JANUARI 1984, Halmashauri Kuu [NEC] ya Chama Cha Mapinduzi [CCM] iliyoketi kwa dharura mjini Dodoma, ilimvua Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, nyadhifa zote za chama na serikali, Visiwani na kwenye Serikali ya Muungano kwa “dhambi” ya kuhoji muundo upi wa Muungano uliokusudiwa; na kwa kuandaa hati ya mashitaka kutaka Mahakama Maalum ya Katiba itoe tafsiri na uamuzi juu ya utata huo.

Kutekeleza hilo, Jumbe alitumia ibara ya 125 na 126 ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1977, ambazo zinaipa uwezo na mamlaka Mahakama hiyo “kusikiliza shauri lililotolewa mbele yake na kutoa uamuzi wa usuluhishi juu ya jambo lolote, iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar”.
Na Joseph Mihangwa
Na Joseph Mihangwa

Nyadhifa alizovuliwa kwa kujaribu kukanyaga “patakatifu” hapo bila kuvua viatu, ni pamoja na Urais na Uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; Umakamu Mwenyekiti wa CCM na Ujumbe wa NEC na Kamati Kuu ya CCM.

Sababu za kuitishwa kikao hicho cha dharura, ilikuwa ni kufuatia kuibwa kwa Hati hiyo ya Mashitaka iliyoandaliwa kwa niaba ya Jumbe, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar wa wakati huo, Abubakar Swanzy na kufikishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Nyerere kabla Jumbe hajaitia sahihi, ambapo inanong’onwa kwamba Seif Shariff Hamad, alikuwa mmoja wa waliofanikisha kuibwa kwa Hati hiyo na kumfikia Mwalimu. Hamad aliwahi kuwa mwanafunzi wa Jumbe wakati akisoma elimu ya sekondari katika skuli ya Lumumba.
Kufuatia kutunguliwa kwa Aboud Jumbe, Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa Rais wa awamu ya tatu Zanzibar, kuchukua nafasi ya Jumbe; na Seif Shariff Hamad akapaa kwa kuteuliwa kuwa Waziri Kiongozi kuchukua nafasi ya Brigedia Ramadhan Haji, aliyetunguliwa pamoja na Jumbe.
Uongozi Visiwani chini ya Mwinyi na Hamad ulikonga roho za wengi, Bara na Visiwani, kwa sera zake za uwazi na katika nyanja za kufufua uchumi na kuanzisha sera na soko huria, zilizomkera Mwalimu Nyerere kwa hofu ya kuuwa “ujamaa”.
Hata hivyo, furaha hiyo haikudumu baada ya Mwinyi kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa Muungano miezi 18 baadaye, kufuatia kustaafu [kung’atuka] kwa Rais Nyerere.
Kutunguliwa kwa Jumbe na Ramadhan Haji kulizua taharuki, kutoelewana na kuzua makundi miongoni mwa Uongozi wa Zanzibar, huku kundi moja, lililojiita “Liberators” [Wakombozi] na wahafidhina wa sera za hayati Karume wakijiona pia kama wamiliki wa Zanzibar, likiona Jumbe kaonewa; na kundi la pili la “wenye maono” ya Zanzibar mpya, lililojiita “Frontliners” [Wanamstari wa mbele], akiwamo Seif Shariff Hamad, likiona hatua iliyochukuliwa na NEC ilikuwa sahihi katika kuimarisha Muungano.
Kufuatia kupendekezwa kwa Mwinyi kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, nafasi ya Rais Visiwani ilibaki wazi; na katika kikao cha uteuzi, “Wakombozi” walitaja kwa kelele na nderemo jina la aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Abdul Wakil Nombe; ambapo wanamstari wa mbele walimtaja Hamad kwenye kikao cha Kamati Kuu [CC] cha uteuzi na majina kupelekwa NEC kupigiwa kura, ambapo Wakil alimshinda Hamad kwa tofauti ndogo ya kura saba tu kati ya wajumbe 1,746 wa NEC waliopiga kura siku hiyo, Agosti 15, 1985.
Hata hivyo, taarifa za Ki-intelijensia zilitoa nafasi ndogo kwa Wakil kuweza kupata asilimia 50 ya kura katika Uchaguzi Mkuu ambapo bila hivyo chama kingelazimika kuteua mgombea mwingine, hatua ambayo ingekipotezea sifa na heshima kama chama cha kidemokrasia ya kweli.
