Kiilivyo si mada kubwa na isingepata nafasi kwenye mtandao huu kama si gazeti la Mwananchi kupitikiwa na kujikuta likinasa kwenye siasa za maji-taka za mwakilishi wake visiwani Zanzibar, ambaye aliwafanya wachapishe stori waliyoipa kichwa cha habari “Bendera za ASP zazua taharuki Z’bar” ambayo ina upotofu mkubwa.

Msingi wa stori hiyo ni kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, ambaye aliitisha mkutano wa waandishi wa habari siku moja tu baada ya mkutano mkubwa wa hadhara wa Chama cha Wananchi (CUF) uliofanyika tarehe 21 Februari 2015 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, akidai kwamba CUF inachochea mgogoro visiwani humo kwa kutumia bendera za chama cha Afro-Shirazi (ASP) kwenye mikutano yake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za UVCCM huko Gymkhana mjini Zanzibar, Shaka alisema CUF kimeamua kuleta chokochoko za kisiasa ambazo zinaweza kuitingisha na kuzorotesha amani, utulivu na maridhaino yaliofikiwa visiwani humu. “Kitendo cha kubeba alama za chama chetu cha zamani ASP na kuzitumia kwenye mikutano yao ya hadhara  licha ya kuwa ni uvunjaji wa sheria lakini kinaweza kuibua mitafaruku na mapigano yasiohitajika, tunaonya kwa mara ya mwisho ikishindikana tutazilinda bendera zetu,” alisema Shaka. (Mwananchi, 24 Februari 2015)

Nimesema kwamba stori yenyewe isingelikuwa kubwa na pengine wala isingelipata nafasi kwenye Zanzibar Daima lau si kubebwa kwake na gazeti kubwa kama la Mwananchi na ukweli kwamba gazeti hilo lilikuwa linaiendeleza stori hiyo kutoka ile ya siku moja nyuma yake, ambapo liliandika kwenye stori kubwa ya mkutano wa maandalizi ya uchaguzi wa CUF, kwamba “CUF yatoa vifaa, yapeperusha bendera ya Afro Shiraz Zanzibar”.

Inaonekana naye Shaka alirukia hii stori hapo kwenye kile kilichoandikwa na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Mwinyi Sadallah, na yumkini wote wawili – Shaka na Mwinyi – wakidhani kwamba sasa wameshapata mahala pa kuishika CUF.

Katika hatua nyingine CUF kimeendelea kupeperusha bendera ya zamani ya chama cha Afro Shiraz Party (ASP), ambacho kimefutwa kisheria baada ya kuungana na chama cha Tanu na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi(CCM), Februari 5, 1977.

Bendera hiyo ya ASP ilipamba mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika jana kwenye uwanja wa Mnazi Mmoja ambako chama hicho kilikuwa kinazindua rasmi kamati za uchaguzi za chama hicho ambazo ni maalumu kwa ajili ya kushughulikia masuala yote yanayohusu uchaguzi mkuu ujao ikiwa ni pamoja na maandalizi.

Tofauti na ilivyozoeleka wafuasi wa chama hicho waliingia uwanjani hapo kwa makundi huku karibu kila mmoja akiwa amebeba bendera ya ASP, yenye rangi tatu za kijani, nyeusi na bluu bahari.

Kwa mujibu wa taarifa wafuasi wa CUF wameanza utaratibu wa kupeperusha bendera ya ASP kwa madai ya kuienzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), na pia kutanguliza uzanzibari kwanza. (Mwananchi, 23 Februari 2015).

Kitu kibaya, hata hivyo, ni kwamba badala ya kuishika CUF, stori hii inawashika wote wawili na, bahati mbaya zaidi, inalijumuisha gazeti na timu ya uhariri wa gazeti la Mwananchi kwamba wana mapungufu ya kuijua historia ya Zanzibar, kwa ukweli mwepesi tu – kwamba CUF haijapeperusha bendera ya ASP.

Ufafanuzi unafuatia hapo chini, lakini kabla ya yote angalia vidio hii ya vijana wa Mguu Mbele Mguu Nyuma, ambao ndio wanaotajwa na stori ya Mwinyi na Shaka kwamba wanapepea bendera ya ASP na kazia macho yako kwenye bendera zinazopeperushwa nao.

Bendera inayopeperushwa kwenye mikutano ya CUF si ya ASP, bali bendera ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyotumika kati ya tarehe 29 Januari 1964 hadi 26 Aprili mwaka huo kuliwakilisha taifa la Zanzibar. Bendera hiyo ni hii hapa chini:

Bendera ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar baina ya tarehe 29 Januari 1964 hadi 26 Aprili 1964.
Bendera ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar baina ya tarehe 29 Januari 1964 hadi 26 Aprili 1964.

