udsm

Na Joseph Zablon

Dar es Salaam. Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), kimeshika nafasi ya 11 kwa ubora barani Afrika kulingana na utafiti wa hivi karibuni wa Shirika la Utafiti wa Kielimu la Cybermetric Lab lenye makazi yake nchini Hispania.

Utafiti huo unakiweka chuo hicho katika nafasi hiyo wakati ile ya kwanza inashikiliwa na Chuo Kikuu Kwazulu Natal cha Afrika Kusini na shirika hilo limekuwa likifanya utafiti wa namna hiyo kwa vyuo mbalimbali ulimwenguni kwa miaka kadhaa sasa.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa utafiti huo ulikuwa ukiangalia masuala ya ubora wa elimu inayotolewa, muonekano, uwazi katika utendaji na vigezo vyote vilikuwa na alama 50 na kwa Afrika Mashariki chuo ambacho kimeshika nafasi za juu ni Makerere cha Uganda ambacho awamu iliyopita kilishika nafasi ya nne.

“Makerere kinatanguliwa na vyuo vitatu vya Afrika Kusini na ukiacha Kwazulu kinachoshika nafasi ya pili ni Chuo Kikuu cha Cape Town ambacho kiliwahi kushika nafasi ya kwanza katika utafiti uliopita na Stellenbosch” inasema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa Chuo Kikuu Nairobi kipo nafasi ya 14.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala akizungumzia matokeo hayo alisema kuwa yanatia faraja laini hata hivyo anaamini kuwa chuo chake kilistahili nafasi nzuri zaidi ya hiyo kutokana na jinsi ambavyo kimejiimarisha hivi sasa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.