Na Foum Kimara

Tunaposema kuna maradhi ya woga wa mabadiliko au chuki tu za kuupandikiza Uarabu kama adui huwa hatukosei. Mwaka huu tutayaona na kuyasikia mengi hasa kwa upande wa Zanzibar. Tena tunaposema mkoloni kaishiwa hoja huthibitika kauli yetu pale wanapoibuka na hoja za ajabu zisizo na mantiki.

Tulimsikia waziri anayehusika na uratibu wa bunge la Tanzania, William Lukuvi, na tukapiga kelele sana juu ya chuki anazopandikiza na istifhamu ya udini alioibeba. Lakini kama yale uliyaona madogo, basi hebu msikilize huyu Samuel Sitta namna anavyozungumza pumba isiyo na kichwa wala miguu.

Anasema Oman kuna Wazanzibari matajiri 200,000, wenye nia ya kuipindua serikali ya Tanzania. Hivi mantiki ya Wazanzibari 200,000 kuipindua serikali ya watu 45,000,000 iko wapi? Woga dhidi ya Waarabu umepewa nafasi maalum na serikali ya Mkuu wetu.

Wanapokwenda na mabuibui na makanzu na baragashia kama omba omba hakuna khofu ya kupinduliwa lakini wanapokaa kwa faragha khofu hio huibuka. Sasa fikiri kama huyu ndie atakaemrithi Rais wa sasa, nafasi ya Zanzibar itakuwa katika hali gani katika muungano wa Rasimu ya “nyoka mwenye makengeza?”

Tuliitwa wauza vitunguu, tukaambiwa jeshi litapindua mfumo aa serikali tatu, tukaambiwa hatuwezi kuiacha Zanzibar ya asilimia 95 waislam ikajitawala, na sasa tunaambiwa kuna watu laki mbili kutoka Oman wanaotaka kuipindua serikali ya Tanzania. Tutaishia wapi?

Hivi inaingia kweli akilini kwamba Rais Jakaya Kikwete katika safari zake za Oman pamoja na majopo ya safari za Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambao kwa pamoja wamewakaribisha diaspora ya Oman kuwekeza nchini Tanzania katika miradi mingi tu bila ya woga wa kupinduliwa, leo hii aje waziri wake wa mwandamizi na kauli za ajabu kwa ajili tu ya kuhalalisha rasimu ya hadaa ya katiba mpya?

Munawakaribishia nini hao munaowaona maadui wanaotaka kuipindua serikali kuwekeza katika sekta kubwa kubwa na nyeti nchini ikiwa kweli ni kitisho kwa Tanzania? Tena basi hujibebesha majoho, vilemba, mitandio na mabuibui wakati wa kuombaomba, lakini wakiwapa visogo tu utasikia wanataka kutupindua.

Serikali ya kalbi kaasi, iliojaa uongozi wa kishirikina na wapiga ramli, yenye woga wa mabadiliko huwa haina tafauti na ya mkoloni. Wakati wa ukoloni serikali za Kiingereza na nyengine barani Afrika zilikuja na visa kama hivi tunavyoviona sasa ilimradi tu waendelee kuwagawa watu na kujitwalia madaraka kwa misingi ya khofu, hasama na mgawanyiko.

Naisikitikia sana siku Sitta atapopitishwa kuwa mgombea wa watawala kwa urais. Woga alionao dhidi ya Uarabu haitaishia hapo, itakwenda mpaka kwenye wenye asili hizo na mwisho mpaka kwa tamaduni zinazofuatana nazo.

One thought on “Sitta anapoonesha rangi yake halisi”

  1. Hawa watu hawaeleweki kila siku wanapishano Oman lakini leo eti watawapindua! lakini mimi siwashangai ninao washangaa ni hawa CCM Zanzibar wenzao wana faidika kwa mapesa ya Oman wao wanatiwa kasumba tu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.