Kwa hakika, hii ndiyo hii hii bendera ya sasa ya Zanzibar kama ukitoa kijibendera kidogo cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichopo juu upande wa kulia wa bendera hii iliyozinduliwa tarehe 9 Januari 2005 kama inavyoonekana hapo chini:

Bendera ya sasa ya Zanzibar ambayo ilianza kupeperushwa tarehe 9 Januari 2005.
Bendera ya sasa ya Zanzibar ambayo ilianza kupeperushwa tarehe 9 Januari 2005.

Sheria ya Vyama Vingi vya Siasa ya 1992 ambayo Mwinyi na Shaka wanataka kuonesha inavunjwa na kitendo cha kupeperusha bendera hiyo, haihusu bendera ya zamani ya nchi, bali bendera na alama za vyama vya zamani vilivyokuwapo kabla ya mwaka 1977. Bendera ya ASP wanayosema wao ni hii hapa chini:

Bendera ya chama cha Afro-Shiraz iliyotumika kutoka mwaka 1957 hadi kilipovunjwa mwaka 1977.
Bendera ya chama cha Afro-Shiraz iliyotumika kutoka mwaka 1957 hadi kilipovunjwa mwaka 1977.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Laiti gazeti la Mwananchi lingelifanya utafiti wake mwenyewe mdogo tu, basi lisingeandika stori yenye upotoshaji mkubwa kama huu na kumruhusu mwandishi wake, Mwinyi Sadallah, kumpatia jukwaa Shaka Hamdu Shaka kuendeleza siasa zake za vitisho na vita visiwani Zanzibar.

Uandishi wa habari wa aina hii una mashaka kama alivyo Shaka mwenyewe, maana unakuwa hauongozwi na maadili wala utaalamu, bali jazba na hamasa.

Zanzibar inahitaji salama, lakini hilo haliizuwii kupiga mayowe ya kutaka isikilizwe madai yake ya mamlaka kamili ambao ndio ujumbe uliomo kwenye kubeba bendera za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar miaka 50 baada ya kuzikwa kwake. Ndio ujumbe uliomo kwenye vuguvugu la Vijana wa Mguu Mbele Mguu Nyuma.

3 thoughts on “Ukomo wa akili za Shaka na Sadallah mbele ya “Mguu Mbele Mguu Nyuma””

  1. Ahsante sana muandishi maana hata ho CUF wenyewe wameshindwa kuwajibu kwani nilimsikia Bimani akisema kuwa sio chama cha CUF kilichopeperusha bendera ya ASP bali ni Raia wao chama hawana mahusiano nao hata mimi nikakubaliana nae lakini kiukweli kwamba hakuna hata bendera ya ASP iliyokuwepe isipokuwa Huya Mwinyi Sadala na Shaka wote ni wapumbavu tu hawajui walalo lisema, sema ule uCCM wao ndio unao wadhalilisha na kuwaondolea heshima yao. Na hawa wasajili wavyama nao ni majuha pia kwani wamasema malalamiko ya Shaka na Mwinyi Sadala wanayafanyia kazi na washayapeleka Bara kwamsajili wa vyama vya siasa sasa wanasubiri hatua zitakazochukuliwa na ni majuha pia kwali wanashindwa kutafautisha bendera ya Zanzibar na ya ASP.

  2. mi kwauoni wangu wakaribu, mi nadhani alichofanya Bimani ni vyema alivyokanusha kwamba chama hakitumii bendera hiyo kitu ambacho ni sahihi, kwa kuwa angeanza kueleza kama alivyoeleza mwandishi wa zanzibar daima, ingelioneka kwamba hawa vijana walitumwa na CUF kufanya hivyo.

  3. Lakini kwa upande mwengine, muandishi amefanya juhudi kubwa kuelimisha umma, na hiyo ndio kazi na wajibu wake, natumai bwana shaka na wenziwe wakiliona taarifa hii pia wanaweza kujutia maamuzi yao ya kulizungumzia taifa bila ya kuhakiki mazungumzo yao.

    Na ikiwa watasimama na msimamo wao huo, kwamba hata hiyo bendera ya nchi ya zamani hairuhusiwi basi na wao bado wamo hatiani, coz zipo shahidi za picha walizotumia na wao bendera hio katika maandamano yao na mikutano.

    Ikiwa kunahatuwa inapaswa kuchukuliwa basi sheria ni msumeno.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.