Kuokoa jahazi, kiliitishwa kikao cha Kamati Kuu [CC] ya chama kwa agenda moja tu: “Hali na matarajio ya Uchaguzi wa Rais Visiwani”. Mwalimu, huku akinukuu taarifa hizo za ki-intelijensia, aliwatahadharisha wajumbe kwamba, huenda Wakil asingeweza kupata asilimia 50 ya kura inayotakiwa kushinda katika uchaguzi.
Seif Sharrif Hamad alisikika baadaye akisema, kwa Wakil kukubali kuwania nafasi hiyo, alikuwa anapiga ngumi ukutani. Akabainisha kwamba, Mwalimu na Mwinyi walimwita yeye mara tatu kumtaka ampigie kampeni Wakil, hasa huko Pemba; akaona ilikuwa ni kazi ngumu kumuuza na isiyowezekana.
Alisema, ingawa aliitika wito wa CC kugombea Urais wa Zanzibar kushindana na Wakil, baadhi ya wajumbe wa NEC [akiwamo Salmin Amour] waliojiita “Washindi” – [Wakombozi], na yeye kumwita “Mchakazwa”, hawakuonesha nia njema na maridhiano kwa manufaa ya Zanzibar na Muungano, huku wakijigamba kwamba, walimweka Wakil kugombea ili “kuipindua Serikali ya Awamu ya tatu”, kwa maana ya Mwinyi na Hamad, na ili Zanzibar iweze kutawaliwa kwa staili ya ASP badala ya staili ya CCM.
Ni Abdallah Natepe aliyetafsiri hadharani kuwa hivyo ndivyo ilivyotakiwa, akisema: “Mapinduzi ya 1964 yalikusudia kumkomboa Mwafrika Mweusi; lakini Serikali ya Mwinyi na CCM Visiwani inataka kuturejesha utumwani.
Akaongeza akisema: “Siwezi kukubaliana na mwanachama yeyote wa zamani wa Zanzibar Nationalist Party [ZNP], Zanzibar and Pemba Peoples Party [ZPPP] au Umma Party [UP], kwa sababu hawa ni maadui wanaotaka kulipa kisasi dhidi yaASP”.
Ilikuwa wazi kuwa Natepe alikuwa anasumbuliwa na mzimu wa watu wa kale ASP; ZNP na UP.
Nyerere, huku akionesha kuchukizwa dhahiri na kauli ya Natepe, alimwambia kwa ukali: “Najua, wewe ni kiongozi [ring leader] wa njama hizi; una kundi lako, najua!.Lakini elewa kwamba, nchi hii ni ya Watanzania wote; ubaguzi na udikteta wa kale hauwezi kuvumilika; chunga ulimi wako!”.
Kisha Mwinyi akaingia kuokoa jahazi alipomshambulia Natepe kwa maneno makali kwa kuendekeza na kuendesha ubaguzi wa rangi. Na katika hotuba yake ya kufunga kikao Nyerere alipoza moto kwa kusema: “Nataka muelewe kwamba, nawaelewa vizuri vijana hawa [Frontliners]; ni vijana wakweli, wasiovumilia wala kuishi kwa majungu, uzushi na ubaguzi; sio wasaliti. Sitavumilia kuona wakitendewa kama maadui ndani ya nchi yao”.
Lakini Ali Mzee wa kambi ya Natepe alikuwa jasiri vya kutosha kuomba maridhiano ili mambo yaishe, na kwamba, Chama katika ujumla wake, kimuunge mkono Wakil. Kwa uamuzi huo, iliazimiwa kuundwe kikosi cha kampeni kumsaidia Wakil, kilichojumuisha Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Rashid Kawawa, Salim Ahmed Salim na Seif Shariff Hamad.
Katika mikutano yote ya hadhara, viongozi hao watano walilaani kundi la “Wakombozi” [Liberators] kwa kuwaita wanafiki na wachochezi; huku Kawawa na Mwinyi wakiwahakikishia Wazanzibari kwamba ni sera za CCM pekee ndizo zitakazowaongoza Wazanzibari, na kwamba ASP kilishakufa; kwamba wale wote wanaoishi kwa kuongozwa na mzimu wa ASP [Liberators] ni maadui wa Wazanzibari na wa Muungano, wanaotaka kuirejesha Zanzibar kwenye enzi za udikteta wa ASP.
Mwalimu kwa upande wake, aliwashambulia kambi ya “Liberators” akisema: “Msiwasikilize hao, ni watu mfilisi kisiasa; ni masalia ya udikteta wa kale katika Zanzibar huru inayosonga mbele”, wakataeni, hawafai”.
