Wiki hii, Rais Jakaya Kikwete amezungumza na wananchi kupitia kutoa hotuba yake ya kila mwezi kwa njia ya televisheni – dasturi aliyoirithi kutoka kwa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, ya kila mwisho wa mwezi (anaopata wasaa) kuzungumzia masuala, matukio, na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika nchi yetu kwa mwezi uliokwisha.

Lakini kwa mara nyengine tena, akiwa ni kiongozi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyongeka kwa nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar, Rais Kikwete alizungumzia mambo mbali mbali yanayoihusu Tanzania ya upande mmoja wa Tanganyika, akipuuzia kabisa kuzungumzia matatizo, matukio na changamoto mbalimbali zilizotokea katika visiwa vya Zanzibar.

ali
Na Ali Mohammed

Labda ni kwa kuwa kuwa Zanzibar hakukuwa na uporaji wa silaha kwa mwezi wa Febuari, hakukuwa na mauwaji wala ukataji viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi na mengine kama hayo, ndio maana Rais Kikwete hakuona umuhimu wa kuiangazia sehemu hii muhimu ya Jamhuri ya Muungano anaioitawala.

Lakini kuna mambo mengine kadhaa ya Tanganyika ambayo Rais Kikwete aliyazungumzia ambayo pia yalitokezea Zanzibar. Hilo linatufanya sisi Wazanzibari tujiulize ikiwa kweli tuna nafasi kwake, na ikiwa kweli anajihisi yeye mwenyewe, ndani ya nafsi yake, ikiwa rais wetu ni mmoja?

Nisieleweka kuwa nina wivu. Lakini kitendo cha Rais Kikwete kumtaja kwa namna ya kipekee na kumtukuza aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi na mpigadebe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Marehemu Kapteni John Komba, kwenye hotuba yake kama kwamba ni mtu pekee muhimu aliyefariki dunia ndani ya Tanzania nzima tangu atowe hotuba yake ya mwisho kwa taifa, huku akipuuzilia mbali kifo cha Mnadhimu Mkuu wa CCM na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Salmin Awadh Salmin, ni cha kushangaza sana.

Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema:

“Wakati tulipokuwa tunajiandaa kurekodi hotuba hii tukapata habari ya huzuni na majonzi makubwa ya kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi, Mheshimiwa Capt. John Damian Komba.  Kifo chake kimeliondolea taifa letu mmoja wa viongozi wake wazuri, msanii mahiri, raia mwema na mzalendo wa kweli.  Marehemu alitumia muda mwingi wa maisha yake kuelimisha jamii kuhusu mambo mema, amefanya hivyo akiwa mwalimu na baadaye Kiongozi wa Kikundi cha Sanaa cha JWTZ na hapa mwishoni kiongozi wa kikundi cha Tanzania One Theatre cha Chama Cha Mapinduzi.  Kwa kutumia kipaji alichojaaliwa na Mola wake ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa Chama Tawala.  Daima tutamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoifanyia jamii ya nchi yetu na taifa kwa jumla.

“Katika salamu zangu za rambirambi kwa Spika wa Bunge na Katibu Mkuu wa CCM niliwaomba kupitia kwao salamu ziwafikie Wabunge wote na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.  Hali kadhalika, niliomba kupitia kwao salamu ziwafikie familia ya marehemu Capt. John Komba.  Kwa familia ya ndugu yetu mpendwa, napenda  kuwahakikishia kuwa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo.  Tunawaombea kwa Mola awape moyo wa subira na uvumilivu.  Wananchi wa Wilaya ya Nyasa tunawapa pole nyingi kwa msiba mkubwa uliowakuta na pengo kubwa mlilolipata.  Nawaomba watambue kuwa namna bora zaidi ya kumlilia Mbunge wao aliyewapenda ni kudumisha mema yote aliyofanya na kukamilisha zile kazi ambazo alikusudia kuzifanya lakini hakuweza kufanya hivyo kwa sababu ya kukutwa na umauti. Mwisho nawaomba, Watanzania wote tuungane na familia yake kumwombea marehemu Capt. John Damian Komba mapumziko mema. Amin.”

Kwa nukuu hii, inaonyesha dhahiri kwamba Rais Kikwete alikuwa na nia ya kudharau kifo cha Salmin Awadh kwa kuwa yeye alifariki dunia mwanzo kuliko Kapteni Komba lakini hakupata nafasi ya kutajwa na kukumbukwa kwenye hotuba hiyo muhimu kwa taifa.

Kipande hicho cha rambirambi ya maneno 250, kisingeharibika kama mungelikuwa na maneno 50 tu ya kumtaja Marehemu Salmin Awadh na muda wa kuwekwa maneno hayo ungelikuwepo kama angelitaka, maana kama alivyosema Rais Kikwete mwenyewe kwamba taarifa ya kifo cha Kapteni Komba ilimfikia akiwa anaandaa hotuba hiyo.

Swali la awali linarudi tena kichwani mwa Mzanzibari na hasa hasa mwana-CCM: ipi nafasi yako kwenye Muungano? Ipi nafasi yako kwenye vichwa na nyoyo za wenye Muungano huo?

Tafakari. Fanya maamuzi sahihi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.