NAPE

Ahmed Rajab,

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) ni chama cha siasa chenye uzoefu wa kutawala kwa muda mrefu barani Afrika kuvipita vyama vyote vingine. Ni chama chenye ujanja mwingi, ulaghai mwingi lakini pia kina umahiri wa aina yake.

Nadhani cha pili yake barani humo ni kile cha Movimento Popular de Libertação de Angola – Partido do Trabalho (kwa ufupi, MPLA) kilichoanza kuitawala Angola tangu nchi hiyo ilipopewa uhuru wake na Wareno mwaka 1975.

Hiki cha MPLA nacho kina ujanja mwingi, ulaghai mwingi lakini pia kina umahiri wa aina yake. Vyote vinanuka uvundo wa ufisadi, ingawa kuna kuzidiana.

Kweli ufisadi ni ufisadi lakini tukiwaweka kwenye mizani tutaona kwamba viongozi wa MPLA wamewazidi wenzao wa CCM kwa ufisadi. Ufisadi wao umefurutu ada nani wa babu kubwa.

Ingawa CCM kiliundwa 1977 vilipounganishwa vyama vya Tanganyika African Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) kwa hakika kimekuwa na uzoefu wa kutawala tangu Tanganyika ipate uhuru 1961 na hatamu za utawala kukabidhiwa chama cha TANU.

ASP kilianza kutawala tangu 1964 baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wakati wa enzi ya mfumo wa chama kimoja CCM kilikuwa hakishikiki. Kilijifanyia kitakavyo.

Kulikuwa hakuna wa kukisemesha nje ya chama. Na hata pangekuwako kisingelimsikiliza. Kibri chake kilikuwa kikubwa. Ndo maana kikawa na mazoea ya kujitwaza.

Ndani ya chama kikimsikiliza Mwalimu Julius Nyerere peke yake wakati wa uhai wake.

Wala chama hicho hakikukabiliwa na upinzani rasmi nchini kwa vile ulipigwa marufuku. Hata ndani ya chama chenyewe upinzani au ukinzani wa aina yoyote ile haukuwa ukivumiliwa.

Waliokuwa wakienda kinyume na sera za chama au wale waliozikosoa sera hizo wakionekana kuwa ni maadui si wa chama tu bali hata wa taifa. Kwa ufupi, wapinzani hao wakichukuliwa kuwa ni wasaliti au wahaini wa nchi yao.

Kwa kiwango fulani, dhana hiyo hadi hii leo bado wanayo baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho.

Siku hizi kuna vyama vingine, rai nyingine na taasisi nyingine za kukisemesha. Kuna mipaka ya kiutendaji ambayo kisheria hakiruhusiwi kuikiuka.

Hata hivyo kama nilivyokwishagusia CCM ina umahiri wa aina yake. Ina mbinu zake inazozitumia kuhakikisha kwamba inayapata inayoyataka ikiwa pamoja na kuendelea kuselelea kwenye madaraka.

Kulifikia lengo hili CCM kinajaribu kutumia mbinu zile zile kama zinazotumiwa na MPLA nchini Angola kwani ni wazi kwamba viongozi wa CCM wana mengi ya kujifunza kutoka kwa viongozi wa MPLA kuhusu namna ya kusehelea katika madaraka.

Kwa hili viongozi wa MPLA wamewapiku wa CCM na zaidi kwa kuwa Angola nayo siku hizi ina mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Viongozi wa MPLA wameweza kuwapiku wale wa CCM kwa sababu vyama vya upinzani vya Angola ni dhaifu mno na havifui dafu kwa MPLA. Vyama hivyo ni dhaifu kwa sababu MPLA imekuwa ikitumia hila na mbinu mahususi za kuvivunja nguvu.

La kushangaza na labda linalohusudiwa zaidi na viongozi wa juu wa CCM ni jinsi viongozi wa MPLA walivyoweza kuwa madarakani kwa muda mrefu, wengine tangu 1975.

José Eduardo dos Santos bado ni Rais tangu ayashike madaraka hayo Septemba 21, 1979 siku kumi na moja baada ya kufariki Agostinho Neto, Rais wa kwanza wa nchi hiyo.

Nchini Tanzania licha ya upinzani mkali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huko Bara na Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar — CCM kimejiandaa vilivyo kukiuka vizingiti vilivyopo bila ya kuonekana kwamba kinafanya hivyo.

Mfano mzuri ni mchezo uliochezwa na makada pamoja na wafuasi wengine wa CCM katika Mabaraza ya Katiba ya wilaya za Unguja. Ninasema ‘mchezo’ kwa sababu wana-CCM hao walicheza.

