Mkanda wa sauti iliyonaswa kwenye mazungumzo yanayoaminika kufanywa na Waziri wa Tawala za Mikoa visiwani Zanzibar, Haji Omari Kheri, na “watu wake“, yumkini akiwa kijiji cha Jongowe, Tumbatu, umesambazwa mitandaoni.

Kwenye mazungumzo hayo, anasikika mwakilishi huyo wa jimbo la Tumbatu akipanga mikakati ya kuwapata watu wa Tumbatu ambao wanaunga mkono Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchukuwa nafasi za ukurugenzi kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, yumkini kukisaidia chama hicho, akisema hayo ni maamuzi ya Kamati ya Siasa ya chama hicho kinachotawala.

“Tumepania sasa. Ndio nia yangu. Maana yake mbali ya wale ambao sasa hivi hawana kazi, lakini hata wale ambao wana kazi, lakini wenye muelekeo wetu ni wepi tunaweza tukawaombea posts (nafasi)! Nyie ndio munaowajua…“, anasikika kiongozi huyo ambaye amekuwa waziri mwandamizi serikalini kwa takribani miongo miwili sasa.

Mwezi uliopita pia, vidio nyengine ya kiongozi huyu wa serikali ilisambazwa akihutubia mahala fulani katika mkoa wa Kaskazini Unguja, akiapa kwamba vijana watakaojaribu kuharibu maskani na mali za CCM, wataishia kukamatwa na kutendewa kama yale wanayotendewa viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Tanzania Bara. Miongoni mwa wanaotendewa masheikh hao, inasemekana, ni kuingiliwa kinyume na maumbile.

La kwamba CCM na serikali zake wanawateuwa watu kushika nafasi za juu kiutendaji serikalini kwa misingi ya ufuasi wao kwa chama hicho ni jambo linalofahamika, ingawa hiyo haimaanishi kuwa ni jambo sahihi. Hli linamaanisha kuwa kiongozi mwandamizi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa anashiriki kupanga mikakati ya kuihujumu serikali hiyo kwa misingi ya “huyu ni mwenzetu na yule si wetu“. Ni siasa za maji ya karo.

La kwamba kiongozi wa Serikali ya Zanzibar anawatishia Wazanzibari wengine kuwa watachukuliwa na kupelekwa korokoroni Bara, ambako watatendewa ukatili kama wanaotendewa leo viongozi wa Uamsho, ni kiwango cha chini kabisa cha adabu za kisiasa. Jamii ya watu wa kaskazini anayotokea yeye Haji Omari Kheri ina sifa mbili kubwa – kujituma na kufanya dhikri. Ni watu wa dini na wacha Mungu. Taasisi ya Uamsho ina ufuasi mkubwa kaskazini ya Unguja kwa sababu ya khulka ya jamii ya huko kupenda dini.

Sio tu kwamba kauli kama hizi zinaonesha ukosefu wa uadilifu wa kiongozi huyu na mfumo anaouwakilisha, bali zaidi zinaonesha ukosefu wa nidhamu ya kisiasa kwenye mfumo wa utawala wa sheria. Kwengineko duniani ambako heshima kwa utawala wa sheria na haki za binaadamu ni jambo la msingi kwa kiongozi, Haji Omari Kheri angelikwishapoteza zamani nafasi zake za kisiasa kwa kile kilichoibuliwa na kauli zake hizi, na yumkini akawa ameshapandishwa kizimbani.

Yafuatayo ni mazungumzo yake na “watu wake“ kama yalivyonukuliwa kwenye vidio ya sauti iliyopo sasa mitandaoni. Yasome kisha ujiulize ikiwa Zanzibar inayopigania kujenga jamii ya kidemokrasia na utawala wa sheria inamuhitaji kiongozi wa aina hii.

Haji Omari Kheri: Maazimio yake ni hicho kikao cha kamati ya siasa sasa cha kuja kutoa mambo. Kwenda kutengeneza “databenki“ (yumkini anakusudia database)kujua ni akina nani wetu – maana tulishashema kuwa wakurugenzi si wetu, sasa tunawatengeneza wakurugenzi wengine, ili mimi nikipata nafasi ya kuzungumza na Bwana Mkubwa niseme Khalidi Zuberi… mbona hamuniulizi Khalidi Zuberi gani… Maalim Ali Mtumwa, Bamtumweni. Tumepania sasa. Ndio nia yangu. Maana yake mbali ya wale ambao sasa hivi hawana kazi, lakini hata wale ambao wana kazi, lakini wenye muelekeo wetu ni wepi tunaweza tukawaombea posts (nafasi)! Nyie ndio munaowajua… Tumefahamiana? Kwa hivyo kuwe na data benki mbili – kuna data benki ya wale ambao miye nawajua, lakini ikitoka kwenu ntafurahi zaidi. Mimi sio kwamba siwajui… miye nawajua, lakini ikitoka kwenu, si ndio “priority“ yenu? Kwa hao walioko serikalini, miye nawajuwa watu wa kuwapa umuhimu na kipaumbele. Lakini hawa wapya hawa…

Mtu Mwengine 1: Hawa wapya ndio tutakutengenezea. Kama unawajuwa, wafanyie tu.

Mtu Mwengine 2: Lakini jambo jengine…

Haji Omari Kheri: Lilikuwa lipi lile?

Mtu Mwengine 2: Hawa jamaa zetu. Kwa nini upinzani?

Haji Omari Kheri: Ahaaa… Kwa nini upinzani? Mimi kwa kweli sielewi, kwa sababu ndugu zetu Wapemba…. Kwa sababu tu wanataka

Mtu Mwengine 2: ….Wanataka?

Haji Omari Kheri: ….wanataka Sefu asishshhhh… (inaonekana alikuwa anasema “ashinde” lakini rikodi ya sauti ni mbaya kusikika) mwanzo walikuwa wakisema wapate rais Mpemba, lakini Sheni wanamuona kama sio Mpemba, kwa sababu kweli kachanganya… Kwa ivyo wao utawaelewa hivyo. Sisi (Watumbatu) tungepaswa kubakia kwenye “opposition” kama tungekuwa hatujapata mafanikio. Sizungumzi Jongowe kwa jumla, kwa peke yake, nazungumza as a Tumbatu. Historia ya Tumbatu ilivyo mpaka mwaka 64, barua mpaka aje Maalimu Taibu ndiyo anasoma barua ya mtu. Kushanifahamu? Hakuna Mtumbatu ambaye ameenda shule mpaka 64.

One thought on “Haji Omari Kheri bado una moyo wa kuongoza?”

  1. Sasa mtu kama huyu akija akifa watu wakimsema vibaya munaanza kulalamika kama dini hasemi hivyo waislam wanataka waombeane dua njema! lakini munashindwa kufafanua hapa kwani wanaotakiwa kuombewa dua njema ni waislam sio wale wanafiki wanaodhulumu na kuwatesa wanziwao na kuchochea mifarakano. Kwa kweli kumsema mtu mbaya sio kosa maana hata Abduli ibn Selul alikuwa akiswali nyuma ya Mtume S.A.W alini M/mungu alikataa hata asiswaliwe alipokura kwa ubaya wake kwehiyo tunatakiwa tujitahidi kufanya mema na kuwafanyia watu mema tukifa angalau watu watukumbuke kwa wema wetu sio kwa ubaya wetu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.