wasichana-wa-kiingereza-564x272

Na Kerry Stokes. Mimi ninaishi Zanzibar na ninatamani ningeliweza kuyavunganya mazuri yote ya kisiwa hiki kidogo kwenye kipande cha pamba na kuyaweka kisandukuni na kugawana na ulimwengu. Hivyo nachukia kuona “nyumba” yangu hii ndogo ikiwa kwenye jinamizi kama hili.

Ninahisi fadhaa kwa wasichana hao walioshambuliwa usiku wa jana Mji Mkongwe na ninaweza kufikiria khofu ambayo lazima itakuwa imewajaa. Hata hivyo, nina maswali – na sababu pekee nionayo inanifanya niulize ni kwa sababu ya yale niyaonayo kila wakati.

Je, wasichana hao walikuwa wanatembea wapi kwa miguu na kwa nini walikuwa peke yao? Je, walikuwa wamejitanda? Zanzibar ni nchi ambayo ina Waislamu wengi lakini ninawaona watalii wengi wakitembea mitaani na viguo vifupi. Bila ya shaka hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuwashambulia. Lakini watu wanaovaa hivyo huwa hawaoneshi kwamba wana heshima.

Na kuna wengine ambao wanabusiana na kupapasana mitaani au kuvuta sigara hadharani – yote hayo ni mambo ambayo yanachukiwa. Unaweza kuendesha chombo cha moto cha maringi mawili bila ya kofia la chuma na kuzungumza na simu yako ya mkononi au kuwa na watu wamejaza mizigo kwenye baiskeli na hakuna atakayekutupia jicho. Lakini kama ukionekana unavuta huku unaendesha utavutwa mara moja na unaweza kushitakiwa.

Kwa wakati huu, mazingira ni magumu zaidi kwa ujumla kwani ndio kwanza tunaondoka kwenye mwezi mtukufu kwa Waislamu wa Ramadhani na kuingia kwenye sikukuu ya Idd.

Naupenda Mji Mkongwe na mara kwa mara huwa nakwenda huko na rafiki yangu kwa ajili ya kunywa na chakula cha jioni, chakula cha mchana au kutembelea duka la vileo. Najihisi niko salama kuingia kwenye teksi na kutembea dakika 30 kuelekea Mji Mkongwe kuufuata ulipo mkahawa. Najihisi salama kufanya hivyo.

Lakini sijawahi kutoka nje baada ya Futari (chakula cha jioni katika mwezi wa Ramadhani) tangu Ramadhani ianze na bila ya shaka nisingeliweza kwenye peke yangu sasa – ningelikaa kama wiki moja au mbili kwa kisiwa hiki kutulia baada ya Idd.

Zanzibar si eneo la kuogofya na hakuna tatizo la uhalifu wa kutumia nguvu. Hapa hakuna uhalifu wa aina hiyo. Ikiwa kitu kama hicho kimetokea, ni jambo tafauti.

Tukio kama hilo haliitii Zanzibar nzima lawamani.

Tanbihi: Makala hii ya Kerry Stokes ilichapishwa na mtandao wa gazeti la Mirror la Uingereza toleo la Alhamis (Agosti 8, 2013). Kerry alihamia Zanzibar kutokea Afrika ya Kusini mwezi Januari 2013 na anafanya kazi kwenye hoteli ya nyota tano. Tumeichapisha hapa tena kwa sababu ya umuhimu wake.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.