mzalendo_balozi_seif-564x272

Ahmed Rajab

KUNA ukweli mmoja ulionipitikia hii leo na ulionishtua. Ni ukweli au uhakika ulio mchungu. Ingawa tumeumezea miaka nenda miaka rudi, sasa umefika wakati wa kuwa lazima tuuteme.

Tusipofanya hivyo nasi pia tutakuwa kama tunayaridhia na kuyakubali mabaya yaliopo na tutakuwa tunashiriki kuuendeleza uovu.

Uhakika wenyewe ni kuwa jeshi Visiwani Zanzibar si kioo cha jamii ya Wazanzibari, jamii iliyo ya mchanganyiko wa makabila, dini, rangi na itikadi tafauti za kisiasa.

Kwa yalivyo hivi sasa majeshi yalioko Zanzibar yanaonekana kuwa ni yenye kuwatenga Wazanzibari wa nasaba fulani au muelekeo fulani wa kisiasa.

Makabila fulani hayana hata mtu wao mmoja jeshini, si miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu na wala si miongoni mwa askari kuruti.

Hawamo katika vikosi vya jeshi la maji, hawamo katika vikosi vya jeshi la nchi kavu, hawamo katika vikosi vya tawi jeshi la anga wala hawamo katika jeshi la polisi. Hawamo kwenye idara ya usalama. Hawamo katika jeshi lolote la ulinzi.

Hii ni hali ya kusikitisha. Kwa hakika, ni ya uonevu. Inadhihirisha ubaguzi uliowazi unaofanywa kwa makusudi kuwabagua Wazanzibari wenye vijitone vya damu visivyo vya Kiafrika.

Vijitone hivyo vya damu ngeni — view vya Kiarabu au vya Kihindi —vinawafanya wanuke, wawe kama wanadamu ya kunguni. Kwa ufupi, hawaaminiki.

Kuna shtuma kwamba hata watu wenye kudhaniwa kuwa wanatokana na familia zenye kukiunga mkono Chama cha Wananchi (CUF) hawaaminiwi kuingizwa katika majeshi.

Ni aibu kuwa kuna ubaguzi wa aina hiyo katika karne hii ya 21. Inazidi kukirihisha kuona ubaguzi aina hiyo ukifanywa wakati ambapo Tanzania, kwa jumla, inajigamba kuwa inaufuata mfumo wa demokrasia, wa uwazi, wenye kuziheshimu haki za binadamu na wenye kuwaona wananchi wake wote kuwa ni sawa bila ya kujali kabila zao, rangi zao, dini zao au itikadi zao za kisiasa.

Demokrasia ya kweli lazima iwe ni ya mfumo wenye kuwakubali wote katika jamii. Madhali ni wananchi na raia wa nchi basi lazima wakubaliwe na waingizwe katika taasisi zote kuu za nchi hata zile zilizo nyeti na zilizo mihimili ya dola kama kwa mfano, majeshi.

Bila ya shaka wote wenye kuomba ajira katika taasisi hizo watabidi wachunguliwe kuangalia kama hawatohatarisha usalama wa taifa.

Kufanya hivyo ni sawa lakini haijuzu kuwachuja kwenye chujio lenye kuwatafautisha kikabila, kirangi, kidini au kichama.

Wala haifai kuyafanya matawi ya chama chenye nguvu yawe mahala pa kuwapatia wananchi ajira. Huko ndiko wanaokubalika wanapoelekezwa wapi wende ili wapate ajira.

Kuwabagua wananchi kwa sababu ya makabila yao au rangi zao ni kuwadhalilisha nchini mwao wanakostahili wapatiwe haki zilizo sawa kama wanazopatiwa raia wenzao wenye kukubalika.

Idhilali wanayofanyiwa raia wenye kubaguliwa inazusha dhana ya kuwako aina mbili za raia machoni mwa watawala.

Aina ya kwanza ni ya wale wanaotumbukizwa kwenye kapu la ‘wananchi’ na aina ya pili ni ya wale wenye kutukuzwa na wanaofanywa waamini kwamba ni wao na si wengine ‘wenye nchi’.

