Uambishaji ni dhana inayowakilisha upachikaji wa vipashio vya kisarufi kwenye mzizi wa neno kwa minajili ya kujenga ama neno jipya au kubadilisha tu hali ya neno.

Kwa mfano, mzizi wa neno -pig- ukiwekewa viambishi ku-pig-a unakuwa kitenzi au kitenzi nomino na ukiwekewa pig-o unakuwa nomino. Inaweza kuwa u-pig-aji, ma-pig-ano, m-pig-aji na kadhalika.

Kuna utata wa kitaalamu juu ya ikiwa Kiswahili kina aina tatu za viambishi – yaani awali, kati na tamati – au kina aina mbili tu – yaani awali na tamati. Hoja zote mbili zina nafasi yake katika taaluma ya lugha na haziondowi ukweli kwamba Kiswahili kinaambisha.

Kwa upande mwengine, unyumbuaji ni kuvipachua hivyo vipashio vilivyounganishwa kwenye neno moja na kuvipa tafsiri yake ya kisarufi. Kwa mfano, neno (au sentensi) “Ninakuona” inaweza kunyumbuliwa hivi ifuatavyo:

i. Ni-: kiambishi awali cha nafsi ya kwanza umoja, yaani mimi, katika hali ya utendaji
ii. -na-: kiambishi awali kinachowakilisha wakati uliopo
iii. -ku-: kiambishi awali kinachowakisha nafsi ya pili, umoja, yaani wewe, katika hali ya utendwaji
iv. -on-: mzizi wa neno wa kitenzi ona
v. -a: kiambishi tamati kinachowakilisha hali ya utendaji

Kwa hivyo, kwa muhtasari uambishaji ni upachikaji vipashio vya kisarufi kwenye mzizi wa neno na unyumbulishaji au unyumbuaji ni upachuwaji wa vipashio hivyo na kuvichambua kisarufi.

Ni hayo kwa sasa. Je, una mifano au maoni zaidi juu ya uambishaji na unyambulishaji? Karibu tukisemee Kiswahili.

11 thoughts on “Hisabati ya Kiswahili: Baina ya uambishaji na unyambulishaji”

 1. mm kwa upeo wangu mdogo nafahamu uambishaji(inflaction) kuwa ni upachikaji wa viambishi ktk mzizi ambao una sababisha mabadiliko ya kisarufi kama hali umoja ya wingi , njeo n.k.kwa mfano: m-tu na wa-tu.a-na-som-a. hivyo uambishaji haubadili kategoria ya neno.

  1. Upeo wako si mdogo hata kidogo Ulfat. Tunataraji ndivyo pia uchambuzi huu ulivyosema. Ingawa la ikiwa uambishaji unaweza kubadili kundi la meno (kategoria kwa kutumia utohoaji wako), tunaamini kuwa uambishaji hufanya hivyo, yaani huweza kuliondoa meno kutoka kundi moja ya neno (kama vile zuri ambayo ni kivumishi) na kuw aina nyengine ya neno (kama vile uzuri ambayo ni nomino). Ahsante sana.

 2. Je, Unyambulishaji ni kupachika viambishi tamati peke yake au pamoja na viambishi awali?
  Dhana ya mnyumbuliko bado haijakaa vizuri

 3. Nashukuru kwa mtoa mada.
  Mimi sijakuelewa unapotoa fasili ya unyumbulishaji kuwa nikitendo cha kupachuwa viambishi. ukiwa na maana ya kufafanua kiambishi na kazi yake .kwa uelewa wangu , nsfahamu kuwa
  UNYAMBULISHAJI ni kitendo cha kupachika viambishi mwishoni mwa mzizi wa neno au shina LA neno.

  MF. chez- cheza, chezea, chezesha
  safi- safisha , safika, safishika, safishana n.k.

  mfano wa kwanza nimetumia mzizi.
  MF 2 nimetumia shina

 4. Mtoa mada kiukweli anapaswa kwenda kuangalia namna wanaisimu nbalimbali kama akina prof massamba, akna mgullu na kina Kindija wanavyozitazama dhana hizo

 5. Ni sawa kabisa jinsi wenzangu walivyojaribu kusema kuhusu uambishaji na unyambuaji lakini bado kuna utata ambao watalaamu Wa lugha into wanafaa kutafiti zaidi

 6. Dhana ya mnyambuliko ni dhana zelezi kwa wanaisimu wengi

  nijuavyo kutokana na chambuzi za wanaisimu wengi ni kwamba DHANA KUU NI

  MNYAMBULIKO/UNYAMBUAJI ambao ni kitendo cha kupachika viambishi kwenze mzizi wa neno

  Aina zake ni

  1. Uambishaji…kitendo cha kupachika viambishi kabla ya mzizi mfano a-na-vyo-lima

  2. Unyumbuaji….kitendo cha kupachika viambishi baada ya mzizi wa neno mfano Lim-i-a

 7. dhana ya unyambuaji bado inawatatiza wengi hasa wanao soma kiswahili kijuu juu .mm nasema kiufupi kwamba unyambuaji ni hali au kitendo cha kuongeza viambishi tamati mwishon mwa mzizi WA neno ili kupata maneno zaidi mfano mzizi chez utapta maneno kama cheza , chezea,chezesha,chezeshwa,chezeana n.k

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.