ccm+makinda

Spika wa Bunge, Anna Makinda akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha siku tatu cha wabunge wa Chama cha Wabunge Wanawake Bungeni (TWGP) kilichoanza jana mjini Bagamoyo. Picha na Fidelis Felix

Na Elias Msuya na Patricia Kimelemeta

Wakati maandalizi ya muswada wa sheria ya kura ya maoni wa mwaka 2013 yakianza jana jijini Dar es Salaam, kumezuka mvutano mkali kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Chama Cha Mapinduzi.

Mvutano huo umekuja wakati kamati hiyo ya Bunge ikikutana na vyama vya siasa, wasomi, asasi za kiraia na wadau wengine kwa wiki mbili mfululizo ambapo jana ilikutana na vyama vya siasa vya CCM, NCCR Mageuzi, Sauti ya Ukombozi, UPDP, huku Chadema kikiomba kwenda leo.

Mwakilishi wa CCM ambaye ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM, Joseph Tadayo ndiye alikuwa wa kwanza kutoa maoni ya chama hicho kwa kukosoa vifungu vya muswada huo likiwemo suala la muungano.

“Kifungu cha 41(3) kinachozungumzia kura za ‘NDIYO’ kina utata hasa kwa kuwa Zanzibar ni ndogo kwa Tanzania Bara, sasa ukiweka asilimia 50 kwa 50 itakuwaje? Alihoji Tadayo na kuongeza:

“Ikitokea asilimia 99 ya Bara imesema ndiyo na asilimia moja tu ya Zanziba imesema hapana, itakuwaje? Hii ni hatari kwani tutazuia maoni ya watu.”

Alipinga pia kifungu cha 16(1) kinachoruhusu watu kupiga kampeni wakati wa kura ya maoni.

Baada ya Tadayo kutoa maoni yake, wajumbe wa kamati hiyo walianza kumuuliza maswali ambapo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alihoji kuhusu Muungano akimtaka afafanue kuhusu kura ya theluthi mbili kwa pande za muungano.

“Sheria hii itatumika kwa muungano ambao kwa Katiba ya sasa ina mambo 22. Kwa utaratibu wa sasa ili jambo liamuliwe ni lazima likubaliwe na theluthi mbili kwa kila upande, mapendekezo yenu yanaendana na katiba hii?” alihoji Lissu na kuongeza:

“Kwa kuwa Katiba ya sasa haizungumzii kura ya maoni, mnaona suala hili ni la kikatiba?”

Huku akionyesha katiba za Kenya, Zanzibar na Zimbabwe na Afrika Kusini zinazoeleza kuhusu mambo maalumu ya kupigia kura ya maoni, Lissu alimuuliza Tadayo kuhusu muswada huo kumtaka Rais kuitisha kura hiyo kwa jambo lolote lile.

Akijibu hoja hizo, Tadayo alisema hawezi kufafanua kuhusu masuala ya muungano hadi atakapowasiliana na katibu mkuu wa chama hicho na kuleta majibu kwa maandishi. ‘Tusilitazame suala la kura ya maoni kama la Muungano. Halafu siyo sahihi kusema kuwa kura hiyo haiko kikatiba. Hata kama halijatajwa katiba yetu imetoa utaratibu wa kidemokrasia,” alisema Tadayo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.