Image
Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Othman Masoud
 • Awashangaa wanaotaka Zanzibar iendelee kuwa manispaa
 • Asema kutokuwepo Serikali ya Tanganyika ndio kero kuu ya Muungano
 • Awasuta wanaotaka Serikali Mbili

Na Salim Salim. Mwanaseria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema lengo la mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania si kuifanyia marekebisho katiba iliyopo sasa, bali ni kuandika katiba mpya ambayo itakuwa Muarubaini kwa kero za Muungano na Muungano wenyewe.

Mwanasheria Mkuu huyo aliyasema hayo leo asubuhi alipokuwa akifunguwa Baraza la Katiba la Vyuo Vikuu liliondaliwa na Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar (ZAHLIFE) na kufanyika katika Ukumbi wa Salama, Bwawani mjini Zanzibar.

“Msingi wa Muungano wa Tanzania ni kuungana kwa nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar. Lengo la kuungana kwa nchi mbili hizi ni kufanya mambo yao pamoja na kupata faida zaidi na sio nchi moja kuitawala nchi nyengine,” alisema Mwanasheria Othman na kuongeza kwamba Zanzibar si mkoa wala wilaya bali ni nchi kamili. “Katika Muungano, tulikubaliana baadhi ya mambo kufanya pamoja na sio Zanzibar kuwa jimbo la Tanganyika.”

Mwanasheria Othman alitumia fursa hiyo kuweka sawa rikodi inayopotoshwa sana ya aina miungano duniani, akiutoleoa mfano ule wa Uswisi ambao una serikali 24 na wa Marekani wenye serikali 52 ambayo imedumu kwa muda mrefu sana.

“Ni uongo kuwa serikali tatu zitavunja Muungano. Serikali mbili ndizo zitakazouvunja Muungano huu. Lakini hata muungano wa serikali tatu ukivunjika, si kioja.

Alisema uruhani wa serikali ya Tanganyika ndio kero kubwa ya Muungano na kwamba muundo wa muungano wa serikali tatu utairudisha serikali ya Tanganyika na hivyo kero kubwa itakuwa ishatatuliwa.

Miongoni mwa mambo aliyoyataja kuwa yamedhihirisha namna muungano wa serikali mbili ulivyoinamia Zanzibar ni lile la Sheria ya Kuanzishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo pamoja na kuwa aliisaini Mzee Abeid Karume mwenyewe, akiwa kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, lakini ni yeye pia aliyekuja kung’amua mapungufu makubwa ya Sheria hiyo na ndio maana akaanzisha Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).

Jengine ni lile la Shirikisho la Mpira la Tanzania Bara (TFF) ambalo siku zote limejivika joho la kuiwakilisha soka ya Jamhuri nzima ya Tanzania ilhali michezo si jambo la Muungano na haijawahi kuwa.

“Kama Zanzibar inataka kuishtaki TFF itashinda na TFF haitokuwemo kwenye Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwani TFF haiwakilishi Tanzania kama ilivyokuwa ZFA haiwakilishi Tanzania,” alisema Mwanasheria Mkuu.

“Hivi hatuoni haya kubakia hivi hivi kuwa manispaa, wakati Zanzibar ilikuwa Empire (dola)?” alihoji Mwanasheria Mkuu huyo, na kuendelea kudadisi ni vipi Wazanzibari watamuamini mtu ambaye leo anasema Zanzibar si nchi.

“Atakapokuwa Rais wa Tanzania ambapo Zanzibar haitokuwa na mamlaka, si  atasema kuwa Zanzibar ni jimbo la Tanganyika?”

Mwanasheria huyo alitumia fursa hiyo kuwasifu wanafunzi wa vyuo vikuu Zanzibar na akawataka kuzungumzia mambo ya Muungano kwa misingi ya usawa.

“Bila ya kuwa na usawa katika Muungano huu, huo si Muungano bali ni ukoloni” alisema, na kutaka kuwe na mfumo wa usawa katika baraza la mawaziri, bunge na kuwe na makubaliano ya thuluthi mbili kila upande katika kupitisha sheria na kuongezwa au kupunguzwa mambo ya Muungano.

Alisema katika muungano wa serikali tatu ni lazima rasilimali zitumike kwa usawa na sio kama hivi sasa ambapo upande wa Tanganyika unatumia rasilimali za Muungano peke yake na kuinyima Zanzibar.

“Tume ya Pamoja ya Fedha haijaanza kazi mpaka leo, na katika Muungano kuna mapato na matumizi ya Muungano na mapato ya Muungano siku zote huwa mengi, lakini Tanganyika hawataki tugawane.”

