Safari yangu nyumbani Zanzibar ilikuwa ya muda mfupi tu – siku tano tu za wiki ya pili ya mwezi huu wa Februari 2015, lakini mafanikio yake yalikuwa ni makubwa panapohusika jicho la uchambuzi wa kisiasa, hasa kwa wakati huu ambapo nchi inajitayarisha kwa kura mbili – ile ya maoni ya katiba mpya mwishoni mwa mwezi Aprili na ile ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba. Kura zote mbili ni muhimu, na nikakuta Chama cha Wananchi (CUF)  – mshirika mdogo kwenye serikali ya umoja wa kitaifa – kimeubatiza mwaka huu kuwa ni “Mwaka wa Maamuzi.”

Sadfa ilinikutanisha na watu wawili mashuhuri kwenye mazungumzo ya ana kwa ana, kwanza Waziri wa Nchi (Ikulu) Utawala Bora, Mwinyihaji Makame (CCM), na kisha Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Prof. Abdul Sheriff.

Prof. Abdul Sherif
Prof. Abdul Sherif

Kwa wote wawili, nikajadiliana nao suala kongwe ambalo nimekuwa nikiwatupia takribani viongozi wote wa kisiasa na kijamii kutoka Zanzibar ninaopata fursa ya kukutana nao: “Ni kwa namna gani moyo wa maridhiano na roho ya serikali ya umoja wa kitaifa vitahimili vishindo vya kupatikana kwa katiba mpya?”

Swali hili, hapana shaka, lina msingi wake, ambao ni kauli kali za kuuvunja moyo huo wa maridhiano na hata kitisho kwamba serikali ya umoja wa kitaifa haitadumu, kwani vyama viwili vinavyoiunda serikali hiyo, CUF na CCM, viliamua kuchukua njia mbili tafauti kuelekea kwenye katiba hiyo.

Ajabu ni kuwa washirika hawa wawili kwenye serikali ya umoja wa kitaifa wanasema kitu kimoja panapohusika madaraka zaidi kwa Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanzania, lakini wanatafautiana sana panapohusika namna ya kuyapata na kuyatumia madaraka hayo.

Kwa upande wake, CCM inasema yanaweza kupatikana kwenye muundo wa serikali mbili uliomo kwenye Rasimu Inayopendekezwa na ambayo itapigiwa kura mwishoni mwa mwezi Aprili.

“Tuzungumze hoja,” aliniambia Waziri Mwinyihaji kwenye mazungumzo yetu katika hoteli ya Serena siku ya ujio wa Rais Joachim Gauck wa Ujerumani. “Tulikuwa na matatizo ya kuchimba mafuta. Katiba hii mpya inasema sasa mafuta tutaweza kuchimba. Tulitaka Rais wa Zanzibar atambulikane kama makamu wa rais (wa Muungano wa Tanzania) atakapokwenda nje. Tumefanikiwa. Zanzibar tunasema sasa tunataka fursa ya kukopa nje. Tumefanikiwa..”, akaendelea na orodha ya mambo ambayo kwa maoni yake ni madaraka makubwa zaidi iliyovuna Zanzibar kwenye Rasimu Inayopendekezwa, na mwisho akasema kwa hayo Wazanzibari wana kila sababu ya kuikubali Rasimu hiyo kwa kura ya ndiyo.

Lakini CUF inasema sio tu madaraka hayo anayoyasema hayamo kwenye rasimu hiyo kwa udhati wake, bali pia Rasimu hiyo imeyapoteza hata yale madaraka madogo ambayo tayari Zanzibar ilishakuwa nayo kwenye yake yenyewe kupitia Mabadiliko ya Kumi ya 2010 na hata kwenye Katiba ya 1977 inayotumika sasa kuongoza Serikali ya Muungano.

“Wanasema Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Rais wa Muungano, lakini waulize atakuwa makamu wa aina gani na atakuwa na nguvu gani?” anauliza Waziri wa Mawasiliano wa Zanzibar, Juma Duni Haji (CUF), katika mkutano wa tarehe 24 Januari 2015, Magomeni, kisha anajijibu mwenyewe. “Atakuwa makamu wa tatu wa rais ambaye si mjumbe wa baraza la mawaziri la muungano na hana nguvu zozote. Hata kama rais wa muungano hayupo, si makamu wa rais ambaye ni rais wa Zanzibar atakaimu nafasi yake.”

