Isifike wakati raia akajenga hisia kuwa hatapanda zaidi ya alipo kwa sababu hafanani au hakubaliki kimtizamo au hatapanda alipo kwa sababu tayari ana chapa ya kuwa sio mwenzetu, ingawa hilo hufanywa kwa hila na kwa siri. Ila zama hizi za sayansi na teknolojia Mheshimiwa Rais zimemuumbua Waziri wako aitwae Haji Omar Kheir, kama kipande cha sauti kinachosambaa katika mitandao ya kijamii ni kweli sauti yake na sisi tunaomjua tunaona ni sauti yake halisi. Soma barua kamili ya Ally Saleh kwa Rais Ali Mohammed Shein.

BARUA YA WAZI KWA RAIS WA ZANZIBAR

Mheshimiwa Rais wangu Dk. Ali Muhammed Shein niruhusu nikuandikie barua hii ya wazi ili pia wananchi wenzangu wajue kuwa nimekuandikia na inshallah ninavyokujua wewe utaisoma barua hii, maana ni msomaji mzuri.
Au itakeyapo wasaidizi wako wataisoma basi nawasihi wakupe taarifa na wasikubanie maana barua hii itanoga iwapo utaisoma na nakujua wewe ni msomaji makini, naambiwa kwenye vikao vya Bango Kititi hata sentensi moja haikupiti kwenye taarifa zinazokufikia.

Na Ally Saleh
Na Ally Saleh

Pili nimeona muhimu niyaseme haya kwa sababu ya kujua kuwa wewe ni muumini mkubwa wa utawala bora na wa sheria na kwa hivyo ni mlindaji mkubwa wa Katiba ya Zanzibar ambayo ulikula kiapo kuwa utailinda na kuitetea.
Mheshimiwa Rais moja ya jambo ambalo lina msingi mkubwa katika Katiba ya Zanzibar ni suala la kutokubaguliwa mtu kwa hali yoyote ile. Yaani iwe ya dini, rangi, kabila au hata sehemu anayotoka kwa maana nyengine wananchi wote katika nchi wawe sawa.
Wawe sawa katika kazi, ajira na fursa nyengine zozote zile na ambacho kitamtenganisha raia mmoja na mwengine ni sifa zinazohitajika kwa mfano katika ajira au uteuzi, si zaidi si kasoro na hilo likifanyika sote tutakuwa radhi maana kila mtu anajua sio sote tutapata ajira moja au sio sote tutapata uteuzi, lakini wanaoteuliwa au kuajiriwa wasiwe wamepata nafasi kwa upendeleo.
Upendeleo ninaotaka kuusisitiza hapa ni ule wa umajimbo au wa kiitikadi yaani kuwa muumini wa upande mmoja wa siasa zetu za Zanzibar ambapo ukiwa huko upande wa CCM husemwa kuwa “huyu sio mwenzetu.”

Mheshimiwa Rais msingi mwengine wa Katiba yetu ni suala la kuwa kila mtu ana haki ya kupata fursa katika uongozi wa nchi na kushiriki katika kiwango cha maamuzi kwa kadri itakavyokuwa kwake. Katiba haitafuni maneno katika hili, chembilecho maneno ya watu.
Isifike wakati raia akajenga hisia kuwa hatapanda zaidi ya alipo kwa sababu hafanani au hakubaliki kimtizamo au hatapanda alipo kwa sababu tayari ana chapa ya kuwa sio mwenzetu, ingawa hilo hufanywa kwa hila na kwa siri.
Ila zama hizi za sayansi na teknolojia Mheshimiwa Rais zimemuumbua Waziri wako aitwae Haji Omar Kheir, kama kipande cha sauti kinachosambaa katika mitandao ya kijamii ni kweli sauti yake na sisi tunaomjua tunaona ni sauti yake halisi.
Mheshimiwa sijui kama wasaidizi wako yaani wawe wa ofisi au wa Idara ya Usalama wamekuarifu juu ya kipande hicho cha sauti ya Waziri Haji Omar Kheir akitoa matamshi ambayo yanamuondolea sifa kabisa za kuwa Waziri katika Serikali yako.
Na katika sauti hiyo amekushirikisha na kuonyesha muelekeo kuwa na wewe unashiriki katika kukubali kufanywa ubaguzi katika suala zima la uteuzi kwa kusema akishapewa majina ya watu ambao ni “wenzetu” basi atakashauri uwape uteuzi

