Waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere (kushoto) na Abeid Karume.
Waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere (kushoto) na Abeid Karume.

NCHI yetu kwa sasa inapita katika kipindi muhimu cha kujadili na kuboresha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Pamoja na mambo mengine, rasimu  imependekeza kuwa na Muungano wa Shirikisho lenye serikali tatu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara. Mapendekezo haya yameibua mjadala mzito, baadhi wakiunga mkono na wengine kupinga.

Lakini kilichojitokeza katika mijadala hiyo ni watu wengi kutojua dhana ya shirikisho. Nami nitajadili maana hasa ya dhana ya shirikisho kama ifuatavyo.

Muundo wa Shirikisho ni nini?

Kwa asili ya muundo wa shirikisho, wananchi wanatawaliwa na ngazi mbili za serikali yaani Serikali ya Muungano na Serikali za Washirika. Kila serikali inakuwa na mamlaka kulingana na majukumu iliyokabidhiwa kikatiba. Kwa kawaida, Serikali ya Muungano inakuwa na mamlaka kwa masuala yote yaliyokubaliwa kuwa ya Muungano wakati Serikali za Washirika zinakuwa na mamlaka ya kikatiba kushughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano.

Katika mfumo huu, kwa kawaida Katiba ya Muungano inaweka uwepo wa serikali (utendaji), Bunge/Baraza la wawakilishi na Mahakama katika ngazi ya Muungano  na vivyo hivyo kwa Washirika wa Muungano. Katika mgawanyiko huo, serikali ya shirikisho pekee huwa na mamlaka ya kushughulikia masuala makuu ya kidola (sovereign functions).

Kwa sababu, hiyo, majukumu yote yanayohusu mamlaka kuu ya nchi kama vile ulinzi na usalama, mambo ya nje, fedha na uraia huwa chini ya serikali ya shirikisho. Hivyo, serikali ya shirikisho inakuwa na mamlaka juu ya wananchi wote waliopo katika eneo lote la nchi wakati washirika wanakuwa na mamlaka katika maeneo yao pekee.

Katiba ya nchi inaweza ikaamua mgawanyo wa majukumu wa masuala mengine yote baina ya serikali ya shirikisho na serikali za washirika. Katika muundo huu katiba ya shirikisho ina mamlaka kuu katika nchi (supremacy status).

Historia inaonyesha kuwa nchi  zinazofuata muundo huu zimefanya kwa sababu mbalimbali. Kuna nchi ambazo zimetokana na muungano wa nchi zilizokuwa huru au makoloni  na hivyo zikaamua kufuata muundo huu ili kutoa fursa kwa Washirika wa Muungano kubakisha utambulisho wao na kufanya mambo yao kadiri wanavyoona.  Shirikisho la Marekani, Canada na Ujerumani ni mfano wa mashirikisho ya namna hii. Katika nchi hizi kuna serikali ya shirikisho na serikali za majimbo zenye mamlaka kuhusu masuala ya majimbo yao.

Pia, kuna mashirikisho yaliyotokana na msukumo wa kidemokrasia unaoambatana na utambulisho wa aina mbalimbali ndani ya  nchi. Utambulisho huu unaweza kuwa ni wa dini, makabila, historia, lugha na tofauti za kieneo. Katika mazingira hayo, muundo wa shirikisho unafaa zaidi kwa kuwa unawafanya watu wabaki na utambulisho wao wa asili na kuendelea kuwa raia wa nchi zao. India, Nigeria na Ubelgiji ni mfano wa ambayo kwa kiwango kikubwa yametokana na msukumo huu.

Muundo wa Shirikisho Tanzania

Mfumo wa shirikisho unaonekana kuendelea kuungwa mkono maeneo mengi duniani kwa sababu ya manufaa yake. Sina hakika kuhusu sababu ambazo Tume ya Mzee Warioba ilitumia kufikia uamuzi wa kupendekeza muundo huu.

Hata hivyo, uzoefu wa nchi zingine na changamoto zilizopo kwetu zinaonyesha kuwa muundo huu unaweza ukakuza demokrasia ndani ya nchi kwa kuwezesha kila upande wa Muungano kubaki na utambulisho wake wa kihistoria na kiutamaduni.

Hii ina maana Wazanzibari naWatanganyika wataweza kupitia serikali zao kufuata na kutekeleza mambo wanayotaka wao kwa maslahi yao. Kwa mantiki hiyo, kero za Muungano zinazotokana na hisia za upande mmoja kunufaika zaidi na Muungano zitapungua. Sifa hii ya  muundo wa shirikisho umefanya nchi zote  zenye idadi kubwa ya watu zaidi ya 100 (ukiacha Japan na Indonesia) zinafuata mfumo wa shirikisho.

Nakubaliana na wanaosema muundo wa shirikisho unaweza kusaidia kuimarisha amani na utulivu zaidi ya muundo mwingine wowote. Kumekuwa na chokochoko za muda mrefu ambazo kwa baadhi ya nyakati ilichochea kuchafuka kwa hali ya usalama wa nchi hasa kutoka Zanzibar kutokana na hisia za kutaka madaraka zaidi juu ya mambo yao.