Ya Bara siyajui; ya Pemba ni mengine lakini ya hapa Unguja yanaonyesha wazi jinsi CCM/Zanzibar ilivyojiandaa kuucheza mchezo wao wakati wa kuichambua Rasimu ya Katiba mpya iliyozinduliwa Juni 3 na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Kuna jambo moja lililodhihirika katika vikao vya Unguja vya Mabaraza ya Katiba ambapo Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokea maoni ya wajumbe wa mabaraza hayo waliochaguliwa na wananchi. Nalo ni kwamba wengi wa wajumbe hao walikuwa ni wana-CCM na walikuwa ‘wamekwishapikwa’ na CCM.

Si hayo tu bali wamesikika wazi wakiimba nyimbo yao hiyo hiyo moja ya kutaka muundo wa Muungano ubakie uwe wa serikali mbili, kama ulivyo sasa.

Hapa Unguja ni wajumbe wachache waliopendekeza pawepo muundo wa shirikisho la serikali tatu. Na wachache mno waliopendekeza Muungano wa Mkataba.

Isitoshe. Hao wajumbe waliotaka serikali mbili wamekuwa pia wakitoa hoja zilizo sare, zisizotafautiana hata kwa kauli. Wengine wakionekana wakisoma kutoka waraka wa mwongozo ambao inasemekana walipewa na CCM kuhusu suala hilo.

Ni mapema kwa sasa kuweza kujua iwapo mbinu hiyo ya CCM itafanikiwa hatimaye au la kwa sababu baada ya kumalizika mikutano ya Mabaraza ya Katiba Septemba 2 mwaka huu, kutabaki hatua mbili nyingine za kufikiwa kabla ya kupatikana Katiba Mpya.

Ya kwanza ni kujadiliwa Rasimu katika Bunge la Katiba na ya pili ni ya kuwaachia wananchi waamue kuhusu Rasimu hiyo kwenye Kura ya Maoni.

Binafsi siamini kwamba mbinu hiyo itafanikiwa. Sababu kubwa niliyo nayo ni kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba amekwishatoa kauli yake kwamba vikao hivyo vya Mabaraza ya Katiba vinafuata taratibu maalum zilizopo.

Mimi ninaifasiri ifuatavyo kauli ya Warioba: lengo la Mabaraza ya Katiba ni kuwapa wananchi fursa ya kutoa maoni yao juu ya namna ya kuifanya Rasimu ya Katiba iwe bora — sio kubadili mapendekezo makuu ya Rasimu hiyo au kuijadili Rasimu Mbadala ambayo inasemekana imeandaliwa na CCM.

Aidha Warioba amekwishasema wazi kwamba hakuna yoyote, ikiwa pamoja na vyama vya siasa, mwenye ruhusa ya kuingia katika Mabaraza hayo kwa lengo la kushawishi maoni ya aina fulani yakubaliwe.

Lengo la vikao vya Mabaraza ya Katiba, kwa mujibu wa Warioba, siyo kupiga kura bali ni kujadili na kutoa hoja.

Idadi ya Mabaraza yote ya Katiba ni 177. Kati ya haya Bara ina mabaraza 163 na Zanzibar ina 13. Muundo wa Muungano wa serikali tatu umekuwa ukiungwa mkono sana huko Bara.

Hata hivyo lazima tukubali kwamba CCM/Zanzibar ‘ilicheza’ kama ilivyozoea kucheza. CCM haikumkiuka Warioba aliyevionya vyama vya siasa visiviingilie vikao vya Mabaraza ya Katiba.

CCM/Zanzibar ilikuwa na mkakati mwingine. Baada ya Rasimu ya Katiba kusambazwa katika vijiji, mitaa na shehia kwa ajili ya kujadiliwa na wananchi CCM/Zanzibar ilikuwa na vikao vya siri vya kuwaandaa watu wao waliokuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuwapa mwongozo wa kufuata walipokuwa wanachangia mawazo yao juu ya Rasimu ya Katiba.

Hivyo CCM/Zanzibar haikulala. Muda wote huu tangu izinduliwe Rasimu ya Katiba imekuwa ikifanya kampeni ya chini kwa chini na ya dhahiri ya kuwaeleza wanachama wake msimamo wake kuhusu muundo wa Muungano.

Kwa upande mwingine, watetezi wa muundo wa Muungano utaoipa Zanzibar mamlaka kamili wamepata pigo kubwa tangu watiwe ndani mashekhe wa Uamsho ambao ingawa si wanasiasa waliwahamasisha Wazanzibari na kuwaunganisha juu ya suala hilo. Hivyo sitostaajabu ikiwa wenye nguvu wataendelea kuwaweka ndani mashekhe hao hadi itapopatikana Katiba mpya au hata mpaka uchaguzi ujao wa 2015.

raiamwema

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.