Tumesikia matamshi ya mbunge wa Nkasi Kaskazini kupitia CCM, Ally Mohammed Keissy alipochangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akisema Zanzibar haichangii katika Muungano, hivyo haina haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili.

Laiti kama angelijua kuwa matamshi yake yangeweza kuwatibua Wazanzibari, pengine asingesema hayo ambayo ameyasema.

Athari ya matamshi yake yanaakisi tatizo la msingi katika Muungano huu ambao umetimiza miaka 50.

Hatuwezi kumtupia lawama  kwani ndiyo yaleyale aliyoyasema mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kwamba kuna dhana ya Tanzania Bara kuona kwamba Tanganyika ndiyo Serikali ya Muungano au Tanganyika kuvaa koti la Muungano.

Nimkumbushe mbunge huyu kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilisita kuchangia suala la Muungano tangu mwaka 1984.

Sababu kuu iliyosababisha kufikia hatua hiyo ni kwamba Zanzibar haifahamu ina wajibu wa kuchangia kiasi gani na mgawanyo wa mapato ya Muungano ukoje?

Hadi leo Tume ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haifahamiki nini hasa inafanya, bado kuna giza nene kuhusu mgawanyo wa masilahi na gharama za Serikali ya Muungano ikiwa ni pamoja kugawana mapato, misaada ya kutoka nje masilahi mengine, ikiwamo gesi asilia ambayo hadi naandika makala haya Zanzibar haipati kitu. Kuna tetesi kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha  imeshatoa mapendekezo ya namna Zanzibar na Tanzania Bara zitakavyochangia gharama za uendeshaji wa Serikali ya Muungano.

Taarifa zilizopo ni kuwa SMZ imeshatoa mapendelezo yake muda mrefu wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasemekana imo mbioni kufanyia kazi mapendelezo hayo.

Aidha, Serikali hizi mbili mwaka 1994 ziliomba msaada wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kuzishauri kuhusiana na Benki Kuu (BoT), mgawanyo wa misaada na uhusiano wa kifedha.

Kwa msingi huo ndiyo sasa yanazuka hayo ya kusema kuwa Zanzibar haijachangii gharama za uendeshaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Pia, kuna suala la mapato yatokanayo na mafuta na gesi asili. Licha ya suala hilo kuwa la Muungano, Zanzibar haijawahi kupata gawio lake.

Wakati hayo yakiendelea, Zanzibar inahitaji kuwahudumia watu wake katika afya, elimu, majisafi na salama, umeme na mengineyo. Mambo hayo siyo ya Muungano.

Ukiacha hili la gesi asilia, kuna suala la hisa za Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, nalo ni kizungumkuti.

Pia, kuna wizara na idara za serikali ambazo siyo za Muungano, lakini zimewekwa katika Wizara za Muungano, nalo ni tatizo jingine ambalo linatatiza suala zima la uchangiaji na ugawanaji wa mapato.

Ndipo wengine wanapodai Serikali ya Tanganyika ‘imejibanza’ upenuni mwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Mathalan, mambo ya kilimo, elimu ya msingi na kati, tawala za mikoa na serikali za mitaa siyo katika mambo ya Muungano, nani anayesimamia? Jibu ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Yapo mambo yanayolalamikiwa siku nyingi na Zanzibar katika Muungano huu kama suala la uwakilishi wake kwenye Bodi za Baraza la Mitihani (Necta), Shirika la Ndege (ATCL), Shirika la Simu (TTCL). Inadaiwa kuwa Zanzibar haifaidiki kutokana na biashara ya mashirika haya.

Malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili wanapokwenda Tanzania Bara kwa bidhaa ambayo tayari imeshalipiwa ushuru  ambapo jambo hili limezungumzwa mara nyingi, lakini hali ni ile ile.

Suala la uchumi siyo la Muungano kwa maana ya kila upande una wizara yake inayoshughulikia uchumi, mipango na sera zake za uchumi na bajeti yake.

Aidha, kila upande una mfuko wake mkuu wa serikali na hivyo mapato yake, kila upande una jukumu la kushughulikia huduma za jamii, miundombinu, kila upande una sera na sheria zake za biashara na uwekezaji na hata sheria za ajira.

Wataalamu wa mambo ya katiba wanasema licha ya ukweli huo, Katiba ya Muungano haiweki bayana na ndiyo inayofanya kusiwe na majibu ya wazi ya suala hili kwa sababu kodi ya mapato, mikopo ya nje na biashara za nje bado yamefanywa ni mambo ya Muungano.

Kodi ya mapato ambayo ni nyenzo kuu ya uchumi wa visiwa ambao ni ‘service oriented’ badala ya kuwa ‘resource based’ kama ilivyo kwa bara, bado ni jambo la Muungano kisera, ingawa mapato halisi yanatumika Zanzibar .

Kingine katika muundo wa Muungano ni kwamba sera za fedha na uhusiano wa kikanda upo chini ya Serikali ya Muungano bila ya kuwa na uwazi wala sheria inayoilazimisha kushughulikia maslahi ya kiuchumi ya Zanzibar.

Kwa misingi hiyo, ndiyo maana Dk Salmin Amour ‘Komandoo’ katika utawala wake wa awamu ya tano alitilia mkazo maeneo huru kiuchumi , bandari huru na kampuni nyingine za kibiashara ikiwa njia ya kujinasua na hali ngumu ya uchumi.

Ikiwa mfumo wa muundo wa Muungano utakuwa wa serikali tatu, Zanzibar kwa jiografia yake inaweza kupata fedha nyingi za kigeni kwa kutoa huduma za bandari  na inaweza kuhudumia meli kubwa za tani  100,000.

Maumbile ya bahari ya Zanzibar yanaruhusu meli kubwa kufunga gati wakati wote iwe maji yamekupwa au kujaa. Hii itasaidia zile meli zinazozunguka Afrika Kusini na kufunga gati Dubai sasa zinaweza kutumia bandari ya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha meli kubwa za mizigo na hivyo kuchangia uchumi. Kukiwa na mfumo imara wa shirikisho nina hakika Zanzibar baada ya miaka kumi ijayo inaweza kufanya maajabu katika uchumi ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kiasi cha kuwa  ‘Singapore’ ya Afrika.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.