Raia mwenye kutambuliwa na Katiba kwamba ni ‘mwananchi’ anakuwa wa daraja ya pili; wa daraja ya kwanza anakuwa yule anayetambuliwa na watawala kuwa ni ‘mwenyenchi’.

Demokrasia imekuwa na maumbile tafauti katika nchi tafauti. Hakuna mfumo wa demokrasia ulio sawa na wenye kutumika kote duniani.

Hata hivyo, kuna mambo ya kimsingi yenye kuonekana kuwa ni mihimili ya aina zote za demokrasia. Miongoni mwa hayo ni ule msingi wa kuwa serikali lazima iwajibike kwa wapiga kura walioichagua.

Aidha, haki za raia wote lazima zilindwe zikiwa pamoja na za wale walio wachache katika jamii, kwa mfano watu wanaotokana na makabila madogo. Haki za raia wote huwa zinalindwa na sheria zinazotekelezwa na polisi na mahakama iliyo huru.

Katika nchi za kidemokrasi majeshi nayo yanatakiwa yawe na sifa maalumu ili yaweze kutakasika. Kwanza, yanatakikana yawe na utiifu kwa nchi yao, na sio kwa mtu mmoja, au chama kimoja, au kabila moja au dini moja.

Ilivyo hivi sasa Zanzibar ni kuwa majeshi yana utiifu kwa chama kimoja tu cha siasa. Chama cha Mapinduzi (CCM) kina mahusiano maalumu na majeshi, vyombo vya usalama na polisi.

Hivi ni kinyume na inavyotakiwa iwe katika mfumo wa kidemokrasia ambapo majeshi hayatakiwi yakiunge mkono chama chochote cha siasa.

Jeshi la Zanzibar lina historia ndefu. Liliundwa 1877 pale William Lloyd Mathews alipohamishwa kutoka jeshi la maji la Uingereza na kupelekwa Zanzibar ende kuunda jeshi la kizungu la muundo wa kileo.

Dhamira ilikuwa kuunda jeshi litalomsaidia Sultan Barghash bin Said aweze kupenya na kuingia Bara ambako alitaka kuonyesha jinsi mamlaka yake yalivyoenea katika eneo zima la huko Bara.

Hadi hapo jeshi la Sultan lilikuwa likibagua. Lilikuwa na wanajeshi Wakiarabu na Wakiajemi tu. Lakini jeshi jipya lililoundwa na Mathews liliwaingiza Waafrika 500 waliokuwa wakivaa sare ya kofia nyekundu, majeketi mafupi meusi na suruwali nyeupe.

Katika miaka ya mwanzo baada ya Mapinduzi ya 1964 hakukuwa na ubaguzi katika majeshi ya Zanzibar. Wakati huo watu wa makabila takriban yote yaliopo Zanzibar walikuwemo jeshini na wakitendewa sawa kwa kupatiwa nafasi za kwenda nje kupata mafunzo zaidi ya kijeshi. Baadhi yao walikuwa na vyeo vya juu.

Mambo yalianza kubadilika utawala wa kimabavu uliposhamiri na chuki za kikabila zilipoibuka.

Hali hiyo ilizidi kuchacha baada ya mwanajeshi mmoja mwenye asili ya Kiarabu kumpiga risasi na kumuua Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar Aprili 7, 1972. Lakini mwanajeshi huyo hakuwa peke yake. Alikuwa na wenzake wa makabila yote ya Zanzibar.

Hata hivyo, tangu wakati huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikawa na sera ya siri ya kutowakubali Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu kuingia jeshini pamoja na wengine wasioaminika au wasiotambuliwa kuwa ni ‘wenyenchi’.

Huo ni ubaguzi usiona shaka yoyote. Haujuzu wala haukubaliki hasa tukiona jinsi Zanzibar ya leo inavyo utetea umoja wa kitaifa na mshikamano wa Wazanzibari kama alivyoashiria Rais Ali Mohamed Shein kwenye ujumbe alioutoa Jumatatu iliyopita alipowafuturisha watu Ikulu.

raiamwema

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.