FITINA nyengine inapandwa dhidi ya Wazanzibari na dhidi ya Zanzibar. Na mpandikizaji wa mara hii ni Samuel Sitta, waziri mwandamizi kwenye serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye dhamana ya mawasiliano na uchukuzi, na ambaye ndiye aliyekuwa pia spika wa Bunge Maalum la Katiba lililomazika kwa kutoa kile kiitwacho Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inayotazamiwa kupigiwa kura mwishoni mwa mwezi Aprili 2015.

Samuel Sitta.
Samuel Sitta.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA) juu ya bunge hilo aliloliongoza kutopitisha kipengele cha katiba kinachowaruhusu Watanzania kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja, Sitta alisema yafuatayo:

“….ukumbuke historia, hususan historia ya Zanzibar, na Watanzania takriban zaidi ya laki mbili walioko Oman ambao walivyotoka kama 20,000 mwaka ule wa 1964, sasa ni kundi zito ambalo lina uwezo kifedha ambalo lipo pale Oman. Ukikaribisha uraia pacha, kwa maana ya papo kwa papo, maana yake wale wote wanakuwa ni raia wa Tanzania pia, lakini wengi wao wana nia ya kuipindua serikali. Kwa hivyo ukileta sura hiyo (kipengele hicho cha katiba) inaleta tabu kidogo – kumpa uraia mtu ambaye kwa matamshi yake na tabia yake na uwezo alionao ana lengo la kupindua serikali….”

Angalia vidio kamili hapa chini ili kupata chote alichokizungumza kwenye suala hili.

Tusiangalie mapungufu ya hoja dhidi ya uraia wa zaidi ya nchi moja kwa Watanzania wanaoishi nje kwa sasa, ingawa si kweli kuwa ilitokana na khofu ya kupinduliwa kwa serikali. Dunia ya leo haimuhitaji mtu kuwa raia wa nchi fulani kuweza kuupindua utawala wa nchi hiyo. Wamarekani wanaokwenda kupindua serikali za mataifa mengine hawana uraia wa nchi hizo, bali wana nguvu, sera na teknolojia ya kufanya hivyo.

Wala tusiangalie ukweli kuwa hoja ya Sitta ina mapungufu ya ujinga kwa sheria za Oman ambazo haziruhusu mtu mwenye uraia wa nchi hiyo kuwa na uraia wa nchi nyengine – na kwa hivyo moja kwa moja hao Waomani 200,000 anaowazungumzia – kama kweli wanafika idadi hiyo na kama kweli wana nia ya kuchukuwa uraia wa Tanzania – hawawezi kuwamo kwenye kundi hilo la Watanzania wenye uraia wa nchi zaidi ya moja.

Fitina ya makusudi

Tuangalie fitina ya makusudi ya mtawala dhidi ya Zanzibar hasa katika wakati ambapo, kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 50 na pamoja na udhaifu wake wa ndani, Zanzibar imeweza kuianika aibu ya kutawaliwa na Dodoma kupitia Mabadiliko ya 10 ya Katiba yake na mchakato wote wa kupatikana Katiba Mpya unaoendelea sasa.

Kwa mfano, kile kilichotokea kwenye Bunge Maalum la Katiba ambalo liliongozwa na yeye, Sitta, kimsingi kilimzuwia mtawala kuandika rasimu ya katiba mpya hadi alipolazimika kutumia nguvu, hila na mizengwe kuifanya hiyo Rasimu Inayopendekezwa.

Hili lilimkasirisha mtawala pamoja na mawakala wake tangu awali kabisa. Msikize hapa chini Waziri William Lukuvi, ambaye naye kama alivyo Sitta ni kiongozi mwandamizi kwenye serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kubaini kiwango ambacho Zanzibar ndani Bunge hilo Maalum la Katiba iliivuruga kabisa akili ya mtawala na mawakala wake.

