa kutumia hadithi yangu binafsi. Nitaisimulia.

Uchaguzi wa kwanza kabisa wa vyama vingi tangu baada ya Mapinduzi ya 1964 uliofanyika Zanzibar mwaka 1995, ulinikuta nikiwa na miaka 18 na nikiwa kijijini kwetu nilikozaliwa na kukulia kisiwani Pemba. Huo ndio uchaguzi pekee nilioweza kupiga kura hadi sasa. Chaguzi nyengine mbili – ule wa 2000 na 2005 nilizuiwa na masheha – na uchaguzi wa 2010 ulifanyika nikiwa sipo tena Zanzibar.  Hapo katikati yake pia palifanyika upigaji kura mara mbili, ambao pia sikuruhusiwa na masheha. Nitafafanua.

Uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 ulinikuta kisiwani Unguja, ambako nilihamia tangu mwaka 1996 kwa ajili ya masomo. Nilianza maisha nikiwa dakhalia ya Tumekuja, kisha nikachukuliwa na jamaa yangu kukaa naye Mkunazini, kisha nikahamia Mtendeni. Mote humo muna shehia tafauti, ingawa ni jimbo moja kwa sasa.

Kwa hivyo wakati uchaguzi unakuja, nilikuwa nimeshahama na kuhamia shehia tatu ndani ya kipindi cha miaka minne. Licha ya kwamba kila nilipohama na kuhamia nilichukuwa barua ya sheha mmoja kwenda kwa mwengine, hakuna sheha aliyenikubali kuwa mimi ni mkaazi wake kwa kipindi nilichotakiwa kujiandikisha kupiga kura.

Kama ilivyokuwa kwa Mmarekani mweusi wa kabla ya mwaka 1965, ndivyo ilivyokuwa kwangu. Katiba ya nchi inaniruhusu kupiga kura, lakini kuna kanuni na sheria za kuwa mpigakura zinazosimamiwa na mamlaka za kati na chini, ambazo zilinizuwia kupiga kura.

Baina ya mwaka 2001 na 2003 niliishi shehia ya Mpendae na uchaguzi wa 2005 ulifanyika nikiwa mkaazi wa kudumu wa shehia ya Kibweni, ambako hadi leo ndipo yalipo maskani yangu, lakini nilikuwa nimehamia hapo mwanzoni mwa mwaka 2004. Si sheha Haji Seti wa Mpendae wala Bi Asha wa Kibweni waliokuwa tayari kunipa haki yangu ya kupiga kura. Kwa wote wawili, mimi sikuwa na sifa za kutosha kuwa mpiga kura.

Hata kura ya maoni ya mwaka 2010, ambayo ilinikuta nikiwa mkaazi wa kudumu wa shehia ya Kibweni kwa miaka sita, hali ilikuwa hiyo hiyo. Sheha alisema hajui ikiwa kwenye nyumba Na. SK/108 munakaa watu, na kama wanakaa hajui ikiwa jina langu ni miongoni mwa yaliyomo kwenye daftari lake. Nyumba hiyo niliijenga kwa jasho langu na katika kila hatua ya ujenzi wake ilipatiwa na ililipiwa vibali vya serikali.

Miradi na shughuli nyengine zote za kiserikali huwa inahusishwa  kama vile kampeni ya kupambana na malaria, sensa na nyenginezo. Watoto wangu wanne walizaliwa kwenye nyumba hiyo baina ya mwaka 2004 na 2010. Lakini baba yao hakuwahi kustahiki kuwa mpigakura halali kwa mujibu wa sheha na nguvu alizopewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mwaka jana katika nchi hii niliyopo sasa palikuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na mabaraza ya miji. Siku moja nimerudi nyumbani kwangu kutoka kazini, nikakuta barua kutoka baraza la mji wa Bonn ikiniarifu kwamba kuna kampeni za uchaguzi wa vyama zinafanyika na ikiwa ningependelea kushiriki.

Siku nyengine nikakuta barua kutoka kwa wagombea mbalimbali wakinishawishi kuwapigia kura. Siku nyengine nikakuta karatasi ya kura imetumwa na jina la kituo ninachoweza kupiga kura, tarehe na saa kwa ajili ya kumchagua mwakilishi wangu kwenye baraza la mji ambaye atatetea maslahi ya kundi langu la wahamiaji. Nikamuonesha mke wangu barua. Hatukuweza kujizuwia. Mimi na yeye, sote kama tumeambiana tukajikuta tunalia. Machozi hayakauki.

Nchi iliyonizaa na kunilea kwa miaka 33 ya uhai wangu ilininyima haki yangu ya kikatiba ya kupiga kura takribani mara nne ndani ya kipindi cha miaka 15. Nchi niliyohamia kwa dharura ya miaka michache, inanipa haki hiyo ndani ya kipindi cha miaka minne.

Zanzibar sasa inaelekea kwenye uchaguzi mwengine mkuu. Ni bahati mbaya kwamba sipo ndani ya nchi, lakini kwa hakika kabisa ningelirejea tena kituoni kwenda kujiandikisha, hata kama sheha wangu angelisimama tena kunipinga. Na najua siko wala nisingelikuwa peke yangu.

Wa Selma waliandamana watu wasiofikia 1,000 tarehe 7 Machi 1965. Waliposhambuliwa na vyombo vya dola, wakarudi wiki moja baadaye wakiwa 2,500. Walipozuiwa na mahakama, wakarudi wiki mbili baadaye wakiwa 25,000. Miezi michache baadaye, wakaibadilisha historia nzima ya Marekani panapohusika haki ya Mmarekani Mweusi kupiga kura. Wazanzibari wanaweza kufanya hivyo hivyo panapohusika haki yao hiyo ya kupiga kura.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.