Tuziangalie na tuzilinganishe nchi tatu – Seychelles, Mauritius na Zanzibar – ambazo zote ni visiwa vinavyoelea kwenye Bahari ya Hindi. Jamhuri ya Seychelles iko umbali wa kilomita 1,500 kutoka kusini mashariki mwa Afrika, ikiwa na wakaazi 90,000 na kidogo, Jamhuri ya Mauritius iko umbali wa kilomita 2,000 kutoka upande huo huo wa bara la Afrika ikiwa na raia milioni 1.26 na Zanzibar iko umbali wa kilomita 50 kutoka bara la Afrika ikiwa na wakaazi milioni 1.3.

Zote tatu zilitawaliwa na Muingereza kwa njia zinazofanana, ikatangulia Zanzibar kupata uhuru mwaka 1963, ikifuatiwa na Mauritius mwaka 1967 na takribani muongo mzima baadaye, Seychelles ikapata uhuru mwaka 1976. Mauritius ilipata uhuru ikiwa inategemea kilimo cha miwa, Zanzibar ikiwa inategemea kilimo cha karafuu na Seychelles ikitegemea kilimo cha mdalasini, vanila na nazi.

Mfanano wa mataifa haya matatu uliendelea hata kwenye malezi ya kisiasa na mitazamo ya kilimwengu, angalau kwa muongo wa kwanza baada ya uhuru. Zote tatu zilijielekeza kwenye siasa za mrengo wa kushoto wa Kisoshalisti. Seychelles, kwa mfano, mwaka 1979 ilijitangaza kikatiba kwamba ni nchi ya chama kimoja inayofuata mfumo wa Kisoshalisti, ikitanguliwa na Zanzibar ambayo hata kama haikuwa na katiba baada ya Mapinduzi ya 1964, mapinduzi yenyewe yalikuwa na chembechembe za mapambano ya kitabaka, huku chama cha Labour kilichopokea uhuru nchini Mauritius na hata kilichokuja kuongoza baadaye cha Mauritian Militant Movement (MMM), vyote vilikuwa na mtazamo wa kuelekea kushoto.

Lakini miaka takribani 50 baada ya uhuru wa Mauritius na Mapinduzi ya Zanzibar, na takribani miaka 40 baada ya uhuru wa Seychelles, visiwa hivi dada vinavyoelea kwenye Bahari ya Hindi vina hadithi tafauti ya kuyaelezea maisha yake ya kiuchumi na kisiasa kwa watoto wake. Mtoto wa Zanzibar anaishi kwenye kiwango cha chini cha kiuchumi, pato lake likiwa dola 656 kwa mwaka, wa Mauritius na Seychelles wanaishi kwenye kiwango cha uchumi wa kati wakiwa na pato la kati ya dola 16,000 na 17,000 kwa mwaka.

Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alisema kwenye kilele cha matembezi ya vijana wa chama chake hajui kwa nini Zanzibar haiendelei kama visiwa vyengine. Angalia hii vidio ya hapo chini:

Naye waziri wake wa Biashara na Viwanda, Nassor Ahmed Mazrui, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), aliuliza swali mfano wa hilo kwenye kongamano la tarehe 1 Machi 2015.

“Mauritius ilipata uhuru miaka miwili baada ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ilikuwa ikitegemea kilimo cha miwa kama ambavyo Zanzibar ikitegemea karafuu. Iko umbali wa kilomita 2,000 kutoka Bara la Afrika na hivyo haina fursa ya kuwa karibu na nchi za bara hilo ambayo Zanzibar yenye umbali wa kilomita 40 inayo. Lakini leo pato la mwananchi wa Mauritius ni dola 16,500 za Kimarekani kwa mwaka hali la Mzanzibari ni dola 650. Tatizo letu liko wapi?”

Tatizo lipo na sababu ipo ya Zanzibar kuwa ilipo leo. Lakini tatizo kubwa zaidi hasa ni kwamba pande hizi mbili kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, yaani CCM na CUF, zinaliangalia kwa mitazamo tafauti; na hivyo wana njia tafauti ya kulitatua.

Kwa mintarafu ya mazungumzo ya Rais Shein na Waziri Mazrui, tatizo wanaloliona ni Zanzibar kutenda vile ambavyo visiwa mfano wake ni kujikwamisha kwake kwenye Muungano na jirani yake, Tanganyika.

Rais Shein anasema kwa kujiuliza na kushangaa.

“Mimi nashangaa sana na wakati mwengine huwa najiuliza – tumekosa nini sisi? Nikiangalia Dar es Salaam inavyokuwa…..unavyoona inabadilika, watu wanavyojenga majengo ya kisasa, makubwa sana yameinuka, halafu unakuja zako Unguja unatizama, sisi tuko na Mji wetu Mkongwe ule ule. Haupanuki….”

Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zanzibar, Nassor Mazrui.
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zanzibar, Nassor Mazrui.

Ndani ya kauli hii, Rais Shein analionesha tatizo lilipo kwa kuoanisha na mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania Bara ulio umbali wa kilomita 50 tu kutoka mji mkuu wa Zanzibar. Hata hivyo, hawaambii wazi wasikilizaji wake kuwa tatizo na hilo, kinyume na Waziri Mazrui ambaye baada ya kushangaa anasema kuwa “nchi isiyo na uwezo wa kumiliki sera, nguvu na taasisi zake za kiuchumi, haiwezi kusonga mbele na haiwezi kukabiliana na umasikini.”

Mfano anaoutoa kushabihisha uhusiano wa Tanganyika na Zanzibar kwenye Muungano ni sawa na mwana aliyepewa maziwa kwenye chupa isiyokuwa yake. Matokeo yake, hapati maziwa wala hapati chupa, maana maziwa hawezi kuyachukuwa kiganjani.

Katiba ya Muungano ya mwaka 1977 na Inayopendekezwa, zote, zinaipa Zanzibar wajibu wa kusimamia uchumi wake (maziwa) lakini zinawanyima uwezo (chupa) wa kusimamia uchumi huo. Kodi, ushuru, sarafu na usimamizi wa masuala ya fedha – yote yako mikononi mwa Tanganyika.

Seychelles na Mauritius zinaweza kuwa na historia inayofanana na Zanzibar na zinaweza kuwa zilianza mguu mmoja kwenye safari zao kuelekea uhuru kamili na uwezo wa kujiamulia. Lakini safari ya Zanzibar ilikatishwa njiani kupitia ajali ya kisiasa – Muungano wake na Tanganyika.

Na inawezekana kabisa ikawa si Muungano kama Muungano ambao kimekuwa kizingiti cha Zanzibar kusonga mbele kutoka uchumi wa chini kufikia angalau kwenye uchumi wa kati walionao Mauritius na Seychelles, lakini ni aina ya Muungano uliopo na siasa ya Muungano huo kuelekea Zanzibar.

Siasa hiyo inafupishwa kwa sentensi moja tu: “Kujenga Muungano imara ni kuwa na Zanzibar dhaifu na Zanzibar imara ni kuwa na Muungano dhaifu”. Hivyo pale Rais Shein na wenzake kwenye CCM Zanzibar wanapoapa kuulinda Muungano kwa vyovyote iwavyo, basi huwa pia anaapa kuendelea kuwa na Zanzibar dhaifu – kwa mtazamo wa wenzake wa CCM kutoka Tanganyika. Na ikiwa hivyo ndivyo ilivyo, ataendelea kushangaa na kujiuliza sana.

One thought on “Mauritius, Seychelles, Zanzibar na hadithi yenye ncha saba”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.