Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa, ametoboa siri ya chama hicho kung’ang’ania Muungano serikali mbili akisema hiyo ndiyo sera yake pekee iliyopitishwa na wanachama wake wote kwa kura ya maoni.

Msekwa alieleza hayo katika mahojiano maalumu na wahariri wa gazeti hili yaliyofanyika nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam.

Msekwa ambaye katika habari iliyochapishwa na gazeti hili jana alieleza kuwa binafsi, hana tatizo na suala la idadi ya Serikali katika Muungano, alisema kamwe hawezi kukishauri chama chake kukubaliana na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya muundo wa serikali tatu.

“Siwezi kuishauri CCM kukubali serikali tatu. Hili la Serikali mbili ni sera ya CCM, siyo tu sera ya kawaida, bali hii ni sera pekee iliyopitishwa na wanachama wote kwa kura ya maoni,” alisema Msekwa ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge.

Alisema tofauti na sera hiyo ya serikali mbili, sera nyingine za chama hicho huanzia katika ngazi ya Kamati Kuu, kujadiliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na kupitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa.

Msimamo ulikoanzia

Kiini cha sera hiyo kutengenezewa utaratibu maalumu, kilitokana na sakata la Kundi la Wabunge 55 (G55), kuanzisha agenda ya kutaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano na hatimaye Bunge kupitisha Azimio la kuanzisha serikali hiyo.

Msekwa ambaye wakati huo alikuwa Naibu Spika lakini akiongoza Bunge kutokana na aliyekuwa Spika, Chifu Adam Sapi Mkwawa kuwa mgonjwa, alisema ushauri wa kurudi kwa wanachama wa CCM kuwauliza wanataka serikali ngapi ulitolewa na Mwalimu Julius Nyerere.

Itakumbukwa kuwa hatua ya Bunge kupitisha azimio hilo la kuanzisha Serikali ya Tanganyika ilimkera Mwalimu hadi akatunga kitabu, Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania akiwashutumu aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela na aliyekuwa Katibu Mkuu wa (CCM), Horace Kolimba. “Mwalimu alitueleza kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa, kuwa Bunge limekwishapitisha azimio na likipitishwa ni lazima litekelezwe na Serikali. Alisema mkikataa azimio la Bunge hivihivi mtaleta mgongano wa kikatiba, msiamue peke yenu, nendeni kwa wanachama wote muwaulize ili uamuzi uwe wa wote,” alisema.

Alisema kutokana na ushauri huo, mwaka 1993 CCM iliandaa na kusimamia upigaji kura za siri za maoni katika kila tawi, wanachama wakitakiwa kujadili na kuchagua kati ya serikali moja, mbili au tatu.

“Matokeo yalipofika katika Halmashauri Kuu, ilionekana wanachama walio wengi katika matawi mengi walitaka serikali mbili, na hapo ndipo ikapitishwa sera ya serikali mbili,” alisema na kusisitiza:

“Siwezi kwenda kinyume na wanachama wengi wa CCM, ila mimi binafsi kama mtaalamu wa katiba na baada ya kusoma mambo mengi, hili la idadi ya serikali halinipi shida, bali ninachoona cha muhimu ni uimara wa Muungano.”

Mvutano wa muundo wa serikali uliibuka baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba kupendekeza Tanzania kuwa na serikali tatu; ya shirikisho, Tanganyika na Zanzibar.

Huku baadhi ya wananchi hususan vyama vya upinzani vikiunga mkono mapendekezo hayo, CCM kimeweka wazi msimamo wake wa kupinga msuguano ambao ulichangia kwa kiwango kikubwa mpasuko ndani ya Bunge Maalumu la Katiba na kuwafanya wajumbe ambao waliunda Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao huku wakiweka sharti la kujadiliwa kwa mapendekezo ya Tume ya Warioba kurejea bungeni.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi la tarehe 26 Juni 2014

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.