Na pale matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar yalipotangazwa, Oktoba 1985, Wakil alikuwa amepita kwa ushindi duni wa asilimia 58.6 ya kura zilizopigwa, huku wengi wa wagombea wa Baraza la Wawakilishi wa mrengo wa “Liberators” wakiwa wameshindwa vibaya.
Mwinyi alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na Wakil akajaza nafasi ya Rais wa Zanzibar;Seif Shariff Hamad akabakia Waziri Kiongozi, pengine kama suluhisho la Wakil kwa kambi mbili hasimu,ya “Liberators” na “Frontliners”.
Visiwani, migogoro ya kisiasa haiishi, tangu harakati za kupigania uhuru miaka ya 1950 hadi sasa. Hivyo, vita ya kupigania ukuu ndani ya CCM kati ya makundi hasimu ya “Liberators” na “Frontliners” ilivaa sura mpya baada ya baadhi ya “Frontliners” kubadili kambi kwa kujiunga na kambi ya “Liberators”.Baadhi ya hao walikuwa ni Adam Mwakanjuki, Isaac Sepetu na Ali Ameir. Kambi ya “Frontliners” ilidhoofu na kuvunjika moyo.
Pigo zaidi kwa kambi hiyo lilikuja pale kundi la “Liberators” lilipoanzisha kampeni dhidi ya Dk. Salim Ahmed Salim ingawa hakuwa na mahusiano ya moja kwa moja na “Frontliners”; kukaibuka vita ya kutafuta “mchawi” na hasira kutawala kwenye mikutano mingi; huku kila kundi likitafuta mbinu za kulipa kisasi kwa uhasama wa kale.
Hatimaye kundi la “Liberators” ambao walikuwa wengi kwenye NEC ya CCM liliibuka washindi. Hii ilikuwa dhahiri kwenye uchaguzi waNEC, ambapo Seif Shariff Hamad alipita kwa mbinde kuwa Mjumbe wa NEC, lakini akapoteza nafasi ya Ujumbe wa Kamati Kuu [CC], kuashiria kuanza kwake kuwekwa pembeni kwa nafasi za Chama na Serikali.
Mara Wakil akavunja Serikali ya Zanzibar lakini bila kuvunja Baraza la Wawakilishi;na wakati huohuo akawateua Makatibu Wakuu wa Wizara kusimamia na kuongoza shughuli za Serikali. Na alipoteua Baraza jipya la Mawaziri, Hamad na wenzake wa kambi ya “Frontliners”, walipoteza nafasi zao. Seif Sharrif Hamad akawa ametunguliwa Zanzibar.
Kana kwamba hilo halikutosha, mwaka mmoja baadaye, kikao cha CCM kiliitishwa Kizota, Dodoma ambapo Hamad, Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid na wengine, walifukuzwa kwenye chama na hivyo kukamilisha anguko la kishindo la Hamad na wenzake hao.
Kwa kufanya hivyo, CCM kilidhani kundi hilo limekatwa miguu na ulimi, kwamba sasa kingeweza kuendesha mambo yake kwa amani na utulivu, lakini ukweli ilikuwa ni kinyume chake kwa sababu kitendo hicho kiliwafanya waungane na kujipanga upya kuweza kutoa upinzani mkubwa nje ya Chama na Serikali.
Muungano wa kundi hili lililoonekana kama “Wasaliti” wa chama, lilitia hofu kwa Serikali dhaifu Visiwani na kusababisha Hamad na wenzake kukamatwa na kutiwa kizuizini, kisha wakashtakiwa kwa kosa la uhaini, la kutaka kupindua Serikali ya Zanzibar.
Na baada ya milolongo mirefu ya kisheria, hatimaye Hamad na wenzake waliachiwa huru na Mahakama kwa hoja kwamba tuhuma za kutakakupindua Serikali zilikuwa hazina mashiko kwa sababu Zanzibar si nchi wala dola inayoweza kupinduliwa.
Kutiwa kizuizini kwa Hamad na kundi lake hakukuwaogofya, badala yake kuliwakomaza kisiasa kuwa wanamageuzi waliokubuhu. Kwa ujasiri mkubwa na kujiamini, walianzisha Umoja wa upinzani wa chini kwa chini uliojulikana kama “Kamati ya Mwelekeo wa Vyama huru” – KAMAHURU; kwa lengo la kuimarisha demokrasia kisiasa Visiwani. Kufikia hapo, upepo wa kisiasa ukaanza kuvuma kuelekea kwao.