Lugha ya Sitta na ya Lukuvi zinafanana. Dhamira zao zinaoana. Njia yao ni moja kwa kuwa lengo lao pia ni moja – lengo la mtawala, ambalo ni kuiadhibu Zanzibar kadiri inavyoyumkinika kutokana na uthubutu wake dhidi ya mtawala.

Ni staili inayotumiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina – adhibu vikali kadiri inavyowezekana ili liwe fundisho na iwe mwisho. Wakati mtoto wa Kipalestina anapokirushia mawe kifaru cha kijeshi cha Israel ambacho kimeivunja nyumba yao na kuikalia kwa nguvu ardhi yao, hupigwa, akakamatwa na kufungwa jela, kama si kurushiwa risasi na kuuliwa kabisa.

Kila kombora moja la Hamas, ambalo hata haliwahi kutua chini kwenye ardhi ya Israel kabla ya kutunguliwa huko huko angani, hujibiwa kwa kuangushiwa bomu la kilogramu 500 katikati ya makaazi ya watu, linalouwa makumi kwa mamia ya watoto, wanawake na wazee wa Kipalestina.

Ndivyo anavyofanya mtawala dhidi ya mtawaliwa wake anayethubutu. Fuatilia mwenendo wa mambo visiwani Zanzibar tangu mchakato wa katiba mpya uanze – kesi za viongozi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho, watu wanaochukuliwa na kupelekwa korokoroni Bara, na kile kinachoitwa “matukio na kesi za ugaidi” utajua Zanzibar iliyothubutu inaelekezwa wapi na mtawala.

Nadharia dhahanifu ya khofu dhidi ya Waarabu

Kuna kitu kinaitwa “conspiracy theory” kwa Kizungu, ambacho Kiswahili chake kinaweza kuwa ni “nadharia dhahanifu”. Fasili yake ni kuwa haya ni maelezo yanayomtuhumu mtu au kundi la watu, taasisi au jumuiya kwa aidha kupanga, kuficha, au kufanya jambo ambalo ni kinyume cha sheria na lenye madhara kwa wengine.

Kuitwa kwake “dhahanifu” kunaeleza ukweli mmoja muhimu – kuwa hii ni dhana ya kudhania tu, lakini ukweli mwengine muhimu zaidi ni kuwa mara kadhaa ni dhana hizi za kudhanika tu ndizo ambazo huumba mitazamo ya wengi wetu, badala ya zile dhana zilizofanyiwa utafiti na kujengewa ushahidi wa kihistoria, kisayansi na kimantiki.

Hata hivyo, “nadharia dhahanifu” ina msingi wake; na kwa hakika ni msingi huo ndio unaoipa nguvu za kuifanya ikubalike miongoni mwa waumini wake, na kufikia mahala ya kuzichukulia hatua, hata kama mbunifu wake haiamini. Kwa mbunifu, hii huwa ni nyenzo yake ya kisaikolojia, kijamii au kisiasa wa jamii inayohusika nazo.

Waziri mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu wa Oman , Mhe. Sayyid Fahad Mahmoud El Said kabla ya mazungumzo yao rasmi ya kiserikali kwenye Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu wa Oman mjini Muscat Oktoba 28, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu wa Oman , Mhe. Sayyid Fahad Mahmoud El Said kabla ya mazungumzo yao rasmi ya kiserikali kwenye Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu wa Oman mjini Muscat Oktoba 28, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Hapa ndipo inapotuwama hii fitina ya mtawala, kupitia sasa akina Lukuvi na Sitta. Mtawala anajuwa vyema anachokifanya kwenye nadharia hii dhahanifu ya Tanzania kuwaogopa ‘Waarabu wa Zanzibar’. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – kwa sera na muelekeo wake – haina la kukhofia kutoka kwa “Watanzania hao 200,000” walioko Oman.

Kinyume chake ndicho inachokifanya hivi sasa. Kwa siku za karibuni, serikali nzima ya Rais Kikwete imekuwa haishi kiguu na njia kwenda kuomba misaada na ushirikiano wa kimaendeleo na Oman, ikiwatumia Watanzania hao hao wenye asili za Oman na Waomani wenye asili za Tanzania.

