Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akifafanua jambo.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akifafanua jambo.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameeleza tofauti yake na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akisema imesababishwa na watu aliowaita wapambe.

Zitto (37), ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa Chadema, alisema kuwa hata kuvuliwa nyadhifa zake ndani ya chama kulisababishwa na wapambe hao, lakini akasisitiza kuwa hana kinyongo tena kwa kuwa alishamwomba Mungu na sasa amesamehe kabisa.

Tofauti za wawili hao hazijawahi kutolewa hadharani licha ya mitandao mbalimbali kuzungumzia kuharibika kwa uhusiano wao ikinukuu habari kutoka vikao vya ndani vya Chadema.

Hata hivyo, mapema mwaka huu, Zitto alirushiwa tuhuma nzito na Chadema kutokana na uhusiano wake na baadhi ya makada wa CCM, lakini mbunge huyo aliyahusisha maneno hayo na mwenyekiti wake na aliandika maneno makali dhidi ya Mbowe kwenye ukurasa wake wa facebook.

Lakini katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika wiki iliyopita nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam, Zitto alionekana kujutia kuharibika huko kwa uhusiano wao na kusema “wapambe ndiyo wanatugombanisha”.

“Sina shida yoyote na Mbowe, naamini ipo siku tutagundua wapambe walituathiri na ndiyo waliotufikisha hapa,” alisisitiza Zitto bila kutaja ni kina nani hasa.

Zitto alisema yeye na Mbowe wametoka mbali tangu akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hafurahii uhusiano wao ukiishia katika hali hiyo.

“Naumia sana, lakini naamini ipo siku ama nikiwa hai au nimekufa watu wataujua ukweli,” alisema mwanasiasa huyo kijana aliyepata umaarufu kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja.

Alisema, akiwa mwenyekiti wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu (Daruso) yeye na mwenyekiti wake ndiyo waliokijenga chama wakati huo Mbowe akiwa mbunge wa Hai.

Alisema wakati huo Mbowe alikuwa akienda chumbani kwake kusuka mikakati ya kuiinua Chadema na kwamba walikuwa wakila chips pamoja na wakati mwingine kwenye klabu ya usiku ya Bilicanas inayomilikiwa na Mbowe.

“Wakati mwingine naangalia, naumia sana. Wakati tunafanya hayo yote wengine walikuwa CCM, wengine walikuwa wafanyabiashara, lakini sasa ndiyo wana sauti katika chama,” alisema Zitto.

Zitto alisema kuwa wakati huo walikuwa na kampeni yao waliyoiita ‘Real Madrid’ ambayo ilikuwa na lengo la kuingiza kila mwanasiasa bora katika chama chao.

Real Madrid ni klabu ya soka ya Hispania yenye mafanikio makubwa duniani na sera yake ni kusajili wachezaji nyota duniani kwa gharama zozote.

“Na kweli tulifanikiwa na kuongeza wabunge kutoka watano hadi 48 wa sasa,” alisema.

“I real miss that (nakumbuka sana). Naumia sana, mimi leo sina maelewano na watu ambao tulikuwa nao katika mapambano. Lakini nasononeshwa zaidi na kitu kinachoendelea ndani ya Chadema.

“Nini kimetokea Chadema? Kwa nini tumejikuta tumeondoka katika mstari? Tupo wabunge 48 bungeni sasa, lakini hatusogezi mbele nchi, tumerudi nyuma wakati huo tulikuwa watano lakini tulikuwa tunaenda vizuri sana.”

Akizungumzia jinsi wapambe walivyoharibu uhusiano wao, Zitto alisema kuna siku Mbowe alimtuhumu kuwa ameanzisha chama cha umma, pia akasema ana majina mawili tofauti katika mtandao wa Jamii forums ambayo anayatumia kuwasema viongozi wa Chadema.

“Kukatokea vurugu, baadaye nikasema naondoka. Ile nataka kutoka wabunge wakanizuia mlangoni nisipite, waliponizuia nilikuwa na hasira sana, nikawaambia lazima nitoke. Waliponizuia hasira zikanipanda nikaanguka chini nikalia sana, yaani sana” alisema akionekana mwenye hisia huku machozi yakimlengalenga.

