balozi karume

Balozi Mstaafu Ali Karume

NA MWINYI SADALLAH

Balozi mstaafu, Ali Abeid Karume amesema kama wananchi wa England chini ya Malkia Elizabeth wa II hawafikirii na kutamani mamlaka kamili au kujitoa katika Muungano wa UK hakuna ulazima kwa Tanganyika na Zanzibar kuwa na viti Umoja wa Mataifa.

Balozi Karume alisema hayo katika mahojiano maalum na NIPASHE yaliofanyika nyumbani kwake huko Maisara Suleiman mjini Unguja.

Alisema pamoja na nchi za Scotchland, Wales na Northern Island kuwa na serikali za ndani, bado England haina mamlaka kamili na haifikirii kuwa na kiti Umoja wa Mataifa au kujitoa katika Muungano wa Uingereza.

Alisema England ndiyo nchi anayotoka Malkia Elizabeth II ambayo haina serikali ya ndani lakini makubaliano ya kimuungano ya nchi nne ni kuwa chini ya UK huku mambo ya msingi kama sarafu, benki kuu, mambo ya nje, ulinzi na usalama vikisimamiwa na kuongozwa na serikali ya Waziri Mkuu.

Akiwashangaa baadhi ya wanasiasa wanaokaza misuli, kuwashawishi wananchi ili kuhoji hati ya Muungano na kubadili mfumo uliopo ili kuwa na serikali tatu, alisema wanachojaribu kukifanya ni kuwayumbisha wananchi na kutazama maslahi binafsi kuliko ya umma.

“Hati ya ndoa si muhimu kuliko upendo, maelewano na mapatano kati ya mke na mume, cheti cha ndoa hakiwezi kulea ndoa, ni ushahidi utokanao na mapatano yasiojenga wala kubatilisha ndoa,”alisema Balozi Karume.

Mwanadiplomasia huyo ambaye alikuwa Balozi katika nchi za Marekani, Ujerumani, Ubeligiji na Italia kwa miaka kadhaa, alisema wanadamu werevu siku zote huongozwa na shauku ya kushamirisha nguvu ya umoja ili kujijenga kiuchumi na kuwaletea maisha bora wananchi.

Aidha alisema jambo muhimu katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni pande mbili kuzungumzia kero zilizopo na kuzipatia utatuzi na wala si kuwa na ndoto ya kuvunja Muungano au ongezeko la idadi ya serikali .

Alisema ikiwa Tanganyika itaachiwa kupata mamlaka kamili kuna hatari ya Rais wake siku moja akatamani mamlaka zaidi na kusababisha Muungano kuvunjika.

Alisema hata leo ikiwa England itaamua kuunda serikali yake, Muungano wa UK hautabaki salama utazua mzozo hatimaye utasambaratika na kuvunjika kwa kuwa nchi zote nne zitataka kuwa na kiti UN.

Balozi Karume alisema ikiwa Tanganyika itaachiwa na kuwa na serikali yake na Rais wake akawa si mwenye kujua historia na kukosa ustahimilivu, anaweza kufikiria kuwa nchi yake ilishapata uhuru tokea mwaka 1961 hivyo ni rahisi kujitoa katika Muungano na kuchukua kiti chake UN.

4 thoughts on “Hata England haina mamlaka kamili – Karume”

  1. Wewe ulikuwa unakula kuku huko nje hujui hata matatizo ya wazanzibar huku! Unarudi kule kule kwenye kero, watu wamechoka na ahadi wanataka vitendo!

  2. mheshimiwa wewe nyamaza tu hao wanolalamika ni wale maskini za Mungu, ambao miaka yote 50 hawajapata faida yoyote ya smz wala smt, wewe huwezi kulalamika kwasababu umepata maslahi kibao, wewe tumia jasho letu tu hapo lakini usitukejeli

  3. Muungano uliopo UK sio muungano wa kisiasa ni muungano wa kiuchumi ndo maana serikali za weles, scotland zina mamlaka kamili pia zinauwezo wa kushiriki hata kombe la dunia. kinachotusikitisha zanzibar hatuna fursa ya kushiriki hilo kombe la dunia, hatuna wigo wa kufangamana na nchi yoyote kibiashara mpaka tupate kibali au ridhaa kutoka Tanganyika wewe hulioni hilo au unaongea ujinga tu. FIKIRI KABLA YA KUSEMA.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.