Kwa muundo wa shirikisho, kila upande utakuwa na mamlaka ya kushughulikia mambo yake na hivyo bila shaka hali ya hewa ya kisiasa inaweza ikawa na utulivu wa kudumu. Miaka 60 iliyopita hakuna mtu aliyefikiria kuwa India inaweza ikawa na amani kama nchi ya kidemokrasia lakini kwa kiwango kikubwa kudumu kwa amani na demokrasia iliyopo India kwa sasa kumetokana na kuamua kufuata mfumo wa shirikisho.

Pamoja na faida hizo,bado kuna baadhi ya wana wasiwasi na woga juu ya muudo huu wa shirikisho. Maoni mengi yanayotolewa kupinga mfumo huu ni hofu ya kuwa mfumo huu unaongeza gharama za uendeshaji wa serikali  na utaifanya serikali ya muungano iwe tegemezi kwa washirika. Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa serikali ya shirikisho huwa na vyanzo vyake vya fedha ili iweze kujiendesha bila kuwa tegemezi kwa washirika.

Bila shaka ni kwa sababu hiyo, Mzee Warioba na wenzake wanapendekeza chanzo cha mapato ya serikali ya muungano kiwe ni kodi ya ushuru wa bidhaa na maduhuli yatokanayo na huduma mbalimbali zinazopatikana kwenye mambo ya muungano. Jukumu letu sasa ni kutathmni na kuona kama pendekezo hilo linakidhi haja ya kuendesha serikali ya Muungano kulingana na muundo uliopendekezwa.Kwa maoni yangu, serikali ya muungano inaweza pia kupata mapato kutoka kwa uwekezaji kwenye maeneo maalum ya uwekezaji baharini (Exclusive Economic Zone).

Pia, inadaiwa kuwa, muundo huu unaweza kuleta utata na urasimu katika uendeshaji wa shughuli za maendeleo na hata kusababisha migongano ya kisheria na kiutawala na kuleta hatari ya kuvunjika kwa muungano. Hasa kwa kuwa, rasimu imependekeza kuwa serikali zote zitakuwa chini ya viongozi wanoitwa Rais. Hata hivyo,  hili si tatizo la mfumo  kwa maana migongano inaweza kutokea kwenye mfumo wowote. Hata sasa kwenye muundo wa serikali mbili, kuna migongano na sintofahamu nyingi zijulikanazo kama kero za muungano. Tatizo hili linaweza kukabiliwa kwa kuwa na mfumo unaojielekeza katika utiii wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Mara nyingi, Jamhuri ya Kisovieti na Jamhuri ya Czechoslovakia hutolewa kama mifano ya nchi zilivunjika kwa kuwa na muundo wa shirikisho. Hata hivyo, dola hizo zilikuwa shirikisho kwa jina tu ingawa zilikuwa na katiba za shirikisho. Madaraka yote yalikuwa chini ya chama cha kikomunisti. Kukosekana kwa utii wa sheria na demokrasia na uimla wa chamacha kikomunisti kwa kiwango kikubwa ndicho chanzo cha kuanguka kwa dola hizo. Kwa kwetu hapa, uimla huo haupo.

Aidha, tunaweza kupendekeza majina mbadala ya viongozi wakuu wa washirika wa muungano na jina la Rais libaki kwa Rais wa Jamhuri  ya Muungano pekee. Nilivyoisoma rasimu inaonekana kwa kweli kuwa Rais mwenye mamlaka ya kidola ni mmoja na  wale viongozi  wa Tanzania Bara na Zanzibar tunaweza kuwaita jina lingine lolote bila athari zozote. Kama nilivyoona mimi, madaraka yao ni sawa na madaraka ya magavana wa majimbo katika nchi kama Marekani au mawaziri wakuu wa majimbo ya Afrika ya Kusini.

Na kama wanavyosema wengi, inawezekana hakuna sababu ya msingi kuwaita viongozi hao Marais. Bila shaka  wajumbe wa mabaraza ya katiba watalifikiria hili na kupendekeza  majina tofauti ambayo hayataleta mgongano.

Aidha, mfumo huu tofauti na mifumo mingine inayopendekezwa unaweza kupunguza migongano kwa kuwa unaweka bayana madaraka ya mamlaka zote tatu. Baadhi ya kero ambazo zinaweza kuondoka au kupungua kwa kufuata muundo wa shirikisho ni pamoja na  manung’uniko kuwa muundo uliopo umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika, ushiriki wa wabunge wa Zanzibar  katika kujadili na  kupitisha sheria kwa masuala yasiyo ya Muungano ndani ya Bunge na hofu ya Zanzibar kumezwa katika Muungano.

Madai mengine ambayo yamekuwa kero ni pamoja na hoja Tanganyika kudaiwa kujigeuza kuwa Serikali ya Tanzania na ugawanyaji wa mapato na uchangiaji gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano usio wa haki.

Chanzo: Makala ya John Missanga kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 17 Julai 2013.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.