Kwa mujibu wa Zitto, jioni ya siku hiyo walijikuta wamekaa meza moja na Mbowe na baada ya kuzungumza waligundua kuwa walikuwa wamelishwa maneno.

“Tulizungumza na wote tulilia sana. Wakati kama huu nikikumbuka nasikia uchungu kwa sababu ni wapambe wametufikisha hapa,” alisema.

Hata hivyo, Zitto alisema kuwa migogoro ni sehemu ya maisha na kwamba yeye anachukulia kama changamoto kwa kuwa hakuna njia inayonyooka moja kwa moja na hiyo ni sehemu ya kuendelea kumkomaza.

“Mmoja wa viongozi ambao ni role model wangu ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Malaysia, Mahathir Mohamad ambaye kila mwezi Oktoba huwa nakwenda Malaysia kuonana naye.

Mwaka jana wakati vurugu hizi zimeanza kushika kasi, watu wakaniambia unaweza vipi kukabili mambo kama haya, ila Mahathir ambaye alifukuzwa kwenye chama chake akiwa mbunge na baadaye akaja kuwa Waziri Mkuu, aliniambia hizi ni changamoto ambazo lazima upite,” alisisitiza Zitto.

Aliongeza kuwa hata Makamu wa Rais wa Kenya, Raila Odinga, alionana naye mwanzoni mwa mwaka na akamshauri asikate tamaa na kumweleza kuwa yeye hajafikia hata robo ya changamoto ambazo amepitia.

“Kwangu mimi changamoto hizi ni kukomazwa na sizungumzii kuonewa au kutoonewa, what I know (ninachojua) ni kwamba sijafanya kosa lolote na kwangu mimi nimesamehe na sina kinyongo na mtu yoyote.”

Mwaka huu baada ya msiba wa mama nimekwenda Umra Maka nimemuomba Mwenyezi Mungu na nimetoa vinyongo vyangu vyote na nimesema I have to move on (sina budi kusonga mbele) katika maisha yangu, sina chuki na tatizo na mtu.

“Huwezi kujua huko mbele mtakutanaje, just few months ago (miezi michache iliyopita) wabunge wa Chadema waliwaambia wabunge wa CUF kuwa ni mashoga, lakini leo ni marafiki.

Alikuwa akirejea kauli ya Chadema kuwa CUF ni mwanachama wa taasisi ya kimataifa ya kiliberali ambayo moja ya misingi yake ni kutetea usagaji, ushoga na ndoa za jinsia moja.

“Hivyo ndivyo ninavyoiona na huko mbele usishangae kuona tunafanya kazi pamoja. Kwangu mimi nimeshasahau kila kitu nimelia Umra na kila kitu nimesamehe,” alisema.

Alipoulizwa sababu za kutomfuata Mbowe ili wayazungumze na kuondoa tofauti zao, Zitto alisema sasa hivi siyo muda wa kumbugudhi kwa sababu yuko bize na Ukawa na uchaguzi, lakini anachoamini kuwa hata kama yeye Mbowe hatutakuwa hai, ipo siku itagundulika kuwa huu mgogoro ulipikwa na wapambe tu.

Akizungumzia uhusiano wake na katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, mbunge huyo alisema kuwa alikuwa na ukaribu wa kikazi tu na katibu huyo kutokana na kuwa kiongozi wake bungeni.

Kutelekeza ofisi

Akijibu tuhuma za kutelekeza ofisi ya naibu katibu mkuu, mbunge huyo alisema kuwa hizo ni tuhuma kama tuhuma nyingine na kwamba alikuwa anafanya kazi zake kama kawaida na kuhudhuria vikao, lakini kuna taratibu za kikatiba za kushughulika na jambo kama hilo.

“Hamuwezi mkakaa miaka miwili siji ofisini halafu mnakurupuka na kusema tumemfukuza kwa sababu alikuwa haendi ofisini. Kuna taratibu za kikatiba kwa mtu ambaye hashughuliki na kazi za chama au vikao mfululizo.