Khofu halisi ya mtawala kwa Zanzibar

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – kama mtawala – inaikhofia Zanzibar kama “koloni” lake, endapo Zanzibar itasimama kwa miguu yake katika masuala kadhaa ya kisiasa na kiuchumi, ndani na nje ya mipaka yake. Ile fursa ya Zanzibar kuwa “Cuba ya Afrika” iliyowahi kuwatisha Wamarekani katika miaka ya ’60 kufikia umbali wa kuchochea kuisakamiza Zanzibar kwenye kabari za Tanganyika, ndiyo fursa ile ile ambayo miaka 50 baadaye Zanzibar inayo.

Muonekano wa jiji la Dar es Salaam kutokea baharini ukiakisi ukuwaji wa uchumi, ambao unaweza kufikiwa na kupitwa na Zanzibar iliyothubutu.
Muonekano wa jiji la Dar es Salaam kutokea baharini ukiakisi ukuwaji wa uchumi, ambao unaweza kufikiwa na kupitwa na Zanzibar iliyothubutu.

Hata baada ya kuzikwa kwenye shimo kwa nusu karne, Zanzibar bado ina nafasi ya kuwa “Dubai ya Afrika” na hivyo inamtisha mtawala, ambaye sasa anafikia umbali wa kuiandalia hujuma kubwa. Miaka mitano inayokatika sasa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, licha ya mapungufu yake kadhaa, imedhihirisha kuwa ndoto hiyo ya Zanzibar inaweza kuja kuwa kweli, lau uhuru zaidi wa kisiasa na kiuchumi utakuwa mikononi mwa Wazanzibari wenyewe.

Hapo ndipo penye chimbuko la fitina hii, ambao huenda mtawala anaamini haitakuwa na madhara kwake, zaidi tu ya kuiadhibu na kuidhuru Zanzibar vile inavyostahiki kwa kuonesha kiburi mbele yake. Zanzibar inapangiwa kuadhibiwa na vijenzi vya adhabu hiyo vinaendelea kujengwa kwa utaratibu na mkakati maalum ambao unadhihirika kwenye kauli na hatua kama hizi za kina Sitta na Lukuvi.

Hata hivyo, kufanikiwa na kutofanikiwa kwa hujuma hii ya mtawala kunatokana, kwa kiasi kikubwa, na udhaifu wa Zanzibar na Wazanzibari wenyewe na sio tu nguvu za mtawala pekee. Na tukiwa wakweli wa nafsi zetu, sisi Wazanzibari wenyewe tumeuonesha udhaifu huo mbele ya mtawala tangu kwenye vikao vya Bunge Maalum la Katiba na tunaendelea kumuonesha hadi sasa.

Tuligawika Dodoma kwenye Bunge hilo, tumeendelea kugawika Zanzibar nje ya bunge hilo. Hatujasimama pamoja kwa maslahi ya nchi yetu, bali tumesimama kwa maslahi ya makundi na vyama vyetu. Na hapo lazima tubebe sehemu yetu ya lawama. Tunalaumika.

2 thoughts on “Ni kweli Tanzania inawaogopa ‘Waarabu wa Zanzibar’?”

 1. Si kweli kama Tanzania wawaogopa waarabu wa Zanzibar. Kwanza kwa usahihi Zanzibar hakuna waarabu. waliokuwepo ni Wazanzibari kwa sifa zote zinazohitajiwa. kwani hakuna asiejuwa yakuwa Wazanzibari ni mchanganyiko wa damu nyingi za kizazi kwa kizazi, na kwa mfano uliowazi, hata wachina tumechanganya nao.
  Kinachoogopwa khasa ni Wazanzibari kwa uislamu wao wa damu na kuzalika. na wala hili halikujificha hata siku moja!! hebu natujiulize, wale viongozi wa UAMSHO ni waarabu? na kweli ya kwamba wamekamatwa kwa uaraabu wao? Si kweli hata kidogo. Sasa kwa mfano huu mdogo tu, tumejihakikishia ya kwamba unaopigwa kabare na kuogopwa ni huo UISLAMU wenyewe, na hio ndio khofu yao kuu, na wala haina kificho !!

