Miongoni mwa ujasiri wa kuandika tanzia ni kusema uongo kidogo kwa ajili ya marehemu, maana jamii yetu imejengwa juu ya imani kuwa maiti haisemwi kwa ubaya, na hivyo nawe hupaswa kumsifia kwa kila jambo, ikiwemo kuongeza sentensi mashuhuri kuwa “marehemu ameondoka duniani katika wakati ambapo jamii yake ikimuhitaji sana na amewacha pengo ambalo halitazibika.”

Nami wacha niseme uongo huo kidogo kwa ajili ya Salmin Awadhi nisiyemjua, kisha nimuage Salmin Awadh niliyemjua kwa kutokumjua na kumuombea kwa Mungu ampokee hali keshamsamehe makosa yake, maana hakuna mwanaadamu mkamilifu.

Salmin Awadhi nisiyemjua nimemsikia akisifiwa na mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Sera za Kijamii ya Zanzibar, Muhammad Yussuf, ambaye anaandika kwenye ukurasa wa Facebook: “Hapana shaka yoyote ile kuwa kifo cha Mheshimiwa Salmin Awadh kimetuondolea mjenga hoja shupavu katika nyanja ya siasa za Zanzibar. Ingawaje sikukubaliana naye kwa mengi, lakini nimeendelea kumuheshimu kwa umahiri wake na ustadi mkubwa katika kujenga hoja.”

Salmin Awadhi huyo sikumjua, lakini inawezekana kuwa alikuwapo. Niliyemjua mimi ni yule niliyemualika siku moja kwenye kipindi cha Maoni Mbele ya Meza ya Duara baada ya kupitishwa kwa ile iitwayo Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa mwishoni mwa mwaka jana, ambaye hakuwa na uwezo wa kujenga hoja, bali kujenga hamasa.

Lakini kanuni inanitaka nimseme kwa wema. Naam, Salmin Awadhi alikuwa akijua kukitetetea anachokisema kwa hamasa na jazba, hasa hasa linapohusika suala la kulinda kile alichoamini ni siasa ya Chama chake cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar.

Na ni wazi kuwa CCM ililiona hilo ndani ya Salmin Awadhi, ndio maana iliwekeza kadiri ilivyoweza. Ndiye aliyepewa jukumu la kulinda nidhamu ya wawakilishi wenziwe wa CCM katika Baraza la Wawakilishi, nafasi ambayo ina maana kubwa kwenye kujenga ushawishi. Hakuna, kwa hivyo, anayeweza kumdharau kwenye hilo; na CCM ina mengi ya kujisifia kwake.

Lakini hapo pia ndipo penye Salmin Awadh mwengine, ambaye ninadhani ndiye niliyemjua kama mwandishi wa habari na mfuatiliaji wa masuala ya siasa za Zanzibar. Huyo ni Salmin ambaye kwake CCM inatangulia kila kitu, ikiwemo hadhi  na heshima ya Zanzibar yake, ukiwemo Umoja wa Wazanzibari na Maridhiano.

Ni Salmin Awadhi, akiwa kama mnadhimu mkuu na mwakilishi wa watu wa Magomeni kwenye Baraza la Wawakilishi ambaye alitamka kwamba yuko tayari kuwasilisha mswaada wa dharura kupinga serikali ya Umoja wa Kitaifa. Ni yeye – na hilo halisemi kwamba alikuwa peke yake – ambaye alikuwa hachelei wala kukhofia kuikosoa dhana nzima ya Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, akitumia msemo kwamba “bora kila mmoja aende njia yake.”

Katika kipindi cha Maoni Mbele ya Meza ya Duara nilichokitaja hapo juu, nilimuuliza ikiwa anajisikiaje kuwa mpinzani wa maridhiano ya Wazanzibari akiwa kama kiongozi wa kisiasa na Mzanzibari halisi, na jibu lake lilikuwa kwamba “Zanzibar ina historia yake,” akimaanisha historia ya vyama pinzani vya Afro Shirazi (ASP) – ambacho baadaye kiliungana na TANU ya Tanganyika kuunda CCM – na Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) – ambavyo akina Salmin Awadh wanaamini kuwa ndivyo leo vinavyokiunda Chama cha Wananchi (CUF). Historia hii, kwa mujibu wao, inasema kwamba huwezi kuwa na serikali inayoundwa na mahasimu hawa daima visiwani Zanzibar.

Zanzibar, kwa mujibu wake, ilipaswa kutawaliwa na CCM pekee, ambayo ina historia ya Mapinduzi ya 1964 kupitia ASP. Hakuna namna ambapo Zanzibar inaweza kuwa mikononi mwa wale wasio na mizizi kwenye Mapinduzi hayo, na hivyo ni doa kubwa kuwa na CUF kwenye serikali ya sasa ya Umoja wa Kitaifa.

