Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (pichani), amesema kumekuwapo na wimbi kubwa la uvunjwaji wa haki za binadamu unaosababishwa na vyombo vya dola pamoja na wananchi.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Haki za Binaadamu Duniani yaliyowashirikisha wanachama wa jumuiya mbalimbali zisizokuwa za kiserikali. Alisema vyombo vya dola hutumika kuvunja haki za binaadamu, lakini ni ukweli usiopingika kwamba wananchi nao wanahusika. Alieleza kuwa ni jukumu la kila upande kuhakikisha unatekeleza wajibu wake kulinda na kusimamia haki za binaadamu na elimu ienezwe kwa wananchi wote. “Hebu tujiulize vile vilio vya kukiukwa haki za wafungwa na walio vizuizini, ubakaji, watu kunyimwa fursa za kujumuika na kutoa maoni yao, mateso kutoka vyombo vya dola na rushwa havisikiki tena?” alihoji Maalim Seif. Alisema kwa mtazamo wake, vitendo hivyo bado vipo na vinazidi kuongezeka kwa kasi na ndiyo maana kuna watu hawaoni shida kupoteza maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi au wazee kwa imani za kishirikina. Jumuiya zisizokuwa za kiserikali Zanzibar katika Tamko lao zimesema zinasikitishwa kuona baadhi ya taasisi za kusimamia haki za binaadamu zimekuwa zikiongoza katika kuzivunja haki hizo. Akisoma tamko hilo, Fatma Said alisema kuna watendaji wa Idara za Mahakama, Polisi, Masheha na mamlaka zinazosimamia ardhi wapo mstari wa mbele kuvunja haki hizo. Mwenyekiti wa kituo cha huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Profesa Chris Maina Peter, alisema kuna haja jamii na wadau wote kuliona suala la kulinda haki za binaadamu ni la kila siku na siyo kusubiri wakati wa maadhimisho pekee.
CHANZO: NIPASHE, 11 Disemba 2014