Alipinga vikali hoja kwamba mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu una gharama kubwa zaidi, bali akasema muungano wa Serikali Mbili ndio wenye gharama kubwa sana na Zanzibar ndio inayogharamika zaidi. “Hebu viongozi nawawe wakweli na waache kuwapotosha wananchi.”

Hata hivyo, Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali ya Zanzibar aliwaonya Wazanzibari kuacha kulumbana wenyewe kwa wenyewe hasa kwenye kipindi hiki cha kutafuta Katiba Mpya na badala yake wakae pamoja kuidai nchi yao.

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa ili kuondowa tofauti baina ya Wazanzibari. Kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kulikuwa kugumu zaidi kuliko mabadiliko ya Muungano.”

Alisema hoja za wanaotaka serikali mbili hazina msingi zaidi ya kulinda maslahi yao ya kidunia, lakini umefika wakati wa watu wote kushirikiana.

“Hoja yangu nawataka wanaotaka serikali mbili na wanaotaka Mkataba wakae pamoja wajadiliane mfumo wa muungano wa Serikali Tatu kwani ni mfumo ambao utakuwa na maslahi kwa Zanzibar.”

Awali Mwenyekiti wa ZAHILFE alikanusha kuwa taasisi yake iliandaa kongamano la tarehe 6 Julai 2013 lililofanyika kwenye ukumbi wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kingeni Zanzibar.

“Kongamano hilo liliandaliwa na Mkoa wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa CCM. ZAHLIFE haina mafungamano na chama chochote cha siasa,” alisema mwenyekiti huyo, Bakar Hamad.

Kongamano hilo lilianza kwa wimbo wa taifa wa Zanzibar na kuhudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Marais 10 wa Serikali za Wanafunzi waliochangia katika kongamano hilo walitaka Zanzibar yenye mamlaka kamili na usawa katika Muungano.

7 thoughts on “Serikali Mbili zitavunja Muungano – Mwanasheria Mkuu Z’bar”

 1. bado tu wazanzibari tupo na tumelala hasa viongozi wa juu wa CCM wao wameridhika ya dunia kuliko ya akhera mpaka leo wanawaangamiza wananchi kwa maslah yao sisi tunataka serikali tu zanzibar iwe na mamlaka kamili tena ya usawa Rais wa Tanganyika Mwalimu Julias Nyerere amefika kusema Tumechoka na WaZanzibari na uislam bado tuna’nga’nagia Tanganyika basi tena watuwachie tuji endeshe wenyewe waoataka kulipa fadhila wawatowe watoto wao wa kike ndio wawalipie hizo fadhila sio visiwa vyetu

  1. Kama unataka matokeo ya Misri endeleeni tuu.
   Nataka kuwa kumbusha wa Zanzibari sisi ni kidogo sana.
   Tunaomba salama kheri ya watoto wetu na vizazi vyetu.
   Ugomvi, Nuksi, na Vita sio jadi yetu.

   1. Ya mwanasheria mkuu ndio maneno kwa hakika serikali tatu ndio suluhu pekee ya kero za muungano huu , viongozi musiangalie maslahi yenu binafsi kwa mambo ya kidunia angalieni kilichobora kwa wanchi wenu zingatieni maoni ya waliowengi. kwa hakika wazanzibar tumechoka na hali hii na inshaallah mukifanya kwa maslahi yaliobora kwa wananchiwenu m/mungu atakupendeni na atawaongezeeini upendo na atakuengezeeni neema na atakuondoleeni hofu hapa duniani na akhera

 2. kama wa Tanganyika wanataka muungano kwanini wasiungane na malawi kongo watapata jina zuri tu MATAKO

  1. ndugu yangu hao tanganyika hawawezi kuungana na nchi yyte ile kwan hata hao malawi hawaelewani

 3. Huyu mwanasheria mkuu naona hajui maadili ya kazi yake, hakuitwa pale kwenda kupigia debe muundo fulani wa muungano! Katiba ina mambo mengi zaidi ya huo muundo wa muungano……..kwa kuwa mwanasheria huyu hajisomi, anajiona kama na yeye ni mwakilishi……..anajivisha joho la uwanasiasa! Nasikitika tu kuona eti Mwanasheria Mkuu anaburuzwa na wanasiasa….shame on him!

 4. ndugu yangu nyota njema,kila mtu ana uhuru katika kutoa maoni yake km ya mwanasheria umeyasikia na kuyasoma inaoneka na ww ndio waleee wasioitakia mema zbar na watu wake.MSG SENT kwa wengine

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.