Zanzibar iliingia katika historia ya kupewa uhuru wake kutoka kwa Muingereza na serikali ya kwanza ikaundwa visiwani katika uongozi wa Waziri Mkuu Mohamed Shamte chini ya utawala wa kifalme.

Nimepitia tena katika nyaraka zilizovujishwa na mtandao wa Wikileaks na kukuta mazungumzo ya faragha yaliyofanyika baina ya Ali Sultan Issa na Ujumbe wa Balozi wa Marekani ambaye naye akautuma kwa wahusika kama ilivyo ada yao.

Ali Sultan aliulizwa kama alikuwa na uhusiano na Oscar Kambona wakati alipokuwa uhamishoni nchini Uingereza. Majibu yake ni kwamba hawakuwa katika mazungumzo yoyote na Kambona na akafika mbali zaidi ya kumuita Kambona ni Mbaguzi. Anasimulia zama za kupigania uhuru walipokuwa katika mkutano wa umoja wa vijana ulioandaliwa na serikali ya kikomunist ya Urusi, ambao Kambona aliiwakilisha TANU, huku yeye Ali Sultan akiwa ni muwakilisha wa Umma Party.

Anaeleza walipokutana katika ukumbi wa majadiliano, Kambona akamshambulia Ali Sultan kwa maneno machafu akimuita Muarabu ambaye hakupaswa kuiwakilisha Zanzibar. Ikafika hadi akamfurusha katika sehemu ya malazi yaliyoandaliwa kwa ajili ya Waafrika naye Ali Sultan kuishia kukodi sehemu pamoja na wasomali tena kwa gharama zake mwenyewe baada ya Kambona kushiriki katika kadhia ya ubaguzi dhidi yake.

Nimeeleza hadithi hii kuonyesha namna ya masuala ya kabila na asili za watu zilivyochangia kuzima ukweli na kuweka propaganda katika mambo ambayo hayahitaji kupotoshwa kwa vile ni sehemu ya historia isiyobadilika.

Tarehe 10 Disemba 1963 ilikubaliwa kuwa siku ya uhuru wa Zanzibar na kila upande wa kisiasa visiwani na tukio hili ndilo lililotoa mwanya wa kuwezekana Mapinduzi ya 12 Januari 1964, ambayo inawezekana yalilenga mabadiliko ya utawala wa kidemokrasia lakini yakazaa makubwa yaliofuta na kuuatia dosari malengo ya mapinduzi yenyewe.

Binafsi si mpenzi wa utawala wowote wa urithi kuanzia uchifu mpaka ufalme ambao huondoa demokrasia pana ya uongozi wa wananchi kwa nchi. Hivyo nafahamu changamoto za uhuru uliotolewa kwa kuundwa kwa serikali ambayo ilikuwa na mapenzi kwa mfumo wa utawala wa monarchy badala ya jamhuri yenye uwakilishi wa wananchi moja kwa moja. Kwa njia moja au nyengine kulikuwa na hoja ya kuubadili mfumo uweze kuendana na kiu ya wananchi walio wengi waliotamani mabadiliko ya uongozi usio na ishara za urithi wa kudumu.

Kinachosikitisha ni kwa makusudi kufuta historia muhimu ya uhuru ambao uliondosha utawala wa kiingereza wenye misngi yote ya kikoloni katika Afrika Mashariki nzima. Sifahamu kwa nini iwe sawa kwa Kenya, Tanganyika na wengine waliotawaliwa na muingereza kushehereka uhuru wao lakini kwa Zanzibar tukapuuza huku tukitaka kuamini kwamba bila ya muingereza kuutoa uhuru mapinduzi yangeliwezekana.

Sifahamu kwa nini tufiche ukweli wa uhuru uliotufanya kuweza kupandisha bendera katika umoja wa mataifa, tukafungua balozi katika nchi tafauti lakini bado tuamini kwamba Mapinduzi na mafanikio yake yatazimwa na tarehe ya uhuru kutoka kwa Muingereza. Kuficha historia kwa misingi ya propaganda katika karne hii ni kujipalilia makaa ya kuzipa nguvu conspiracies zisizihotajika katika ujenzi wa taifa na maendeleo ya nchi.