  1. Tafadhali fungua usome maqala ya Muhammad Ghassany yaliyotoka katika Zanzibar Daima tarekhe 25-2-15 (utaiona humu chini) kukhusu maneno ya Wahishimiwa wa Kitanganyika wa ngazi za juu kabisa na uwasikilize mwenyewe maneno wasemayo yenye kufichua siri ya dhamira zao kukhusu Zanzibar. Wasikilize kwa makini fitina wanazojaribu kutapakaza ili Wazanzibari wasiwe na masikilizano, ili wao walifikie lengo lao la kuimeza Zanzibar. Sikiliza pia kwa makini sababu ya kuitaka kuimeza Zanzibar. Kwa miaka mingi baadhi yetu tulikuwa tukiwatahadharisha Wazanzibari juu ya nia ya wenye siasa kali za udini kutoka Tanganyika. Kuwa lengo khasa la hawa wenye siasa hizo ni kuimeza Zanzbar iwe sehemu ya jimbo tu katika majimbo ya Tanganyika. Wengi waliona hayo ni “mazungumzo baada ya khabari.” Hivi karibubni Mhishimiwa Jaji Warioba alialikwa katika kipindi cha runinga cha ITV kiitwacho “Dakika 45.” Alipoulizwa na Mtangazaji Emmanuel Buhalela juu ya fikra za Mwalimu Nyerere kukhusu serikali moja na tatu. Jaji Warioba alijibu kwa kuanza kusema kuwa alimfahamu Nyerere vizuri sana kwa kuwa alifanya kazi naye kwa karibu kwa miaka mingi na alikuwa mmoja katika washauri wake wakuu na aliongeza haya yafuatayo:

   “Mwalimu… Wote, wote, ambao tumefanya kazi na Mwalimu […] Mwalimu yeye alikuwa anaona serikali mbili kwenda moja. Anasema itachukua mda mrefu lakini twende moja. Yeye hakuwa na mawazo ya kwenda seikali tatu. Yeye ni kwenda moja. Kwahiyo kama ni mawazo ya Mwalimu na alikuwa ‘very clear’ [wazi kabisa] ilikuwa ni kwenda [moja] lakini uende polepole. Mnaongeza mmeongeza na mambo kumi na moja, mtaongeza mpaka siku moja mambo yote ya Zanzibar yatakuwa yataingia katika muungano.”

   Tusisahau kuwa Nyerere hakuwa na kificho na chuki zake dhidi ya Zanzibar na Wazanzibari. Kabla ya mavamizi na muungano alisikiwa waziwazi akisema kuwa angelikuwa na uwezo angeliiburura na kuitokomeza mbali sana katika Bahari ya Hindi. Ndugu anayewapenda nduguze hangesema kwa kutamani haya; na hilo la kuimeza Zanzibar ili isiwe nchi tena ndilo lililokuwa lengo na mpango wake Nyerere tokea awali. Mpango huo bado unaendelezwa na wafuasi wake. Kwa miaka yote hii ya “muungano” hajajitokeza Mhishimiwa yoyote na kuelezea, waziwazi bila ya khofu, sababu khasa zilizowafanya Watanganyika wenye siasa kali za udini watake kuimeza Zanzibar; lakini, hivi karibuni Mhishimiwa William Lukuvi ambaye ni Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu amejitokeza na kukhubiria Kanisani waziwazi na bila ya khofu yoyote lengo lao na sababu zake. Soma maneno yanayofuata ya Mheshimiwa Lukuvi ikisha ujiulize ukweli na yasiyokuwa na ukweli anayoyakhubiri. Ni yepi katika aliyoyabirua anamlaumu mdhulumiwa Zanzibar kwa ajili ina Waislamu wengi? Ametumia mbinu gani za kuwatisha wasikilizaji wake? Pia ujiulize ni nani mwenye siasa kali za udini na za kikoloni kichwani mwake? Waislamu au Lukuvi? Mhishimiwa Lukuvi ameanza na hoja ifuatayo:

   “Tunataka tuwaache Wazanzibari wajitawale wenyewe na Tanganyika… Wazanzibari kule waliko asilimia tisini na tano ni Waislamu. Tunataka wajitangazie serikali ya Kiislamu kule! Mnajua madhara yake? Wale Waarabu watarudi; watazalisha siasa kali kule, watakuja kutusumbua. Mimi najua. Kabisa.”

