Licha ya mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, kunukuliwa mara kadhaa akisema kuwa ni yeye aliyependekeza wazo la mfumo uliopo sasa wa serikali mbili, huku mwenzake wa Zanzibar, Sheikh Abeid Karume, akiwa amependekeza wa serikali moja, inafahamika kuwa ni yeye Nyerere ndiye aliyekuwa na dira ya Tanzania moja, yenye chama kimoja na serikali moja.

Joseph Sinde Warioba, aliyekuwa waziri wa sheria, mwanasheria mkuu na katibu mkuu wa kamati ya ulinzi na usalama anasema:

“Mwalimu Nyerere alikuwa anaona serikali mbili kuelekea moja. Alisema itachukuwa muda mrefu lakini twende moja. Yeye hakuwa na mawazo ya kwenda serikali tatu, (bali nia yake) yeye ilikuwa ni kwenda moja.”

Kwa nafasi alizokuwa nazo, Jaji Warioba alikuwa ndiye mshauri mkuu wa masuala ya kisheria wa Mwalimu Nyerere.

Mwalimu Nyerere aliondoka duniani kabla ya kuiona Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikivunjwa rasmi kivitendo, huku Chama chake cha Mapinduzi (CCM) alichokiasisi kikishindwa kuitamka ndoto hiyo waziwazi. Aliondoka akiuwacha woga wa kuitetea ndoto yake hiyo, kama vile ambavyo alishuhudia woga wa kulitetea Azimio la Arusha miongoni mwa wana-CCM wenyewe.

Lakini je, hilo linamaanisha kwamba ndoto hiyo hawaiishi? Hapana. Ukimsikiliza Jaji Warioba kwenye vidio ya hapo juu, na kuuangalia uhalisia wa mambo kwenye mwenendo wa siasa za Muungano, utapata jibu kwamba CCM iliamua kuiishi ndoto hiyo kimya kimya, yumkini kwa kutumia sera ya “Tenda Usinene” (Do, Don’t Tell).

“…mawazo ya Mwalimu (Nyerere) – na ambayo yalikuwa very clear (wazi kabisa) – ilikuwa ni kwenda (kwenye serikali moja) lakini muende pole pole, muanze mambo 11, mtaongeza (kidogo kidogo) mpaka siku moja mambo yote ya Zanzibar yatakuwa yameingia kwenye Muungano,” anasema Jaji Warioba.

Na, naam, Orodha ya Mambo ya Muungano ndani ya nusu karne ilishaongezeka zaidi ya mara mbili – kutoka 11 ya awali hadi makontena 22 – kwa kutumia msamiati wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud, ambayo ukiyapakua utapata megine zaidi ya 22.

Kwa mfano, jambo la 12 kuongezwa linasomeka kama ifuatavyo: “Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yoyote halali (pamoja na noti); mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni”, lakini ndani ya “kontena” hili moja, muna mambo manne kama si zaidi: (i) sarafu, (ii) fedha, (iii) mabenki na shughuli zake, na (iv) fedha za kigeni na usimamizi wake.

Kwa hivyo, la kwenda taratibu kwa kuchukuwa jambo moja moja hadi hatimaye mambo yote ya Zanzibar yajikute kwenye kapu moja la Muungano, ndio mwendo ambao CCM imekuwa ikiufuata tangu mwaka 1964. Nalo limechangiwa na sera iliyojificha ya siasa za Muungano kuelekea Zanzibar, ambayo inasema: “Muungano imara unahitaji Zanzibar dhaifu.” Kuidhoofisha Zanzibar ndiko huko kuinyang’anya kila lake na kila chake, na kuuimarisha Muungano ni kuipa kila kile kilichokuwa cha Zanzibar.

Lakini bahati mbaya pekee kwa Mwalimu Nyerere ni kuwa alizipiga vibaya hisabu zake za kisiasa kwenye hili na kwa hivyo akafanya makosa mawili makubwa: la kwanza ni kuzidharau hisia za utaifa ndani ya jamii ya Zanzibar, akizifananisha na hisia kama hizo ndani ya iliyokuwa Tanganyika yake, ambako alifanikiwa kwa urahisi na kwa kasi ya ajabu kuufuta kabisa Utanganyika.

La pili, ilikuwa ni khiyana aliyokuwa nayo kwa kuelekea kwenye Muungano akiwa na mawazo ya utanuaji wa himaya akilini mwake kwa kuwa na Tanganyika iliyo kubwa zaidi yenye jina jipya, mipaka mipya na himaya mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kosa hili la pili, limesalidia sana kosa la mwanzo, maana limehalalisha “porapora” ya kila cha Zanzibar kukiweka kwenye kapu la Muungano, na matokeo yake kuwafanya Wazanzibari wagunduwe haraka azma iliyo nyuma ya dhamira hiyo na wachukuwe hatua kwa namna yao, maana hakuna binaadamu wa kawaida anayevumilia khiyana.

Matokeo yake, hata baada ya miaka 50 ya Muungano, bado Wazanzibari wameng’ang’ania kile kile walichokuwa wametakiwa kuachana nacho miaka michache baada ya Aprili 1964 – hisia kali za utaifa wa Zanzibar.

Ni ajabu kubwa kuwa hata vijana waliozaliwa zaidi ya miongo mitatu baada ya Zanzibar kupoteza kila kitu kwenye kapu la Muungano, wana hisia zile zile za kujifaharisha na Uzanzibari wao. Na kama hili ni kosa, bali lilikuwa kosa la Nyerere.

Kuna hoja maarufu miongoni mwa wale wanaojinasibisha na utetezi wa mfumo wa Muungano uliopo kwamba Watanzania walio wengi ni wale waliozaliwa ndani ya Muungano na ambao hawakumbuki chengine kisichokuwa Utanzania wao. Lakini kila mara, ndani ya miaka hii 50, Zanzibar imekuwa ikionesha udhaifu wa hoja hiyo.

Ndio maana hata hivi leo wakati ikielekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, bado ajenda ya nafasi ya Zanzibar kwenye Muungano una makali yale yale – na hata pengine kuzidi – ya ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa kwanza baada ya kurudi vyama vingi, wa 1995. Maswali yanayoulizwa na vijana wa Kizanzibari ni yale yale: “I wapi nafasi ya nchi yetu kwenye Muungano? Kwa nini nchi yetu haisongi mbele kiuchumi licha ya kuwa kwenye Muungano?”

Na kwa kuwa aliowaacha Nyerere hawana majibu ya kuridhisha kwa maswali kama haya, wamebakia na mbinu na njia zile zile tu za zama zake – vitisho, njama, fitina. Vijana wa Zanzibar wanatishiwa mizinga na vifaru, na mauaji na jela na vipigo. Vitu vilivyoshindwa kuua Uzanzibari kwa miaka 50, vinatumiwa tena hivi leo. Lilikuwa kosa la Nyerere.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.