Kwa nini taratibu hizo hazikutumika wakati hiyo ni justification (uthibitisho) za mambo ambayo yalitokea, ambayo nisingependa kuyarejea kama vilivyosema hapo mwanzo.” aliongeza.

“Kazi za siasa siyo za ofisini ni kazi za field na kazi za field nimezifanya kwa kuendesha Operesheni Sangara na matunda yake ni kupata wabunge wengi Kanda ya Ziwa.

“Ni justification (uhalalishaji) tu kwamba kuna kitu kimetokea unatafuta sababu tu na kwangu mimi ni jambo dogo sana. Muhimu zaidi ni wapi tumekitoa chama na kukifikisha na wengine wakifikishe mbele zaidi,” alisema na kuongeza:

“Mimi nilikuwa nafanya kazi zangu kama kawaida na nilikuwa na ushirikiano mzuri na katibu mkuu kama inavyotakiwa,” alisisitiza.

Kuhusu madai kuwa CCM ilimuomba kujiunga na chama chao baada ya mgogoro huo kutokea, Zitto alisema hawajawahi kumtaka kabisa.

“Moja ya vitu ambavyo nashutumiwa na wenzangu ni kwamba mimi natumiwa na CCM lakini haijawahi kutokea kiongozi yeyote wa chama hicho, licha ya kuwa na uhusiano nao mzuri, kunitaka nijiunge nacho.

“January Makamba, Deo Filikunjombe, Kangi Lugola ni baadhi ya marafiki zangu walioko CCM lakini si vibaya kwa sababu hata watu wa Chadema wana marafiki ambao wapo CCM na wapo ambao wanaishi pamoja,” alisema Zitto.

Alisema mke wa Dk Slaa alikuwa diwani wa CCM lakini halikuwa tatizo, ila kwa Zitto kuwa na marafiki CCM lilikuwa tatizo.

Kujiunga chama kingine

Kuhusu kujiunga na chama kingine cha upinzani, Zitto alisema kuna vitu ambavyo unapokuwa kiongozi huwezi kuviweka wazi kwani kuna mazungumzo na watu ambayo ameyafanya lakini hawezi kuyatoa.

“Niishie kusema kwamba viongozi wengi sana nimezungumza nao. Wapo walionipa pole kwa yaliyonikuta na wengine kuniomba niungane nao, lakini sikuona sababu ya kutoka chama hiki kwenda chama kingine. Utapata faida ya siku mbili tatu katika kurasa za mbele za magazeti kuwa Zitto kaingia chama fulani lakini hutapata sustainable benefit (manufaa ya kudumu)” alisema.

“(Wilfred) Lwakatale alitoka CUF na kwenda Chadema, lakini hivi sasa wanafanya kazi pamoja. Kafulila katoka Chadema kaingia NCCR, Chadema wakamshambulia kuwa ni sisimizi lakini leo Kafulila ni shadow minister (waziri kivuli) chini ya Mbowe.”

Aliongeza kuwa hizo yeye anaona ni siasa nyepesi, kwa kuwa ana ndoto ya kuona nchi inabadilika na inabadilika kwa watu wanyonge na watu ambao leo hii hawana matumaini. Alisema kwa muda mrefu wananchi wanavumilia kuwa Watanzania, lakini hawajivunii kuwa Watanzania. Ndiyo maana katika ubunge wake ana kazi ya kuibua mambo mazito ili yafanyiwe kazi.

Akizungumzia mambo ambayo anaamini alifanikiwa katika maisha yake, Zitto alisema kuwa ni Bunge la 2005 hadi 2010 ambalo alizungumzia suala la madini kuhusu Buzwagi mpaka sheria mpya ya madini ikapatikana mwaka 2010.

“Leo hii katika tanzanite, Serikali inamiliki asilimia 50 kwa sababu ya sheria mpya. Pia Stamico ina hisa katika migodi na hii ilitokana na hoja za Buzwagi,” alisema Zitto ambaye ana shahada ya uchumi.

