Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa mwaka 2010 baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu imesaidia kumaliza uhasama, chuki, dharau na mambo mengine ambayo yaliwagawa Wazanzibari tangu ulipoingia mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka 1992.

Tangu wakati huo uliopoanza mfumo wa vyama vingi na hususani ulipofika wakati wa uchaguzi kulizuka mambo mengi ambayo yalitokana na masuala ya kisiasa kati ya vyama vya CCM na CUF na kusababisha wananchi wa kawaida kushindwa kusalimiana na kuzikana.

Hali hiyo iliwaathiri Wazanzibari wengi na haikuleta tija kwa maisha yao ya kila siku kwa kuwa wananchi walikuwa wanahitaji siasa za upendo na kuvumiliana.

Waziri kiongozi mstaafu wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha anasema hali ya utulivu iliyorejea kuanzia mwaka 2010 inaweza kutoweka kutokana na vitendo vya wanasiasa wanaoeneza siasa za chuki na matusi hususani kwa viongozi wa kitaifa.

Anasema lengo kubwa la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), lilikuwa ni kuzika tofauti za kisiasa zilizoanza tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi ambavyo vimeleta madhara makubwa.

Kwa sasa anasema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipanda katika majukwaa bila aibu na kumtukana kiongozi wa kitaifa, jambo ambalo linaweza kuhatarisha SUK kuvunjika.

Anawataka wanasiasa kuacha malumbano na chuki badala yake washiriki katika kuibua ajenda zitakazoleta mabadiliko kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na kwamba kuendelea na tabia ya malumbano hakujengi misingi ya demokrasia.

Nahodha anasema wakati umefika kufunguliwa mjadala wa ajenda ya maendeleo na kuachana na siasa za malumbano ambazo zimerudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar.

Alifahamisha kuwa sasa kinachohitajika ni nguvu za kisiasa za kufikia lengo la kuwa na bandari huru na kuimarisha huduma za afya, elimu ambazo anasema hazijakamilika.

Kuhusu Katiba Mpya, Nahodha anamshangaa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kupinga rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Anasema kupitia Katiba Mpya inayopendekezwa Zanzibar itakuwa na fursa ya kukopa nje na kuwapo chombo cha kusimamia mapato na matumizi ya fedha zinazopatikana kupitia vyanzo vya mapato vya Muungano.

Kuhusu suala la mafuta, Nahodha ansema Katiba Mpya inayopendekezwa limeondolewa katika mambo ya muungano na kwamba Wazanzibari hawanabudi   kuipigia kura ya ndiyo wakati utakapowadia.

Suala la urais wa Zanzibar anasema, Katiba Mpya inayopendekezwa Rais wa Zanzibar atakuwa Makumu wa Pili rais jambo ambalo limeleta faraja kwa Zanzibar.

Sambamba na hayo anawataka wanachama wa CCM na wananchi wa Zanzibar kuipigia kura ya ndiyo Aprili 30 mwakani, ili waweze kupata katiba bora yenye maslahi kwa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Nahodha anasema muundo wa serikali tatu haukuwa muafaka na utekelezaji wake ungekuwa mgumu kama ilivyokuwa imependekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba.

Anasema Bunge Maalum la Katiba lilitafakari mfumo huo na kuona utekelezaji wake ulikuwa mgumu na kuamua kubaki katika muundo wa serikali mbili kwa maslahi ya muungano wenyewe pamoja na wananchi wake.

“Lazima wananchi mfahamu tulitafakari mfumo wa Muungano wa Mkataba na ule wa Serikali tatu tukaona utekelezaji utakuwa mgumu, na mfumo wa muungano wa Serikali tatu haukuwa na ubavu wa kuleta mamlaka kamili ya Zanzibar,” anasisitiza Nahodha.

Aidha,  alisema wapo Wazanzibari  wanaamini  Zanzibar nje ya  Muungano  itakuwa tajiri jambo ambalo siyo kweli kwa sababu Zanzibar ilitawaliwa na wakoloni kwa miaka 200 nyuma kutoka Oman na hadi Mapinduzi ya mwaka 1964 ilikuwa nyuma kimaendeleo na huku Wananchi wake wakiishi katika nyumba zilizoezekwa Madebe.

Anasema ni muhimu wananchi wakasoma rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na bunge la Katiba kabla ya kufanya maamuzi kupitia kura ya maoni itakayofanyika mwakani.

Anataja mambo ambayo Zanzibar imenufaika nayo katika Katiba mpya ni pamoja na suala la mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya muungano, uwezo wa Zanzibar  kujiunga na jumuiya za kikanda.

CHANZO: NIPASHE, 10 Disemba 2014

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.