   Yaani, Wazanzibari wasipewe fursa ya kuwa na uhuru wao abadan kwa sababu asilimia tisini na tano yao ni Waislamu! Kwa hivyo ni Uislamu wao ndio unaomchukiza Lukuvi. Katika mhadhara wake Kanisani anawatia khofu Wakristo walioko Tanganyika ili nao wawakhofu na kuwachukia Waislamu. Suala: Ni lini Waislamu wa Zanzibar walikuwa na uhusiano mbaya na Wakristo? Wazanzibari Waislamu wameishi na Wakristo kama ndugu tokea walipoanza kuja hao Wakristo wa Bara Zanzibar katika kati ya karne ya 19. Waislamu wamefika hadi ya kuwagaia bure ardhi za kujenga makanisa yao Wakristo. Ni dhahiri kabisa kuwa mwenye chuki si Mzanzibari Muislamu dhidi ya Mkristo, bali ni Mkristo Lukuvi na wanaokubaliana na hoja zake zisizokuwa na msingi wala Ukristo mwema ndio wenye chuki na Waislamu.

   Ni wazi kabisa kuwa alipokuwa anazungumza na waumini wenziwe alikuwa akiwatia sumu dhidi ya Waislamu na Uislamu ili wawe na chuki kama alizonazo yeye. Na jambo analowatishia ni pale anaposema “Mnajua madhara yake? Wale Waarabu watarudi; watazalisha siasa kali kule, watakuja kutusumbua. Mimi najua. Kabisa.” Asilolitaka ni kurudi kwa Waarabu! Sijui nicheke au nimsikitikie Lukuvi na wenye fikra kama zake! Hivyo hajui kama Waarabu wamejaa tele Zanzibar! Hana hata haja ya kwenda kuwatafuta Waarabu mivunguni. Hivyo hajui kama wahishimiwa wengi Zanzibar kuwa wameoana na Waarabu! Leo ukizungumza juu ya Waarabu Zanzibar, jua kuwa unawazungumzia wake na watoto wa viongozi wengi wa CCM na katika hawa watoto na wajukuu wa Rais Abedi Karume pia wamo. Kwa mtu mwenye cheo kama chake iwapo hayajui haya, basi inasikitisha sana. La, iwapo anayajua, basi itakuwa anaucheza mchezo muovu sana wa siasa za kibaguzi zenye kupalilia mwisho mbaya.

   Lukuvi ameendelea na hoja yake ya pili:

   “Kwahiyo ndugu zanguni … Zanzibar ni nchi ndogo sana, ina watu milioni moja na laki tatu. Sisi tuna milioni arubaini. Unaweza ukauliza: Kwanini sisi tunaig’ang’ania sana ile? Lakini, sisi tunaangalia mbele, madhara ni makubwa kuiacha Zanzibar kama ilivyo. Kile ni kisiwa. Visiwa hivi vinasumbua sana. Vinasumbua sana. Huwezi kujua kitu gani kitaingia kule na kitavuka na kuja huku, kwasababu hamna uwezo wa kulinda mipaka ya bahari, ni mipana sana. Sasa bora tuwe nao, nchi moja, ulinzi mmoja ambao unadhibitiwa na Jamadari na Kamanda ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Mungano, Polisi wa Jamhuri ya Muungano, Uhamiaji wa Jamhuri ya Muungano, Mambo ya Nje na Paspot Jamhuri ya Muungano, tuwe wamoja, angalau tutakuwa na uwezo wa kujua kinachoingia na kutoka kila upande. Ili tuwe salama. Sisi tunataka usalama wa watu wetu.”