Inawezekana kulikuwa na umuhimu mkubwa wakati ule kuficha ukweli, lakini baada ya miaka hamsini ya mapinduzi kuna faida gani kubaki na itikadi ya kuficha ukweli usio na taathira yoyote kwa jamii na nchi kwa ujumla?

Ninachokiona ni chuki kubwa zilizopandwa za kuchukia jamii zetu kiasi kwamba tumekuwa wazuri kuwapigia magoti wakoloni wa kiingereza waliojineemesha kwa siasa za wagawe uwatawale na kutufanya tuamini kwamba ni waarabu, wahindi na hata waafrika waliowafiki mfumo wa monarchy kuwa ni maadui wakubwa wasiohitajika nchini.

Kuwapo kwa mfumo wa kifalme na kudumu kwake ni kwa sababu ya ulinzi wa Uingereza na ndio iliowafiki kuwapo kwa matabaka ili kuvunja umoja wa wananchi uliokuwa na tishio kwao. Kuufuta uhuru huu kwa vile tu ulipelekea kupatikana kwa serikali ilioegemea kwa mfumo wa kifalme hautaweza daima kueleza ukweli wa hali halisi ilivyokuwa au hata kujustify mapinduzi kwa vile taswira iliopo ni kwamba serikali iliochaguliwa na wananchi na kukabidhiwa uhuru ilipinduliwa na kufichwa ukweli wake wakati inawezekana kuweka ukweli mbele kwamba ASP ilikuwa na wingi wa wapiga kura na kushindwa kwake kuongoza nchi kulitokana na upendeleo wa sheria zilizoegemea upande mmoja.

Ukiangalia hadithi ya Ali Sultan utafahamu athari ya ubaguzi baina ya Waafrika na Waarabu kiasi kwamba muarabu wa kiafrika hawezi kujivunia uafrika wake bila ya kuwekewa shaka na hata uarabu wake kwa vile bado anabaki na asli ya kiafrika aliozaliwa na kukulia nayo. Unaposikia Kambona kamfukuza Ali Sultan kwa sababu ya rangi yake utafahamu kwa nini ubaguzi uliopewa taswira ya kukataa mabeberu imekuzwana kutukuzwa kama ndio njia sahihi ya kuutwaa uafrika na kuutukuza.

Tusome namna ya Mandela alivyoweza kuongoza Afrika ya Kusini yenye raia wa rangi tafauti kwa usawa na kuweka mbele zaidi utu, heshima na uadilifu wa kuhakikisha hakuna yeyote ambae ataweza kujihakikishia haki kubwa zaidi ya mwenziwe kwa misingi yoyote zaidi ya sheria za nchi. Naamini sababu kubwa ya kuendelea na propaganda dhaifu na yenye kuifedhehesha historia yetu ni dhana ya kufikiri uhuru utaondosha uhalali wa mapinduzi wakati ukweli ufichwaji wa ukweli huu unatoa mwanya zaidi ya masuali mengi bila ya majibu na baya zaidi unawapa fursa ya wachocheaji kuwa mbele na simulizi isiojadilika.

Binafsi kama Mwafrika, nathamini siku ya leo iliotoa mwanya wa kuondokana na utawala wa mkoloni wa Kiingereza aliyetawala Afrika kwa fujo na fitna baina ya waafrika wenyewe. Na masikitiko yangu yanakuja pale waafrika wa kila rangi kuendelea kubeba fikra na chuki zilizopandikizwa katika kila pande kiasi kwamba uadui ukawa miongoni mwetu kutokana tu aila zetu na tukasahau mkoloni halisi anaendelea kututawala kifikra na kutuaminisha ni rafiki wa maslahi yetu.

Pale tutapokubali kuwa wakweli, tukaombana radhi tulipokosana na kuzichukuwa historia zetu kama kurasa za kuelimishana kwa mazuri na mabaya ya nyuma ndipo tutapoweza kujikunjuwa katika minyororo ya kikoloni iliofungashwa zaidi katika vichwa na kutupa uhuru wa kuthaminiana bila ya vikwazo vya aila, rangi na historia zetu.

*Makala ya Foum Kimara kwenye mtandao wa Facebook, tarehe 10 Disemba 2014.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.