Sheikh Mselllem, mmoja wa masheikh wa Uamsho waliowekwa ndani karibuni mwaka sasa na serikali ya Zanzibar.
Sheikh Mselllem, mmoja wa masheikh wa Uamsho waliowekwa ndani karibuni mwaka sasa na serikali ya Zanzibar.

Kuna kimya kinachonishangaza. Nacho ni cha ‘wanaharakati’ wa Kizanzibari walioziba midomo yao kuhusu madhila yanayowakuta wale waliokuwa wakiwaita “mashekhe wetu wa Uamsho”.

Tangu mashekhe hao 10 waanze kukamatwa Oktoba 16, 2012 mpaka leo kesi yao haijatajwa mahakamani. Hadi sasa wamesomewa tu mashtaka dhidi yao, mashtaka ambayo yanahusika na vurugu zilizotokea Zanzibar Mei mwaka jana.

Washtakiwa hao walifikishwa mara ya mwisho mahakamani Julai 3 mwaka huu na wanatarajiwa kupandishwa tena mahakamani Julai 18.

Washtakiwa wenyewe ni Farid Hadi Ahmed, Msellem Ali Msellem, Mussa Juma Issa, Azan Khalid Hamdani, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman, Ghalib Ahmada Omar, Abdalla Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini.

Mashtaka yanayowakabili ni kuchochea vurugu, kuharibu mali za umma na za watu binafsi zenye thamani ya shilingi milioni 500, kufanya vurugu katika eneo la Magogoni na kuhatarisha usalama wa taifa la Zanzibar.

Wanashtakiwa pia kuhusu kadhia ya Farid Hadi Ahmed aliyetoweka Oktoba 16, 2012.
Shekhe huyo aliibuka siku nne baadaye akidai kwamba alitekwa nyara na watu waliovaa barkoa waliojitambulisha kuwa ni polisi. Serikali imelikanusha dai hilo.
Mashekhe hao wamefungiwa kwenye gereza la Kiinua Miguu wakiwa chini ya ulinzi mkali. Kama wiki mbili za mwanzo baada ya kutiwa nguvuni wakidhalilishwa kwa kunyimwa hata nafasi ya kubadili nguo au ya kuonana na familia zao.

Tena kila mtuhumiwa alikuwa akiwekwa katika chumba cha peke yake. Tunavyosikia ni kwamba siku hizi wameondoshewa madhila hayo ingawa bado mazingira yao si ya kuridhisha.

Cha kushangaza ni kwamba hatusikii sauti zozote zenye kuwatetea. Labda kwa sababu wao ni mashekhe na si wanasiasa. Labda wangekuwa wanasiasa tungewaona wanaharakati, kwa mfano, wakiwasiliana na jumuiya za kimataifa za haki za binadamu na kuzizindua kuhusu janga lililowafika mashekhe hao.

Labda madevu ya hao mashekhe yanawatia hofu wanaharakati, wanachelea wasije wakashtumiwa kuwa wanawatetea ‘magaidi’ maana siku hizi kwa wakubwa wa dunia hii madevu, Uislamu na utetezi wa haki ni mchanganyiko wa hatari.

Na si kwa hao wakubwa tu bali hatakwa baadhi ya taasisi, magazeti, na wanasiasa wa Tanzania Bara ambao bila ya ushahidi wowote wameihusisha Uamsho na vitendo vya kigaidi.

Juu ya yote hayo, kuna sababu halali za kuwatetea. Sababu kubwa ni kazi walioifanya ya ‘kuwaamsha’ Wazanzibariwenzao wautambue utaifa wao na waachane na chuki na uhasama uliokuwepo baina yao kwa muda mrefu.

Jengine jema walilolifanya ni kuwahimiza vijana wa Kizanzibari warudi kwenye maadili ya Kiislamu badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoleta madhara katika jamii kama vile vya kubugia mihadarati na uasherati.

Pengine kuna wanaharakati wenye kujuta, wenye kuona kwamba walipoteza nguvu zao walipokuwa wakiwaunga mkono hao mashekhe. Wale waliokuwa na majazba waliokuwa wakiota kwamba siku moja nchi yao itaamka ghafla ionekane na sura nyingine sasa itawabidi waote ndotonyingine.

Sina dhamira ya kuingilia kesi inayowakabili washtakiwa hao. Hiyo ni kazi ya mahakama na ya mawakili.

Dhamiri yangu ni kukizungumzia hiki kimya kilichotanda kama wingu juu ya kesi hii.Na zaidi nataka kugusiahaki wanayonyimwa washtakiwa ya kuachiwakwa dhamana huku kesi ikiwa inaendelea. Kucheleweshwa kusikilizwa kwa kesi hiyoni adha kubwa kwa washtakiwa.

Inavyoonyesha nikama serikali imeamua kuwatia adabu ingawa hawakupatikana na hatia.

Ikiwa dhana hiyo ni sahihi basi serikali itakuwa imeamua hivyo kwa sababu za kisiasa. Serikali inazidi kujifaragua ikiamini kwamba kuwatia adabu viongozi wenye muelekeo wa Kiislamu hakutowakera wakubwa wa dunia hii.

Labda serikali inaamini kwamba balozi za Marekani na Uingereza zitayafumbia macho wanayotendewa mashekhe hao kwa sababu zimekwishatiwa sumu ya Uamsho kusingiziwa ugaidi.

Ndio maana kesi hiyo ikawa inaakhirishwa na kuakhirishwa kwa lengo la kuwaweka ndani tu mashekhe hao. Mara ya mwisho Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar alisema wanasubiri waletewe daftari la kesi kutoka Mahakama ya Rufaa, Dar es Salaam.
Sijui Wazanzibari wenzangu wanapofuturu na aila zao katika mwezi huu mtukufu kama wanawafikiria wananchi wenzao walio gerezani.

Nijualo ni kwamba ingawa uamuzi ni wa mahakama wengi wenye kuifuatilia kesi hii wanaamini washtakiwa hao wanaendelea kuwekwa ndani kwa sababu hivyo ndivyo watakavyo viongozi wa juu wa serikali ya Zanzibar.

Mara mbili tatu hivi Rais Ali Mohamed Shein mwenyewe amesema hadharani kuwa atawashughulikia wanaochochea fujo.Wakati mwingine huwataja Uamsho.
Zanzibar ya leo ni nchi yenye kuhuzunisha; haisikitishi tu bali inahuzunisha. Ni nchi yenye kutatanisha, wakati mwingine hujikanganya yenyewe.Na viongozi wake? Naona hata haina haja ya kuwaeleza walivyo; bora tulifunike kombe…

Chanzo: Hii ni sehemu ya makala “Ya Malala, Taliban na Uamsho” ya Ahmed Rajab kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 17 Julai 2013.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.