MBUNGE wa viti Maalum, Mariam Msabaha (CHADEMA), amemuonya mbunge mwenzake wa Mpendae kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Turky na kumtaka aache tabia ya kutumia madaraka na kinga za kibunge kunyanyasa wananchi katika masuala yasiyohusiana na siasa.

Mbali na kumuonya kwa tabia ya unyanyasaji, pia Msabaha amesema mbunge huyo anapaswa kuwaomba radhi wabunge wenzake wa kutoka Zanzibar, kwa kile alichoeleza kuwa tabia ya kujisifu, kukebehi na kuonyesha jeuri wananchi, kwani si asili na utamaduni wa wazanzibari.

Kutokana na hali hiyo, Msabaha alisema anajiandaa kukabidhi CD za vitisho vilivyofanywa na Turky, ofisi ya Spika wa Bunge kwa ajili ya hatua zaidi.

Msabaha, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea taarifa mbalimbali zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari vinavyomuonesha Mbunge Turky, akitoa lugha ya kuudhi kwa wananchi mbele ya askari Polisi.

Katika mitandao hiyo, pamoja na CD iliyogawiwa kwa waandishi wa habari na Msabaha, Turky, anakaririwa akiwaeleza washindani wake katika mgogoro wa msikiti wa Sunni, kuwa ni sawa na CHADEMA huku akiwaeleza kuwa hawana jambo lolote watakaloweza kufanya zaidi ya kupiga kelele.

Msabaha, alisema kuelezea kuwa CHADEMA haiwezi kufanya jambo lolote ni matusi na kukengeuka kwa mbunge huyo, kwa kuwa hata wananchi waliomchagua hawaujui msaada wake zaidi ya kusikia akiongoza migogoro katika matukio tofauti.

“Kwanini Turky atumie ubunge wake kama fimbo ya kuwanyanyasa wengine katika masuala ya kijamii, mfano ni hivi karibuni alipowajaza askari katika ukumbi wa uchaguzi pale Blue Pearl wakati waumini wa madhehebu ya  Sunni walipokuwa wakifanya uchaguzi, lengo lake likiwa ni kuwatisha na kuwaweka watu anaowataka yeye, huku akiwatambia wapinzani wake kuwa hawana sauti kama CHADEMA, hapa anakiingizaje chama chetu katika masuala binafsi ya kiimani,” alisema Msabaha.

Aliongeza kuwa watu wanaopewa mamlaka ya kuwaongoza wananchi na kuamua kuyatumia vibaya mamlaka hayo kwa kuwatisha waliompa nafasi hiyo, mwisho wake huwa ni machafuko makubwa na kwamba Mbunge Turky anataka kuleta hayo machafuko.

Alisema kiburi cha Turky kimepitiliza hata kwa mamlaka za Umma, kwa kile alichoeleza kuwa hivi karibuni ofisi ya msajili wa vizazi na vifo (RITA), iliagizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania ithibitishe wapiga kura wa baraza la wadhamini wa msikiti wa Sunny, lakini Mbunge huyo akalazimisha kufanyika kwa uchaguzi na kujaza polisi idadi ambayo haikutegemewa.

Jitihada za kumpata Turky kuelezea tuhuma za kutumia madaraka yake ya kibunge kuwanyanyasa wananchi na kukidhalilisha CHADEMA, zilishindikana baada ya simu yake ya kiganjani kutokupokewa na hata alipotumiwa ujumbe wa maneno hakujibu

CHANZO: TANZANIA DAIMA.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.