KAMAHURU kilibadili jina na kuitwa “Zanziabar United Front” [ZUF], Chama ambacho kufuatia kufunguliwa milango kwa Vyama vingi nchini, ZUFkiliungana na Chama cha Bara kilichoitwa “Chama cha Wananchi” [CCW],Mei 1992, kuunda Chama kipya kijulikanacho kama “Civic United Front” [CUF], na Mwenyekiti wake wa kwanza alikuwa James Mapalala na kufuatiwa na Musobi Mageni; wakati wote huo Hamad akiwa Makamu Mwenyekiti na Shaaban Mloo, Katibu Mkuu, nafasi ambayo sasa inashikiliwa na Hamad.
Kufurukuta kwa Seif Shariff Hamad kutoka Waziri wa Elimu Visiwani mwaka 1977 hadi kuwa Waziri Kiongozi na kutunguliwa mwaka 1985; na kutoka “Haini” na Habusu kwa miezi 30, hadi Kiongozi wa Chama cha upinzani [CUF] chenye nguvu na yeye kushika nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, ni safari ndefu yenye mabonde na milima inayohitaji ujasiri na moyo wa aina yake.
Kwa namna siasa za upinzani zinavyoenda Visiwani, inatukumbusha mitafaruku na uhasama wa kale, kati ya Vyama vya “Zanzibar Nationalist Party” [ZNP] na ASP; ambapo CUF kinaonekana kuchukua nafasi ya ZNPtofauti tu kwamba CUF ni cha kitaifa [Tanzania], na CCM kuchukua nafasi ya ASP. Ilivyo huko Visiwani, CCM Zanzibar ni tofauti na CCM Bara; na vivyo hivyo CUF Zanzibar na CUF Bara, kwa sababu ya tamaduni na mazingira tofauti ya kisiasa.
Ni Rais wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume, wakati akiteta na Hamad, aliuliza: “Mwenzangu, hadi lini nchi yetu [Zanzibar], tutaiongoza kwa misingi ya historia ya uhasama wa kisiasa wa kale? Tunataka tuwarithishe nini watoto [wetu] wa Kizanzibari chini ya uhasama huu?”.
Majibu ya maswali haya ndiyo yaliyozaa wazo la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa [SUK] Visiwani, ambayo Hamad ni Makamu wa kwanza wa Rais.Na kwa sababu hiyo, huenda busara za Karume na Hamad, zimekuwa chachu na sehemu ya suluhisho la siasa za uhasama zilizoigawa jamii ya Kizanzibari kwa miaka mingi.
Je, sasa tuamini kwamba, kitendo cha baadhi ya wafuasi wa CUF, cha kupeperusha bendera za ASP kwenye mikutano yao, ni wito wa Chama hicho kwa Wazanzibari kuungana chini ya nembo ya Uhuru wa Zanzibar kwa ajili ya Wazanzibari, bila kujali itikadi zao za kisiasa?
Lakini, swali lingine la kujiuliza ni hili; Wanaungana dhidi ya nani?

One thought on “Kupaa, kutunguliwa na kupaa tena kwa Seif Shariff Hamad Zanzibar”

  1. Kwa mifumo wa taarifa ilivyo, zaidi miaka ya 1980, hamadi huyu tunaemuona huwezi kumzuia na urais na mapambano yake katika siasa za Tanzania hazina mbadala, hakuna mwenye kifua cha kumzuia hamad.
    Pili kwa mfumo wa taarifa kama kundi la liberators ilikuwa ni kupata Zanzibar huru na kujenga misingi ya Asp ambao ndio vinara wa ccm ya unguja, na sera za cuf kwa kiongozi hamadi hazipishani na asp sasa wapi tunatofautiana, kama utachunguuza utakuta ccm. Wa Zanzibar wanahitaji asp yao na cuf nchi yao na kwa mfumo huu huwezi mtenganisha mansour na cuf na wito wa mapinduzi pia unafaa kuwa wito wa cuf mana haujatoa ladha ya zamira ya asp Kwa mapinduzi ya Zanzibar

    Sasa hawa ccm unguja na Pemba ni kina nani mana liberators na frontliners wamejigita kwenye Zanzibar mpya na uhalali wa mapinduzi akiweno mh mansour, sasa tunapishana wapi? Ni dhahiri ccm Wa zenj c wa zenj ni wageni Wa visiwa, ni halali kabisa bendera za asp kupeperushwa kwenye mikutano ya cuf, na ndio mana ikipata cuf tumepata sote.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.