   Kama kuna mtu haelewi maana ya “siasa kali za udini,” haya ya juu aliyoyazungumzia Mhishimiwa Lukuvi ni mfano mzuri sana wa siasa kali za udini. Siasa kali za udini si Waislamu kuwabagua Wakristo, bali Wakristo kuwabagua na kutaka kuwakandamiza Waislamu. Hili liko wazi kabisa. Ingawa kijujuu unaonekana ni ubaguzi wa wenye siasa kali za udini Tanganyika dhidi ya Wazanzibari Waislamu, kwa wenye kutumia akili zao sawasawa, hizi ni siasa chafu zilizojaa khatari kwa sababu ni siasa za ubaguzi dhidi ya Waislamu kwa jumla. Lukuvi anasahau kuwa hata Tanganyika idadi ya Waislamu ni kubwa. Na ni maneno na itikadi zake na wenziwe wenye fikra kama hizo ndio khasa wenye kuwawasha moto Waislamu Tanganyika pia wasiweze kuvumilia ubaguzi kama huu. Bila ya shaka mwisho wake ni muovu kwa Watanzania wote. Ubaguzi wa siasa kali za udini tuliokuwa tukiuzungumzia kwa miaka mingi leo umejitokeza waziwazi katika kinywa cha Mhishimiwa Lukuvi. Na sababu na lengo la kutaka kuimeza Zanzibar, kwa ajili ni nchi yenye Waislamu wengi, pia ameidhihirisha. Ile azma ya Kuimeza kabisa Zanzibar aliyokuwa akiificha Nyerere, leo Lukuvi ameifichua tena bila ya khofu.

   Angalia vizuri hoja zake, vile anavyowatia khofu na chuki waumini wenziwe na hapohapo kujinata kuwa yeye, kama mtume wa Mungu, anajua yatakayotokea baadaye! Kuna visiwa vya Ngazija ambavyo viko karibu na Tanzania pia na huko Ngazija Waislamu wana asilimia kubwa sana pengine zaidi ya Zanzibar na wameupata uhuru wao kwa miaka mingi, mbona hatujawaona Waislamu wa Ngazija kuyafanya hayo anayotutisha nayo Lukuvi?

   Hakuna chochote wanachoweza kukifanya Wazanzibari dhidi ya Tanganyika, na ni yakini kabisa kuwa hawana azma hiyo, si jana, si leo na haielekei kuwa Wazanzibari watakuwa na azma hiyo kesho. Lakini ni Wazanzibari ndio ambao daima lazima wawe na khofu na Wafuasi wa Nyerere kama akina Lukuvi kwa ajili ya siasa kali za udini na chuki zilizowavama katika nyoyo zao kwa sababu wamekwisha kuteremsha Zanzibar makatili wao kutoka Tanganyika na kufyeka roho za Waislamu wengi katika mwezi wa Juni 1961 na Januari 1964 na pia katika Januari 2001. Kwa Lukuvi kuikhofia na kutaka kuing’ang’ania Zanzibar kwa ajili akili zake zinamwambia kuwa Zanzibar itawaletea madhara makubwa wakiiipa uhuru wake ni upeo wa hoja ya udanganyifu isiyoweza kukubalika katika ubongo wa mtu yoyote mwenye akili zake timamu.

   Lukuvi anawatisha wasiouelewa ukweli kuwa Waarabu watarudi. Waarabu waliowahi kutawala Zanzibar ni Waomani. Jee, Lukuvi ameiangalia nchi hiyo na watu wake vizuri akaona kuwa katika watu na nchi isiyokuwa na siasa kali za udini duniani basi Oman ni moja katika chache kabisa zinazosifikana ulimwengu mzima kwa uhuru unaowapa waumini wa kila dini?