Ukosoaji pia umo kwenye madaraka ya kiuchumi – kukopa, kujiunga na mashirika ya nje na kuchimba mafuta – wakati Rasimu Inayopendekezwa inaifunga Zanzibar mikono nyuma kwa kuwa haiipi nguvu za kukusanya kodi wala kudhibiti na kumiliki mfumo wake wa fedha na mapato.

Mwinyihaji na Duni wote ni mawaziri wa ngazi za juu kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais Ali Mohammed Shein (CCM) na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) na Makamu wake wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi (CCM). Wote wa CCM wanaitetea katiba inayopendekezwa kama ilivyo, na wote kwenye CUF wanaipinga katiba hiyo. CCM inashajiisha kufanyika kwa Kura ya Maoni na kupigiwa ndiyo katiba mpya, CUF inashajiisha isifanyike na ikifanyika hawatashiriki. Huo ni mkwamo.

Jibu la kundi la wahafidhina kwenye CCM kwa mkwamo huu ni jepesi kama zilivyo siasa zao – vunja serikali ya umoja wa kitaifa, bomoa maridhiano. Huu, hata hivyo, si msimamo ambao ungelitakiwa utangazwe hadharani na wana-CCM, ndio maana nilipomuuliza Waziri Mwinyihaji juu ya uhai wa serikali ya umoja wa kitaifa kwenye kiwingu cha kupatikana kwa Katiba Mpya, jibu lake lilikuwa la tahadhari: “Natuangalie msingi wa serikali ya umoja wa kitaifa. Tulidhani kwamba tunapaswa kuishi pamoja, kubakia wamoja, ili kuzika chuki miongoni mwetu. Na hilo litabakia kuwa hivyo.”

Lakini ni vipi litabakia hivyo, ikiwa kuna ushahidi wa hadharani wa viongozi wenzake waandamizi ndani ya serikali na CCM unaoonesha kuwa chama hicho kimeshaamua kuwapa CUF kimoja cha kuamua: ama wapitishe Rasimu Inayopendekezwa au waondoke serikalini.

Kwa hili, anasema Profesa Abdul Sherif, hali haionekani shwari kuelekea Aprili 30 ya Kura ya Maoni ya Katiba. “Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayumba sasa. Kwa sababu chama tawala kilitoka na msimamo mmoja na CUF ikatoka na msimamo mwengine. Wahafidhina sasa wanasema wanataka kubadilisha katiba ya Zanzibar ili kuivuruga serikali ya kitaifa, na kichocheo kikubwa ni katiba mpya. Katiba mpya imekuwa nyenzo ya kuigawa Zanzibar na wala si ya kuiunganisha.”

Kuna matumaini kwamba Mabadiliko ya Kumi ya 2010 kwenye Katiba ya Zanzibar yaliyopitishwa chini ya uongozi wa Rais Amani Karume ina kile kinachoitwa “kufuli” za kufungia – yaani vifungu vinavyozuia kubadilisha mambo ya msingi kwenye katiba hiyo, miongoni mwao ni  huo uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Lakini Maridhiano ya Wazanzibari yanaweza kuvunjwa hata kama katiba inayalinda, maana tendo lenyewe la kuyavunja si la kikatiba halihitaji nguvu wala baraka za katiba. Na kwa kuwa serikali ya umoja wa kitaifa inasimamia juu ya Maridhiano hayo, hayawezi kuvunjika kisha serikali hiyo ikasalimika.

Bali busara ya kibinaadamu na hekima ya kiutu inatwambia kwamba serikali hii haipaswi kufa, maana uhai wa taifa la Zanzibar unaitegemea. Ikifa, Zanzibar nayo imekwenda. Ndio maana wengine tunasema pawe au pasiwe na Katiba Mpya, maridhiano na umoja wa kitaifa wa Zanzibar lazima ubakie.

Kiwango ambacho CUF imeshautangaza mwaka 2015 kuwa “Mwaka wa Maamuzi” ni kiwango kile kile cha kuyafanya maamuzi hayo kuwa ni kuilinda heshima, uhai na mamlaka ya Zanzibar, na kwa msingi huo ni kuyalinda Maridhiano na Umoja wa Kitaifa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.