UwanjaJengo-la-uwanja-wa-ndege

Na A K Simai

Niliwahi kuandika takriban mwaka mmoja uliopita kwamba kulikuwa na matatizo katika ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege katika makala yangu ‘Jengo jipya la uwanja wa ndege kunaini?’

Hivi karibuni kupitia kwa Waziri mwenye dhamana ya Mawasiliano na Miundo mbinu alisema katika baraza la wawakilishi wakati akiwasilisha bajeti ya makadirio na mapato ya wizara yake na nanukuu:

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa ruhusa ya kuendelea kwa ujenzi wa Jengo jipya la Abiria katika Uwanja wa ndege wa Zanzibar lililosita kwa muda baada ya kuonekana kasoro za kiufundi zilizojitokeza hapo awali katika jengo hilo.

Amesema katika kutekeleza hilo ujenzi huo umeanza mara baada kukamilika kwa taratibu za Michoro mipya kwa baadhi ya sehemu za jengo baada ya kupata Mshauri elekezi kutoka Nchini Ufaransa.

“Mnamo mwezi wa Machi mwaka huu tulimpata mshauri elekezi na kuanza kazi mwezi April na kutoa ripoti yake mwezi Juni mwaka huu ambavyo ilionesha namna ya kasoro zilivyojitokeza na kuweza kutatuliwa haraka ipasavyo .”alisema Waziri Rashid Seif.

Nikiwa kama mwananchi na mkereketwa nimebakia tena na masuali yangu yale yale niliyoyaanika mwaka mmoja uliopita na si vibaya kama nitayakariri kwani maelezo ya Waziri hayajanipatia majibu ya kuridhisha.

Pia sikusikia waheshimiwa wawakilishi wakitishia angalau kuzuia shilingi katika bajeti hii mpaka wapate maelezo hatua gani zilichukuliwa dhidi ya watendaji waliopelekea dosari hizi kutokea.

  1. Ni timu gani iliyokuwemo katika kuandaa plan ya jengo hili ni watu waliokuwa na uzoefu kwenye aviation au ni watu wa kuokoteza tu?
  2. Hakukuwa na consultancy wakati wa kuandaa plan yenyewe na hakukuwa na kureview kuangalia kama kila kinachohitajika katika Airport ya kile kimewekwa?
  3. Tulikurupuka katika kuingia mkataba huu ambao kwa sasa utaweza kutuingiza kwenye janga zito la deni lenye kuongezeka kwa riba pamoja na kuongezeka kwa gharama?
  4. Kutakuwa na hatua zozote za kinidhamu au kuwajibika kwa waliotuingiza katika balaa hili au kulikuwa na mazingira ya ten percent?

Jengo lilisimamishwa mwezi July mwaka 2012 na tokea wakati huo Serikali ilikuwa ikihangaika kupata mshauri mwelekezi na katika hatua hii iliwachukua miezi 9 kumpata mshauri mwelekezi mwenye uweledi wa aina za kazi hizi. Well done Waziri kwa kulitatua hili haraka ipasavyo.

Maelezo ya Waziri hayaoneshi katika sehemu yoyote kwamba Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu au kuwawajibisha wale wote ambao walihusika kwa njia moja au nyengine katika kuitia hasara kubwa Serikali hii na kuiongezea deni maradufu kwa kuombwa mkopo wa ziada zaidi ya ule wa wa US$ 70.4 milioni kutoka Exim Bank ya China.
Sijui interest rate yake ni kiasi gani ila kulilipa hili itakuwa shughuli pevu kwani nilitarajia mhe Waziri angalau angelitutajia ziada iliyoombwa kwenye mkopo huu ili nasi walipa kodi tuanze kujiandaa.

Serikali haioni haja ya kuwawajibisha watendaji waliomtia aibu hata Rais wetu wakati alipokuwa akikaguwa jengo hilo mwaka 2012 na kumhakikishia kwamba litakamilka katika muda wake uliopangwa.

Dhana ya utawala bora inayosimamiwa na serikali haionekani kutekelezeka kwa vitendo bali imebaki katika miongozo na kwenye semina elekezi tu?.

Mojawapo ya mipangilio ya utawala bora ni sera ya uwajibikaji kutekelezwa kikamilifu kwa kila aliyekwenda kinyume na malengo au maafikiano na dhamana alizokabidhiwa bila ya kuoneana muhali au kuchukuliana baada ya kuthibitika kwamba ni kweli uzembe ulikuwa umetendeka.

Tunataka ushahidi gani tena katika suala hili kama kulikuwa na uzembe?

One thought on “Dhana ya utawala bora ilipokosa meno”

  1. ukiona hivyo wewe jua kuna wakubwa wameshiriki kuhujumu jasho letu hapo, sisi tutabaki hivi hivi mpaka kiama kitafika

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.