   Mhishimiwa Lukuvi ametumia garasa la kipropaganda lililokwisha kupitwa na wakati kitambo sana la kutapakaza chuki dhidi ya Waarabu wa Omani. Wenye siasa kali za udini kutoka Tanganyika waivamie Zanzibar wao, wawauwe Wazanzibari wao, wauibe uhuru wa Zanzibar wao, watake kuimeza Zanzibar wao, ikisha wawanyooshee kidole cha lawama Wazanzibari Waislamu na ndugu zao Waislamu wenzao ambao hawana lengo hilo analolituhumu Lukuvi kwa propaganda zisizoingia akilini na kwa vitendo ambavyo Wazanzibari hata hawajavifikiria kuvitenda ni upeo wa utumiaji mbaya wa propaganda za udanganyifu na dhulma kutaka kuzidi kumlaumu mdhulumiwa. Na hizi ndizo khasa propaganda za wenye siasa kali za udini. Nastaajabu Lukuvi bado hajawabandika Wazanzibari wenye kupigania haki zao na za nchi yao lakabu ya Alkaida au Al-Shabaab au Boko Haram!

   Kwa ustaarabu wao Waomani na siasa zao za kupendelea usalama na udugu na kila nchi na watu wake, alialikwa Lukuvi na Wahishimiwa wengine kutoka Tanzania na siku ya Ijumaatatu tarekhe 20 Oktoba, 2014 Wahishimiwa hao walifanya mkutano katika Hoteli ya Intercontinental Muscat. Wakati wa masuala, Lukuvi aliulizwa kukhusu maneno yake yaliyorekodiwa wakati akiwakhubiria waumini wenziwe kanisani (maneno niliyoyanakili kabla). Kama unavyoelewa, wanasiasa ni watu wenye maneno mengi sana na mengi ya kutubabaisha tu. Kwa mukhtasari, tukiyatowa manyamyamu, muhimu kwangu zilikuwa nukta tatu: (1) alikataa kabisa kuwa hawezi kusema maneno kama hayo. (2) Aliongeza kuwa hawezi kusema maneno kama hayo kwani ana ndugu na marafiki wengi wa Kiislamu. (3) Kuwa yalirekodiwa yalikuwa “out of context.“ Ingelikuwa mimi mwenyewe sikuwepo kwenye mkutano huo na kumsikia, bali nilikhadithiwa tu, ningelisema wanamsingizia.

   Vipi mtu mkweli anasema aliyoyasema kanisani ikisha akakataa namna hii, nashindwa kuelewa! Lakini jambo moja liko wazi kabisa, nalo ni kuwa akitaka asitake, aliyoyasema kanisani anaelewa fika kuwa ni mabaya sana, kwani yana khatari pevu kwa Tanzania, ndipo alipojisuta mwenyewe kuwa hawezi kuyasema. La muhimu ni kuwa huko kanisani kayasema yaliyokuwa moyoni mwake bila ya kizuizi wala kificho.

   Leo, Mhishimiwa Samuel Sita naye ameibuka na chuki zilezile za kuwachochea na kuwagawa Wazanzibari ili wapate kuwatawala vizuri zaidi; wafanye uadui na ndugu zao walioko Oman ili hata ile misaada wanayopeyana kidugu waisitishe kwa uzushi aliouzua usiokuwa na ushahidi wowote. La muhimu zaidi, hakuna hiyo fikra ya kutaka kuipindua serikali ya Zanzibar. Hata ingelikuweko, huwezi kuipindua serikali ya Zanzibar bila ya kuipindua ya Tanganyika pia. Ni fitina ya wazi kabisa na ni uhasidi wa nyoka wa mdimu na kuwafanya Wazanzibari ni wajinga milele. Hakuna anayebakia mjinga milele khasa ukimmtumilia kipumbavu. Muyaka bin Haji Al-Ghassany ametueleza zamani haya yafuatayo:

   Jinga lalikuwa kale zamani za ulegevu.
   Jinga lisikae mbele ya watu kwa upumbavu.
   Jinga lierevushile kwa mambo yenu maovu
   Jinga leo ni jerevu hilino si jinga tena.

   Kila la kheri,
   Ibrahim Noor

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.