“Nilisimama bungeni kuzungumzia madini na siyo kuwa kulikuwa hakuna wabunge, lakini walikaa miaka mingi bungeni na hawakuona kuwa madini ni tatizo.

Nilichekwa na kuonekana sina maana lakini Rais aliunda Tume ya Bomani na watu wakaniambia nisiingie katika hiyo Tume lakini kwa mara ya kwanza ripoti ya Bomani ndiyo ripoti pekee iliyojadiliwa bungeni kati ya ripoti zote zilizoundwa kwenye sekta ya madini.”

Alisema kuwa katika Bunge la 2010 na 2015 alianza vibaya na hoja yake ya kuinua zao la mkonge ilikataliwa. Lakini hakuchoka na Aprili 2012 ripoti ya CAG ikatoka na akiwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) alitaka waliohusika kuwajibika na ndiyo akaibua hoja ya kutokuwa na imani na waziri mkuu na mawaziri wanane wakafukuzwa.

Kujiunga ACT

Alipoulizwa kuhusu mipango ya kujiunga chama kipya cha ACT, Zitto alisema pamoja na kwamba kauli yake kwamba atakuwa wa mwisho kuihama Chadema iko palepale na ndiyo maana ameenda mahakamani kutetea uanachama wake, kuna mambo matatu ya kuzingatia:

Moja, “viongozi wa ACT ni marafiki zangu na ni washirika wangu na falsafa (ideology) ya ACT ndiyo aidiolojia ninayoiamini ambayo ni ujamaa na tatu mimi ni mwanasiasa na hapa Tanzania mpaka sasa ili ufanye siasa lazima uwe kwenye chama cha siasa.”

Kutokana na matokeo ya mahakamani yatakavyokuwa kwa vyovyote vile Watanzania watarajie kuniona katika siasa na katika chama cha siasa ila hawataniona CCM.

“Siwezi kung’ang’ania kama wenzangu wa Chadema hawataki kuwa na mimi.

Lakini nafuatilia kwa karibu shughuli zinazofanywa na ACT na mimi siasa zangu ni hoja, ndiyo maana hamnioni nagombana wala natukana mtu na mkisikia Zitto mtasikia katika hoja na ACT wanajenga siasa za hoja.

“Wanaoongoza ACT ni watu ambao ninawaamini na haitakuwa jambo la ajabu itakapobidi kuwa nao, lakini cha msingi sasa hivi ni kwamba tuna kesi na leo mwanasheria wangu alitakiwa kuwasilisha majibu na tunasubiri hatima ya kesi ambayo ufafanuzi mkubwa ni kupata jibu la, hivi mtu anaweza kukurupuka tu na kumfukuza uanachama mtu bila kufuata taratibu zinazotakiwa?

Nikiiacha kesi bila kupata uamuzi, kuna watu wengi zaidi watakuja kuumia kwenye uamuzi wa aina hii.”

Alisema lazima mahakama itoe uamuzi kwamba taratibu za chama chenu ni hizi, zifuateni mzimalize, hamna sababu za haraka za kumnyonga mtu. Jaji mmoja alisema huwezi kumnyonga mtu halafu baadaye ndiyo unataka ajibu mashtaka.

Mabilioni ya Uswisi

Kuhusu mabilioni ya Uswisi, Zitto alisema kwa mara ya kwanza kwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, Bunge la Tanzania lilikuwa la kwanza kupitisha azimio la kutaka masuala ya utoroshaji fedha yachunguzwe, likitokana na hoja yake.

Alisema uchunguzi wa mabilioni ya Uswisi bado unaendelea ingawa watu wanataka majina ila kwake majina si tatizo kwa sababu yataandikwa tu katika magazeti kwa siku mbili kama ambavyo ilitokea yalipotajwa majina ya mafisadi, lakini waliotajwa mpaka leo bado ni mawaziri.

“Mwaka jana nilikwenda kwenye mkutano Uingereza kumweleza Waziri Mkuu wa Uingereza kabla ya mkutano wa G8 nikiwa na Rakesh Rajan na leo hii kuna uchunguzi unaendelea.

CHANZO: MWANANCHI.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.