Ni bahati mbaya sana, tena sana, kwamba rikodi ya mwisho ya Salmin Awadh kwenye akili za wengi hadharani, ni mkanda wa vidio ambao unamuonesha akihutubia kwenye mkutano wa hadhara wa chama chake katika jimbo lake la Magomeni, ambapo alitamka maneno yafuatayo kwa jazba na hamasa kuu:

“Mumeiona mizinga ya kivita?” Anawauliza waliohudhuria kwenye mkutano huo, ambao nao wanaitikia “ndiyo”, wakimaanisha waliiona mizinga hiyo. Yumkini wakikusudia maonesho ya silaha za kivita kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi mwaka jana visiwani Zanzibar. Kisha anaendelea Salmin Awadh: “Sasa wao (wapinzani) kama wana ubavu, basi wachukuwe (serikali). Lakini hatutotoa (madaraka ya kuongoza serikali) kwa kura. Mutapiga kura katika chaguzi zote, na Chama cha Mapinduzi kitashinda.”

Kwa kauli zake, Zanzibar haikuwa salama, maana ilikuwa inapaswa kupoteza serikali yake ya Umoja wa Kitaifa na kuyavunja Maridhiano. Ilikuwa inapaswa kumwaga damu ikiwa wananchi walikuwa wanataka kubadilisha utawala, maana mizinga ya kijeshi isingeruhusu serikali kuchukuliwa kwa kura.

Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba CCM imempoteza mwanasiasa wake mwenye uthubutu mkubwa ndani ya rubaa za mikakati ya kisiasa Zanzibar. CCM ina mengi ya kulilia kwa kifo cha ghafla cha mjumbe wake huyu kwa Kamati Kuu.

Lakini sina hakika kama Zanzibar – kama taifa – ina mengi ya kulilia, zaidi ya kumuombea dua kwamba Mwenyezi Mungu amughufirie madhambi yake. Nasi tujiombee kuwa ukifika mwisho wetu, basi atupe mwisho mwema, maana hii dunia ni mapito.

Anaandika mshairi wa Kizanzibari, Nassor Barsheiba:

Tuitizame kauli, mja anapoitowa
Ikiwa ni ya ukweli,  na wengi hufurahiwa
Ikiubeba muhali, na umati huchukiwa
Zile zenye ukatili, na umma hulaaniwa
Asemaye ya halali, dua njema huombewa.

2 thoughts on “Kwaheri Salmin Awadh Salmin”

  1. Asalam aleikum!
    Kwakweli haya maelezo ni mazuri sana lakini bado tunawashangaa nyinyi waandisha kwa kushishitiza kuwa dini ya Kiislam hairuhusu kuisema maiti vibaya na wengine hudiriki kusema kama munaanza kumsema vibaya huuyu Marehemu basi musicoment kwenye wall yangu sasa kweli huu ni uhuru wa mawazo? kwa maoni yangu mini ingawa kweli ipo hadith ya Mutume (S.A.W) kuwa tuwazungumze kwa uzuri maiti zetu lakini pia haikatazi kumsema vibaya kama alikuwa ni mtu mbaya.
    kuna hadith inasema siku moja Mtume (S.A.W) alikuwa amekaa na maswahaba zake basi likapita jeneza wale maswahaba wakamasema vizuri yule marehemu na wakasema ni mtu mwema na Mtume (S.A.W) akasibitisha hilo mara likapita jeneza jengine wale maswahaba wakamsema yule marehemu kwa ubaya kala alikuwa ni mtu muavu basi na Mtume (S.A.W) akasibitisha kama ni kweli kwa hiyo maswahaba wakamuuliza kwanini mara zote 2 yeye Mtume (S.A.W) alikubaliana na yale wanayosema wale aliokaa nayo kuwa ni kweli ndipo Mtume (S.A.W) akawaambia kuwa hawa watu walioko ulimwenguni ni mashahidi wa yule marehemu mbele ya Allah.
    Kwahiyo Salum Awadh mimi si mjui maana sijawahi kumuona wala kuzungumza nae lakini nafuatilia siasa za kwetu na namsikia akisema maneno maovu juya wale anaowaona ni wapinzani wa CCM na nimmoja wa wale tunao waita madalali wa kuiuza Zanzibar na nimmoja wa wale CCM walioko mstari wa mbele kutaka kuivunja serikali ya umoja wa kitaifa kwa hiyo si rahisi kwa watu kumsema kwa wema labta kwa lale wasaliti wenzake. Allah amseamehe makosa yake kwa yale aliyo mkosea yeye lakini aliyowakosea Wazanzibar hiyo ni yeye na Wazanzibar.

    1. Kwa hakika sijui ikiwa ni makatazo ya kidini kutokumsema aliyetangulia mbele ya haki au ni utamaduni wetu tu lakini nilicho na hakika ni kuwa hili la kuandika marehemu alikuwa mtu mwema, na ambaye pengo lake halitozibika ndio mazoea

Leave a Reply to Chris Cancel reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.