Anagusia Upemba katika kipande hicho lakini pia anasema kwamba kwa sasa anajua kwamba Wakurugenzi wote hawako upande wao, kwa maana ya kwamba Wakurugenzi wapo upande wa Upinzani kwa taarifa au labda uchunguzi alioufanya yeye na kwa hivyo hawako upande wa Serikali na mnasaba huo upande wa CCM.

Kipande hicho cha sauti hakina tarehe ya matamshi yalipofanywa lakini ni wazi alisema akiwa na ushawishi katika suala la ajira, iwe Wizara aliyokuwa ameishika kabla kuiongoza au ile ambayo anayo hivi sasa. Kwangu mimi hilo si muhimu isipokuwa muhimu ni kwamba kama amesema akiwa ni Waziri na ambae nae pia ameapa kuilinda Katiba.

Mheshimiwa Rais kuna umuhimu ya kujenga na kubakiza sifa stahili kwa Serikali yako ambayo inatakiwa ione raia wote sawa, ingawa kwa sasa sote tunajua kuwa ajira katika Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haziko wazi kwa Wazanzibari wote.

Tukio hili nionavyo halifai kunyamaziwa nawe. Kama kiongozi wetu mkuu tungependa tusikie kauli au hatua zako maana likiachiwa linatia doa kubwa katika uogozi wako na halisaidii kuendeleza suala la umoja wa kitaifa ambalo kwa sasa Serikali yake inatekeleza masharti yake kwa mujibu wa Katiba.
Bila ya shaka katika baadhi ya nchi Waziri Haji Omar Kheir ingekuwa zamani amejiuzulu kwa sababu kauli yake hiyo baada ya kutoka hadharani imemshushia kama nilivyosema sifa ya kuwa Waziri lakini pia amekwenda kinyume kabisa na Katiba yetu ya Zanzibar.

Siamini kuwa Waziri Haji Omar Kheir anaweza hata kufikiria suala la kukaa upande kwa kujionyesha kuwa mbaguzi na ataposoma makala haya atakuja na hoja nyingi za kujilinda na kuhoji mantiki ya makala hii na hata kuhoji uhalali wa mwandishi wake.

Ila huo ndio utamaduni uliopo hivi sasa ingawa mimi siamini. Kama nitapaswa kurudia basi Waziri Haji Omar Kheir sehemu nyengine hata angekuwa amefanyiwa maandamano ya kushindikizwa kuondoka kwa sababu amefanya jambo la hatari kwa umoja na udhabiti wa nchi yetu.

Mheshimiwa Rais najua, na wewe unajua kuwa najua, kwamba ni mamlaka yako kuteua na kutengua na hatuwezi kukuengua. Ila nakusihi tu utizame jinsi suala la ubaguzi linavyoendelea kuila Zanzibar kwa miaka 50 ya uhuru sasa na ambapo tuliapa kwa Sera za Afro Shirazi kuliondoa.

Tunachoweza kusema tu ni kuwa tungependa kuendelea kuwa na imani na Serikali yetu na kwa hivyo tungependa tuwe na mawaziri ambao wanachunga kauli zao wakiwa ndani au mikutano ya faragha, na wasipofanya hivyo, bakora yako inawarudisha katika mstari, maana mwisho wa siku Wapemba na Waunguja wana hisa sawa katika Zanzibar yao wanayoipenda na Mtumbatu hana haki ya kumbagua Mmakunduchi au vyenginevyo, na maeneo tutakayo iwe ni kwa ajili ya kutambuana tu.

Barua hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mtanzania la tarehe 26 Februari 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.